UZOEFU (14) - CnZ Media

CnZ Media

Jisomee Simulizi Mpya Kila Siku

Jumanne, 6 Aprili 2021

UZOEFU (14)

Je unajua kwamba Simulizi zote unazozipata hapa zipo kwenye app ya CnZ Media?

Humo Pia Utakuta:
πŸ“– KUSOMA SIMULIZI
🎬 FILAMU na TAMTHILIA za KITANZANIA
πŸ˜‚ VIDEO za KUCHEKESHA
πŸ“‘ MAKALA za AFYA na MAPENZI

Install app hii GUSA HAPA utavipata vyote hivyo bure kabisa

JINA: UZOEFU
Mwandishi: Elisha Msafiri

SEHEMU YA KUMI NA NNE
ILIPOISHIA...
Lisa alipofika kwenye kona ya mwisho alinipungia mkono nami nikamtumia busu la upepo kisha akapotea kwenye mboni za macho yangu. Nilikitazama tena kile kidani chake cha silver kilivyong'aa kwa mkono wangu kisha nikakichum na moyo ukatabasam. Nikaianza safari ya kurudi nyumbani huku nafsi ikinisifu kwa kumiliki mtoto mkali.
SASA ENDELEA...
Baada ya muda mrefu kupita huku Lisa akiwa ameshaanza masomo yake ya chuo mkoani mbeya baada ya kukosa credit moja iliyomnyima kwenda elimu ya juu ya sekondari ( A level ).

Hapo ndipo penzi letu lilipozidi kupata changamoto. Awali nikiwa mkoani Tabora nakumbuka nilikuwa ni mtu mwenye pesa mingi hivyo nilitamani kuzitumia na mpenzi wangu Lisa kila wakati lakini cha ajabu Lisa alikataa kata kata, hakuhitaji hata senti tano kutoka kwangu, Hali hiyo ilinishangaza na kuniumiza pia. 

Kwanini mpenzi wangu hataki pesa zangu? Ama nikidogo? Kila nilipomuuliza Lisa ni kwanini hakuwa na jibu la msingi na wakati mwingine alijibu kiufupi " sasa mimi pesa za nini? " cha ajabu zaidi Lisa alikataa hata out (kutoka) mara kwa mara nahisi aliona ni matumizi mabaya ya pesa. 

Nilizoea hali hiyo na siku zikapita pamoja na changamoto zake. Lakini sasa siku hizo zilizopita zilirudi kivingine na changamoto zingine. Changamoto mpya ya sasa ilikuwa ni kutoa pesa.

Ilianza kama utani vile, nimekaa nimetulia unaingia ujumbe mfupi ' bby nna shida na elfu kumi plz' .Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kabisa Lisa kuomba pesa, moyoni mwangu nikafurahi kweli kwani nilipata nafasi ya kumuonyesha mrembo wangu jinsi nnavyomjali.Sikutuma elfu kumi elfu kumi niliyoombwa nilituma elfu ishirini na ya ziada. 

Pia nikajipongeza kwa kuwa na akiba tigo pesa kila wakati. Mwanaume akiba bwana, nilijisifu nilipokuwa nausoma ujumbe wa Lisa akinishukuru. 'No need to thank hun (huna haja ya kushukuru mpenzi) chako changu, changu chako' 

Nilimjibu Lisa kinamna hiyo huku moyoni mwangu kweli nikiona mimi na yeye ni kitu kimoja hivyo hapaswi kunishukuru, Hazikuisha siku tatu kipenzi changu Lisa alirudi tena na Shida ya shilingi elfu thelathini, Pia hiyo nayo kwangu haikuwa tatizo kwani shida za Lisa si ndio shida zangu pia? Au mimi naweza kutabasam vipi hali yakuwa Lisa hana raha? Bila shaka haiwezekani!! Hima hima nikatuma shilingi elfu thelathini na tano pamoja na pesa ya kutolea. 

Mpenzi wangu Lisa akashukuru sana na kwa mara nyingine nikamsisitiza kuwa hana haja ya kufanya hivyo kwani kunishukuru mimi ni sawa na kijishukuru mwenyewe. Sikushangaa hata kidogo Lisa kurudi baada ya siku tatu tu mara baada ya kuchukua hela, niliamini kuwa pesa niliyompa awali haikutosha kulimaliza tatizo alilokuwa nalo au pengine aliona haya kuniomba pesa nyingi

Siku zikapita na walau sasa palitulia kidogo ila siku ya Jumapili nikiwa nyumani naangalia tv, simu ilipiga kelele kuashiria kuwa ina ujumbe mfupi,japo mi ni mvivu kusoma ujumbe unaotoka kwa namba ngeni lakini nikausoma, nao ulisomeka hivi 'bby sory nw sitokuwa hewan 4n angu leo imedumbukia kwa maji akati nafua, hii no. Ya ma frnd! ur cwry Lisa'.

Lisa anipa taarifa hiyo ya kutokuwa hewani lakini mimi sikuwa na mawazo ya kizembe taarifa hiyo kwangu ilikuwa na maana ya kununua simu nyingine.

Sikuujibu ujumbe huo na badala yake nikapiga simu, Lisa akapokea tukaongea mawili matatu na kikubwa nikamuahidi kuwa atapata simu nyingine kabla ya siku tatu kuisha, akafurahi sana na simu ikakata.Siku iliyofuata mara baada tu ya kutoka shule, break ya kwanza ikawa Kariakoo, 

Nilipita kwenye maduka tofauti tofauti ya simu nikimtafutia mpenzi wangu simu, pesa kitu gani bwana mbele ya sauti tamu ya Lisa inayonipa usingizi mnono, niliweza kuzishuhudia simu nzuri ( kali ) tofauti tofauti zikiwa zinatabasam katika 

Maduka ya wahindi Kariakoo hali yakuwa wallet yangu imenuna kwa uhaba wa fedha. Mtu anajikuna mkono unapoishia, nikanunua moja niliyokuwa na uwezo nayo na jioni niliporudi nyumbani nilikuwa na sababu ya kumtafuta Lisa kwa kuwa nilikuwa na habari njema ya kumpa. 

Naam! Simu yake ilikuwa tayari na nilichohitaji toka kwake ni maelekezo jinsi ya kumtumia. Hilo nalo halikuwa tatizo tena mara baada ya kumpata hewani na mazungumzo kufika tamati, Kazi ikabaki asubuhi kudamkia stendi ya Ubungo kulikamilisha zoezi hilo.

Siku iliyofuata niliituma simu hiyo na majira ya saa nne za usiku Lisa alinipigia kwa namba yake tena kumaanisha kuwa ameupata mzigo wake.Japo alinishukuru lakini sauti yake ilionyesha wazi kuwa hakuridhika na nililithibitisha hilo mara baada ya wiki moja kupita, Lisa aliponitumia ujumbe mfupi kupitia namba ya rafiki yake tena kunijuza kuwa mchana alipoenda mjini wakati wa kurudi simu yake iliibwa kwenye daladala.

Japo mimi ni mwepesi sana katika kufanya maamuzi au kutoa ahadi kwenye mambo kama hayo.Siku hiyo nilikuwa mzito kidogo, Sikuwa mzito kwa sababu sikutaka kutoa anha anha! Hatua niliyokuwepo inaitwa ' natamani nikupe ila sina' . Wiki moja tu iliyopita nilimnunulia 

Lisa simu iliyokomba akiba yangu yote kiasi cha kuniacha mwanaume suruali leo hii wiki haijaisha karudi tena, hivi huyu Lisa anafikiri mimi pesa napata wapi hali ya kuwa anajua mimi ni mwanafunzi! Eti mi ni mtoto wa kiume hiyo ni sawa lakini mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. 

Ni sawa na askari hatakiwi kulalamika mshahara mdogo akati yeye ni polisi, Kwani Polisi ndio hawana tumbo?

Nilijikuta nawaza mambo mengi kwa mpigo bila kujua pesa ntapata wapi.

Nakumbuka maishani mwangu nilikuwa na ndoto tatu kubwa Ya kwanza nikuifanya familia yangu ijivunie kuwa na mtoto kama mimi na hilo nilifanikiwa, ndoto ya pili ilikuwa nikupata kazi nzuri itakayonifanya niishi bila matatizo ya pesa, hii ilikuwa bado haijatekelezeka na ya tatu ilikuwa nikuwa na msichana mkali mwenye vigezo vyote vya kuitwa mrembo hii nayo ilitekelezeka kwa asilimia zote. 

Lakini tatizo ni kwamba ndoto ya tatu ilitimia kabla ya yapili.Yaani niliweza kumiliki mtoto mkali kabla sijawa na kazi nzuri, sasa ntamuhudumia vipi!? Hapo ndipo tatizo lilipojibanza. Nilitaka kujilaumu kwa kung'ang'ania nisivyoviweza lakini sikuthubutu kufanya hivyo, Kazi nzuri kwangu mimi itakuwa na umuhimu gani badae iwapo sitapata kigoli mzuri nnayempenda. Hiyo ilikuwa ni hatua tu.Nikaamini siku moja ntaivuka na mambo yatakuwa sawa.

Wiki chache baadae baada ya mawasiliano yatabu baina yangu mimi na Lisa kutokana na mpenzi wangu kukosa simu.Hatimaye nilikuwa na habari njema tena ya kumpa. Niliweza kumnunulia smart phone kali ambayo aliipenda na kuifurahia huku akiiniacha mimi katika dimbwi la matatizo ya kupambana na walinzi wa shule kutokana na kutokulipa ada. Huku nyumbani napo nikilazimika kumpelekea mzee risiti ya kugushi ili anipunguzie tabu.

Matatizo yote hayo sikuyajali ili nimrizishe mke wangu mtarajiwa, Na usiku ulipowadia sauti yake mwanana kwenye simu ikanifanya nizisahau shida zangu zote za mchana.

Ulimwengu wa mapenzi sasa ulianza kunikaribisha kwenye maisha mapya ya madeni na ulaghai, Ili kuyatimiza mahitaji ya kifedha ya Lisa kila mara nililazimika kuwakopa marafiki ( washkaji) au kumlaghai baba anipe hela chini ya kofia ya michango ya shule, michango isiyokwisha kila uchao. Kama mtu asivyoweza kuipiga deki bahari ndivyo na mimi nilivyoshindwa kuyamudu majitaji ya Lisa, Kadri nilivyojitahidi kuyapangua ndivyo yalivyozidi kumiminika mithili ya bondia Mayweather. leo hiki kesho kile kila kinachokuja kina uzito kuliko mwenzake. 

Nilichoanza kuwaza sasa ni kwamba nakomolewa. Ivi inakuaje baba yake Lisa anashindwa kumuhudumia mwanae hali yakuwa jina lake linavuma Tabora yote kwa umaarufu wa pesa! wazo hilo likaniacha mdomo wazi, kwani familia ya kina Lisa ilikuwa vizuri kiuchumi. Mara ya kwanza nilijua pengine Lisa ananipima ni kiasi gani namjali lakini ni kipimo gani hicho kisichoisha kila uchao??.

Ukweli ni kwamba maisha ya ulaghai, mikopo na kuomba omba pesa kila siku kwa wazazi yalishanichosha na jambo moja nililolifikiria kwa wakati huo ni kuachana na Lisa ama kutafuta njia nyingine ya kunipatia kipato, tofauti na kuomba omba na kukopa!!

Maji ukishayavulia nguo kuyaoga hauna budi, nilishaamua kuwa na Lisa maisha yangu yote sasa vipi nimuache sababu ya pesa, Sikuwa nampenda tu Lisa shauri ya uzuri wake uliopitiliza. Ila moyo wangu haukuwahi kumsajili mpenzi mwingine zaidi yake, Hao ambao nimewahi kuwa nao walisajiliwa na kichwa tu na walipoenda mbali, ubongo nao uliwafutilia mbali kabisa, Lisa daima huishi moyoni mwangu, hata nampofikiria kwenye joto huhisi upepo mwanana unanipuliza.

Sababu hizo ndizo hunifanya nisimshirikishe mtu yeyote yule kwenye mambo yanayonihusu mimi na Lisa japo mficha maradhi kifo humuumbua ni bora kufa kwajili ya kitu flani kuliko kuishi bila sababu. Kwa tabia za Lisa alizozianzisha niliamini nikimueleza mtu yoyote yule basi ushauri wa haraka ambao angenipatia ni kuachana na msichana huyo, ushauri ambao nisingependa kabisa kuusikia. Niliamini ya kuwa hakuna anaejua ni kiasi gani nampenda Lisa zaidi yangu naMungu wangu, hata Lisa mwenyewe sidhani kama anafahamu ni kiasi gani sifurukuti kwake.

Siku chache baadae tangu wazo la kutafuta njia ya kuniingizia pesa lilipotia nanga kumkichwa nilimtafuta na kumpata Bwana Amani.Huyu alikuwa ni rafiki yangu kipenzi wa siku nyingi isipokuwa tofauti zetu mimi nayeye ilikuwa mimi ni mwanafunzi na yeye ni mfanyakazi, ingawa alikuwa ni kijana mdogo bado alikuwa na wadhifa mkubwa katika kampuni yao ya 

Numerator's Entertainment.Kampuni inayohusika na kuandaa matamasha ya burudani kila mwisho wa wiki. Nakumbuka mara ya kwanza rafiki yangu Amani alikuwa akinisisitiza kufanya kazi katika kampuni yao lakini nilikataa kila siku kwa kigezo kwamba shule kwanza alafu mambo mengine baadae. Lakini leo Bwana Amani alishangaa nimemfwata kwa miguu yangu mwenyewe nataka kazi.
" Lakini wewe si ulisema shule kwanza mambo mengine baadae!? " Amani aliuliza kwa mshangao akizani labda namtania.
"Sikiliza mshkaji (rafiki) wangu Amani mwanzo sikuwa na sababu yeyote ya mimi kufanya hivyo lakini sasa nnayo hiyo sababu ndomana nna haja ya kazi!" Nilimuelezea Amani kwa msisitizo naye akaonekana kuanza kunielewa.
"Wewe au umempiga mtu mimba nini hebu kuwa muwazi!'
" Hamna kitu kama hiyo unajua saivi nakaribia kuua skonga ( kumaliza shule) hivyo nimeamua kutafuta mchongo (kazi) ya kufanya mapema, si unajua tena kukaa hom ( nyumbani) sio issue eenh!!" Nilimfafanulia Amani huku sababu kuu nikiiweka nyuma ya pazia na yeye kwa kuwa ni rafiki yangu kipenzi lazima anielewe tu hata kama nisingekuwa na sababu hata moja.
" Nafurahi shughuli zenyewe unazielewa afu jumlisha na swagger (mikogo) zako tena mbona sana tu!"

Tuliongea mengi siku hiyo na Amani na uhakika wa kufanya kazi ukawa umetiki kwa asilimia mia, mjini Network (mtandao) bhana. Bila mtandao utaishia kuwa mtu wa mipango isiyotekelezeka.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA KWENYE APPLICATION YETU HIVYO UKIYAONA NAOMBA BONYEZA HAPO NDIO UNANIPA SAPOTI MIMI, UKIBONYEZA UNAWEZA KUCANCEL SIO LAZIMA UENDELE ULIKOPELEKWA, KIKUBWA UBONYEZE HATA MARA 2-3 KILA UKIFUNGUA APP YETU

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

TAZAMA KICHEKESHO HIKI KISHA BONYEZA SUBSCRIBE ILIYOPO CHINI YAKE WAKATI TUKIELEKEA KWENYE MUENDELEZO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni