KUTI KAVU (1) Jina: KUTI KAVU Mwandishi: Changas Mwangalela SEHEMU YA KWANZA MGUU wa kushoto ulipiga hatua ukifuatiwa na ule wa kulia, hatua kwa hatua lengo likiwa ni kufika kule alikokusudia. Bila kujali amechoka kiasi gani, aliendelea kusonga mbele licha ya utitiri wa mawazo uliofurika kichwani mwake. Viatu vyake aina ya mokasini nyeusi vilivyoanza kuchakaa, suruali yake nyeusi iliyopauka kiasi, na shati jeupe alilovaa, kwa pamoja vilitosha kabisa kudhihirisha hali ngumu ya uchumi aliyonayo kijana Dominic Masaka , au Domi kama wengi walivyolifupisha jina lake. Domi alikuwa amechomekea vema, na kuonekana maridadi kwa mavazi yake licha ya mpauko uliodhihiri waziwazi kwenye mavazi aliyovaa. Njaa iliyokuwa ikimfukuta tumboni mwake haikutosha kumkatisha tamaa na badala yake ilimuongezea hasira na kiu ya mafanikio ambayo ilikuwa ikijipambanua wazi wazi usoni pake. Kijana huyu mrefu wa wastani, mwenye sura jamali alikuwa akikatisha katika mtaa wa Azikiwe maeneo ya Posta mpya , eneo ambalo liko katikati kabisa ya j…