Vita vya Mapenzi (12)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
“Tafadhali usinikoroge kichwa, nadhani tulikwishaliongea hilo kuwa haliwezekani kutokana na hali ya nyumbani” Suhail alijitutumua na kujibu kiukali kidogo japo alijua kuwa nguvu za Shekhia hawezi kupambana nazo ila kwakuwa alijua kuwa anapendwa sana na jina mtu Yule hivyo aliitumia fursa hiyo ipasavyo, Shekhia akanywea, wakakubaliana na kuwanza maandalizi ya kurejea Bagamoyo na walikubaliana kufikia Mbezi ili isiwe rahisi kwa jamii inayomfahamu kumtilia shaka.
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Masaa mawili Baadae walikuwa Mbezi, mipango ya safari ikaratibiwa kwa haraka ili kesho yake awe Tabora,
*****
KIASI cha saa nne asubuhi ndege ya FastJet ilishusha matairi yake na hatimaye kushuka katika Uwanja wa Ndege mkoani Tabora ikiwa inatokea jijini Dar es Salaam. hapakuwa na pilikapilika ya watu uwanjani hapo kama ilivyozoeleka katika viwanja vikubwa vya ndege vilivyopo katika majiji kama vile Arusha, Mwanza, na Dar. Uwanja huu ulitawaliwa na mafungu ya watu wachache waliohudhuria uwanjani hapo bila shaka kuwapokea wageni wao.
Suhail Kusekwa alikuwa ni miongoni mwa Abiria walioteremka katika Ndege ile ya wastani huku mkononi akiwa na Begi moja tu kubwa huku macho yake akiwa ameyaficha ndani ya miwani myeusi. Aliinua mkono wake wa kulia na kuwangalia majira kupitia saa yake ya mkononi huku Akiendelea kutoka uwanjani hapo baada ya kukamilisha taratibu zilizowekwa makhsusi kwa ajili ya usalama kisha akainua kichwa juu akiangalia dereva Teksi yoyote wa kumchukuwa mpaka kwao.
Hakuwa na haja ya kuwaangalia watu waliokuwa wakipokea ndugu zao kwaku alijua hakuna alikwenda kumpokea kwakuwa hakutoa taarifa ya ujio wake kwa mtu yoyote. Akaenda mpaka akatoka katika geti maalum la kutokea uwanjano hapo, akamuona kijana mmoja dereva wa teksi akiwa tayari ameshafungua mlango wa gari yake huku akimuoneshea kwa Ishara Suhail kuwa amefungua mlango ule kwa ajili yake, ni uchangamfu wa kibiashara tu!
“Twende afisa tuwahi,” Aliongea dereva Yule huku akionesha shauku ya kumbeba mteja yule alieonekana ‘Matawi yaj uu’ kwa jinsi alivyo ‘Vunja kabati’ kwa vitu alivyonyuka, Miwani ghali usoni, Mkononi kuna saa aina ya Oxlux, Jinzi ya Deckies, na Shati kali la ‘draft draft’ na miguuni ameji’komelea’ raba kali za Reebok
“Mambo vipi kaka?,” Alisalimia Suhail baada ya kuwa ameketi ndani ya Teksi ile na wakati huo dereva nae akiitoa gari barabarani kuianza safari
“Poa mkubwa, Hongera kwa safari”
“Hivi hua ni Hongera kwa safari au Pole kwa safari?” Suhail alihoji kwa hali ya mzaha, na majibu aliyopewa yalikuwa ya mzaha kama ambavyo alivyotania yeye
“Aah Pole wanapewa wanaoshuka kwenye gari moshi huko kaka, ila we ulikuwa kwenye ‘Mwewe’ hata haujui kwanza umefikaje hapa” Kicheko kikafuata kabla ya Dereva kuwanza kuhoji muelekeo wa safari yao,
“Tunaenda mtaa wa Rufita.”
“Oooh kule kwa akina Mheshimiwa Rage”
“No, kule inakuwa mbele sana, mimi naishia mwanzomwanzo tu”
“Au pale karibu ya Berenja Hotel?”
“Enhee Kwa mbele kidogo sasa kuna Kona inayoingia mtaa wa Usagara”
“Nimekupata, hiyo kona inakuwa kulia wakati kushoto kuna nyumba moja kubwa ya zamani hua kuna bi mkubwa mmoja hivi hua anapika vitumbua pale”
“Duuh kaka inaonesha we mwenyeji sana na mitaa ile? Umemjua mpaka Bit Rajab Kanyoro muuza vitumbua mashuhuri wa tangu dahar” Dereva Teksi akacheka kidogo kufuatia swali la Suhail
“Si unajua tena kaka Kazi zetu zinatupasa kuyajua maeneo mengi zaidi ili kurahisisha utendaji kazi”
“Ok vizuri, basi ni maeneo hayohayo ukishakatiza hiyo kona basi kwa mbele kidogo tu Nyumba yetu inatazamana na nyumba moja hivi ina Ofisi kubwa ya mafundi wa mageti ya kuchomelea na ya ‘Aluminiam’..”
“Aaah kumbe hapo, nimekusoma mkuu, hapo kwenye hao mafundi ni kwao na jamaa mmoja hivi alwatan sana anaitwa Kijukuu cha Soud”
“Eee bwana eeh hapohapo, aisee nimekuvulia kofia, we ni hatari” wakacheka tena kwa pamoja kisha Safari ikaendelea
Ni mbali kiasi chake kutokea ulipo uwanja wa ndege mpaka mjini kati yalipo makazi ya watoto wa mjini, hivyo iliwagharimu kiasi cha dakika thelathini ama telathini na tano hivi mpaka upeo wa macho yao yalipoanza kushuhudia Soko, Shule nyingi, Bank, ofisi za mashirika makubwa, purukushani za waendesha baisekeli na waenda kwa miguu, ikawa ni ishara tosha kwao kwamba wameingia mjini Tabora. na kutokea mjini kwenda mtaa wa Rufita ni umbali kama wa dakika saba tu, sidhani kama ni haram ukisema kuwa Rufita ni mingoni mwa mitaa ya mjini.
“Shilingi ngapi kaka?,” Suhail aliuliza bei baada ya kuwa gari imeegesha nje ya nyumba yao
“Elfu Saba tu kaka” Suhail hakujibu akaingiza mkono mfukoni akatoa noti ya shilingi elfu kumi akampa dereva
“Chenji utanunua soda kaka”
“Oooh ahsante sana mtu wangu, Mungu akubariki,” Alijibu dereva na kumuacha Suhail akiteremka na begi lake mkononi kasha yeye akipiga msele na kuwacha vumbi hafifu wakati anaondoka
Mlango wa barabarani ulikuwa wazi lakini sebuleni hapakuwa na watu hivyo Suhail akaingia moja kwa moja na kwenda kupigia hodi angali sebuleni kabisa,
“Hodi wenyewe”
“Karibuu,” Mama Suhail aliitikia akiwa uani na wanawe na mumewe wakipata zao Chai na viazi vitamu vya kuchemsha almaarufu kama ‘Vinumbu’ au ‘Ndombolo ya Solo’ na asali kwa pembeni. Suhail akapitiliza mpaka uani, alipofika tu akakutanisha macho yake na wanafamilia, hakuna alieamini kumuona kijana Yule, wadogo zake watatu mmoja akiwa wa kike kwa shangwe na kelele za furaha, wakaacha sinia la viazi likishangaa tu wakamkimbilia kaka yao na kumrukia kama Simba achezavyo na wanawe, Mama mtu nae uzalendo ukashinda nae akatoka mbio huku akijifunga khanga yake vizuri na kwenda kumlaki kijana wake alieondoka kitambo.
Mzee Kusekwa nae akawa amesimama tu huku akiwa hana hata kumbukumbu ya alipozipotezea hasira zake alizolala nazo usiku kucha, akajikuta tu sasa nae ‘Akiganyala’ kama dume la nyani taratibu akaenda kupokea Begi la mwanae na kulipeleka ndani huku mkononi akiwa na gilasi ya maziwa mgando almaarufu kama Mtindi au ‘Mbobhoto’ kwa pale Tabora
“Haya jamani habari za masiku tele?” aliuliza Suhail baada ya kuketi katika kigoda huku akitembeza macho yake kwa kila mmoja pale uani kwao, alipozaliwa na kukulia
“Yaani hata siamini jamani, haya kwanza ni Basi gani ulilopanda la kukufikisha Tabora saa hizi?”
“Mama bana, nimekuja na Ndege” Jibu la Suhail likawafanya wazazi wake waangaliane kwa macho ya kuulizana
“We Suhail pesa ya kupanda Ndege umetoa wapi we mtoto ?” Safari hii swali lilitoka kwa Mzee Kusekwa
“Baba dunia imebadilika sasa hivi, hakuna cha ajabu tena, hata wewe utapanda tu tuombe uzima, hebi nipeni maji ya kunawa kwanza nipate chai mie” Haraka wadogo zake wakamsogezea maji akanawa na akaanza kujipatia ‘Vinumbu’ vyake taratibu
“Duh jamani Tabora yetu haibadiliki kabisa, nilitegemea kuwa nitakuta hali ime’change’ hata kidogo lakini wapi,” Suhail alivunja ukimya
“Yaani huu mkoa sijui ni nini hasa, nasikia eti wanasema kuna Sharifu sijui alioachiaga laana zamani sana” Majibu ya Mzee kusekwa yalisababisha kicheko kikanguruma pale uani kabla ya Suhail kujibu tena
“Aah baba hizo ni imani tu lakini kama watapatikana viongozi wenye dhamira safi hakika patabadilika tu”
“Sio viongozi tu, yatupasa wanachi sote tuwe na nia ndio mabadiliko yatakuja” Basi ikawa ni habari za hapa na pale mpaka zoezi la kupata chai likakamilika, ndipo wakahamia sasa Sebuleni kwa ajili ya mazungumzo, wakati huo wadogo zake Suhail wakiondoa vyombo walivyovitumia kupatia kifungua kinywa chao na kuviosha.
“Haya kwanza pole kwa mkasa wa ajali” Alianza kuongea Mama Suhail huku akimuangalia mwanae wa kwanza kwa furaha
“Aisee ahsante, ilikuwa ni balaa” Kimya kikatanda kidogo kabla ya Mzee Kusekwa nae kuongeza neno
“Enhee haya hebu tuambie ilikuwaje siku hiyo ya ajali maana leo tunaongea huku tunacheka pengine saa hizi tungekuwa tunaongea mengine kabisa” Suhail akaanza kuwahadithia jinsi safari ilivyokuwa mpaka walipopata ajali na ilivyokuwa mpaka akaokoa na kuwamua kurejea kwanza Dar, katika simulizi yake hiyo alificha mambo mengi sana ikiwemo kuhusu Mzee Shamhurish, pia aliunda habari ya uongo kuwa alipata lift ya kurjra Dar hivyo akaona ni bora atumie fursa hiyo ili kujiepusha na mshikemshike pindi wanausalama watakapo wasili eneo lile, Habari ilikuwa ni nzuri nay a kusikitisha ukizingatia ajali iliondoka na roho za watu, wakati simulizi ikiwa inafikia tamati Mzee Kusekwa akamuita mwanae wa kike ambaye ni Mdogo wake na Suhail akampa kazi ya kukamata Jogoo mmoja bandani kwake kwa ajili ya Takrima kwa mgeni,
“Haya ikawaje tena mwenzetu ukang’ang’ania Dar mpaka tunataka kutoleana radhi?” Suhail akatoa historia ndefu ya uongo “Unajua ile ajali iliniathiri sana kwa ndani lakini mwanzo sikujielewa, sasa nilipofika Dar baada ya kufanya vipimo ndipo nikajibaini kuwa sikuwa sawa sana ndipo nikaanza kupatiwa matibabu
“Pesa ya matibabu ulitoa wapi?,” alisaili Mzee Kusekwa
“Ndio nakuja huko baba, usiwe na haraka. Wakati nilipohitimu tu masomo nilibahatika kukutana na Mzee mmjoa hivi ana asili ya kiasia akawa anatafuta kijana mmoja muaminifu aliesoma fani ya biashara kwa ajili ya kumsimamia kazi zake kwakuwa yeye mara nyingi anakuwa nje ya Nchi, ndipo kuna mwalimu mmoja akanipendekeza mimi, nikawa nimefahamiana na Mzee Yule na tukaingia mkataba mzuri tu wa kazi na kwakuwa hakutaka kuwandika jina lake kwenye makampuni yake hivyo akaniambia kuwa makampuni yote anayofungua yatakuwa kwa jina langu hivyo watu wengi wanajua makampuni yale ni yangu na mpaka vijana walioajiriwa wananijua mimi kuwa mmiliki wa makampuni hayo hivyo wote wananiita Boss..”
“Alhamdulillah mwanangu na wewe sasa umekuwa Boss, Mungu ashukuriwe jamani, hata siamini.. Sasa na wadogo zako hawa wakimaliza tu Shule uwapachike huko..” Aliongea Bi Mkubwa yule kwa furaha sana lakini alikatishwa na mume wake aliyekuwa na hoja nyingi kichwani mwake
“Wee Mama Suhail acha kupenda sana hela we mwanamke zitakuja kukutokea puani, unamjua huyo mtu anaempa tu mwanao mali kiajabuajabu mpaka unashabikia tu? Badala uhoji umekalia tu ulimbukeni” Alibwata Mzee Kusekwa huku akimuangalia mkewe kwa wahka, akageuza macho yake mpaka kwa Suhail akataka kuhoji juu ya hizo nyumba inazosemekana nazo ni za kwake lakini akajua tu jibu litakuwa kama la kwenye umiliki wa kampuni kuwa ameziandikisha kwa jina lake lakini si za kwake akajua ameshafilisiwa hoja akatulia na kuwanza tena
“Suhail mwanangu nisikilize kwa makini sana.. umekuja Tabora leo umetukuta wazazi wako wote, Una Baba hapa na Mama pale lakini hofu yangu usije ukaondoka ukiwa na Mama tu badala ya wote wawili, kitu ambacho ni hatari sana katika maisha yako yote yaliyosalia..”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni