Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA THELATHINI NA TISA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Wakiwa bado wanashangaa kule nje, Yule Nesi naye akiwa ametapakaa damu waliishia kumwona tu akijitoma ndani ya gari nyingine iliyokuwa imeegesha pembeni na kutoweka kwa kasi ileile, Koplo Salum alimtupia macho yule nesi haraka
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
‘Ama!’ alikumbwa na mshangao wa haja, hakuamini alichokiona, alimtambua vilivyo nesi yule
Amefuata nini huku?
Anahusikaje na mchezo huu?
Maswali yalibarizi kichwani mwake, ghafla akakatizwa na kelele za matairi ya gari yaliyotaabishwa na dereva wa Inspekta Kenjah aliyekuwa amefunga breki karibu ya miguu yake!
Akashuka Inspekta Kenjah na kukutana na Saluti za kumwaga kutoka kwa askari waliotapakaa eneo lile
“Nipe Ripoti ‘corporal’..” Aliongea kwa wahka Insp
“Hali mbaya Mkuu..” aliongea Koplo Salum Mrando, halafu akaanza kutiririsha mkasa mzima ulivyokuwa
“Nilikutahadharisha mapema Koplo.., sasa mlijuwaje kuwa ameingia huko Wodini?”
“Kelele alizopiga huyo mtu mwenye meno ya dhahabu bila shaka kwa kibano alichopokea toka kwa yule Nesi ndizo zilizotufanya sisi tugundue kule ndani kuna mtafaruku, tulipoingia ndo tukapambana na hali ile ya hatari mpaka Afande Lau akapigwa risasi” alijibu mmoja wa wale askari waliokuwa wakilinda pale hospitali, majibu yake yalimshitua sana Inspekta, Si tu kwa kusikia kuwa askari wake amejeruhiwa kwa risasi ya Joram lakini pia kusikia eti Joram alipiga kelele ya maumivu kwa kupewa kichapo na nesi tu, tena Mrembo!
“Yaani Joram Ndege apigwe na nesi mpaka atoe yowe?”
“Joram?” alishtuka Yule Askari kusikia hilo jina ambalo amekuwa akilisikia tu kama hadithi, Insp hakujibu chochote zaidi ya kuongeza swali
“Huyo nesi naye alipitia wapi mpaka akaingia Wodini?”
“Hakuna aliyemwona Afande,” alijibu mmoja kati ya wale askari walionusurika huku akitetemeka kwa hofu
“Daktari.. mnamjua huyo nesi?” Alisaili tena Kenjah huku akimgeukia daktari aliyekuwa ubavuni mwake, lakini tofauti na matarajio yake swali lake likajibiwa na Koplo Salum Marando
“Hawezi kumjua hata chembe..” Ukimya ukatawala kwa sekunde kadhaa, kundi zima likamgeulkia Koplo Salum, akaendelea “Yule ni Lillian Ufoo..”
“WHAAT..” Alimaka Inspekta “..Lilly?!, it can’t be.. Yule Sekre.. si alitek..” kila alilotaka kulisema lilishia njiani, alimjua Lillian kuwa ni msichana dhaifu tu aliyetekwa na watu wasiofahamika sasa iweje tena awe nesi ambaye ana ujasiri wa kupambana na jitu kama lile!
“Ndiye huyo afande” Alijibu Koplo Salum, na muda huohuo simu ya Inpekta ikaita, akaitoa na kupokea. Maelezo aliyopewa yalionesha ni muhimu sana kiasi cha kusahau kila kilichotukia pale hospitalini, akatoa amri
“Koplo Salum na watu wako tuondokeni haraka.”
*****
Katika Hoteli ya Shree Godha iliyopo Ilala Boma aliingia mtu mmoja aliyeonekana nadhifu kwa mavazi yake aghali yaliyomkaa vyema mauongoni, Kanzu nyeupe pee, Kofia ya mkono, makubazi, na saa ya rangi ya almasi huku mkononi akiwa ameshika Tasbihi na kijibegi kidogo
“Karibu Ustadh Hussein,” Aliongea kwa sura yenye bashasha mhudumu aliyekuwa mapokezi baada ya mtu huyo kuwasili mapokezi
“Shukrani habibi.. Nija’alie hali ya maungo yako?” Alijibu Sheikh Yule ambaye ni kweli jina lake ni Hussein, Ustadh Hussein Chaullah.. mwanzo alidhamiria kuficha jina lake lakini alipoona amejulikana ikabidi tu atulie, ni kama hakutegemea umaarufu wake kuwa katika kiwango kile..
Japo ni Kiongozi mkubwa wa dini huko Tabora lakini kupitia huduma za kitabibu na Elimu kubwa anayoitoa kupitia katika vipindi kadhaa vya luninga hasa siku ya ijumaa vimemfanya awe maarufu nchi nzima mpaka huku katika hoteli za vichochoroni
“Mimi sijambo Sheikh, kumbe upo Dar? Jana tu nilikuona kwenye Televisheni ukitoa darasa ukiwa Tabora..”
“Ooh! Ni kweli nimeingia leo na ndege.. Sasa mimi sina jambo kubwa sana ila nimekuja hapa kwa maelekezo tu kuna Bwana mmoja ni mpangaji wenu hapa anaitwa Joram ameniambia nifike hapa hotelini kuonana naye”
“Joram? Amekwambia namba ya chumba chake?”
“Hapana hakuwahi kufanya hivyo, ila yupo hapa hotelini kwa muda mrefu kidogo.. ni mteja wenu wa kudumu”
“Ooh itakua Yule mwenye meno ya dhahabu maana ndiye mteja wetu pekee aliyepanga hapa kwa takribani miezi miwili sasa”
“Naam, Masha’allah ndiye huyo yakhe! Ni kweli ana meno ya rangi ya dhabu.
Mhudumu akacheka kidogo na kuongea tena
“Kama ndiye huyo meno ya dhahabu yuko chumba namba thelathini na nne japo hapa hajaandika hilo jina la Joram...”
“Ameandika jina gani?” Alihoji Sheikh Chaullah huku hamaniko likichukua nafasi ya tabasamu lake lililotamalaki tangu awasili pale Hotelini, alijua sasa ameshayakoroga
“Yaani Sheikh wangu nawe bwana hata jina la mtu unayemtafuta hulijui! Sasa asingekuwa na hayo meno ya dhahabu ungempataje?..” aliongea kwa utani kidogo mhudumu yule na kuongezea “..Hapa ameandika A-bashir”
“Ooh umeona sasa Nd’o huyohuyo sheikh wangu maana ni kama miezi miwili iliyopita tu amebadili dini akachagua jina hilo sasa sikutaraji kuwa angelitumia mpaka kwenye masuala ya kawaida kama haya,” Ustadh akasema uongo japo sidhani kama alipata dhambi kutokana na uwongo ule uliokuwa na dhamira Fulani ndani ya nafsi yake
“Ooh kumbe amesilimu? Haya sawa Sheikh Nenda ukajaribu kumwangalia maana hua anaondoka na fungo yake… Pitia hapa moja kwa moja halafu utakata kona mkono wako wa kushoto, utaona vyumba.. chumba chake ni namba 34”
Baada ya ruhusa ile Sheikh Chaullah hakutaka kumpa tena nafasi mhudumu Yule ya kuzidi kumdodosa, akaanza kutembea kwa haraka kuelekea kule alikoelekezwa.
Haikuwa mbali sana, akawasili katika korido ndefu iliyopangika vizuri kwa mfuatano wa vyumba, akakiona chumba namba Thelathini na nne, akasogea na kuusukuma mlango, Ulifungwa!
Haraka akaangaza huku na kule, alipoona hakuna mtu akaingiza mkono kwenye mfuko wa kanzu yake akatoa Funguo ‘Malaya’ kama tano hivi, ya kwanza ikagoma, ya pili ikagoma pia, ya tatu ikatii kiu yake,
Mlango ukaachama, akajitosa ndani!
Hapakuwa na makolokolo yoyote ndani ya chumba kile kilichotandikwa va kupangwa vizuri zaidi ya Begi lilioachwa wazi sehemu kubwa ya zipu ya kati na kufanya nguo kuchungulia nje, Akaingiza mkono ndani ya Begi hilo na kulipekuwa, hakupata alichotaka! akafungua ndani ya kabati hapakuwa na kitu, akaenda chini ya uvungu wa kitanda akainama na kuchungulia hakukuta kitu, akainuka na kuangaza huko na kule kwa haraka kama Muha aliyeachwa na Treni ya kwenda Dar! ndipo wazo likamjia akainua Godoro nako hakuna kitu!
Akaliendea Kochi dogo la sofa na kulitikisa akasikia vitu vikigongana, akalipekenyua Waooh akakutana na vitu alivyovikusudia, ilikuwa ni Laptop na Flash, akavitoa! pia kulikuwapo na Bastola nayo akaichukuwa japo hakuwa na haja nayo. Akarejesha kila kitu kama kilivyokuwa! Akaikunja kanzu yake pamoja na Msuli aliouvaa kwa ndani, akaweka Flash na ile Bastola katika mifuko ya Kaptula yake ya Jinzi aliyoivaa kwa ndani kisha akajirejesha katika hali yake ya unadhifu.. Laptop akaiweka katika kile kijibegi chake alichoingia nacho. Haraka akatoka na kukifunga chumba na kuondoka zake
Alipokata tu kona ya kwanza akakutana uso kwa macho na Joram Ndege akiingia ndani, wakapishana bila ya salamu kila mmoja akiwa anajiamini vilivyo! Hisia za hatari zikafukuta kichwani mwa Joram akapeleka mkono wake kiunoni na kuipapasa silaha yake kisha akamgeukia Ustadh yule aliyepishana naye bahati mbaya ama nzuri hakumwona tena, alikwishakata kona na kutoka kwa kasi mpaka pale Kaunta ambapo alimkukuta Yule Mhudumu amezungukwa na wateja wengi hivyo ikawa ni ponepone kutokana na mtungo wa maswali,
Akatoka zake kimyakimya kwa mwendo wa ki-sheikh, mwendo wa kichamungu, tar’tib mwendo wa maringo!
Kitokeo cha hapo Ustadh akaenda mpaka mbele kidogo tu akaangaza huku na kule na kujiridhisha juu ya hali ya usalama kisha akaiendea teksi iliyokuwa imeegesha pembeni kama inayomsubiri yeye, akaingia ndani na hapohapo dereva akaondoa gari.. wakaenda mpaka mbele kidogo kasha wakasimama, haikuchukua dakika mbili akawasogelea kijana mchafu wa mwili na nguo, akiwa amevalia nguo zake chakavu na mgongoni akiwa amening’iniza mfuko wake mkubwa sandarusi uliosheni chupa za maji na juisi anazopita kuokota mjini
Kijana huyo anayeonekana kama aliyekolea na kutopea katika matumizi ya dawa za kulevya alipoifikia tu teksi ile mlango ukafunguliwa na kitendo bila kuchelewa ustadh Chaullah akatoa lile begi lake alilolitumia kuhifadhia ile Laptop aliyoichukuwa chumbani mwa Joram na kumkabidhi muuza makopo huyo! Mbali na Laptop pia ndani ya begi kulikuwa na ile Flash pamoja na Bastola alizoziweka humo baada ya kuingia ndani ya teksi ile. Kijana muokota makopo akalipokea begi lile na kulisweka ndani ya mfuko wake mchafu wa sandarusi na kuondoka zake
Hakuna aliyeelewa tukio lile la aina yake!
Ni kama vile ustadh alichanganyikiwa au amerogwa maana kukabidhi vitu hatari kama vile kwa mtu wa ajabu kama yule, vitu ambavyo yeye mwenyewe kuvipata kwake kulihatarisha maisha yake, Hasha!
Baada ya makabidhiano yale Ustadh na dereva wake wakarejea mpaka sehemu Fulani wakaegesha gari yao!
Nje ya Hoteli hiyo palikuwa na Msururu mkubwa wa Askari kanzu, wengine wakiwa ndani ya magari, wengine wakiwa miongoni mwa wale wateja waliopitwa na Sheikh Chaullah pale mapokezi, na wengine wakiwa katika mitindo yao tofauti ambayo isingekuwa rahisi kuwagundua! Lakini Joram Ndege alikwishagunduwa kuwa anafuatiliwa hivyo haraka alidhamiria kuvichukuwa vile vitu muhimu kwake ambavyo kwa muda ule vilikuwa vikimilikiwa na Ustadh Chaullah
Inspekta Kenjah alikuwa ni miongoni mwa Wana usalama wale waliotanda nje ya Hoteli ile ambapo aliwasili kufuatia taarifa aliyopokea kutoka kwa Sajenti Malumbo aliyekuwa nje ya hospitali na kumshuhudia Joram akitoweka, akamfuatilia mpaka alipoona kuwa uelekeo wake ni wa kurejea huku hotelini alikokuwa mwanzo!
Baada ya utulivu wa muda ndipo Insp akaamua kushuka ndani ya gari na kuelekea ndani ya hotel ile akifuatana na kijana wake mmoja mpaka mapokezi ambapo alikuta idadi ya watu kidogo ikiwa imetulia
“Habari yako kijana?” Inspekta alimsalimu mhudumu
“Salama bwana mkubwa, unahitaji vyumba?”
“Kwani kwa unene huu nilionao naweza kuhitaji vyumba vingapi kwa ajili ya kulala,” Alidhihaki Inspekta baada ya kuambiwa kama angehitaji vyumba
“Samahani sikuwa na nia mbaya, nina maana unahitaji chumba?”
“Kwani hapa mnauza na Simenti?..” Kenjah aliendelea kujibu kifedhuli tu kiasi cha kumfanya mhudumu aishiwe cha kusema “..Namuhitaji mteja wako aitwaye Joram Ndege, yupo chumba namba ngapi?”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi