Vita vya Mapenzi (40)

0

SEHEMU YA AROBAINI
TULIPOISHIA...
“Samahani sikuwa na nia mbaya, nina maana unahitaji chumba?”

“Kwani hapa mnauza na Simenti?..” Kenjah aliendelea kujibu kifedhuli tu kiasi cha kumfanya mhudumu aishiwe cha kusema “..Namuhitaji mteja wako aitwaye Joram Ndege, yupo chumba namba ngapi?”

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
“Nani? Joram? We nani? Mbona mnanichanganya kila anayeingia humu anamtaka Joram mtu.. mwenyewe wala hatumii jina hilo, hebu mpigie simu mwenyewe,” Alijibu kwa hasira mhudumu Yule aliyeudhiwa na majibu ya Kenjah, na hicho ndicho alichokikusudia Inspekta Kenjah, Kumuudhi kijana Yule ili aropoke chochote chenye manufaa, hakutaka kufanya haraka kumfuta ndani Joram maana hukujua ni chumba gani yupo japo amemwona akiingia mle hotelini, akabaki akijiliza sasa

Kila anayekuja anamtaka Joram?

Nani mwingine amekuja kumtaka Joram?

Anatumia jina gani linguine?

“Hatuna muda wa kupoteza,” Aliongea Inspekta huku akimwangalia mmoja kati ya askari alioongozana nao mle ndani, akampa ishara na Yule askari akaielewa. Akatoa Bastola akaiweka juu ya meza ya kaunta, kisha kitambulisho chake cha kazi na kumwonesha mhudumu

“Sisi ni maofisa wa jeshi la Polisi, tunahitaji kujua Joram ana muda gani tangu apange humu na huwa anawalipa kwa njia gani? Pia tunahitaji kujua anatumia jina gani awapo hapa hotelini na ni nani mwingine aliyekuja kumuulizia, halafu mwisho utuambie umejuaje kua huyo aliyeandikisha hilo jina pia ndiye Joram tunayemuhitaji sisi!” Alifoka Askari Yule na kumfanya mhudumu atetemeke kama anayetaka kuchinjwa.. akautapika ukweli wote ulivyo! kilichomsisimua Insp Kenjah ni pale aliposikia kuwa kuna Sheikh alikuja kumtafuta Joram, na kwamba Sheikh huyo alimsilimisha na kumbandika jina la Al-bashir

Joram asilimu?

Inspekta akatoa simu yake na kumpigia Sajent malumbo “Hallow,” alipokea Sajenti Malumbo

“Hakikisha mnaweka ulinzi wa kutosha nyuma yah ii hoteli, asiingie wala kuondoka mtu, sawa?”

“Sawa mkuu.. tayari nipo huku nyuma muda mrefu hakuna mtu yeyote zaidi ya Mzee mmoja tu aliyekuwa akipiga deki vibaraza vya hoteli hii.. naye kaishaondoka huku, nadhani ni mtumishi wa hapa”

“Good” Inspekta akakata simu na kuwaamuru vijana wake wamfuate kule walipoelekezwa kilipo chumba cha Joram

*****

Yule mzee aliyekuwa akideki kule nyuma aliondoka na beseni lake alilokuwa akilitumia kufanyia usafi, alipofika mbeleakajimwagia maji kidogo sehemu ya kichwa chake kilichosheheni mvi kisha akavuka barabara na kwenda upande wa pili badala ya kuingia huko hotelini mwao. Ni kama aliyekuwa akihofia kitu maana hata mwendo wake ulibadilika ukawa wa kasi na kuondea ile ladha ya utu uzima wake, kama haitoshi akakaza mwendo na kuamua kukimbia tu huku akigeuka nyuma kama kuna mtu anayemwona!

Kwa pembele kidogo ikatokea teksi kama inayotaka kuvuka barabara, ilikuwa ni teksi pekee iliyojipendekeza kwa mzee huyu na kumfanya ajisikie mwenye bahati kama aliyeokota machungwa kwenye shamba la mafenesi, ama bahati ya mtende kustawi jangwani.

“Ondoa gari haraka kwa mwendo wa kasi,” Aliongea mzee Yule baada ua kuingia ndani ya gari

“Mzee pesa iko?”

“Uliza jingine.”

Dereva akafanya kama alivyoambiwa, japo mwendo ulikuwa wa kasi na hapakuwa na dalili zozote za kufuatwa lakini Mzee hakutulia, kila mara alikuwa akigeuka nyuma kuhakiki usalama wake. Hawakufika mbali sana wakapokelewa na foleni ndefu ya magari katika barabara hii ya uhuru!

*****

Insp Kenjah na askari wake hawakuwa na haja ya kuvunja mlango wa Joram maana ulikuwa wazi! Wakaingia wote kwa tahadhari na kuanza kukipekua.. Hapakuwa na mtu zaidi ya begi tupu!

Kaenda wapi?

Si ameingia huku nikimwona mwenyewe?

jambo moja tu likamtia jakamoyo Inspekta, Sehemu ya juu ya chumba hicho kwenye dali ilikuwa wazi! Akakumbuka lile tukio la kule hospitalini baada ya Joram kupita juu kwa juu na kutokezea wodini.. Ghafla akasikia ukulele wa haja ukitokea vyumba vya mbele, ilikuwa ni sauti kali ya kike ikionesha kila dalili ya hamaniko. Haraka Inspekta na vijana wake pamoja na Yule muhudumu aliyekuwa nyuma muda wote wakatoka chumbani kwa Joram na kuifuata kelele ile. Walipotoka wakakutana na Msichana ambaye ni muhudumu wa usafi vyumbani akiendelea kupiga kelele huku macho yake yakiwa yamekodolea ndani ya chumba kimoja kilichokuwa wazi..

Walipoingia walikutana na mwili wa mwanamke aliyekuwa ni mpangaji wa chumba hicho ukiwa hauna uhai, baada ya kuusogelea wakabaini kuwa amenyongwa kwa kutumia taulo, Salam walizoachiwa ilikuwa ni viatu na zile suti walizomuona Joram ndege akiwa amezivaa! Alipopepesa tena macho akakuta dirisha limevunjwa.. Hmadi! Hisia za hatari zikachemka kichwani mwa Inspekta Kenjah, akajiridhisha kuwa Joram alipita juu kwa juu kwenye dari mpaka ndani ya chumba hiki na baada ya mauaji akatoweka.

Sasa kama amevua nguo zake, Je ametoka kama alivozaliwa? Haiwezekani!

Machale yakamcheza, akakumbuka kuwa aliambiwa kuwa kuna mzee alikuwa akifanya usafi huko nyuma, akaona lililo bora na kumkamata huyo mzee ili aseme kama kuna mtu alimwona akitokea dirashani!

“Ni mzee gani alikuwa akifanya usafi huko nje ya hoteli?” Insp alimuuliza Yule Mhudumu wa kaunta

“Mzee?”

“Jibu swali kijana.”

“Hakuna mzee katika hoteli yetu, wahudumu wote ni vijana.. na wanaohusika na usafi ni wasichana tu.”

Jibu likawa hadhir kabisa kuwa Yule mzee ni mtata! Haraka Insp na watu wake wakatoka nje ya hotel na kwenda kujumuika na afande Malumbo ambaye baada maswali kadhaa ilionekana kuwa mzee Yule aweza kuwa Joram! Haikuwachukua muda kuamini hivyo baada ya muuza vitumbua mmoja kuwaeleza kuwa amemwona huyo mzee akiingia ndani ya teksi na kuondoka kwa kasi akielekea mjini..

Hawakupoteza muda nao wakaingia kwenye magari yao na kuanza kufukuzia!

*****

Mzee akamuamuru tena dereva wake akate kona ya kulia waingie mtaa wa Kilwa ambao utawachukuwa mpka kariakoo.. Dereva bila ajizi akatii amri, wakauvamia mtaa wa Kilwa na kuzidi kutokomea. Wakiwa wanaendelea na safari ndipo ghafla kikaibuka kizaazaa cha mwaka.. Ni wakati Yule mzee alipogeuka nyuma ili kuhakiki zaidi kuwa hakuna anayewafuata, Macho yake yakafumaniana na mtu aliyekuwa ameketi siti ya nyuma katika teksi hiyohiyo aliyopanda yeye. Yawezekana ni mteja au shanta lakini mbona mara zote alizokuwa akigeuka tangu wanaondoka hakumwona? Haiwezekani!

Au ameingia ghafla huku gari ikiwa katika kasi yake?

Haiwezekani!

Au alikuwa amelala kwenye siti? Inawezekana!

Kabla hajajuani lipi jibu sahihi la kioja hicho, ndipo ubongo wake ulimkubusha kuwa mtu huyo ameshapata kumwona mara kadhaa!

Wapi vile? Kwenye Luninga.. na mara ya mwisho ni siku hiyohiyo muda mfupi tu aliopita, katika korido ya hoteli ya Shree Goza, tena akiwa amevalia mavazi hayohayo!

Ni Ustadh Hussein Chaullah!

Ama!

Ustadh hakuwa na shaka kuwa sasa anatazamana na Joram Ndege, Mwuaji wa kokodiwa licha ya Nywele na ndevu bandia alizojipachika ili aonekane Mzee! Ustadh aliamini tu kuwa atakapokurupushwa na maaskari atatafuta gari ya kumkimbiza popote atakapo hivyo akaegesha kwa ajili ya kumpa huduma hiyo muhimu sana!

Wakati Joram akiwa anatafuta kujua ni kipi kinaendelea mpaka Ustadh yule akaenda kule Hotelini na hatimaye sasa ameibukia ndani ya gari aliyoikodisha ndipo alipotolewa mawazo yake rasmi. Ngumi iliyojaa sugu ngumu zitokanazo na mazoezi makali ayafanyayo Ustadh Chaullah ilituwa katika kimpuma cha Joram Ndege na kumsababishia si tu maumivu makali bali pia alipata ugeni wa nyotanyota zilizoambatana na giza usoni mwake, Akaangukia karibu ya kioo cha mbele! Hapohapo Ustadh akamvagaa tena na kuporomoshea ngumi nyingi, mfululizo kwa mikono yake yoteyote.. ingekuwa ni uwanjani tungemfananisha na Lionel Messi!

Joram hakuwa mtu legelege kihivyo, mafunzo yake magumu ambayo ni sawa na ukatili aliyoyapata kwa maharamia waliokubuhu hayakumwacha mnyonge kiasi hicho! Alijibinua kidogo tu katika siti aliyokuwa ameketi, akawa kama aliyekalia mgongo, akaufyatua mguu wake kama risasi ukarudi kwa nyuma na kwenda kumtandika Ustadh Chaullah aliyekuwa anataka kumuinamia ili amshushie kipondo kingine, Teke hilo lilitosha kabisa si tu kumgaragaza Ustadh katika siti ya nyuma bali pia kumtoa ‘Mchuzi’ mdomoni baada ya kuchanika!

Hapohapo Joram akamtaza dereva aliyekuwa hawezi kujihami kutokana na mwendo kasi, alipojiridhisha hilo akamwachia pigo takatifu la ngumi iliyotuwa sawa bin sawia ubavuni.. Dereva akayumba na kuuachia usukani kwa maumivu, gari ikahama njia na kwenda kulivaa Jiwe la msingi la chama fulani cha siasa.. Ikawa ni ajali baridi, gari ikiumia kiasi, huku abiria wote kwa wakati huo wakiumilia maumivu ya dozi walizopeana wenyewe

Haraka Joram akashuka akashuka ndani ya gari huku akimwangalia dereva kwa hadhari, alipofika nje akalakiwa tena ngumi nzito kutoka kwa Ustadh ambaye alikwisha shuka haraka kabla yake! Wapita njia wachache waliohudhuria eneo lile walishuhudia sinema ya Bure kati ya Joram aliyekuwa katika mwonekano wake wa kizee na ustadh Chaullah akiwa ameikunja kanzu yake usawa wa kiuononi.. Mzee na Ustadh!

Zilipigwa ngumi mujarab! Ngumi za kifundi, hakuna mjinga kati yao katika fani ya ngumi.. Ustadh alimjua vyema Joram hivyo alikuwa na hadhari kubwa katika mpambano ule, lakini Joram alijidanganya kuwa anapambana na Sheikh Fulani tu aliyejawa na hasira ya kukosa ubwabwa wa harusini, na hilo ndo likawa kosa kubwa! Ustadh alikuwa akizungusha mateke yake kama feni za pangaboi, mateke yalimzuzua akili Joram akawa kama aliyechanganyikiwa, mra kadhaa naye Ustadh alipokea ngumi za haja kutoka kwa Joram

Wakiwa wanaendelea kuwindana kuwindana kama majogoo yaliyobaki taaban baada ya kupigana muda mrefu bila ya kutokea mwamuzi ndipo Joram alipofikia ukipigwa na kitu kizito kichwani na kumpotezea mwelekeo, alikuwa ni Yule Dereva amempiga na ubao mrefu alioupitia chini baada ya kuteremka kutoka ndani ya gari, kabla Joram hajajiweka sawa Ustadh akamnyakia usawa wa mabega na kichwa mithili ya Nyani aliyerushiwa ndizi, na hapo ndipo Ustadh alipofanya hitima kwa kuachia pigo la judo usawa wa kisogo na kumwangusha Joram mpaka chini akiwa hana fahamu

Wapambe waliojitokeza walijikuta wakishangilia tukio lile kama wako sinema vile bila hata ya kudadisi kuwa chanzo cha ugomvi ule ni nini! Haraka Ustadh akatowa Pingu na kumfunga Joram, na kama haitoshi akatoa dubwasha Fulani hivi na kumwekea mdomoni. Muda wote huo Joram alikuwa ulimwengu mwingine kabisa, ulimwengu wa kutofahamu lolote linalotukia.. Naam, sasa angefahamu nini wakati hizo fahamu zenyewe kazipoteza hapohapo!

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)