Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA AROBAINI NA MOJA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Haraka Ustadh akatowa Pingu na kumfunga Joram, na kama haitoshi akatoa dubwasha Fulani hivi na kumwekea mdomoni. Muda wote huo Joram alikuwa ulimwengu mwingine kabisa, ulimwengu wa kutofahamu lolote linalotukia.. Naam, sasa angefahamu nini wakati hizo fahamu zenyewe kazipoteza hapohapo!
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Ustadh akatoa simu na kubofya namba Fulani, Simu ya Insp Kenjah upande wapili akiwa karibu ya mataa ya Karume ikaita
“Hallow,” Alipokea ile simu Insp japo alijawa na hofu kubwa, si tu kwakuwa ni namba mpya iliyompigia, bali amepigiwa katika namba ile maalum aliyopewa na IGP
Nani mwingine mwenye namba hii?
“Inspektah Kenjah, hakuna haja ya kutwawilisha muda njoo haraka hapa mtaa wa Kilwa jirani na msikiti wa Waburushi..”
“Kuna nini huko na wewe ni nani?” alifoka Inspekta
“Huna haja ya kunijua, nimekusaidia kukukamatia mjanja wako… Joram Ndege”
“Whaat?!.. Eti Jora..” alimaka Insp lakini simu ilikwishakatwa, alipojaribu kuipigia tena simu ile iliita mara moja tu,ikakatwa na kuzimwa kabisa. Hakika Insp alihamanika, akawaarifa vijana wake kuwa wasogeze magari pembeni na kutafuta uelekeo wa eneo aliloarifiwa afike.. Moyoni alizidi kuzongwa na hofu akiamini kuwa huyo aliyempigia huenda akawa ni mtu muhimu mpaka akaipata namba ile ya siri, ama wanaweza kuwa ni wale wahalifu wameinyaka na kutaka kumlengesha huko kwenye Domo la mauti! Akatamani ampigia IGP amuulize kama alimpa mtu mwingine namba ile lakini akajionea aibu, akawaamuru askari wake kwa mara nyingine na kuelekea Eneo la tukio
Alipofika eneo husika alilakiwa na kundi la watu likiwa limeuzunguka mwili wa uliolala chini ukiwa hauna fahamu, Mwili wa Inspekta ulizizima baada ya kumwona Joram akiwa ameadhibiwa vilivyo, alipojaribu kuongea na mashuhuda waliobahatika kuuona mchezo ule, wakasimulia ‘Ei to Zedi’
“Huyo aliyempiga yuko wapi?” alisaili Inspekta
“Aliingia kwenye gari yeye na dereva wake wakatoweka!”
*****
Ustadh Hussein na Dereva wake wakiwa ndani ya teksi yao iliyoharibika kidogo sehemu ya mbele kwa ile ajali baridi walikuwa njiani wakianza safari nyingine, Safari ya Bagamoyo kwa mwalimu wake na Ustadh Chaullah. Mwalimu aliyediriki kumpa sehemu kubwa ya elimu yake ambayo inamsaidia kuitumikia jamii yake ki dini na kiusalama!
Si mwingine ni mwalimu Atrash Bin Jamadu
*****
Ilala, Dar Es Salaam.
Kama kawaida ya Jiji la Dar es Salaam, wekundu wa jua la asubuhi unapochomoza tu pilikapilika huanza, hakuna kupumzika, kila mmoja anaukimbiza ‘mwenge’ kuusaka mkate wake wa kila siku. Mitaa mingi huchangamka, kelele za muziki, pilikapilika za vyombo vya usafiri, mpishano wa waungwana na washenzi humfanya hata yule mwenye mawazo na changamoto lukuki za kimaisha naye kufurahi kidogo kiasi cha kuyasahau matatizo yake, Lakini si kwa familia hii ya Suhail Kusekwa ambaye u-taaban wake umewanyong’onyeza wote, hakuna mwenye Furaha, raha, wala amani.
Ni kweli maradhi ni jambo la kawaida tu na laweza kumkumba yeyote, lakini sasa lau kuwe na japo Bima ya matumaini! Suhail anaumwa yu hoi taabani, Ugonjwa haujulikani, hauonekani, hautambuliki. Vipimo vyote vimehusishwa lakini wapi! Hali inazidi kuwa mbaya tu. Kama ungepita karibu na nyumba hii ya kifahari pengine ungehisi wenyewe wamehama kwa jinsi ukimya ulivyotanda! La hasha! palikuwa na watu wengi tu ila kila mmoja kajiinamia kivyake..
Mzee Kusekwa na Fungameza waliketi zao barazani kila mmoja kwenye kochi lake, hakuna aliyemsemesha mwenziye kwa muda mrefu tangu walipomaliza kupata Stiftahi waliyoandaliwa! Mzee Kusekwa alijifanya kumakinika na gazeti alilokuwa amelishika mkononi kama vile anayesoma jambo muhimu, masikini ya Mungu hakujua kwamba hata hilo gazeti lenyewe aliligeuza chini juu juu chini! Mzee Fungameza yeye alijifanya kuangalia Tv lakini lau kama ungelipita mbele ya Tv hiyo wala asingekuona maana ki mwili ni kama yupo pale ila ki fikra alisafiri maili nyingi sana
Kama tu wanaume wazima wameshakata tamaa ya kuuguza kwa haraka kiasi hicho Je hao akina mama huko? Wao ndio kabisa, hakuna hata aliyepata kifungua kinywa kati yao zaidi ya kutoka kwenda msalani kwa zamu na kurejea vyumbani mwao.. Walikuja Dar kumuuguza Sharifa mara wakakutana na kisanga cha Suhail kuwekwa rumande, hawajakaa sawa nao wakawekwa ndani, walipotolewa wanakutana na Sharifa eti amepona ghafla kwa miale ya Pete kutoka kwa mtu asiyemjua, na mara sasa Suhail nd’o amegeuka kuwa mgonjwa, hakika walijichokea wazee wa watu!
Nyumba ikiwa katika hali hiyo ya utulivu ndipo ikasikika kengere maalum ikigongwa kule getini, bila shaka pana mgeni, hakuna aliyejishughulisha nayo kwakuwa Dada wa kazi yuko huko uwani akiendelea na kazi hivyo angemfungulia
“Baba.. kuna Mgeni wenu hapa,” Aliongea msaidizi Yule wa kazi baada ya kuwasili pale barazani
“Mkaribishe ndani,” alijibu mzee Kusekwa, kisha msaidizi Yule akatoka nje na kumruhusu mgeni aingie. Macho ya Mzee Kusekwa na Fungameza kwa pamoja yakajikuta yakitazamana na bwana huyu aliyeingia, Mzee Kusekwa alipatwa na mshangao baada ya kumwona mtu Yule akiingia, hakuwa na madhara yoyote bali hakumtegemea uwepo wake hasa katika mji huu wa ugenini kwao, wanafahamiana, na wote ni wakazi wa mjini Tabora. Alikuwa ni Ustadh Hussein Chaullah!
“Sheikh Chaullah! Ni wewe?”
“Ni mimi Mzee wangu.. Assalamu alaykum,” Alisalimia Ustadh huku akimpa mkono Mzee Kusekwa aliyekua amesimama kumpokea
“Waaleyka Salaam, hata sijui nikuulize za Tabora ama za Dar.. haya karibu kwanza uketi.” Hakujibu kitu Ustadh, akamsogelea Mzee Fungameza naye akamsabahi na kurejea kwenye kochi moja lilokuwa likitazamana na Luninga iliyokuwa ikionesha mpira,
“Haya habarini za hapa?”
“Salama tu karibu sana”
“Ahsante sana.. mimi nimekuja Dar majuzi ila pana mambo yakawa yamenishughulisha, na hata nilipoyamaliza nikaenda Bagamoyo jana na kulala hukohuko mpaka asubuhi hii nd’o nikaianza safari ya kurejea tena Dar”
“Ooh, Pole sana kwa mihangaiko Sheikh.. Sisi tuna muda kiasi hapa mjini, Maradhi nd’o yametuleta huku! Mdogo wako hali yake mahamum”
“Nilisikia khabari hizi lakini sikuzitilia ma’anani sana nikidhani ni maradhi ya kawaida tu.. ila huko Bagamoyo nilipokwenda ndiko kuna bwana mmoja anafahamiana na Suhail akanipasha kiufasaha.. Poleni sana ila tu mkumbuke Maradhi ni mtihani mkubwa nd’o maana Mungu akatuasa kuwa tukakujaribuni kwa njaa, maradhi na vifo.. hatuna budi kulishinda jaribu hili kwa matokeo yoyote ambayo Mola atatukadiria..”
“Ni kweli kabisa,” alijibu Mzee Kusekwa kisha ukimya ukachukua nafasi kabla ya Mzee Kusekwa kumtambulisha Ustadh kwa Mzee Fungameza
“Bwana Fungameza.. huyu ni Kiongozi wetu wa dini kutoka Tabora sijui kama umepata kumwona? Ni Imam na Ustadh wetu, pia huwa ni tabibu mzuri tu wa maradhi ya ajabuajabu kama haya ya Kijana.”
“Namfahamu ila zaidi kwa kumwona kwenye ma televisheni tu.. Ni Shehe Hussein Chaullah kama sijakosema”
“Naam, ndiye yeye wala hujakosea! Au kwakuwa umenisikia nikimtaja wakati akiingia?” alitania kidogo Mzee Kusekwa, wakacheka kidogo kiasi cha kuihuisha upya baraza iliyokuwa kama imekufa..
“Sasa tuongee mawilimawili, hapa umepajuaje? Au ulishawahi kufika?” alihoji Mzee Kusekwa
“Hapana sikuwahi kupajua hapa ila nilianzia kule ofisini kwake.. ndipo nikaelekezwa mpaka namba ya nyumba” Baada ya mazungumzo ya hapa na pale, Ustadh akaomba kuonana na Suhail, Mzee Kusekwa akamchukuwa mgeni mpaka katika mlango wa chumba alichomo Suhail kisha akagonga huku akiita
“Sharifa!.. Sharifa”
“Abee baba.”
“Haya kuna Mgeni anataka kumwona mgonjwa.”
“Sawa, aingie tu.” Ustadh akaingia mpaka chumbani na kumkuta Suhail akiwa amelala kitandani, Mashuka gubigubi! Sharifa aliketi pembeni yake. Kilikuwa ni chumba chenye hadhi ya kumlaki yoyote mwenye ukwasi wa kutosha, kila kilichomo mle ndani kilikuwa kizuri, imara, na chenye thamani kasoro afya ya Suhail tu ndio haikuwa imara japo kidogo.. Hakika alitingwa kijana wa watu, hakuwa hata na uwezo wa kuinuka kumpokea mgeni, alichoweza kufanya ni kujifunua shuka na kuinua jicho tu na kumtazama.. Baada ya salam, Sharifa akawapisha
“Pole sana.. Mungu ataku’afu tu.”
“Ahsante sana ustadhi, nashukuru umekuja kuniona, imenifariji sana!”
“Usijali sisi ni kama ndugu kabisa yatupasa kufarijiana.. ila tu mimi si mkaaji sana, nina machache yamenileta hapa kufuatia hali yako..” aliongea Ustadh kwa utulivu na sauti ya chini
“..haina ubishi kuwa hali yako si nzuri hata chembe, na inahitajika lifanyike jambo ili kujikomboa wewe na familia yako.. nina salamu zako kutoka Bagamoyo..”
Kusikia jina bagamoyo, moyo wa Suhail ukapiga sarakasi, hakuwa tena na hamu japo ya kulisikia jina la mji ule, Ustadh aliliona hamaniko hilo lakini halikumzuia kuendelea kuongea “..Salamu kutoka Kwa Mzee Atrashi, kwanza anakupa pole kwa kila kilichokukumba, kama asingelikuwa hali ya afya yake kuwa na mgogoro basi bila shaka angelikuja mwenyewe” Aliposikia jina la mzee yule akajikuta ameingiwa na nguvu, akahisi kama mkombozi amewasili, akajiinua kutoka pale kitandani na kuketi.
“..Mzee anasema alikukanya kuhusu Tamaa na Uongo.. mbona hujajirekebisha? Kwanini umeendelea kumdanganya mkeo Sharifa kwa kila jambo? Na kwanini mpaka leo licha ya matatizo kukufika shingoni bado hujawaeleza ukweli wazazi wako? Au unasubiri mpaka hawa maharamia wakuangamize ibaki siri sirini?..” Akaweka kituo kidogo Sheikh Chaullah ili kuyapa nafasi maneno yake yamwingie vizuri mkusudiwa, ila akakumbuka kitu akaamua kukisema kabla hajaendelea na
“Nikutoe hofu, usiogope kuongea na mimi kuhusu matatizo yako.. najua kila kitu kuhusu wewe, najua khabari za Mzee Shamhurish, khabari za Khatam Budha, Khabari za Sharifa na Shekhia na nyinginezo! Mimi nimehitimu elimu yangu kwa Mzee Atrash na ndiye kijana pekee aliyenipa sehemu kubwa ya taaluma zake kuliko kijana mwingine yeyote hivyo ananiamini! Tangu siku ulipowasili kwake alikujua kuwa ni kijana wa Tabora ndipo akanipa habari hizi.”
“Sheikh mimi sina usemi, hali yangu ni mbaya sana! Hapa ni siri yangu tu jinsi ninavyoumwa.. na sina hakika kama nitazidisha japo siku mbili nikiwa hai, nitakuwa nimeshakufa tu! Kilichoniponza bila shaka unakifahamu… mbaya zaidi Pete(Khatam Budha) niliyokuwa nikiitegemea imeshindwa kunitibu kamwe!” aliongea Suhail kwa sauti ya chini na ya kutaabika sana
“Khatam Budha haijashindwa kukutibu bali wewe haujaipa chakula chake kama ulivyoelekezwa na Mzee Shamhurish”
“Chakula chake? kipi hicho?”
“Aaah Suhail.. we haukukubaliana na Mzee wako kuwa utakuwa unainywesha damu pete yako kila mwezi?”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi