KIBWE NA SAFARI YA AJABU (6)

0
Mtunzi: Sango Kipozi

SEHEMU YA SITA
ILIPOISHIA...
Naam kwa mara nyingine, Kibwe alikutana na mmoja kati ya jamii ya majini wa bahari, jamaa zake ‘Makatta wa Makattani.’ Wakati hayo yakitokea, wenzake wengine waliokuwa wakija kuangalia chini ya merikebu, walifika na kumkosa yule jini wa bahari kwa sekunde tu!

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

ENDELEA...
“Kwani kuna nini?” waliuliza, na wakati huohuo, ile meli ikawa inasogea mbele!

“Ilikuwa ni mwani tu, ulioshikilia pangaboi! Nimekwisha uondoa , na ndio maana mnaona meli inaondoka. Twendeni tuwahi!” Kibwe alidanganya, akichelea kuwatia hofu watu na hadithi za majini wa bahari! Wote wakarejea melini, na kuendelea na safari.

Kibwe na wenzake waliendelea na safari yao huko mashariki ya katikati ya dunia, kwenye majabali yaliyouzingira mto mkubwa wa maji, mto Sakara, ambako Bhaduri binti Sultani kitinda mimba na mwana wa saba wa Sultani Bashar, alikuwa ameketi juu ya uwanda wa jabali moja, akisubiri kutolewa kafara!

Kwa moyo wa ushujaa, na utiifu kwa amri ya baba yake, mrembo Bhaduri binti Sultani aliketi juu ya jabali kwenye kiti kimoja kizuri cha enzi, akiwa amepambwa kwa sundusi za hariri, mikufu, hereni na vikuku vya dhahabu na vito vya thamani, huku akinukia utuli mchanganyiko kama udi, miski na ambari, akisubiri wakati wake wa kuchukuliwa na hicho kitakachokuja kumchukua!

Kibwe na msafara wake ndani ya merikebu yao ya fahari, waliyoyoma kuelekea huko mashariki ya katikati ya dunia, wakati huo zikiwa zimebaki siku chache tu, kuwasili mwisho wa safari yao. Usiku mmoja alipokuwa amelala na mwenzake Hanga kwenye chumba chao, Kibwe alimuota Bunga, akimpa maelekezo ya safari yao hiyo. “Lazima msafara huu usitishwe haraka iwezekanavyo, mara tu mtakapowasili kwenye bandari yoyote ya jirani,” alisema Bunga. Aliendelea kumwambia kuwa itabidi wasubiri kwenye bandari hiyo kwa siku mbili zaidi, kabla ya kuanza tena safari yao. “Katika muda huo mtakapo kuwa mkisubiri kwenye bandari hiyo, mtakuwa mmejinusuru na hatari ya kupambana na mwamba wa barafu majini, na pia mtanusurika na tufani kubwa itakayotokea mnamo saa ishirini na nne zijazo.” Kibwe alimsikiliza Bunga, aliyeonekana akielea hewani kama ndege, na maneno yake yakisikika kwa kukatika katika, kwa sentensi zisizokamilika!

Ndotoni Kibwe alikuwa akimcheka Bunga, na akimshangaa sana kwani kwa mara hii alimuona ni wa ajabu kabisa. Hakuamini maneno yake hata kidogo, “Usinitanie mzee Bunga! Unajua kwamba msafara huu lazima uwahi nchini Shamsi mashariki ya kati kati. Sasa mbona unataka kutuchelewesha?” Kibwe alianza kulumbana na kile kijitu cha ajabu.

“Tutaendelea tu……..na- safa-”Lakini kabla hajamalizia maneno yake, Kibwe akaona ukuta uliokuwa mbele yake ukipasuka, na maji mengi yakianza kumwagika kama mafuriko, na kumzoa Kibwe kutoka pale alipokuwa, akajikuta akitapatapa kujinusuru asizame! Ingawa alikuwa anajitahidi kuogelea, lakini alishindwa, na hivyo akaanza kuzama---! Akazama—akienda moja kwa moja hadi chini kabisa ya dimbwi la maji---! Pumzi zikamwishia kabisa! Halafu ghafla, akajiibua juu, na kutoa kichwa chake nje ya dimbwi la maji, na kisha palepale akasituka na kuamka, huku moyo wake ukienda kwa kasi mno! Aliinuka na kuketi kitako, akiwa anapumua haraka haraka mno!

Mwenzake Hanga aliyekuwa karibu yake, naye aliamka na kumuona Kibwe akiwa katika hali isiyo ya kawaida. “Vipi kibwe, mbona uko hivyo, umeota ndoto mbaya nini?” Kimya! Kibwe hakujibu kitu, bali alizidi kupumua kwa haraka haraka, huku macho yake yakiangalia mbele zaidi ya pale alipokuwa mwenzake, kama kwamba hakumuona wala kumsikia Hanga! Haraka Hanga alichukua gilasi ya maji na kumpa mwenzake huyo anywe, akihisi huenda akajisikia nafuu kidogo. ”Hebu kunywa maji kidoga, labda yatakusaidia.” Kibwe aliyapokea yale maji bila kumwangalia mwenzake, na akanywa funda mbili, na halafu akajilaza kitandani. “Unajisikiaje hivi sasa Kibwe? Ni ndoto gani uliyoota?” Hanga aliuliza, akiwa na wasiwasi na jinsi alivyomuona mwenzake. Kibwe alikohoa kidogo, na kisha akaanza kuongea.

“Nadhani huko mbele kuna tatizo kubwa sana. Nimeota kuwa kutakuwa na kimbunga kikubwa, na meli yetu itapambana na mwamba wa barafu majini,” Kibwe alimwambia mwenzake, ambaye alimshangaa, akimwambia kuwa alichokiona kilikuwa ndotoni tu, wala si lazima kitokee. Lakini Kibwe hakumsikiliza Hanga, bali aliendelea kusema. “Kama hatukusitisha safari yetu kwenye bandari yoyote ya karibu angalau kwa siku moja na nusu hadi hatari hiyo ipite, wote tutapoteza maisha yetu.” Hee! Hanga akaduwaa akimwangalia mwenzake huyo aliyechanganyikiwa, au tuseme vile alivyoamini Hanga kwa wakati ule. Iweje tena jambo la ndotoni, Kibwe akalichukulia kuwa ni jambo kubwa na halisia? Hanga alijaribu kuzungumza na mwenzake akimsihi ajaribu kutulia tu, na atasahau kuhusu ndoto yake. “Na hata hivyo, unadhani kuwa utaeleweka kwa manahodha utakapowaambia wasitishe safari kwa kuwa uliota kuwa mbele kuna hatari? Jaribu kufikiri vizuri Kibwe.” Kibwe alishikilia palepale, akimwambia Hanga kuwa lazima manahodha wamwelewe, ama sivyo, wote wamo hatarini!

Kwa hiyo, Hanga na Kibwe walikwenda hadi kwenye chumba cha manahodha, na kuwaelezea kuhusu hatari iliyoko mbele. “Lazima tusitishe huu msafara, mara tu tutakapofika bandari ndogo ya karibu, kabla ya kuelekea nchini Shamsi, ama sivyo, wote tutateketea.” Kibwe aliwasihi wale manahodha, bila kuwa na uthibitisho wa kutosha wa hoja yake hiyo. Manahodha wakamuona kuwa anafanya utoto tu, hivyo kwa kebehi, wakamwambia; “Hivi unadhani kuwa katika maisha yetu kwenye kazi hii, tungekuwa tunaamini kila tulichokiota, tungeweza kufanya safari kama hizi? Kijana, kumbuka kuwa ndoto ni ndoto tu. Hatuwezi kuacha kusafiri, eti kwa kuwa mtu mmoja miongoni mwetu ameota kuwa mbele kuna hatari!” Pia manahodha wale walisema kuwa kulikuwa na umuhimu wa kuwahi kufika kule waendako, ili waweze kugeuza merikebu yao na kurudi makwao, baada ya kumsindikiza Kibwe.

“Lakini jamani, mmejiuliza kuwa huenda kuna ukweli kwenye maneno ya kijana huyu?” Baadhi ya wahudumu wa meli walihoji, wakinong’ona chinichini. “Kweli eti! Na labda tukiyadharau maneno yake hayo, tutakuja kujuta yatakapotokea hayo anayoyatabiri!” Wahudumu wa meli walisema hivyo, huku wenzao wengine wakihofu sana, walipokisia kuwa huenda kukawa na ukweli kwenye hoja ya yule kijana. ”Ndiyo kusema kuwa wote tutakuwa hatarini!” waliambiana. Hata hivyo wengine miongoni mwa wahudumu wale waliowaunga mkono manahodha na hoja zao, wakasema kuwa yule kijana aliota tu, na wala hakuletewa onyo rasmi la kimazingaombwe kutoka kokote. “Haya jamani na tuendelee na safari yetu, na tuachane na mawazo ya kishirikina!” walisema wahudumu hao, wakiwahimiza manahodha wasipoteze muda. Lakini lo! Laiti kama wangejua!

Haya, safari ikaendelea kama ilivyoamuliwa, na hakuna aliyejuwa kuhusu mkasa ambao ungetokea mnamo saa ishirini na nne zijazo! Kilometa kadhaa kutoka pale walipokuwa, kwenye mwamba mkubwa sana wa barafu majini, pande moja kubwa la barafu lilijigawa kutoka kwenye mwamba huo mkubwa wa barafu majini, uliokuwa kama mlima mkubwa sana! Sehemu hiyo ya mwamba iliyotanda baharini, ilikuwa ikielea na kusukasuka kuelekea kule ilikokua merikebu ya mfalme KashKash, walimokuwemo Kibwe na abiria wengine! Wakati huohuo, mawingu mazito na meusi yakawa yanajikusanya, na hivyo giza nene likaanza kutanda. Upepo nao ukaanza kuchanganya kasi ya mwendo wake, iliyoongezeka kwa kila dakika, na kuvuma kwa kuvuruga mawimbi ya bahari, yaliyonyanyuliwa juu kwa urefu mkubwa wa kustaajabisha, kwani kimbunga nacho kilikwishaanza! Lahaula! Huko kulikokuwa kukijiandaa katika hali hiyo, ndiko ilikokuwa ikielekea merikebu iliyowabeba kina Kibwe na wenzake! Merikebu ile ilisafiri kwa kilometa nyingi humo baharini, na wakati wote huo, Kibwe akiwa na wasiwasi mkubwa, kwani aliamini kabisa kuwa huko mbele sio kuzuri. “Nafahamu kuwa Bunga hawezi kutokea waziwazi ili kutuonya kuhusu hatari hiyo, maana watu wote watashangaa na pia kuhofu sana, mara watakapomuona,” Kibwe aliwaza. Lakini kwa bahati mbaya, ilibidi kijana yule asubiri hatari hiyo ifike, kwani hakuwa na la kufanya! “Haya. Liwalo naliwe!” alijiambia.

Mnamo majira ya saa kumi na mbili asubuhi, abiria ndani ya merikebu ile wakaona hali ya hewa ikibadilika. Upepo ukawa unavuma kwa kasi na kwa hasira, huku bahari ikianza kuchafuka. Maji ya mawimbi yaliyokuwa yakijitupia na kupiga pembezoni mwa merikebu, yaliingia sitahani kwa wingi mno! Chini kabisa ya sitaha humo melini, nako kuilijaa maji tele! Kufikia hatua hiyo, abiria wote wakaanza kuhamanika, wakitoka vyumbani mwao ili kujiunga na wenzao, kuona jinsi hali ile iliyojitokeza, ilivyoashiria kuhatarisha maisha yao. “Haya sasa, tuone kama hakuna atakaye amini maneno yangu,” Kibwe alimwambia mwenzake Hanga, aliyekuwa ametowa macho pima akimshangaa Kibwe kwa kuyajua yote yale mapema! Ah! Laiti kama watu wangemuamini na ndoto yake! Mawazo hayo yalikuwa yakipita kichwani mwa Hanga. “Naam! Utabiri wa Bunga umeanza kuwa kweli!” Kibwe aliwaza, huku akiangalia jinsi walivyokuwa wamezingirwa na maji mle merikebuni.

“Haraka kawaambie abiria waliokuwa chini ya staha waondoke na kuja juu zaidi! Na wa huku juu wawe waangalifu wasisogee pembezoni mwa meli!” Mmoja kati ya manahodha aliwaambia wenzake. “Lo! Kumbe yule kijana alisema kweli kabisa.” Manahodha wale waliambizana, huku wakikimbia kwenda kuwatahadharisha abiria kule walikokusanyika. Huko waliwakuta baadhi ya abiria wakiwa wamejeruhiwa kwa kukimbia kutoka vyumbani mwao, wakitafuta nusura sehemu ambazo maji hayakufika.Wengi wao walikuwa wakianguka na kutereza mara kwa mara, kwani ile merikebu ilikuwa ikisukasuka kwa kusukumwa na mawimbi. Kila ilipoegemea upande mmoja, merikebu hiyo iliwamwaga abiria kwa upande huo! “Kwa hakika maneno yako yalikuwa sahihi kibwe. Leo wote tuko hatarini!” Hanga alimwambia mwenzake , wakati walipokuwa wakijishikiza kwenye nguzo za ile meli, ili wasiteleze na kuangukia sehemu nyingine hatari zaidi. “Ndio hivyo tena. Lakini haina haja kulilia maji yaliyomwagika, kwani si rahisi kuyazoa,” alisema Kibwe. “Iliyobaki ni kuomba Mungu atuvushe salama kutokana na janga hili.”

Huko nchini Hazina mashariki ya dunia jirani kabisa na Azarbarjan, Sultan Hazari Basari, alikuwa akisharehakea sikukuu ya kuzaliwa mwanawe wa kiume, kutokana na nadhiri aliyoiweka miaka kumi na tano iliyopita, baada ya kuota ndoto iliyoashiria kuwa katika umri wa miaka kumi na nne, kijana wake atakumbwa na jini Makata na kupelekwa mashariki ya mbali kwenye hewa inayogeuza watu kuwa mawe!

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)