Mtunzi: Sango Kipozi
SEHEMU YA SABA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Huko nchini Hazina mashariki ya dunia jirani kabisa na Azarbarjan, Sultan Hazari Basari, alikuwa akisharehakea sikukuu ya kuzaliwa mwanawe wa kiume, kutokana na nadhiri aliyoiweka miaka kumi na tano iliyopita, baada ya kuota ndoto iliyoashiria kuwa katika umri wa miaka kumi na nne, kijana wake atakumbwa na jini Makata na kupelekwa mashariki ya mbali kwenye hewa inayogeuza watu kuwa mawe!
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
ENDELEA...
HANGA BIN HAZARI
Katika zama zile za kale, kule mashariki ya dunia nchini Hazina jirani kabisa na nchi ya Azarbajan kwa mfalme KashKash, alikuwepo Sultani mmoja mashuhuri sana, aliyeitwa Hazari bin Basari. Sultani huyo alitawala raia wake kwa amani, uaminifu na upendo mkubwa, na kwa sababu hiyo, raia wake walimpenda sana. Kwa bahati mbaya kwa miaka mingi sana Sultani yule na mkewe hawakujaaliwa kupata mwana ambaye angekuwa mrithi wa kiti cha utawala baada kuondoka Sultani Hazar. Jambo hilo liliwasonesha sana. Siku moja Sultani Hazari aliwaita wazee na washauri wake mashuhuri, akawaelezea masikitiko yake.
“Sijui nifanye nini ili nami niweze kupata mtoto atakayekuwa mrithi wangu pindi nitakapoitoka dunia hii.” Aliwaambia.
Naam wale washauri walipokutanisha vichwa vyao ili kutafuta ufumbuzi wa jambo lile, wote wakapata jibu moja.
“Ama kwa hakika tatizo la namna hiyo hupatiwa ufumbuzi kwa njia moja tu, nayo ni kumuomba Mwenyezi Mungu mwenye kila uwezo. Tunakushauri uandae karamu kubwa na uwaalike yatima, mafakiri na mawalii, ili wamuombe Mwenyezi Mungu akujaalie kupata ufumbuzi wa jambo lako.” Walimshauri.
Sultani Hazari aliupokea ushauri wao kwa dhati. Akaandaa karamu mkubwa na kutoa sadaka kwa wajane, yatima na mawalii, ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
Naam haukupita muda mrefu, mkewe akashika mimba na miezi tisa baadae akajifungua mwana wa kiume, waliyemwita Hanga.
Ndiye Hanga bin Hazari huyo!
Sultani na mkewe walifurahi mno, na wakamlea mtoto wao kwa uangalifu na mapenzi makubwa sana hadi alipofikia umri wa miaka kumi na nne. Walimpa mtoto wao elimu bora na mafunzo mbalimbali ya mambo ya kimaisha, wakitarajia kuwa iko siku angekuwa mtawala wa nchi yake ya Hazina.
Siku moja wakati akiwa usingizini, Sultani Hazari Basari aliota ndoto ya kutisha sana iliyohusiana na mwanawe kipenzi, Hanga. Katika ndoto yake alikuwa kwenye mji mmoja wa ajabu uliokuwa chini kabisa ya bahari, ambako huko alizingirwa na wingu nene la moshi mweusi kupita kiasi. Kila alipojitahadi kukodoa macho ili aone vizuri mbele yake, hakuweza kuona chochote. Wahka ulimzidi aliposikia sauti nzito ya kutisha ikiunguruma masikioni mwake, ikimwambia;“Ewe Hazari! Ewe Hazari! Fahamu kuwa furaha yako ya kupata mtoto haitaendelea! Haitaendelea! Haitaendeleaaaa…! Ha ha ha ha ha…..!” Kile kicheko kilichofuatia maneno yale mazito kilikuwa ni cha kuogofya na kukata matumbo!
Kile kicheko kilisita kidogo na mchekaji yule asiyeonekana akazidi kumshindilia maneno mengine ya kutisha na ya kukatisha tamaa zaidi.
“Kamwe huyo mwanao hatafikisha umri wa miaka kumi na tano, kwani kabla ya kufikia muda huo, atakumbwa na pepo mbaya na kupotelea kwenye msitu wa hatari...msitu wa kindumbwe!”
“Eeg Mungu wangu weee!” Mfal,me Hazari alilalama ndotoni, na wala ile sauti haikusitishwa na mlalamo wake, ikaendelea, “…katika msitu huo daima uovu haulali wala hausinzii, na milima ya huko ni maarufu kwa maangamizi ya moto na hewa ya huko haikuwa ila ni yenye wingi wa sumu kali….Ha ha ha-ha-ha-ha-aaaaaaaa! Huwezi kumnusuru mwanao asilani wewe…huwezii…huweziiiiiiii! HHha-ha-ha-ha-haaaaaaa!”
Ile cheko mbaya ilivuma kwa mudsa mrefu huku ikizidi kufifia taratibu mpaka ikawa kimya cha kutisha kuliko hata ile cheko yenyewe.
Sultani Hazari aligutuka kutoka usingizini na kwenye ndoto ile akiwa na wahka na hofu kubwa! Moyo ulikuwa ukimuenda kasi na jasho lilikuwa likimtiririka kama mtu aliyekuwa akikimbia! Mkewe alipoamka na kumuona katika hali ile, alipatwa na wasiwasi mkubwa.
“Umepatwa na nini mahabuba wangu? Mbona unanitisha?” Mke akadadisi kutaka kujua kilichomsibu Sultani usiku ule. Sultani alikaa kimya kwa muda, kisha akamwambia, “Kwa hakika ndoto niliyoota inanipa wasiwasi mkubwa.”
Na akamsimulia mkewe ndoto yake.
“Usiogope sana mume wangu. Asubuhi kutakapokucha tutawaita waalimu waje kumuombea dua mwanetu, kwani ndoto hiyo ni ya uovu wa majini tu, wapendao kutia wasiwasi katika nyoyo za wanadamu!”
Kwa hiyo siku iliyofuata Sultani Hazari aliandaa kisomo kikubwa cha maombi kwa Mwenyezi Mungu, kilichohudhuriwa karibu na raia wote wa nchi ya Hazina. Siku ile Sultani akaweka nadhiri ya pekee! “Mwanangu atakapofikia umri wa miaka kumi na tano bila kupatwa na madhara yoyote, nitajaza fedha kwenye visima saba, na mafuta ya kupikia kwenye visima vingine saba, iwe sadaka kwa raia wangu wote wa Hazina kwa ajili ya nusura ya mwanangu. Kila mmoja kwa wakati wake atajichukulia kile atakachojaaliwa iwe fedha au mafuta, kadiri ya uwezo wake!”
Kufuatia kisomo kile, Hanga alilelewa kwa uangalifu zaidi na mapenzi makubwa kupita kiasi hadi alipofikia umri wa miaka kumi na tano na nusu, wakati ambao tayari alikuwa amevuka ule umri wa miaka kumi na tano ambao Sultani aliota kuwa angekuwa hatarini. Kwa bahati Sultani Hazari Basari alikumbuka nadhiri yake, hivyo akachimba visima kumi na nne, saba kati yake akavijaza fedha na saba akavijaza mafuta ya kupikia. Akatumwa mjumbe apite mitaani kuwatangazia raia wote wafike kwa Sultani na kujipatia sadaka. Kama kawaida ya matangazo kutoka kwa wafalme, mjumbe yule akapiga la mgambo ambalo kila likilia lazima huwa kuna jambo.
“Naam ndugu zangu, Sultani wenu anawatangazia kuwa mwanawe Hanga bin Sultani kwa bahati nzuri amefikisha umri wa miaka kumi na tano bila kupatwa na madhara yoyote, kama ilivyodhaniwa awali! Ili kudhihirisha furaha yake, kesho Sultani atatimiza ahadi yake ya kutoa sadaka ya fedha na mafuta kwa raia wote wa nchi ya yake! Wote mnatakiwa kufika kwenye kasri lake bila kukosa!”
Naam baada ya ujumbe ule kuwafikia raia wote waliokusudiwa, watu kutoka sehemu mbalimbali za milki ya Sultani yule nchini Hazina walikwenda katika kasri lake, wakajizolea fedha na kujichotea mafuta kwa ajili ya lishe yao bora. Wake kwa waume wazee kwa vijana na watoto kwa wakubwa walifurahia zawadi zile, na kila mmoja alishukuru na kumuombea Hanga anusurike na hasadi na kumtakia maisha mema.
Lakini masikini bibi mmoja mzee aliyejulikana na jamaa zake kwa jina la ‘Ajuza’ aliyeishi nje kabisa ya mji mkuu katika nchi ya Hazina, alichelewa kuzipata habari zile nzuri, na akasikitika sana kwa wenzake waliobahatika.
“Mbona Sultani hakutangaza nchi nzima kama ilivyo kawaida yake?” Alidadisi kizee yule. Wenzake walioshuhudia mjumbe wa Sultani akipita mtaa kwa mtaa kutangaza habari njema kwa raia wa Hazina, walishangazwa na lawama za yule Ajuza.
“Kwani ulikuwa wapi hata ukakosa kumsikia mjumbe akitangaza mitaani?” Walimuuliza. Walimshauri aharakishe kwenda kwa Sultani akajaribu bahati yake.
“Bila shaka utapata japo kidogo, ama mafuta au fedha. Usikate tamaa ndugu yangu.” Aliambiwa na mzee mwenzake aliyeishi jirani naye. Bila ajizi, wakati uleule kibibi ‘Ajuza’ aliondoka na kuelekea kwa Sultani Hazari, ambaye masikini, hakuwa hata na fununu kwamba ujio wa yule ‘Ajuza’ katika jumba lake ungebadili kabisa mwelekeo wa maisha ya Hanga, na kwamba ungefuata mkondo wa njozi yake aliyoiota awali!
Kizee yule alipofika kwenye kasri la Sultani Hazari, bahati haikuwa yake. Visima vyote saba vya fedha havikuwa na kitu, isipokuwa kisima kimoja tu kati ya visima saba vya mafuta ndicho kilichokuwa na mafuta kidogo sana!
“Ah, masikini mimi! Sina la kufanya kwani kila kitu huenda kwa riziki ya mtu. Hii niliyoikuta ndiyo riziki yangu. Nitashuka humo kisimani nikadundulize mafuta yaliyomo.” Alisema na nafsi yake na huku taratibu akijaribu kushuka kisimani kwa ngazi maalum iliyojengewa pembezoni, na huku kichwani kwake akiwa amebeba mtungi. Alipofika chini kabisa alichukua muda mrefu sana kuujaza ule mtungi. Hatimae alipofanikiwa kuujaza, aliunyanyua na taratibu akajitwika kichwani na kuanza safari ya kutoka nje ya kisima, kwa kutumia ile ngazi aliyoshukia. Alitoka kwa mwendo wa pole mno, kwani kutokana na kazi aliyoifanya ya kuujaza mafuta mtungi wake, alihisi maumuvu makali mno kiunoni na mgongoni!
Gorofani, juu kabisa ya kasri la Sultani Hazari, Hanga bin Hazari alikuwa akimwangalia ‘Ajuza’ yule kwa muda mrefu, tangu aliposhuka kisimani, hadi alipokuwa akijaza mafuta mtungi wake na pia wakati alipokuwa akitoka akiwa amejitwika mtungi wake kichwani. Alitabasamu kuona jinsi bibi yule alivyokuwa akihangaika kufanya kazi ndogo kabisa! Kwa utundu wa kitoto, kijana yule aliyekuwa ameshikilia manati, akaulenga mtungi wa ‘Ajuza’ na kuachia kijiwe kilichofika moja kwa moja, tena kwa kasi kubwa kwenye mtungi wa yule bibi , na papo hapo kuupasua mapande mapande, na kumwacha ‘Ajuza’ akiwa amelowa mafuta chapachapa mwili mzima!
Hasira alizopata bibi yule hazielezeki. Aliinua kichwa chake juu kuangalia gorofa ya saba ya jumba la Sultani, kuona ni nani aliyemfanyia kitendo kile cha kiburi! Hasira zake zilizidi alipomuona Hanga bin Sultani akimwangalia kutoka juu, akimcheka!
“Ni mtoto wa nani wewe shetani rajimi usiyekua na adabu wala heshima kwa watu wazima? Hivi hujafunzwa na wazazi wako ukaambiwa kuwa heshima ni kitu cha bure? Kama unajiona kuwa wewe ni bora kuliko wenzako, kwa nini hujaenda Kaskazini mashariki kwenye ‘Paa la dunia’, ukatekeleze yale wanayoyafanya wenzako walio bora, wanaojitahidi kuinusuru sayari kutokana na majanga yanayoikabili?” Bibi kizee aliyaelekeza maneno yake kwa Hanga kwa hasira kubwa, akimwacha kijana yule akiwa kimya, akitafakari kile alichokuwa akikisikia.
“Wewe huwezi kuwa bora kuliko Mwana Mteule ambaye licha ya uwezo na vipaji alivyonavyo vya kupambana na maovu, hata siku moja hajawahi kuwavunjia heshima wazee kama sisi!” Ajuza yule alimalizia maneno yake kwa kusisitiza kuwa ni wakati Hanga atakapofika kule ambako uovu umechukua nafasi kubwa kuliko wema, ndipo atakapotambua kwamba asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu! Maneno haya ya hasira ya Ajuza yalifuatiwa na msonyo mrefu kupita kiasi, ulioufanya moyo wa Hanga uzizime!
Yule bibi aliondoka akiwa amechukia mno. Alikuwa akijifutafuta mafuta usoni kwake na mwilini, wakati Hanga akiwa ameduwaa na kumwangalia kwa tafakuri ya hali ya juu.
“Huyu ni nani? na anafahamu vipi mambo yote yale aliyoyasema?” Alijiuliza na kutafakari kuhusu huyo Mwana Mteule aliyetajwa, na hatari iliyokuwa ikiikabili sayari yao.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi