Mtunzi: ___
SEHEMU YA NNE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Neema akaangua kicheko. “U kiumbe wa ajabu sana Joram. Unaona sasa ulivyochangamka baada ya kuanza mazungumzo ya vifo na mauaji? Nadhani kifo chako kitakuwa cha kusikitisha sana”.
“Ni afadhali kuliko kufia juu ya kitanda Muhimbili, tena baada ya kuugua miezi kadha wa kadha”.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, macho ya Joram yakauacha uso wa Neema na kumtazama mtu ambaye alikuwa ameingia ghafla katika baa hiyo. Pamoja na kuingia kama watu wengine, akiwa katika mavazi ya kawaida, suti nyeusi, macho yake yalimvutia Joram. Macho yake yakaonyesha dalili ya wasiwasi na tahayari. Joram hakuona kama wasiwasi huo ulikuwa wa kuwahi pombe. Hilo alilidhihilisha kutokana na macho hayo yalivyotembea huku na huko ndani ya baa. Yalipokutana na macho ya Joram, yalizidi kupatwa na hofu kubwa. Kisha mtu huyo akageuka ba kutoka nje. Mara kilio kikali kikasikika kutoka nje. Ilikuwa sauti ya msichana, akilia kwa uchungu.
“Mwanamke malaya, anapokula pesa za watu wahuni hupelekwa gizani ambako hufanyiwa unyama”, lilikuwa jibu la Joram.
“Umejuaje kuwa ni mwanamke malaya Joram?”, Neema alihoji. Wakati huo watu walikuwa wakitoka ndani ya baa kwenda nje kutazama. “Anaweza kuwa mke wa mtu aliyekamatwa na kuletwa huku kwa ajili ya kutendewa unyama, twende tukaone”.
“Hatuna muda huo…”
“Twende Joram”. Wakati huo Neema alikuwa wima akimvuta Joram. “Twende tafadhali…” Ikamlazimu Joram kukubali. Umati wa watu ulikuwa ukielekea nyuma ya baa, sehemu ambayo ilikuwa na kivuli chenye giza kilichotokana na msitu wa maua yaliyoizunguka baa hiyo.
Japo ndipo sauti ya msichana huyo ilisikika akilia.
Alikuwa kalala chali, nusu uchi, vazi lake pekee ilikuwa kipande kidogo cha kanga ambacho kilifunika sehemu ya kati na kuruhusu sehemu kubwa isiyostahili kuonekana hovyo, itazamwe na watazamaji.
“Nakufa jamani, nakufa…” binti huyo aliendelea kulia huku akitupa miguu huku na kule.
Mtu mmoja alikuwa na tochi. Akamulika. Mwanga wake ulinisa kitu cha kutisha zaidi. Damu. Damu nzito ilikuwa imetapakaa kando na juu ya mwili wa msichana huyo. Mara kitu cha kutisha zaidi kikaonekana. Kisu! Kisu kirefu chenye damu. Kilikuwa kando ya mwili wa msichana huyo.
“Kisu jamani”, mtu mmoja alilalamika.
“Nakufa… nisaidieni…” msichana huyu aliendelea kulalamika.
Kiasi Joram akaanza kuvutiwa. Hata hivyo Joram hakuvutiwa na kisu wala damu tu. Alikuwa akiutazama uso wa msichana huyo. Aliyaona macho yake. Alikuwa msichana mzuri sana isipokuwa macho yake tu. Yalikuwa macho yale yale aliyoyategemea kitambo. Macho ya msichana mlevi na malaya ambaye amekula vya watu na sasa vinamtokea puani. Hivyo aliushika mkono wa Neema na kumwambia. “Inatosha twende zetu”.
“Joram! Tumwache msichana huyu katika hali hii kweli?” Neema alilalamika.
“Ni kazi ya polisi. Haonyeshi kama atakufa”.
“Nakufa”, binti huyo aliendelea kulia. “Upo hapo Joram? Tafadhali nisaidie. Inama usnishike japo mkono. Naogopa wataniua. Tafadhali Joram”.
Kutajwa kwa jina la Joram kilisababisha watu waliokuwa hapo wamsahau msichana huyo mahututi, wakagauka kumtazama Joram, kijana mzuri wa sura, mrefu, nadhifu kwa mwili na mavazi, alionekana mpole tofauti na ilivyofikiriwa. “Kumbe huyu ndiye Joram Kiango!”, walinongona watazamaji. Mara kadha wamesoma habari zake magazetini na kutegemewa kuwa labda lilikuwa pandikizi la mwanaume linaloweza kuwatisha majambazi. Kumbe.
“Nisaidie Joram…” msichana akaendelea kulalamika.
Joram ni mtu anayechukia kutazamwatazamwa na kushangiliwa, basi aliondoka polepole huku akifuatwa na Neema. Alipofika ndani akakiendea kibanda cha simu na kuzungusha 999. Sauti ilipomjibu alisema. “Hapa ni Forest of Flowers Bar… ndiyo Kinondoni. Njooni kuna mtu wenu anavuja damu…”
Polisi waliotummwa kuja kumchukuwa ‘majeruhi’ huyo walikuwa vijana wawili wenye imani moja dhidi ya wanawake malaya; kwamba malaya ni mwizi wa mchana. Hivyo, inapotokea akapigwa hata kuuawa ni haki yake kabisa.
Wakiwa na imani hiyo, polisi hao walimzoa Waridi bila huruma wala kujali malalamiko yake. Kama kuna jambo liliwasikitisha ni kule kuona kuwa kipigo alichopata hakikumsitahili kabisa. Majeraha machache yaliyokuwa usoni mwake na damu kidogo iliyokuwa ikivuja polisi hawa hawakuona kama ni adhabu iliyomtosha malaya kama huyu. Kama kuna jambo liliwashangaza polisi hawa, ni kuona kuwa kisu hicho kikali kilicholala kando yake hakikutimiza wajibu. Yawezekana washambuliaji wake walikuwa waoga, au hawakudhamilia lingine zaidi ya kumtisha tu.
Gari lilipoanza kuondoka, polisi hawakuchelewa kumtupia maswali kadha wa kadha, maswali ambayo hawakujali kusikiliza majibu yake. Na kwanini wapoteze muda kusikiliza uongo ulioandaliwa kitambo? Mmoja wa vijana hawa akajikuta kavutiwa na uzuri wa Waridi. Kwa kisingizio cha kumfuta damu, akanyoosha mkono wake na kumgusa titi lililokuwa wazi likiwatazama kama linawadhihaki. Mkono ukanogewa na kutelemshwa hadi kwenye paja lake jekundu lililonona. Mkono huo ukaanza ziara nyingine ya kupanda juu. Ulipoelekea kuvuka mipaka, Waridi akashindwa kustahamii zaidi. Akainua mkono wake na kuunasa mkono wa askari huyo na kuutoa juu ya paja lake. Baada ya kitendo hicho, Ndipo alipotanabahi kuwa kamgusa askari huyo kwa mkono ulioandaliwa maalumu
kwa ajili ya mtu mmoja tu, Joram Kiango. Waridi alijua kitakachomtokea askari huyo. Mara akaangua kilio kwa sauti kubwa. Kilio ambacho kiliwashagaza askari hao.
Walifanikiwa kumfikisha katika hospitali ya Mwananyamala ambapo alipokelewa na wauguzi wa zamu. Askari hao wakaaga na kuahidi kurudi hospitalini hapo kesho yake ili kuanza upelelezi wao.
Waridi aliwaomba wauguzi kumpeleka moja kwa moja bafuni. Huko alitupa dawa zote alizohifadhi mkononi, akanawa vizuri kwa dawa kama alivyoelekezwa na Proper. Ndipo aliporudi kwa wauguzi ambao hawakuonyesha nia ya kumhudumia kutokana na hali yake alikuwa hajambo. Walimuonyesha kitanda cha kulala katikati ya wagonjwa wawili, mmoja aliyelala fofofo kama maiti, wa pili alionekana akitapatapa kama mtu aliyekaribia kukata roho.
Waridi alilala kitandani hapo kwa dakika tano tu. Alikuwa akiwaza kwa makini. Hakuona anachofanya hapo hospitali. Wala hakuona sababu ya kuendelea kusubiri hadi atokee yule mtu ambaye aliamini angemwua na kushindwa kutimiza jukumu alilotumwa kulifanya. Wazo hilo likamfanya Waridi aamue kutoroka mara moja hospitalini hapo mara moja. Bila kufikiri mara ya pili aliinuka na kutoka kama anaelekea msalaani huku akipitia kanga moja ya yle mgonjwa aliyelala fofofo, akayafunika mavazi ya hospitali aliyovishwa na wauguzi ili ajisitiri. Alipotoka nje, akajitanda kanga hiyo na kufuata njia ya kutokea. Alijiingiza kwenye kundi la watu wengine waliokuwa wakitoka hospitalini hapo. Hakuna aliyemshuku kwa lolote. Dhamira yake ilikuwa kwenda Mburahati, akachukue chochote alichonacho, na senti kadhaa alizoficha chini ya godoro, kisha atoweke Dar na kwenda kokote mbali iwezekanavyo ambako mkono wa Prosper… usingemfikia kwa urahisi.
Lakini hakwenda zaidi ya hatua nne nje ya geti kabla ya kuisikia sauti ya mtu ikimwita kutoka nyuma. Akageuka kwa mshituko na kukutana ana kwa ana na Proper, ambaye alimjia akimchekea huku akisema kwa sauti ya dhihaka.
“Msichana mzuri… Umefanya vizuri… Nilitaka nije nikutoe mimi mwenyewe lakini kumbe umewahi kutoka. Pole kwa yote yaliyokukuta, ok usijali twende zetu, gari ile pale…”
Kesho yake ilikuwa asubuhi yenye mawingu kiasu cha kuvunja nguvu ya jua kali ambalo lilikuwa likitishia kutawala. Mmoja kati ya wale askari waliomchukua Waridi pale baa alikuwa tayari kawasili kazini kwake. Mkuu wake wa kazi alihitaji ripoti kamili ya “Kushambuliwa kwa yule msichana malaya” Akamtaka pia kujitahidi waliotenda tukio hilo watafutwe na kupatikaba haraka iwezekanavyo kwani mchezo wao wa kubaka wasichana si mzuri kimaadili hususan mchezo wa hatari.
Askari huyo akalazimika kumsubiri mwenzake kwa muda mrefu, hakutokea. Ikamshangaza. Kwa kuwa makazi yake hayakuwa mbali na kituo cha polisi cha Magomeni, askari huyo aliamua kumfuata nyumbani, Alimkuta! Lakini alimkuta katika hali ambayo haikuwa ya kawaida, Kwani haikuwa jambo la kawaida mtu aanze kuvaa suruali kabla haijafunika matako, aache kazi hiyo ba kuanza kuinamia sakafu hadi kichwa kigonge chini mfano wa mtu anayeswali. Na zaidi ya hayo mgeni aingie baada ya kupiga hodi mara kadhaa bila kuitikiwa, lakini akukute ukiendelea kuinama kimya kimya. Dakika mbili, tatu hadi tano.
“Bobi”, askari huyo alimwita mwenzake kwa mshangao, akijiuliza huu ni mzaha wa aina gani, na umeanza lini! “Bobi”, aliita tena askari huyo huku akimtazama tena kwa makini zaidi askari huyo. Ndipo alipoanza kuona povu lenye damu damu likimdondoka mwenzake mdomoni na puani. Akaruka nyuma, kisha akakusanya nguvu na kumsogelea ili amchunguze vizuri zaidi. Akayaona macho yake yalivyoduaa, akauona ulimi ulivyotoka na kutembea nje ya meno, akaona… Hofu ikamkumbuka ghafla. alikuwa akitazama maiti ya askari mwenzake. Hima akarudi kituo cha polisi kutoa taarifa.
Marehemu alipelekwa hosptali ambako daktari hakuchelewa kutoa taarifa kuhusu ugonjwa uliosababisha kifo hicho. “Ugonjwa wa moyo”, daktari alidai. Kwamba alikutwa na ugonjwa huo ghafla wakati akivaa nguo zake, ikabainishwa kuwa kifo cha askari huyo kilitokana na shinikizo la damu.
Hakuna aliyeshuku kuwa asakri huyo amekufa kwa sumu ile, ya aina yake, ambayo aliigusa kutoka kwa Waridi, na kuifikisha sehemu iliyokusudiwa kufika, mwilini mwake, bila askari huyo kujua.
Sumu hiyo iliandawaliwa kwa ajili ya Joram Kiango peke yake
Wakati huo huo Joram Kiango alikuwa akipokea simu iliyopigwa ofisini mwake.
“Sauti yako i tamu mno masikioni sister, yaelekea nawe u kiumbe mzuri sana. Siwezi kuukataa kamwe mwaliko wa mtu mwenye sauti nzuri kama hiyo, Baada ya saa moja nadhani nitafika… Haya… Ahsante… Umesema wapi vile… Heh… Light Lodge?… Hapo siyo?. Nitafika baada ya saa moja…”, akaweka simu chini na kuukunja uso wake akimtazama Neema Iddy, katibu wake ambaye pia alikuwa akumtazama.
“Nani?”, Neema alihoji kwa shauku.
“Anajiita waridi”.
“Waridi? Anataka nini?” Joram alipochelewa kujibu. Neema aliongeza. “Sikujua Joram kama nawe u mroho wa wanawake kiasi hicho. Sauti tu unaridhika na kuahidi kumfuata? Angalia Joram. Utaingia katika mtego. Una maadui wengi katika nchi hii”.
“Nalijua hilo”, Joram alisema. “Siendi kwa sababu ya sura wala sauti yake kama nilivyosema. Kilichonivutia ni maelezo yake. Anasema yeye ni yule msichana ambaye alipigwa pale baa ya Forest of Flowers.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)