Mtunzi: ___
SEHEMU YA TATU
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Swali hili lilimshangaza sana Waridi. Muda wote walioishi pamoja hawakuwahi kuulizana maswali ya aina hiyo.
‘Kwanini?” Bomba akaendelea. “Nataka urudi kwenu. Mimi naona maisha hayaniendei vizuri”, Bomba akaeleza.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
Baada ya kunyamaza kwa sekunde kadhaa, akasema.
“Waridi, ni hadithi ndefu ninayo. Hadithi ambayo haifai kulifikia sikio lisilohusika. Ninachoomba ni wewe kwenda zako kesho. Kama hutaki kwenda nyumbani kwenu, rudi kwenye baa niliyokukuta. Naamini ukirudi pale baa haitapita dakika tano kabla hujaokotwa na mwanaume mwingine”.
“Kuokotwa?” Maua alijiuliza kwa hasira. Ghafla alijikuta kamchukulia Bomba kama mtu shetani. Hata sura yake sasa aliiona mbaya kama dhambi. Machozi yalimtoka na kuteleza juu ya mashavu yake. Akainuka na kutoka nje kimya.
Waridi alirudi ndani baada ya kumsikia Bomba akioga bafuni. Akafanya haraka kuuendelea ule mfuko ambao aliufunua. Macho yake yalikutana na furushi kubwa la noti ambalo hakuwahi kuliona katika maisha yake. Kwa kukadilia zilikuwa pesa nyingi. Kando ya pesa hizo, ililala bastola kubwa na tiketi moja ya ndege. Tiketi hiyo ilionyesha jina la Bomba kuelekea Nairobi.
Wazo likamjia Waridi. Bomba alikusudia kumtupa baada ya kupata pesa nyingi kama hizo ili aende zake Nairobi akatumie peke yake! Waridi akajishauri kuchota pesa kidogo afiche. Akasita. Alizihitaji zote. Akaamua kuzipata. Akazirudisha kama zilivyokuwa akatoka zake nje.
Usiku huo, Waridi alikuwa wa kwanza kulala. Alijitia kulia pole pole kwa namna iliyokusudiwa kumfanya Bomba aamini kuwa Waridi alimpenda kwa dhati. Ukweli ni kwamba katika maisha yake Waridi hakuwahi kumpenda mwanaume. Alipeda pesa. Mwanaume alimhitaji kwa ajili ya faraja ya mwili tu.
Bomba alikuwa amelala kando yake, alipoanza kukoroma, Waridi aliamka taratibu, akanyata hadi uani ambako alilibeba kwa taabu jiwe kubwa alilokuwa ameliandaa mchana. Akaingia nalo hadi chumbani ambako Bomba alikuwa akiendelea kukoroma. Akakilenga barabara kichwa chake na kuliachia jiwe lile.
Bamba alikurupuka kutoka usingizini na kupaa juu, alipotua kitandani. Alitoa mlio wa maumivu kwa sauti ndogo nyembamba ambayo ilimwingia Waridi rohoni na kumtia ganzi. Kichwa cha Bomba kilikuwa kimefumuka. Ubongo uliochanganyika na damu ulikuwa ukivuja kitandani na kuchafua mashuka. Lakini bado aliendelea kutapatapa huku na kule, akisema hili na lile, maneno ambayo Waridi hakuweza kuyaelewa. Ni macho yake ambayo yaliweza kumtisha Waridi zaidi… Macho ya Bomba yalikuwa yakimtazama kwa namna ya huruma na kutoamini alichokifanya.
Waridi hakuweza kustahamili. Akapiga kelele kwa hofu akakimbia nje ya chumba hiki ambako aliketi chini akitetemeka. Baada ya muda, alirudi ndani ambako alimkuta Bomba tayari amekuwa marehemu; domo wazi, ulimi ukiwa umesahaulikwa nje, upande mmoja ilikuwa kama picha ya kusikitisha inayotisha mno. Waridi akaona shida kuistahamili. Akajikaza kiume kwa kumfungafunga marehemu Bomba kwa blanketi kubwa kisha akajaribu kumuinua ili amtoe nje. Hakufaulu. Akamvuta hadi uwanni. Huko akajitahidi na kuifikisha mati chooni ambako kulikuwa na tundu kubwa lililofunikwa na bati. Akalifunua bati hilo, na kumtumbukiza marehemu Bomba. Kisha akalifunika kama lilivyokuwa awali.
Wazo lake sasa lilikuwa moja tu; kuzihesabu pesa zake kikamilifu, Lakini mwujiza ulikuwa ukimsubiri. Mfuko wa pesa ulikuwa umetoweka. Haukuwepo tena juu ya kabati, ambapo aliuona kwa mara ya mwisho kabla ya kuutoa mzoga wa aliyekuwa mpenzi wake Bomba ndani. “Uko wapi?”, Waridi alijiuliza huku akiutafuta mfuko huo kila kona ya nyumba bila mafanikio. Akabaki ameduwaa.
Mapambazuko yalimkuta bado kaduwaa katikati ya chumba, macho yakilitazama kabati kwa mshangao kana kwamba limeumeza mfuko huo wenye pesa. Waridi hakujua afuate lipi aache lipi.
Mara akajikuta akitoka nje ya nyumba hiyo. Alitembea kwa mkiguu hajui aendako. Baada ya kutwa nzima ya mzunguko usio na dhamira maalumu, Alielekea Mburahati ambako hakukawia kupata rafiki aliyemkarimu kwa kumsaidia kupata chumba cha muda. Baadae, Waridi alipata chumba chake. Siku zote moyo wake uliteswa na huzuni akikukmbuka kumwaga damu ya mtu asiyekuwa na hatia, hofu kwa kudhani kuwa wakati wowote polisi wangeweza kutokea kwa ajili ya kumchukua, na zaidi, maumivu makali moyoi kwa kuhisi ile sauti ya Bomba alipolia kwa uchungu na picha ya macho yake yalivyokuwa yakisihi.
Waridi hakuwa na la kufanya. Maisha yalimwendea vyema katika mazingira yake mapya, wateja wakimiminika kwa wingi hadi leo alipotokea mtu huyu wa ajabu ajabu ambaye anafahamu kila kitu kuhusu mkasa juu ya kifo cha Bomba.
“Siwezi… Siwezi kuua tena…?”Waridi alisema huku akibubujikwa na machozi.
“Huna ujanja, lazima utaua”.
“Utaua?”, Prosper alifoka kwa nguvu akiachia kofi kali ambalo lilimwingia Waridi kama aliyepigwa na kipande cha ubao. Akiwa msichana asiyezoea kupokea vipigo kutoka kwa wanaume, kofi hili lilimshangaza zaidi zaidi ya jinsi lilivyomwumiza. Lakini mshangao wake ulikoma pindi Prosper alipoongeza vipigo vingine vikali zaidi ambavyo vilimfanya Waridi ajikute akighalaghala chini damu zikimvuja hovyo kutoka usoni, puani na mdomoni.
Prosper akaangua kicheko, “Well”, akasema, nilikuwa sikupigi ila tu ilikuwa kukuandaa katika hali ambayo itakufanya umpate Joram Kiango kwa urahisi. Yeye ni mtu anayevutiwa sana na mambo ya damu. Hivyo atakapokuona atajileta mwenyewe kwako. Utakachofanya wewe ni kuhakikisha umempata dawa ambayo nitakupatia, Baada ya muda mfupi atakuwa marehemu. Itaonekana kafa kwa magonjwa ya kawaida tu. Hakuna atakayefikiria kama wewe na mimi tunahusika na kifo chake”,
Prosper alinyamaza kidogo akimwangalia waridi kuona kama maelezo yake yalikuwa yakimwingia, alipoona maneno yake yameanza kumwingia Waridi. Akaendelea. “Unaona iivyo kazi rahisi. Ni kazi ndogo tu. Inatofati sana na ile kubwa uliyofanya wakati ukimuua marehemu Bomba”.
Moyoni Prosper aliwaza; Waridi angejisikiaje kufahamu kuwa yeye Prosper muda wote ule alikuwa nje akisubiri fursa ya kumuua Bomba! Kwani, Bomba ambaye alikuwa mmoja wa magaidi wake, alikuwa ameshindwa kutimiza kazi fulani aliyopewa. Badala yake alipanga kutoroka na pesa ambazo alipewa kwa ajili ya shughuli maalumu. Ndipo ilipodi Bomba auawe usiku ule. Ni Prosper pia aliyepeya hadi ndani na kuzichukua pesa zile baada ya kuona kazi aliyokusudia kuifanya ilikuwa imefanywa na Waridi.
Prosper aliitazama tena saa yake. “Bado dakika tano Waridi”, Prosper alimwita Waridi, “Simama haraka ujiandae”.
Kiasi fulani Waridi alikuwa hoi, hivyo alishindwa hata kusimama, lakini Prosper akamsaidia na kumwongoza nje ambako walipanda gari. Humo garini, Prosper alitoa amri nyingine ambayo Waridi hakuitegemea.
“Vua nguo zako zote”.
Waridi aliduwaa na akasaidiwa kuzivua. Prosper hakusita kuzitatua.
“Nataka ufanye kazi nzuri tafadhali. Shika hii… Kamata na hii… Ni kazi ndogo sana… Kesho Joram Kiango atakuwa marehemu”?.
Baa hii ilikuwa imejaa watu wa kila aina; waliokuwa wakinywa na kustarehe kwa namna mbalimbali. Miongoni mwa watu hawa, alikuwemo Joram Kiango.
Yeye alitulia pale kaunta, juu ya stuli ndefu, pombe ikiwa wazi mbele yake, sigara ikiteketea mdomoni mwake. Kama ni furaha, yake ilikuwa tofauti na walevi ama wanywaji wengine. Hakusinzia hovyo wala kucheka pasipo sababu. Ukimya wake ulimfanya hata msichana wake Neema, ambaye alikuwa kando akinywa soda, amgeukie na kusema polepole.
“Tatizo lako ndio hilo, Joram. Uwapo huru unashindwa kuutumia uhuru wako. Tazama usivyo na raha. Mtu yeyote anayekufahamu akitokea hapa atadhani uko kizimbani ukisubiri hukumu ya kifo, badala ya kustarehe. Kwa nini?”.
Joram aligeuka kumtazama huku akimtengenezea tabasamu jepesi. Kama kawaida, macho yake yaliona kile ambacho yamezoea kuona katika umbo la msichana huyo. Umbo lenye urefu wa kadri, unene wa kadri na sura ambayo ilioana vizuri na umbo hilo. Sura ambayo ilisisimua moyo wa kila mwanaume aliyepata kumtupia macho Neema. Kadhalika, mavazi ya Neema yalikuwa ya kupendeza na yaliliafiki umbo lake. Lilikuwa gauni la kitambaa chepesi ambacho ni dhahiri kilitokea nje ya Afrika Mashariki. Si hayo tu yaliyomfanya Joram ampende Neema na kumthamini binti huyo. Macho ya mwanadada huyu yalikuwa na uzuri wa pekee, uzuri wa kubembelezabembeleza, uzuri wa kishujaa. Yalikuwa na nuru. Si nuru wa “mapenzi” bali nuru ya ujasiri.
Ujasiri huo ndio aliouhusudu Joram. Na ni kwa ajili ya kuuthamini ndipo mara kwa mara akawa akimshinda nguvu shetani wake ambaye alikuwa akitamani kumtia mweleka kwa kumnong’oneza akisema: “Sikia Joram Neema ni binti mzuri sana… na anakupenda sana… Kwa nini usisahau walao kwa siku moja awe mwenzi wako kikazi akastarehe naye kitandani?… Hujui… Utakuwa usiku mzuri kuliko usiku wowote mwingine…” Hayo Joram aliyapuuza na kuendelea kumwona Neema kama mpenzi wake wa dhati.
Mawazo hayo yalimjia tena Joram. Wakati huo, badala ya kumjibu Neema swali lake, alitabasamu tena, kisha akavuta sigara kwa utulivu. Tayari kusahau yote.
“Tazama!” Neema alilalamika. “Bado hata unashindwa hata kunijibu! Wamekuloga nini kaka yangu? Kwa kweli sijaiona siku yoyote ambayo uko kwenye starehe isipokuwa hapo tu unapokuwa vitani ukipambana na mikasa ya kutatanisha huku maisha yako yakiwa hatarini. Sijasahau niliposoma katika gazeti la Kiongozi jinsi ulivyokuwa ukicheka mbele ya bastola ya kumwuaji yule hatari katika tukio lililoitwa Lazima Ufe… kule Arusha”.
Tabasamu la Joram likageuka kicheko, “Mimi nilidhani kwamba wewe unanielewa vizuri zaidi mpenzi”, alisema. “Tatizo langu ni watu kutokunielewa. Hapa nilipo, kimya kama nilivyo, nina furaha na nimestarehe kabisa. Lakini watu watadhani sina raha. Niwapo mbele ya bastola huwa sicheki bali nimechukia sana. Tabasamu langu huwa ni moja ya silaha zangu kwa ajili ya kumlegeza adui. Kwa kweli silaha hiyo naipenda zaidi ya bastola. Kwani humfanya adui ashindwe kuitumia bastola yake.
“Huwa huna hofu?”.
“Sijui hofu ni kitu cha aina gani kwa kweli. Labda itabidi nimpate daktari mzuri anipime na kuona kama ninazo chembechembe za kitu hicho kinachoitwa hofu katika moyo wangu. Nadhani hili kwangu ni lazima…”
Neema akaangua kicheko. “U kiumbe wa ajabu sana Joram. Unaona sasa ulivyochangamka baada ya kuanza mazungumzo ya vifo na mauaji? Nadhani kifo chako kitakuwa cha kusikitisha sana”.
“Ni afadhali kuliko kufia juu ya kitanda Muhimbili, tena baada ya kuugua miezi kadha wa kadha”.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)