BARUA KUTOKA JELA (27)

Zephiline F Ezekiel
0
Mtunzi: Ibrahim Gama

SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
ILIPOISHIA...
“Naam nakumbuka sana, kwani natambuwa kama umeshakamatwa, kwani nilikuwa nafatilia kwa karibu sana. Ndiyo maana uliponiambia nije nikufae, upo muhimbili,kisha ukanitaka nije na chakula kwa ajili ya wale askari, nikatambuwa natakiwa nifanye nini!

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
Nilipita duka la dawa pale muhimbili, nikanunua zile ‘Njunja’(LAGACTIL) nikimwambia muuzaji, ndugu yangu anasumbuwa mwenye ugonjwa wa akili akiwa hospitali, na manesi wa pale muhimbili, wamenielekeza nije kununua dawa zao za usingizi hapa! Naomba nisaidie dada yangu. Basi Yule muuzaji wa duka la dawa Muhimu. Alinipa dozi kabisa, nami nikampa elfu ishirini, nikimwambia chenji aendelee nayo! Nikaenda pale karibu na Geti lakuingilia, upande wa kushoto, nikanunua maziwa paketi mbili, nikanunua na chipsi mayai, na kuku, nikasaga zile dawa za wehu za usingizi, nikazinyunyizia katika kile chakula, nikamtafuta Yule askari katika namba yake, akanielekeza ndiyo nikaja kukufaa! Nilidhani wangenambia nionje kile chakula, basi ningeonja kisha ningekunywa yale maziwa pakiti moja kuondosha ile sumu ya zile dawa, nabado balaa lingekuwa upande wao!”

Mwakyembe alihitimisha taarifa yake, kwa JM huku akiwa na wingi wa furaha. “Asante sana ndugu yangu kwa kunifaa, kwani nilikuwa sina mtu mwengine zaidi yako, ambae ni shababi na anaeweza kucheza mchezo ulioufanya leo! Sasa kuanzia sasa, jeshi la polisi litakuwa linakutafuta wewe pamoja na mimi, hivyo umakini unahitajika sana! Nakupongeza kwa kuchukua simu za wale askari, kwani wangebaki nazo, ile simu uliyoipigia namba yako ingebaki, na wangekusumbua, ila kwa kuwa umeichukuwa, umefanya jambo la maana sana!”

JM alimwambia Mwakyembe huku akimtizama kama alikuwa na neno la ziada, alipomuona hakuwa na neno, aliendelea. “Itabidi mie niondoke sasa hivi nielekee nyumbani kwangu Vingunguti, kwani kule ndiyo kuna hazina, na nikiwa kule hujihisi nipo pahala salama zaidi.” Jm alisema maneno yale na kutulia huku akijinyoosha viungo vyake!

*******

“Nipe taarifa tafadhali, amebadilisha eneo?” Inspekta Jamila alikuwa akiwasiliana na Koplo Dihenga kutoka makao makuu.

“Hapana Afande, inaonekana bado yupo hapohapo, kwani Imei inasomeka bado katika mnara huohuo, akiwa katika usawa uleule wa nyumba ya kumi na mbili,upande wa kusini, kutoka katika mnara.” Alijibu Koplo Dihenga, huku akiwa anaangalia katika kompyuta iliyokuwa mbele ya macho yake!

“Sawa Koplo umesomeka, nipo Mbagala Kizuiani nasonga eneo la tukio, tafadhali hakikisha hupotezi lada!” Alihitimisha Inspekta Jamila, kisha akakata simu. Akawa anaangalia mbele huku akiwa kimya na mawazo tele!

Sagenti Kubuta, alikuwa anaendesha gari akiongoza msafara ule, huku akiombea wahusika wanaowafata, wawakute ili wamalizane nao!

Wakiwa njiani eneo la Mbagala rangi tatu, simu ya Inspekta Jamila iliita, nae kwa papara akaitwaa simu yake, nakuitazama namba inayopiga, na hata alipoiona akaipokea simu ile chapu kwa haraka! “Unasomeka nipe taarifa!” Ilikuwa ni simu ya Koplo Dihenga kwa Inspekta Jamila. “Afande simu ya Konstebo Iddy Gebo, imewashwa katika mnara huohuo, ila imetolewa line iliyosajiliwa simu hiyo, na sasa imewekwa line nyingine! Hapa inasoma imei yake katika mnara, umenisoma mpaka hapo?” Alimaliza taarifa yake Koplo Dihenga kwa swali. Na Inspekta Jamila kwa wahaka mkubwa alimjibu.

“Nimekusoma Koplo, hiyo inaonesha mtu mwengine yupo na Mwakyembe, anaweza kuwa ni JM, au Mwakyembe ameamua aitumie pia simu yapili! Endelea kunijuza tafadhali,nakaribia eneo la tukio nipo Tanita mpakani mwa Mbagala na Kongowe!” Alijibu Inspekta Jamila na Koplo Dihenga akakata simu.Dakika kumi baadae, wakawa eneo la Kongowe,wakiikaribia nyumba husika, Inspekta Jamila akampigia Koplo Dihenga, na kumwambia “Nipo eneo la tukio, je kupo vilevile, au kuna badiliko?!” Koplo Dihenga aliangalia komptuta yake akamwambia. “Afande simu ya Constebo Iddy Gebo, imezimwa kama dakika tano hivi, ila simu ya Mwakyembe bado taa ya mnara inasomeka yupo hapohapo!” Alisema Koplo Dihenga na Inspekta Jamila,akamwambia “Labda itakuwa imezimika chaji, ngoja tufanye ambushi tutajuwa hapo hapo ndani, je hapa tumeshahesabu nyumba ya kumi na mbili, kutoka katika mnara wa simu, unaoonekana mbele yetu, kwa upande wa kusini, upo sahihi na data?”

“Hapo sahihi kabisa mkuu, hakuna shaka na data, endelea na kazi mkuu!”

Koplo Dihenga, alimjibu mkubwa wake akiwa anajiamini na majibu yake!

Inspekta Jamila, alikata simu, nakupanga timu yake kuzunguka nyumba ile, kisha yeye akaenda mlangoni nakulijaribu geti la nyumba ile, akaliona limefungwa nganganga! Akamtizama Sajenti Kubuta, kama aliekuwa anataka msaada, Sajenti Kubuta, akamwambia kiongozi wake. “Plani B plus mkuu!”

Na hata alipokwisha kusema maneno yale, Inspekta Jamila akamjibu “Plani B, Sajenti!” Kufumba na kufumbua askari wale waliparamia ukuta wa nyumba ile, huku baadhi ya raia wakishangaa kwa kitendo kile, lakini kwa kuwa wao walikuwa kazini, wala hawakutaka kuwajali, waliendelea na hamsini zao. Askari wanne walikuwa juu ya ukuta, na wanne walibaki chini.Wale askari waliokuwa chini, kila mmoja alikuwa na silaha, aina ya SMG,akiwa ameikamata barabara, akiwa doria katika pembe ya nyumba ile, akihakikisha kwamba hakuna mtu, asiyekuwa wao ataeruka kupitia ukuta wa pembe aliyokuwepo!

Inspekta Jamila, Sajenti Kubuta, na askari wawili, wataalam wa mapambano ya mikono, wote kwa pamoja waliparamia ukuta wa nyumba ile uliokuwa na ruva nyingi, kwa ajili ya kuruhusu hewa kuingiza kwa wingi ndani ya nyumba ile. Kwa ustadi mkubwa waliparamia na kufika juu kabisa ya ukuta ule usiopungua futi nane urefu wake, wakachuchumaa huku mikono yao, ikiwa imezama viunoni mwao, ilipokuja ibuka ilikuwa imekamata silaha ndogo ya Bastola mikononi mwao! Vitendo vyote hivyo vilikuwa vikifanyika kwa pamoja tena bila kelele! Wote wakiwa pale juu ya ukuta na bastola mikononi mwao, waliruka pamoja hadi chini ndani ya uwa wa nyumba ile, wakibimbilika walipofika chini na kulalia tumbo huku silaha zao, zikielekezwa mbele tayari kwa matumizi! Walilala pale chini kwa sekunde kadhaa, walipoona kimya hakuna rabsha yoyote iliyotokea, walitambaa kwa matumbo,na viwiko vya mikono, wakiufata mlango mkubwa wa kuingilia ndani, huku wakichelea kuonekana kama wangelisimama kupitia dirisha lililokuwa pana mbele yao! Na hata walipoufikia mlango, waliukuta mlango ule umefungwa kwa funguo, nyumba ikiwa kimya kabisa!

Sasa wakainuka huku wakijigawa wawili kila pande, waliegemea ukuta, huku silaha zao sasa zikikamatwa kwa mikono miwili, zikiwa zimeelekezwa juu!

Inspekta Jamila, alitoa ishara kwa wenzake, na kitendo bila kuchelewa, Sajenti Kubuta alirudi nyuma, kisha akapiga hatua kubwa na kupitia bega lake, aliukumba ule mlango kwa kishindo kimoja kikubwa, na ule mlango bila khiyana, ukafungukia kwa ndani kwa kasi na kujipigiza ukutani!

Askari wale wote wakalala chini kifudifudi kwa kasi ya ajabu,na kutulia pale chini huku sasa wakiwa wanaitazama korido ikiwa tupu haina mtu! Pia wakijikinga kama adui akiwa na silaha,basi kama angefyatua risasi, risasi ile ingepita juu, na wao wangekuwa salama. Askari wale waliinuka kwa ghafla wawili wakiwa upande wa kulia, na wengine wawili wakiwa upande wa kushoto. Wakatembea na ukuta huku wakiwa makini, safari hii wakiwa katika mwendo wa kunyata, askari mmoja wakila upande wa mbele alikuwa ameielekeza silaha yake mbele, na aliekuwa nyuma yake, aliielekeza silaha yake nyuma! Kifupi ilikuwa kila mmoja alikuwa akimlinda mwenzake, huku wakisonga mbele! Walipofika usawa wa iliyoonekana kama mwanzo wa sebule, walisimama huku wakiegemea ukuta, na Inspekta Jamila kupitia mkono mmoja, alikuwa anatowa ishara, ilihali mkono mwingine, alikuwa amekamata silaha yake sawasawa. Askari wale kila mmoja alitikisa kichwa kuwashiria kuwa ameelewa maelekezo aliyokuwa anayatowa kiongozi wao.

Inspekta Jamila na vijana wake, walivamia wakiwa katika mstari mmoja bastola zikilenga mbele, tayari kwa kutumika, naam wakafika katika sebule lakini wasiyaamini macho yao! Wote walipigwa na mzubao wa mwaka, huku wakiongeza umakini mara dufu, walipiga goti, wakawa wanageuka kila upande tayari kwa mashambulizi, lakini bado ulikuwa kama kucheza na kivuli chake mtu, huwa hakina madhara yoyote! Inspekta Jamila huku akiwa ametaharuki kwa hali anayoishuhudia, alitowa ishara ya kusachi vyumbani, katika nyumba ile iliyokuwa mpya kabisa, ikiwa haina samani nyingi ndani yake, pia kulikuwa bado milango ya vyumbani, ilikuwa haijawekwa katika nyumba ile! Hivyo haikuwa shida kufika vyumbani, lakini hadi kinafikiwa chumba cha nne na cha mwisho katika nyumba ile, hakukuwa na majibu yaliyopatikana, yaliyotofautiana na ya vyumba vingine, vilikuwa hakuna mwanaadamu aliekuwa katika vyumba vile, sasa wakiwa wameshusha silaha zao chini, wote walijongea pale sebuleni, wakiwa bado hawaamini kitu wanachokiona kwa macho yao!

Mwakyembe Anthony, alikuwa amelala chali macho yamemtoka pima yakiwa hayaoni yanachotazama! Mwili wake ukiwa na matundu ya risasi usawa wa moyo wake, damu nyingi zilikuwa zimetapakaa sebuleni pale,na zilianza kuganda kuonesha kiasi ya kama dakika kumi na tano hivi, ndiyo roho imeacha mwili wa Mwakyembe Anthony, Lakini Jeradi Mwaipopo, akiwa hajulikani alipo wala hakuwamo katika nyumba ile! simu ya marehemu Mwakyembe, aina ya Blackbery, ilikuwa ipo juu ya stuli ikiwa ipo on! Inspekta Jamila alitikisa kichwa kwa masikitiko, safari hii akimkosa Jeradi Mwaipopo,au JM kwa dakika chache sana!

*******

Jeradi Mwaipopo, alikuwa anajinyoosha viungo vyake,Mwakyembe alitowa simu yake pamoja na simu za wale askari,akawa anazithaminisha, ndipo JM alipoiona ile simu ya Blackbery ya Mwakyembe, na mara moja moyo wake ukapiga paah! Akakumbuka simu hii ndiyo aliyowasiliana na yule askari, akipigiwa na yeye kupiga, JM anatambuwa tangu akiwa askari, madhara ya simu za Blackbery kwani zinaweza kukuonesha kila ulipo, na yeye mwenyewe alishawahi kuwakamata wahalifu waliokuwa wameziiba simu za aina hiyo, kwani hata kama ungebadilisha laini, lakini bado ingeweza kusomwa mahala ulipo, akahisi matatizo mbele yake,yakimjia kwa haraka!

“Akamwambia Mwakyembe, una kitu gani cha kutulinda humu ndani, ikitokezea mahasimu wetu, wakitujia hapa?!” Mwakyembe huku akitabasamu, alimwambia JM. “Ondoa shaka juu ya hilo,hapa nina Bastola inayobeba risasi kumi na nane, tena ikiwa imejaa risasi, lakini kama haitoshi jana tu ndiyo nimepata kiwambo chake cha kuzuia sauti!” Mwakyembe alisema maneno hayo, huku akikigeuza kiti cha kukaa mtu mmoja, aina ya sofa, juu chini na kuibua bastola peke yake ikiwa imevishwa magazini yake, na kiwambo cha kuzuia sauti kikiwa pembeni yake.

Akamkabidhi JM kwa maana ya kumuonesha! JM aliipokea ile silaha huku akitabasamu, akakivesha kiwambo cha kuzuia sauti, akapandisha risasi chemba, akiwa kama anaeijaribu ile silaha kama inafanya kazi sawasawa, huku akiwa ameielekeza juu silaha ile, na risasi ikapanda juu, ikisubiri amri ya kutumwa iende wapi, naam JM akiwa anatizamana uso kwa uso na Mwakyembe, aliishusha ile silaha kwa kasi ikamlenga Mwakyembe, usawa wa moyo, na JM huku akifumba macho, aliziruhusu risasi mbili, kutoka katika silaha ile, naam nazo zikajibu kama zilivyotumwa, zikafumua moyo wa Mwakyembe, kila moja ikipiga katika moyo na kufumua nyama kubwa kwa nyuma!Kwa kuwa Mwakyembe alikuwa karibu kama futi tatu kutoka alipokuwa JM, risasi zile zilimrusha nyuma kama mita nzima na kumtupa chali chini kama mzigo alitupa mikono kidogo akatulia tulii kama maji mtungini, akawa amebadilishwa jina na kuwa marehemu Mwakyembe!

JM aliibusu ile silaha aliekuwa anaihitaji kuliko kitu chochote kile kwa wakati ule, kisha akafunga usalama wa silaha ile automatic, huku risasi nyingine, ikiwa tayari ipo chemba, ikisubiri safari! Jm aliziendea zile simu zilizokuwa zimewekwa katika stuli na marehemu Mwakyembe, akaichukua simu moja iliyouwa inahadhi na heshima kidogo, mali halali ya Konstebo Iddy Gebo, akatowa line iliyokuwemo mle ndani, akatoa line nyingine ya simu, kutoka katika sehemu ya kuvalia mkanda kwa nje, aliibinjua suruali yake, na sehemu iliyokuwa imekatwa, akasogeza kwa vidole vyake, akatowa line ya kampuni ya simu ya Airtel, na kuipachika katika simu ile akaiwasha, na simu ikakubali kuwaka!

Baada ya kujiridhisha kuwa ameshapata simu, silaha kwa ajili ya kujilinda, akaichukua na ile simu ya yule askari mwingine, nokia ya toch, akaziweka mfukoni mwa suruwali yake, mara ile simu aliyoweka line yake, ikatoa mlio wa betri kukosa chaji ya kutosha, na JM akaizima kabisa. Akatoka nje akifunga mlango kwa nje, akaiendea ile pikipiki ya marehemu, akatoka nayo hadi nje, akalifunga lile geti kwa funguo na kuondoka na ufunguo wa nyumba na wa geti, pamoja na ile silaha akatokomea zake, akielekea Vinguguti kwa fida Hussein!

MWISHO

 Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)