
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
JM huku akishusha pumzi ndefu akarejea katika simu na kumwambia mtu aliemuita ndugu yake. “……niletee chipsi mayai, na kuku sahani mbili, weka pilipili nyingi, watengenezee vizuri sana. Mie niletee maziwa fresh yananitosha, ukiniletea na pesa kidogo, utakuwa umenifaa sana!”
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
Baada ya kusema hayo, JM alikata simu, kisha akaifuta ile namba aliyoipigia, na kuirudisha simu kwa mwenyewe huku akiwa anatabasamu.
Dakika arubaini baadae simu ya Yule askari, iliita na alipoitazama ile namba, ilikuwa ngeni machoni mwake, akaipokea. “Halow, ndiyo hii, ehee, sawa njoo hadi hapa Moi, mie nakufata hapo nje, umevaa nguo rangi gani?, Haya basi sogea nakuja!”
Yule askari alikuwa akizungumza na ndugu wa Mwaipopo, kisha akakata simu na kutoka nje, akimuacha mwenzake akiwa anamdhibiti JM.
Kijana mmoja mrefu wa wastani, mweusi tii, aliekuwa amevalia nguo za kubana mwilini mwake,aliingia katika chumba kile, baada ya dakika zisizozidi saba, akiwa pamoja na askari aliemfata, alikuwa amebeba mfuko laini mweusi wa plastiki, akautoa mfuko wa ndani, na kuwakabidha wale askari. Kisha paketi mbili kubwa za maziwa ya Tanga fresh, akimkabidhi Jeradi Mwaipopo, huku akimwambia. “Pole ndugu yangu, nimekuja kukufaa!”
Aliyasema maneno hayo, huku akiwa amewapa mgongo maaskari wale. JM akamwambia ndugu yake, ”Umeniletea pesa nilizokuambia?!” Yule ndugu yake akajibu kwa vitendo, aliingiza mkono mfukoni, na kutoa burungutu la pesa, akazihesabu shilingi laki mbili, nyingine akazirudisha mfukoni. Akataka kumkabidhi JM, lakini JM akamwambia. “Laki moja wape askari, laki moja nipe mwenyewe. Yule ndugu yake JM, akafanya hivyo.
Wale askari walizipokea zile pesa wakagawana palepale huku wakitabasamu, kisha wakanawa mikono katika bomba lililokuwa chooni mle kwa zamu, wakiwa na pesa mfukoni, wakaanza kula chipsi mayai na kuku, kwa fujo!
Hawakufanikiwa kuzimaliza zile chipsi, walianza kunyong’onyea miili yao, nguvu zikawatupa mkono, wakataka kusema jambo midomo ikawa mizito, mikono yao haikuweza kuhimili uzito hafifu wa chakula walichokuwa nacho mikononi mwao, mifuko ile iliwadondoka! Walipotaka kupiga hatua, miguu yao ikakataa kutii, wakaanguka chini kama mizigo, wakaingia katika usingizi mzito!
Geradi Mwaipopo, akamwambia ndugu yake, “Chukua funguo anazo huyo alielala kushoto kwako.”
Yule bwana hakuchukua funguo peke yake, bali alichukua funguo za pingu, pamoja na pesa zake walizogawana askari wale,na simu zao, kisha akamfungua pingu za miguuni kisha akamfungua pingu ya pili ile iliyofungwa kitandani, ikafunguka na kuningg’inia kipande chake cha pili katika mkono wa kulia wa JM. Nae JM aliimalizia mwenyewe kuifungua,pingu ile akaitupa pingu ile chini ya uvungu wa kitanda!
Yule ndugu yake JM alichukua zile chipsi mayai, akaziweka katika mfuko mmoja, akitaka kuondoka nazo, JM akamwambia. “Wacha kubeba mizigo ya bure!” Na yule bwana akauwacha mfuko ule, ambao sasa ulikuwa katika mfuko mmoja! Akakumbatiana na Jeradi Mwaipopo, kisha wakatoka katika chumba kile, wakatoka katika jengo la hospitali ya taifa ya Muhimbili, na kutokomea kusikojulikana!
*******
Askari waliokuwa wanaingia zamu mchana, kuwatowa wenzao walioingia asubuhi, walipigwa na butwaa ya mwaka, baada yakuwakuta wenzao, wakiwa wamelala chini hawana fahamu, na Jeradi Mwaipopo, akiwa ametoweka! Kupitia simu zao za mikononi, walitoa taarifa kwa mkuu wao wakituo, na mkuu wa kituo alirusha hewani taarifa ile kwa simu ya upepo, ‘Radio call’
na ikasambaa kwa kila radio iliyokuwa wazi katika Jiji la Dar es salaam. Na haikushangaza kuwafikia taarifa ile Inspekta Jamila, na Sajenti Kubuta, wakiwa katika kikao na bosi wao IGP.
11
Inpekta Jamila, akiwa na Sajenti kubuta, baada ya kutoka Hospitali ya taifa ya Muhimbili, alikuwa anawaza mengi, akiwazuwa, hatimae akamwambia Sajenji Kubuta. “Inawezekana huu mtandao wa uhalifu wa kina JM bado upo, tena ni mkubwa sana! Sasa hivi inabidi twende katika mtandao wa simu, ili tukaone na huko kama tunaweza kupata lolote la maana, ingawa mie nahisi, huko kutatufanya tuwe karibu na JM, kwa namna moja au nyingine!”
Aliwasilisha ujumbe wake kwa Sajenti Kubuta, na wakawafikiana lazima wafike huko.
Sajenti Kubuta, akamuuliza kiongozi wake. “Tunakwenda kampuni gani ya simu Afande?!” Inspekta Jamila alimtazama Sajenti Kubuta kwa jicho la udadisi, kisha akampa kikaratasi kidogo kilichokuwa kina namba mbili za mitandao tofauti! Huku namba zile mojawapo ilikuwa imewekewa alama ya nyota mbele yake. Na inspekta Jamila akamwambia Sajenti Kubuta “Tunaanza na kampuni ya simu iliyowekewa alama ya nyota!”
Dakika tano baadae, wakawa barabarani, wakielekea Maeneo ya Moroco katika makutano ya barabara ya Ally Hassan Mwinyi, na Kawawa. Wakaingia kushoto katika jengo moja lililojengwa mithili ya meli, wakaegesha gari yao na kuteremka, wakajichoma ndani ya jengo lile.
Wakiwa ndani ya jengo lile, walifika mapokezi na kujitambulisha mapokezi, kisha wakataka kuonana na meneja wa kampuni ile ya simu, na baada ya mawasiliano haya na yale, wakakaribishwa katika ofisi ya meneja wa kampuni ile ya simu.
“Karibuni ofisini kwetu, niwasaidie nini jamani?” Alisema meneja yule akiwa katika sura ya kutabasamu.
“Asante meneja, kama ulivyotambulishwa na katibu muhutasi, sie ni askari polisi kutoka makao makuu. Tumekuja hapa tunahitaji tupate msaada wako, ili kuweza kufanikisha upelelezi wetu.”
Inspekta Jamila alimwambia yule meneja wa kampuni ya simu, huku akitoa kitambulisho chake na kumuonesha.
“Sawa Inspekta, nikusaidieni nini?”
Aliwajibu meneja yule, baada ya kukitazama kitambulisho kile, huku akiwa katika hali ya utulivu mkubwa.
“Askari mwenzetu, ni mteja wenu, na hivi tuongeavyo, anakaribia kufa kwa hicho alichofanywa, sasa tulitaka kufahamu, na tupate ‘PRINT OUT’ ili tuone simu alizowasiliana nazo leo hadi saa sita mchana!” Inspekta Jamila alihitimisha huku akimtazama moja kwa moja usoni, meneja yule.
“Ahaa hilo halina neno, ila tunautaratibu itabidi muufate, kwani siri ya mteja wetu, hatupaswi kumpa mtu mwingine! Hivyo mtasaini kitabu hapo, na kueleza kuwa, mnataka taarifa zipi na kwa nini, kisha mwanasheria wetu, atasaini na hatimae mtapata hayo mnayoyataka!”
Inspekta Jamila, akafanya kama alivyoelekezwa, na nusu saa baadae, ilichapishwa taarifa ya simu zilizowasiliana na namba ile aliyowapa yeye, ikiwa inasomeka ujumbe, simu zilizobeep, zilizobeepiwa, simu zilizopigwa, na simu zilizo ipigia!
Inspekta Jamila, aliiweka karatasi ile juu ya meza, akiwa anakusudia na Sajenti Kubuta, aione kwa umakini, taarifa ile.
Inspekta Jamila, alitoa kalamu na kuanza kuipitisha juu ya karatasi ile kwa umakini mkubwa sana, mara baada yakuimaliza kuipitia, akapiga mstari katika namba ya mwisho, ambayo ilisomeka simu ya yule askari iliipigia, na simu ile dakika arubaini baadae iliipigia simu ya yule askari!
Inspekta Jamila, alitabasamu, pale alipoiona namba iliyofanya mawasiliano na simu ya yule askari mwenzao, pia ilikuwa ni simu ya kampuni ile waliyokuwa katika ofisi zake!
“Meneja tunashukuru kwa msaada wa kwanza, ila bado tunahitaji msaada wako, tunaomba pia ‘PRINT OUT’ za namba ya mwisho kuwasiliana na simu ya askari mwenzetu, ikibidi ianzwe kuchapwa mawasiliano iliyofanya wiki moja nyuma!” Inspekta Jamila, alimwambia yule meneja, huku akionesha msisitizo!
Yule meneja akafanya kama alivyoelezwa, na dakika tano baadae zikaletwa karatasi zilizokuwa na kila kitu walichokihitaji. Wakaagana na meneja wakiwa wanatabasamu, wakarejea ofisini kwao, wakiwa na matumaini mapya!
Inspekta Jamila, na Sajenti Kubuta, walihamia katika chumba cha compyuta kwa muda, wakiwa na wahka ile mbaya!
Koplo Dihenga, mtaalam wa IT,(Imformation Technology) wa jeshi la polisi, aliwapokea na kuwasikiliza shida yao.
“Koplo, hebu tutafutie picha za mtu huyu, na data zake, kadiri utakavyoweza. ”Inspekta Jamila, alimwambia Koplo Dihenga, huku akimkabidhi karatasi waliyotoka nayo kule katika kampuni ya simu.
Koplo Dihenga, aliekuwa amezungukwa na kompyuta kadhaa! Aliipokea ile karatasi na kuilisha data compyuta iliyokuwa mbele yake, kisha akawa anaisubiri, kompyuta ile ikitafuta mambo iliyotakiwa itoe taarifa zake!
Baada ya dakika takribani tano, kompyuta ile, ilinyambua data zifuatazo! Mwenye namba ya simu, anaeulizwa anaitwa Mwakyembe Anthony. Line ya simu yake, inatumiwa katika simu aina ya Blackbery yenye imei:256436-03-020155-7. Imeongea ikitumia mnara wa kampuni ya simu ya Airtel, uliokuwa upanga mashariki, katika wilaya ya Ilala, mkoa wa Dar es salaa, Tanzania. Simu yake ilikuwa katika mnara wa Muhimbili, saa tano zilizopita! Muda huu namba ya simu hiyo imei,inasomeka katika mnara wa Kongowe ya Mbagala! Ikiwa ipo katika nyumba ya kumi na mbili upande wa kusini, kutoka katika mnara!
Koplo Dihenga, aliiprint taarifa ile, na kumkabidhi Inspekta Jamila.
Inspekta Jamila, akampongeza Koplo Dihenga, na kumwambia. “Hatuna muda wa kupoteza, tunaelekea Kongowe, kadiri simu hiyo itapohama eneo,utatupa taarifa!”
“Timamu Afande” Coplo Dihenga alimwambia Inspekta Jamila, huku akiwa katika ukakamavu, kuonesha heshima kwa mkubwa wake.
Inspekta Jamila, alipanga timu yake, dakika ishirini na tano baadae, gari mbili za kiraia, aina ya TOYOTA NOAH zikiwa na askari nane, wenye silaha za kivita smg, walikuwa wamezipakata katika miguu yao, huku Inspekta Jamila, na Sagenti Kubuta, wakiwa katika gari ndogo Toyota Soluna, ikikamilisha idadi ya gari tatu, zinazoelekea eneo la Kongowe,katika wilaya ya Temeke.
*******
Jeradi Mwaipopo akiwa na mtu aliemwita nduguye, anaeitwa Mwakyembe Anthony, baada ya kutoka katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, wakitumia usafiri wa Mwakyembe, pikipiki aina Boxer kutoka India.Ikiendeshwa na Mwakyembe, walivaa elementi wakawa wanaonekana kama abiria amepanda Bodaboda!
Safari yao, ilielekea Maeneo ya wilaya ya Temeke,katika eneo liitwalo Kongowe, kama unaelekea Mkuranga, nyumbani kwake Mwakyembe.
Walipofika waliingiza pikipiki ndani, wakafunga geti na kukumbatiana upya, kama watu waliokuwa hawajaonana muda mrefu nyuma.
“Asante sana ndugu yangu, kumbe bado unakumbuka maagizo yangu kuwa, nikikwita na kukwambia njoo unifae, namaanisha nini?!”
Jeradi Mwaipopo alimwambia mtu aliependa kumwita ndugu yake, kwa sababu wote walikuwa wanatoka katika mkoa mmoja wa Mbeya.
“Naam nakumbuka sana, kwani natambuwa kama umeshakamatwa, kwani nilikuwa nafatilia kwa karibu sana. Ndiyo maana uliponiambia nije nikufae, upo muhimbili,kisha ukanitaka nije na chakula kwa ajili ya wale askari, nikatambuwa natakiwa nifanye nini!
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media