
Mtunzi: Ally Mbetu 'Dr Ambe'
SEHEMU YA KUMI NA SITA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Hiloo linapenda nakutania, wacha nikimbie, bai mmmwaaa,” alimuaga Shuku kwa kumbusu shavuni na kumfuata MJ aliyekuwa amelala kwenye sofa na maumivu makali ya mateso ya Lily ambayo kwake alijua ni kulipa kisasi.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
Alipofika karibu yake alimwinamia na kumbusu.
“Shemeji langu la ukwe..eehe..mmmwaaa, bai,” alimbusu na kumpiga kofi jepesi shavuni na kunyanyuka alirudia tena Shuku na kumbusu tena.
“Mmmwaaa lazima baba mwenye nyumba umzidi mpangaji.”
Lily alielekea nje kwa mwendo wake wa madaha huku akiziachia sehemu zake ya nyuma zitikisike kama zinasikia baridi kali. Wote walimsikindikiza kwa macho kisha
walikutanisha macho na kucheka kwa pamoja, MJ alitoa sifa za uongo kwa Shuku.
“Ndugu yangu demu unaye.”
“Kweli, yaani ananichanganya akili.”
“Mungu kamjalia umbile tata lisilo isha hamu.”
“Wacha uchanganyikiwe hata kazi anaiweza,” Shuku alijisifia.
“Hata mimi najua.”
“Best umejuaje, tunazunguka nini?”
“Shuku mawazo gani hayo, si wewe mwenyewe uliniambia au umesahau, best tumeanza kutoaminia!”
“Samahani si unajua kuchanganyikiwa mtoto kanichanganya vibaya ukiniwezesha naoa kabisa.”
“Wanawake wa mjini si wa kuwaamini unafikiria upo peke yako, mtu hawezi kumpa gari la gharama hivihivi tu mtakuwa mnashea tu.”
“Kwa hiyo?” kauli ile ilimshtua Shuku.
“Wee endelea naye lakini sikushauri kuoa.”
“Mmh! Lakini usemayo yana ukweli maana kama siku mbili tatu hivi alianza kuniyeyusha kila nikimhitaji sababu kibao.”
“Umeona eeh! Kuwa makini wanawake wa mjini wa kugonga na kuacha siku ukimkumbuka unakumbushia lakini kuoa ugonjwa wa moyo.”
“Nimekuelewa mtu wangu, tena nilitaka kurudisha mapenzi kwani niliishapanga kumpiga chini.”
“Utaweza?”
“Naweza, naogopa sana kuumizwa.”
“Basi poa.”
“Wacha nikanyoe nywele saluni.”
“Poa mi nipo.”
Shuku alitoka kuelekea saluni iliyokuwa jirani na wanapoishi na kumuacha MJ akiugulia moyoni na kuapa jeuri ya fedha lazima Lily ampe penzi kwa gharama yoyote
japo alimuapia hawezi kumvulia nguo ya ndani tena. Alipanga kabla Lily hajarudi kwa Shuku basi atamuwahi na kuhakikisha anambadili mwelekeo na kwenda naye
hotelini.
***
Majira ya saa moja na nusu usiku MJ alisimamisha Hammer jirani na nyumba anayoishi Lily. Alipiga honi kama kawaida ambayo ilimshtua Lily aliyekuwa anajiandaa
kwenda kuoga ili aende kwa Shuku kwani wiki ile alikuwa na kazi moja naye kuhakikisha anatangaza ndoa.
Honi ya gari ilimshtua na kufikiria labda Shuku ameamua kumfuata. Alitoka nje akiwa amejifunga upande wa kanga ili kwenda kumueleza amsubiri akaoge kwanza.
Alitembea kwa mwendo wa kasi ili kuwahi kwenye gari.
Alipofika alilisogelea gari alishtuka kumuona MJ akiteremka kwenye gari kitu kilichomshtua na kuuliza:
“Shuku yupo wapi?”
“Lily mpenzi nipo mimi si Shuku, naomba unisikilize.”
“MJ mimi na wewe tumemaliza au kuna kitu umesahau kwangu?”
“Hapana Lily, najua kiasi gani nimekuudhi lakini naomba unisamehe sema kitu chochote ukitakacho nitakupa kwa gharama yoyote.”
“MJ najua wewe ni bingwa wa wanawake naomba uachane na mimi. Nimekubali kumsaliti ndugu yako kwa ajili yako lakini hilo hukuliona. Basi inatosha kwa vile
hakugundua kitu inatosha.”
“Lily nisamehe mpenzi.”
“Koma kuniita mpenzi, nani mpenzi wako?”
“Si wewe!”
“MJ naomba uondoke, usiniharibie penzi langu, Shuku yupo njiani akikukuta hapa unafikiri atanifikiaje?”
“Kwa hiyo?”
“We ondoka, penzi letu lilikufa toka juzi uliponiacha na kwenda kulala na mwanamke mwingine tena si mara ya kwanza, mara ya kwanza nilivumilia umeishaniona nina
dhiki kwa ajili ya vijipesa vyako ndiyo unifanye utakavyo.
“Li...Lily...” MJ alitaka kujitetea lakini Lily alimkata kauli.
“Bwana eeh, hebu achana na mimi,” Lily alisema huku akigeuka na kuelekea nyumbani kwao.
“Lily rudi mpenzi,” MJ alibembeleza bila mafanikio.
Lily hakugeuka alikwenda moja kwa moja ndani na kumwacha MJ akiwa haamini kama kweli yule msichana anayeonekana changudoa amemtolea nje mtu mwenye
fedha kama yeye. Hakuondoka mapema alikaa kwa muda mpaka alipoliona gari la Lily likimpita alijua linakwenda kwake.
Roho ilimuuma moyoni aliapa kumkomesha Lily na kuhakikisha wanaachana na Shuku. Aliingia kwenye gari lake na kwenda Klabu ili akapoteze muda ili akirudi akute
wamelala.
***
MJ alijikuta akiteseka kutokana na makusudi ya Lily kwani kila alipotangaza utajiri wake bado hakueleweka na kuendelea kuteswa bila Shuku kujua kilichokuwa
kikiendelea ilikuwa vita ya siri kati ya Lily ambaye kila kukicha alimchanganya Shuku kwa mapenzi motomoto. Shuku baada ya kuona anabanwa kwenye fedha na MJ
alijitahidi kuweka fedha kidogodogo ili aweze kumweleza ukweli kuwa ile mali si yake ili aweze kuishi kwa uhuru zaidi.
Kila kukicha Shuku aliongeza ufundi wa kukwea mnazi na kumfanya Lily achanganyikiwe na kuamini dunia nzima kuna mwanaume mmoja tu ambaye ni Shuku,
aliyekuwa akimgeuza kinanda akishikwa toka sehemu moja kwenda nyingine abadili milio kama kinanda hasa akiwa juu ya mtumbwi mtoto wa kike apandwa na kichaa
cha mapenzi na kuropokwa maneno huku akimwambia mpenzi wake “Chukua yote.” Kitu kilichomshtua Shuku na kumuuliza mpenzi wake “Unanipa yote kesho
utanipa nini?”
Basi tu raha zikijaa na kumwagika mwanamke hutokwa na maneno kama mtu aliyekatika kichwa na kuropokwa hata akitulia hana hata moja na ukimwambia
aliyoyasema wakati kakamatika atakukatalia kuwa hakuyasema yeye unamsingizia.
Asikuambie mtu mnazi unao yumba una raha yake kwa mkwezi haumchoshi kwani hausimamini muda wote unainamishwa na upepo na kumrahisishia mkwezi na
hata akifika juu ya mnazi anakuwa na nguvu ya kujinywea madafu mengi.
Kitendo cha Lily kumtolea nje huku mpambe wake Shuku akiendelea kula raha kilimuumiza sana MJ kazi yake ikabaki kupiga chabo kila ukiingia usiku kwani Lily
alikuwa hafungi dirisha kwa makusudi mtego uliomnasa MJ bila kujua na kuteseka kila usiku ukiingia na kugeuka mlinzi wa kupigwa na baridi huku akiumwa na
mbu.
Aliamini yeye ndiye anayemweka Shuku mjini hivyo yeye ndiye aliyetakiwa kula vitu vitamu na kuwa na wanawake wazuri kama Lily na si yeye kula kulala.
Baada mateso kuzidi aliamua siku moja kumfuta Lily nyumbani kwao. Tena siku hiyo hakupiga honi ili atoke, alipofika aliteremka na kumfuata kwao. Alipofika aligonga
hodi Lily alipofungua mlango alishtuka kumuona MJ.
“He! We vipi?”
“Lily badala ya kunikaribisha unanishangaa?”
“Nilikukaribishe ili iweje?” Lily alimjibu kwa ukali.
“Lakini mi si shemeji yako?” MJ alijitetea.
“Mmh! Makubwa, haya karibu shemeji,” Lily aliamua kumkaribisha.
“Asante za hapa?”
“Nzuri, karibu ndani,” Lily alimkaribisha ndani MJ.
Baada ya kuingia alikaa kwenye kochi na kutulia. Lily aliyekuwa amejifunga upande mmoja wa kanga aliingia chumbani na kurudi kavaa gauni la vifungo alilovaa kama
koti refu.
“Mmh! Shemeji karibu.”
“Asante.”
“Unatumia kinywaji gani?”
“Nashukuru usisumbuke mi si mkaaji.”
“Haya baba, lete habari.”
“Lily najua kiasi gani nimekuudhi na kuniona adui yako namba moja.”
“MJ hayo si tumeisha yamaliza?”
“Ni kweli lakini nina haki ya kujitetea hata ukinihukumu ujue kosa langu.”
“MJ kuwa muelewa niliisha kusamehe ndiyo maana leo upo hapa ambapo hata mpenzi wangu Shuku hajawahi kufika zaidi ya kuishia nje.”
“Lakini ulivyonipokea bado inaonekana una hasira na mimi.”
“MJ lazima niwe na hasira na wewe, kumbuka kutembea na wanaume wawili wa nyumba moja tena ndugu huoni kama ni hatari? Lakini nilijitolea mwisho wa siku
naonekana malaya.”
“Ni kweli, lakini kumbuka nilivyokuwezesha Lily yale ni makosa ya kibinadamu. Ulitakiwa kunisamehe kwani nilikuwa na mambo makubwa sana kwako.”
“Kwa vile una fedha ndiyo unaamua kunidhalilisha siyo?”
“Hapana Lily nimejua makosa yangu siwezi kurudia tena.”
“Mimi nimekusamehe lakini naomba tuheshimiane tuwe kama zamani mtu na shemeji yake.”
“Hapana Lily bado nakuhitaji, nina mpango wa kukujengea nyumba ya kisasa na kukununulia gari la kisasa la bei mbaya.”
“Nashukuru kwa mipango yako, naomba mipango yako uhamishie kwa wanawake zako wengine kumbuka mimi ni mpenzi wa ndugu yako na tupo katika mipango ya
kuoana.
“Sasa hivi najifunza kuzoea penzi la mtu mmoja ili niweze kudumisha ndoa yangu nampenda sana Shuku nimeuapia moyo wangu siwezi kumsaliti tena.”
MJ aliamini amechemsha hakuwa na jipya lolote la kumshawishi Lily amuelewe kwa kuonyesha ana mapenzi mazito kwa Shuku. Wazo lilikuwa kumharibia Shuku ili
aweze kummiliki Lily kwa vile hakuwa na njia nyingine. MJ aliamua kumvua nguo rafiki yake kwa Lily.
“Lily wewe ni mwanamke mzuri unayetakiwa kumilikiwa na watu wenye fedha kama sisi. Nakuhurumia sana kwa kujua maisha yako ya mbele yatakuwa ya shida sana.”
“Kivipi?”
“Toka mjuane na Shuku amekupa kitu gani kikubwa?”
“Mapenzi.”
“Hayo mapenzi ndiyo utavaa utakula utatembelea?”
“Kwani tatizo nini?”
“Nataka kukueleza ukweli kwa vile nakupenda sana Lily. Shuku kwanza si ndugu yangu kama alivyokutambulisha mwanzo yule ni rafiki yangu tu ambaye
nimemuokota njiani na kuja kumtunza kwangu. Pale hana kitu, kila kitu ni changu ndiyo maana penzi lako kwangu kwa muda mfupi limekupatia gari na sasa nyumba
inakuja.”
“Ha! Muongo mkubwa!” Lily hakuamini.
“Lily ningeweza kukaa kimya lakini najua mwisho wake ungekuwa mbaya kwani Shuku hataki kazi anapenda kukaa na kula tu. Unafikiri nikisitisha misaada nini
kitafuata?”
“Mmh! Siamini najua unataka nikukubali tu huna lolote.”
“Nataka kukueleza kitu ambacho nashangaa hujagundua siku zote. Hushangai chumba chake na changu tofauti yake, pia kama huamini kuanzia leo hatatumia gari
zangu nitampa fedha ya teksi. Lily nakupenda ndiyo maana sitaki upotee.
“Tena kuna kitu nilisahau kukueleza, Shuku tabia zake huwa anakaa na demu mmoja kwa muda mrefu akimpa mimba tu anamkimbia. Kabla ya kuja kwangu alikuwa
anakaa Buguruni Uswahilini ambako anatafutwa na wasichana wawili aliowajaza na kutoroka.”
“Mmh! MJ unasema kweli au unampakazia?”
“Ili kupata ukweli leo jioni mwambie akufuate, utaamini maneno yangu.”
“Mmh! Makubwa, MJ naomba uniache kwanza nimechanganyikiwa sana,” Lily alichanganywa na maneno ya MJ japokuwa hakuyaamini moja kwa moja.
“Usichanganyikiwe nipo kwa ajili yako kuhakikisha unakuwa na maisha mazuri siyo ya kutapeliwa na mtu.”
“Sawa nimekuelewa nitayafanyia kazi,” Lily alisema akijipweteka kwenye kochi.
“Nina imani ukipata ukweli utazidi kuchanganyikiwa. Nakuahidi baada ya kupata ukweli nitakufuata ili kukutuliza akili.”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Zaidi Naomba Share App kwa Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media