NIFANYE NAMIMI KAKA (22) - CnZ Media

CnZ Media

Jisomee Simulizi Mpya Kila Siku

Jumanne, 23 Machi 2021

NIFANYE NAMIMI KAKA (22)

Je unajua kwamba Simulizi zote unazozipata hapa zipo kwenye app ya CnZ Media?

Humo Pia Utakuta:
📖 KUSOMA SIMULIZI
🎬 FILAMU na TAMTHILIA za KITANZANIA
😂 VIDEO za KUCHEKESHA
📑 MAKALA za AFYA na MAPENZI

Install app hii GUSA HAPA utavipata vyote hivyo bure kabisa
Mwandishi: Juma Hiza

SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI
ILIPOISHIA...
“Evadia mjini ni mipango, kila mtu unayemuona anaishi katika mji huu basi fahamu kuwa anaishi kwa mipango. Nilifahamu kuwa utaweza kushangaa hasa kwa mali hizi ambazo nimeweza kuzimiliki lakini nikuondoe wasiwasi mimi ni mtafutaji na siku zote ulizokuwa unaniona nyuma ya pazia kulikuwa kuna mishe nazifanya na ndizo zimeweza kuzaa matunda haya.”

SASA ENDELEA...
“Mishe! Mishe gani hizo?”
“Baby mbona kama huniamini?”
“Lazima niingiwe na hofu ujue mimi nakufahamu sana.”
“Hata kama lakini ufahamu mimi ni mwanaume na sifa kubwa ya mwanaume ni kupambana na wala si kula kama wengi wanavyoamini.”
“Umefanya kazi gani?”
“Kazi nyingi tu! ila nakumbuka kitu kilichonisaidia, nilikuwa nikiwekeza sana pesa yangu katika vitu vya msingi nah ii ndiyo siri kubwa iliyoweza kuniletea mafanikio haya unayoyaona.”
“Mmh! Dick kweli?”
“Ndiyo.”
“Hakuna chochote unachonificha?”
“Hakuna,” nilimjibu.

Uwongo ndiyo uliyokuwa umechukua nafasi kubwa katika maisha yangu, sikuwa naogopa lolote lile hasa katika uwongo niliyokuwa nikidanganya, wanawake wengi waliweza kuniamini na kunikabidhi dhamana ya maisha yao. 

Miongoni mwa hao wanawake Evadia alikuwa ni mmoja wao. Alizidi kuniamini sana hasa baada ya kila kitu alichokuwa akikihisi vibaya, nilipoweza kumuelezea kwa maneno yangu ya uwongo aliweza kunielewa.

Wakati ule nilipokuwa na Evadia mule ndani, simu yangu iliita, nilipoitoa mfukoni na kuitazama nilikutana na jina la Precious. Sikutaka kupokea niliamua kuiacha iite mpaka pale ilipoweza kukata yenyewe.
“Mbona hupokei simu?” aliniuliza Evadia.
“Ah! Achana naye.”
“Ni nani kwani?”
“Mjinga mmoja hivi anasumbua sana.”
“Mwanaume au mwanamke.”
“Mwanaume.”
“Kwani anasemaje?”
“Tangu jana ananitumia meseji zake, ananiambia anataka nimsaidie kumuandikia hadithi yani ni msumbufu.”
“Sawa mpenzi wangu,” alinijibu Evadia kisha hapo hapo nikambeba na kumpeleka chumbani. Kilichoendelea humo ni kufanya mapenzi tu! nilihakikisha namkuna kila sehemu vilivyo ili azidi kunikumbuka kila siku za maisha yake.

Hatimaye ile hadithi yangu ya BADO UNAISHI MOYONI MWANGU iliweza kuhakikiwa na wahariri wa bodi ya filamu pamoja na waandaji wa filamu kwa ujumla.

Ilikuwa ni moja kati ya Hadithi nzuri ambayo waliipenda sana. Irine hakuwa mbali katika hilo alihakikisha kila kitu kinakwenda sawa na baada ya wiki moja kupita kazi ya kushoot filamu hiyo ilikuwa tayari imeshaanza hapa ilikuwa ni baada ya kutafuta Cast za wasanii ambao wangeweza kushiriki katika filamu hiyo ambayo mhusika mkuu alikuwa ni Irine Kisoka.

Nilimtazama Irine kama mhusika mkuu katika filamu hiyo ya BADO UNAISHI MOYONI MWANGU na kwa jinsi ambavyo alikuwa akiigiza, niliamini fika ilikuwa ni filamu ambayo ingeweza kufanya vizuri sana hasa katika upande wa soko zima la filamu nchini Tanzania.

“Vipi kuhusu mumeo?”
“Amefanyaje?”
“Amesemaje kuhusu huu ujauzito?”
“Hajasema kitu halafu ameamini kabisa kuwa huu ujauzito ni wa kwake.”
“Kivipi?”
“Ameamini tu!”
“Hivi siku akigundua kuwa unamchezea mchezo huu mchafu unafikiri itakuwaje?”
“Dick mbona hujiamini yani unaogopa utadhani umekuwa mtoto wa kike.”
“Hayo umesema wewe ila mimi nimekuuliza.”
“Hawezi kufanya lolote bhana embu niamini basi.”

Yalikuwa ni mazungumzo kati yangu na Precious, nilionekana kuwa muoga sana hasa baada ya kuanza kuwaza kuhusu mume wake. Niliwaza siku ambayo ingetokea mume wake akagundua kuwa mimi ndiye nilikuwa sababu ya yote yale pamoja na ukatili ambao angeweza kunifanyia.

Nilikumbuka kesi na matukio mbalimbali ambayo nimewahi kuyashuhudia na jinsi ambavyo mtu akifumaniwa na mke wa mtu kitendo anachofanyiwa. Hilo lilizidi kuniogopesha sana.

“Embu acha kuogopa uko na mimi hakuna kitakachoharibika,” aliniambia Precious tulipokuwa kitandani amejilaza mapajani mwangu akijaribu kudeka deko la kimapenzi. Wakati huo nje jua kali la saa saba lilikuwa likiangaza.
“Lazima niogope ujue mimi nawaza mambo mengi sana,” nilimwambia huku nikilipapasa tumbo lake.
“Mambo gani hayo niambie usinifiche tafadhali.”
“Ni kuhusu mume wako.”
“Kafanyaje tena?”
“Wewe hunipendi.”
“Sikupendi na nini mpenzi wangu.”
“Unataka mumeo aniue.”
“Hawezi kukuua bhana embu acha kuwa na dhana hizo za kijinga.”
“Kwahiyo hapa nazungumza ujinga.”
“Sio hivyo mpenzi wangu sasa wewe kila wakati unaongelea kitu hichohicho tu! mimi nimekuambia jiamini hakuna chochote kitakachotokea.”
“Sawa,” nilimjibu.
Precious alizidi kuniaminisha kuwa hakukuwa na kitu chochote ambacho kingeweza kutokea. Ule wasiwasi wangu uliyoanza kuniingia taratibu ulianza kupotea, nilizidi kuyaamini maneno ya Precious na hivyo sikuwa na hofu yoyote.
“Wewe kweli ni kidume,” aliniambia Precious.
“Kwanini?” nilimuuliza.
“Siamini kama leo nina ujauzito kwakweli yani Dick nitakupenda mpaka mwisho wa maisha yangu,” aliniambia.
“Na mumeo je?”
“Mume wangu wa nini sasa?” aliniuliza kwa ghadhabu kisha akanuna, nikapata kazi mpya ya kumbembeleza mpaka pale alipoamua kutulia. Hakupenda kulisikia jina la mume wake nikilitaja mbele yake.
“Kwanini unakuwa hivyo lakini?”
“Nisamehe mpenzi.”
“Mimi sipendi.”
“Najua mpenzi wangu nisamehe.”
“Niahidi kwanza.”
“Nikuahidi nini?”
“Kuwa hautarudia tena kumtajataja.”
“Ndiyo sitarudia tena kumtaja.”
“Nakupenda sana Dick wangu.”
“Nakupenda pia Mahabuba.”
“Nafurahi sana kusikia hivyo.”
“ Binafsi najivunia kukupata katika maisha yangu, umeyabadilisha maisha yangu Precious.”
“Usijali nitazidi kuyabadilisha na kila kitu ambacho unakitaka niambie nitakutimizia, mimi nipo kwa ajili yako.”
“Sawa mpenzi wangu,” nilimwambia.

Baada ya kupita miezi kadhaa hatimaye filamu ya BADO UNAISHI MOYONI MWANGU iliweza kukamilika na kuingia sokoni, ilikuwa ni moja kati ya filamu bora zilizokuwa zikipendwa sana hata katika upande wa mauzo iliweza kuvunja rekodi. Hakukuwa na filamu nyingine iliyokuwa ikitazamwa tena, kila mtu alibaki akitazama BADO UNAISHI MOYONI MWANGU.

Kwa kweli sikutaka kuamini kabisa kama filamu hiyo ingeweza kunifungulia milango ya mafanikio kila kukicha. Nilikuwa nikipokea simu mbalimbali kwa ajili ya kufanya kazi na makampuni makubwa yaliyoniamini kuutambua uwezo wangu katika kuandika.

Jina langu la Dick Mapenzi sasa lilizidi kuwa jina kubwa mno, kila mtu alianza kunifahamu, hakukuwa na mtu ambaye aliitaja filamu ya BADO UNAISHI MOYONI MWANGU bila kulitaja jina langu kama mwandishi.

Wasichana nao hawakuisha kujipendekeza kwangu, kila msichana ambaye alijipendekeza kwa kweli sikuacha kufanya naye mapenzi, huo ndiyo ulikuwa ugonjwa wangu haswaa!

Niliweza kutengeneza pesa nzuri sana kupitia filamu hiyo, faida nzima niliyoweza kuipata niliamua kwenda kuwekeza katika biashara mbalimbali. Sikuwa na shida yoyote kama ni nyumba nzuri nilikuwa nayo, gari la kifahamu tena BMW nilikuwa nalo, kuhusu pesa wala haikuwa ni moja ya tatizo kwangu, Precious alikuwa akinihudumia kwa kila kitu.

Sikutaka mafanikio yangu pamoja na umaarufu wangu uishie kwenye filamu tu! pamoja na kupokea sifa mbalimbali kutoka kwa watu waliyokuwa wakinifahamu. Nilitamani sana kuwa mtu maarufu na umaarufu ambao nilikuwa nikiutaka ni ule wa kuandikwa kila siku katika magazeti pamoja na kuandikwa sana katika mitandao ya kijamii. 

Hakukuwa na wazo lingine lililonijia kichwani mwangu kwa wakati huo zaidi ya kuamua kutembea na Irine Kisoka miongoni kati ya waigizaji ambao walishiriki kwa asilimia kubwa katika kuhakikisha lengo langu la kutoa filamu linatimia na kweli liliweza kutimia.

Alikuwa ni muigizaji aliyeongoza kwa kuandikwa vibaya katika magazeti ya udaku pamoja na mitandao ya kijamii, hii ilitokana na uzuri pamoja na umaarufu aliyokuwa nao.

Nilijisahaulisha kuhusu urafiki aliyokuwa nao na Evadia. Hata kipindi kile ambacho Evadia alikuwa akihangaika katika kuhakikisha nafanikiwa vyote nilijisahaulisha na sasa kitu nilichokuwa nimepanga ni kutoka kimapenzi na Irine 

Kisoka huku lengo langu likiwa ni kutafuta skendo itakayonifanya niwe maarufu zaidi mpaka nianze kuandikwa katika magazeti ya udaku na mitandao ya kijamii.
“Hongera kwa kazi nzuri uliyoifanya.”

“Asante ila nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nisipokushukuru wewe.”
“Mbona sioni cha kunishukuru hapo wakati kila kitu umehusika.”
“Jina lako na umaarufu wako ndiyo vimefanya nikaweza kulitimiza hili kama si wewe nadhani nisingefika hapa.”
“Kweli?”
“Ndiyo.”

Yalikuwa ni mazungumzo kati yangu na Irine tulipokuwa katika moja ya hoteli kubwa hapa mjini majira ya mchana, tulikuwa tukipata chakula cha mchana lakini pia ilikuwa ni katika harakati za kupongezana baada ya filamu tuliyoitoa kufanya vizuri kimauzo.
“Imekuwa ni filamu ya kipekee sana ujue siamini kama imeweza kufanya vizuri,” aliniambia Irine.
“Hata mimi siamini,” nilimwambia.
“Unajua sana kuandika hadithi za kimapenzi.”
“Hahahaha! mbona hata wewe unajua kuigiza filamu za kimapenzi.”
“Nikwambie kitu.”
“Niambie.”
“Hii imekuwa ni filamu ya kitofauti sana kwangu na filamu zote ambazo nimewahi kuzifanya.”
“Kwanini?”
“Hadithi uliyoiandika ni ya kipekee sana yani kwa kipaji ulichonacho hukustahili kuwa hapa,” aliniambia Irine maneno yaliyonifanya nitoe tabasamu.
“Mbona unacheka?”
“Umenifurahisha.”
“Huo ndiyo ukweli.”
“Kila siku huwa najiambia mwenyewe kuwa kama nisingebahatika kukutana na wewe sijui ni lini ningeweza kuitimiza ndoto yangu.”

“Hapana usiseme hivyo ila unachotakiwa ni kumshukuru Mungu halafu pia nadhani usimsahau Evadia maana nadhani yeye ndiye amekuwa msaada mkubwa sana kwako.”

Nilionekana kuwa mwenye furaha wakati wote wa mazungumzo lakini alipofikia kulitaja jina la Evadia na kuniambia kuwa nilitakiwa kumshukuru kiukweli nilibadilika, sikutaka kulisikia jina la Evadia mahali pale.

Mabadiliko yangu kwa wakati ule yalimshangaza Irine, aliponiangalia usoni alionyesha kuwa na maswali juu ya hali yangu ile, hilo nililifahamu nikajaribu kuwahi kuliunda tabasamu bandia ili niweze kumficha hali niliyokuwa nayo lakini haikuwa kama nilivyowaza aliwahi kuniuliza na hapo nikawahi kutafuta jibu la kumzugia.

“Nini mbona umebadilika ghafla!” aliniuliza Irine, wakati huo macho yangu yalikuwa yakikitazama kifua chake ambacho alikisitiri kwa vazi la wazi lililojaribu kukidhihaki na niliitumia nafasi hiyo kumtazama kwa macho ya uwizi.

“Hapana hakuna kitu,” nilimjibu kisha nikajifanya kuwa bize na sahani ya chakula ambacho nilikuwa nikiendelea kukila.

Kila nilipokuwa nikimtazama Irine na kwa jinsi alivyokuwa ameumbika kiukweli nilizidi kumtamani sana, kuna muda nilitamani kumwambia lakini niliogopa, hapa ni baada ya kuzikumbuka zile skendo za kutembea na wanaume tofautitofauti, nilibaki nikimtazama na kula kwa macho ya uchu.

Kila siku alikuwa akiandikwa vibaya magazetini, alikuwa akiandikwa kuwa alikuwa akitembea na wanaume tofautitofauti ambao wengi wao walikuwa ni watu wenye wadhifa fulani, hilo lilizidi kuniogopesha.
“Kuna kitu unataka kuniambia?” aliniuliza.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA KWENYE APPLICATION YETU HIVYO UKIYAONA NAOMBA BONYEZA HAPO NDIO UNANIPA SAPOTI MIMI, UKIBONYEZA UNAWEZA KUCANCEL SIO LAZIMA UENDELE ULIKOPELEKWA, KIKUBWA UBONYEZE HATA MARA 2-3 KILA UKIFUNGUA APP YETU

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

TAZAMA KICHEKESHO HIKI KISHA BONYEZA SUBSCRIBE ILIYOPO CHINI YAKE WAKATI TUKIELEKEA KWENYE MUENDELEZO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni