UZOEFU (25) - CnZ Media

CnZ Media

Jisomee Simulizi Mpya Kila Siku

Jumatatu, 12 Aprili 2021

UZOEFU (25)

Je unajua kwamba Simulizi zote unazozipata hapa zipo kwenye app ya CnZ Media?

Humo Pia Utakuta:
πŸ“– KUSOMA SIMULIZI
🎬 FILAMU na TAMTHILIA za KITANZANIA
πŸ˜‚ VIDEO za KUCHEKESHA
πŸ“‘ MAKALA za AFYA na MAPENZI

Install app hii GUSA HAPA utavipata vyote hivyo bure kabisa

JINA: UZOEFU
Mwandishi: Elisha Msafiri

SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO
ILIPOISHIA...
Palikuwa na kizingiti kikubwa na kigumu kung'oka kilichoitwa Sunshine.Sunshine ananipenda hadi naogopa! Nilishafanya visa chungu mzima lakini kuachana ilishindikana.Japo avumaye baharini ni papa lakini wengine nao wamo vivyo hivyo avumaye moyoni mwangu ni Lisa lakini Sunshine naye hakuwa wa kubeza hata kidogo.
SASA ENDELEA...
Kiukweli walimbwende hawa wawili waliniweka njia panda nisijue pa kuelekea.

Meseji alizokuwa anatuma Lisa kila siku usiku na mchana tayari zilishaanza kuulemea moyo wangu, nikajihisi simtendei haki mpenzi wangu huyo wazamani kwa kuendelea kumzungusha nisimwambie nimemsamehe au la!

Kwa kawaida nnapokuwa njia panda katika kufanya maamuzi huwa napenda sana kujumuika na wenzangu katika ibada.Hata siku ya mapumziko ilipofika niliwahi kanisani nipate kutuliza yangu nafsi na siku hiyo ikawa kama vile nimeenda kujichoma mwenyewe kwani hubiri la siku hiyo lilihusu upendo.Wengi wanapenda lakini hawazijui kanuni za upendo.Siku hiyo nilipata kuzijua kanuni za upendo zilizoandikwa na Wakorintho.

Kwanza kabisa Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Baada ya kuzijua kanuni hizi za upendo nilijiona kama mwenye hatia.

Nakumbuka siku kadhaa zilizopita Lisa alihoji kama bado nampenda na mie nikajibu bila shaka.
Sasa iweje bado nafikiria mambo mabaya aliyonitenda ili hali upendo hauhesabu mabaya?
Iweje nione Lisa aliniumiza hali yakuwa upendo hauoni uchungu??

Kama nikisema simpendi Lisa mdomo utakuwa umeudanganya moyo na si ajabu mdomo ukapewa ububu na mkono ukalithibitisha hilo kwa maandishi.

Maneno yote muhubiri aliyokuwa anasema siku hiyo ni kama vile alikuwa ananisema mimi, Muda mwingine nilitamani hata kutoka nnje nisisikie maana kile neno lililonenwa lilitangaza hatia juu yangu. Hadi mwisho wa somo ulipofika moyo wangu ulikuwa umepondeka vya kutosha na siku hiyo nikapanga kufanya maamuzi.

Sikutaka tena kusita sita kwenye njia mbili.Jioni ya siku hiyo nilimuomba Sunshine tuonane ili nimueleze vile nimeamua.

Kama kawaida jioni ya siku hiyo nilienda mtaani kwao Sunshine na tukakutana katika eneo ambalo tumekuwa tukifanyia vikao vyetu vya jioni toka tumejuana, isipokuwa tu siku hiyo ilifanywa tofauti na maongezi yake, siku zote tumekuwa tukijadili mipango na malengo ya maisha yetu huku tukifurahi na kucheka lakini kwa siku hiyo vinatawala vilio, masikitiko, majuto, hasira, simanzi pamoja na dukuduku, hiyo yote ni baada ya kumuweka bayana Sunshine juu ya kinachoendelea kati yangu na Lisa.Sunshine alionekana kutoamini 

Chochote nnachomwambia hiyo ni kutokana na kuzoea baby wake ni mtu wa utani kila mara, lakini mara baada ya kumthibitishia kuwa nnachomwambia sitanii ndipo kilio kilipoibuka na maneno ya kunialaumu sana, nilimuonea huruma Sun lakini sikuwa na la kufanya, hakuna lugha yeyote nzuri unayoweza kumueleza mpenzi wako anayekupenda sana kuwa muachane naye akakuelewa. 

Kitendo bila kuchelewa nilimuona Sun chini akiwa kapiga magoti huku akiniomba aongee na Lisa amuachie mpenzi wake, bila Tom yeye hana maana ya kuishi tena kwenye hii Dunia.Kitendo hicho alichokifanya Sun kiliushambulia moyo wangu mithili ya kuku wa kuenyeji waliomwagiwa mchele.Sun hakuwa na kosa lolote hivyo ilikuwa ni haki ausulubu moyo wangu.Hakuna kazi ngumu kama kuachana na mpenzi ambaye hajawahi kukukosea kitu ila mithali niliyoitumia mahali hapo ni hii, ukitaka kumuua Nyani usimuangalie usoni.

" Tom naomba unisindikize kwetu, sina nguvu!" Hiyo ni kauli ya mwisho aliyoitoa Sun baada ya kushindwa kunisihi nisimuache.Taratibu nikamuinua Sun toka chini alipokuwa nikauweka mkono wake begani mwangu na kunza kumsindikiza kwao. Mapenzi yanaweza yakaua niliamini siku hiyo.

Baada ya kumfikisha Sun mahali ambapo aliniruhusu nimuache taratibu nilianza kurudi nyumbani huku njia nzima nikifiria maisha mazuri tuliyoishi na Sun na hatimaye historia hiyo nzuri inafungwa kwa mwisho mbaya.Sikuwa na la kufanya zaidi ya kufumba macho, moyoni nilimpenda sana Lisa pamoja na mifarakano yetu ya mara kwa mara pia Lisa alinipenda sana mimi.Barabara hata iwe ndefu vipi haikosi kuwa na kona. 

Japo Sun naye nilimpenda sana kutokana na mapenzi yake ya dhati kwangu lakini maisha tuliyoishi na Lisa toka utotoni yalinichanganya zaidi, ni kifo pekee ambacho kingenitenganisha na huyo mtoto kwani yeye alikuwa ananijua mimi nnje ndani lakini pia mimi nilimjua yeye hata pengine zaidi ya anavyojijua.

Hatimaye siku hiyo iliyoututenganisha mimi na kipenzi changu Sunshine ilipita salama salimini lakini siku mbili baada ya hiyo kupitai ikawa na walakini.

Ni majira ya saa kumi na moja za alasiri jua likiwa limechoka kuwachoma walala hoi na kuanza kutafuta machweo ili lipate kupumzika ndipo na mimi ambaye nilikuwa nimejipumzisha nyumbani muda mfupi baada ya kutoka shule kelele za simu yangu zinasitisha mapumziko ya akili na naamua kuipokea simu hiyo ambayo imepigwa na mtu nnayemfahamu sana. 

Naipokea kichovu lakini mara tu baada ya kusikia kilichozungumzwa nakurupuka na kuanza kujiandaa kuelekea mahali nilipoitwa.

" Hapa hadi Sinza bei gani!?" Nilimuhoji dereva wa boda boda kuona kama naweza kuelewana naye bei, kwa haraka niliyokuwa nayo nisingeweza kukaa kwenye foleni hata kidogo hasa ukizingatia kuwa muda huo ni jioni na wakazi wengi wa jiji hili wanatumia barabara chache kurudi makwao.

" Shachukua boda boda dakika sifuri tu ntakuwa hapo mwanangu!" Nilimpa tumaini rafiki yangu Amani mara baada ya kunipigia tena ili kujua nimefikia wapi katika safari hiyo.

Kiukweli Amani alikuwa ni rafiki yangu kipenzi tuliyeshibana sana.Kwa kiasi kikubwa shida zangu zilikuwa zake hali kadhalika zake zangu.Hata aliponipigia simu niende nyumbani kwake haraka, niliianza safari bila kufikiri mara mbili mbili.

" sasa atakuwa na nini huyu Amani asichotaka kuniambia kwa simu!?" Nilijiuliza mwenyewe kwa sauti ya chini iliyobebwa na kasi ya upepo uliopambana na boda boda.

Ki ukweli toka nimeachana na Sunshine, nimekuwa sina raha wala amani kabisa hasa ukizingatia hali niliyomuacha nayo, hata ningesikia amekunywa sumu nisingeshangaa sana kwa maana hali hiyo ilimruhusu kufanya hivyo. Japo aliyeeniita ni rafiki yangu Amani lakini akili yangu yote ilikuwa kwa Sunshine.Na sikujua hata kwanini niliposikia jina lake moyo wangu ulinipasuka.

Nikiwa katika hali hiyo ya sintofahamu hatimaye tulifika nilipokuwa nikienda, nilimlipa dereva ujira wake kisha kwa mwendo wa kasi nilianza kutembea huku nikiambatana na hofu kuelekea ilipo nyumba anayoishi Amani.Hatua chache kabla ya kufika nilimpigia simu, sikutaka kwenda moja kwa moja kichwa kichwa kuhofia kujilengesha.

" Oya njoo basi nipo hapa kwa Mangi tukutane!" Niliongea haraka haraka baada ya Amani kupokea simu yangu, kwa akili zangu za haraka haraka nilijua Amani angenilazimisha kufika kwake lakini nilishangaa utayari wake wa bila kusita sita kuja nilipo hivyo na mimi ambaye nilikuwa nikipima maji kwa wakati huo kujua kina chake nikafanya bidii ya kufika kwa Mangi ili tuonane!.

Punde si punde Amani naye akawasili,kwa Muonekano wake wa haraka hakuwa mtu mwenye utulivu kabisa na nywele zake zilikuwa zimevurugika sana. Rafiki yangu huyu anapokuwa na jambo linalomchanganya akili hupendelea kukuna kichwa nilifikiri hiyo ndo sababu ya nywele zake kuvurugika.

" oyaah! Vipi kaka!?" Nilimuhoji kwa shauku Amani aliyeketi na kushika tama kanakwamba anafikiria aanzie wapi.

" Dah! Mwanangu yaliyonikuta we acha tu!"Amani alianza kufunguka taratibu huku akiweka kiti chake vyema kunipasha habari.

"Mwanangu shem wako ndio ananiumiza kichwa………sijui kazinguliwa nini kwao kabeba kilicho chake nimemkuta gheto……sasa sijui inakuwaje hapo mwanangu!" Amani aliongea kwa kifupi huku akionyesha ana mengi ya kusema. Kesi yake nayo ilikuwa ni ile ile iliyonikuta mimi siku chache zilizopita'mapenzi' isipokuwa tu kesi hizi zipo tofauti kidogo.

" Hahaha! Amani bhana…mimi hapo sioni tatizo kwani si mnapendana?……sasa tatizo liko wapi hapo,shem wangu amehamia kwako muishi pamoja!" Niliongea kiutani huku nikijifanya namaanisha nilichokisema hiyo yote ni katika kumchota akili Amani nijue yupo mlengo gani kabla sijampa ushauri kamili.

" Aaah! Tom mwanangu yaani unaongea kama vile huijui familia yao vile walivyo mabandidu! wee unafikiri kama watakuja kuniletea zogo maskani pale itakuwaje, hata hivyo pamoja na kumpenda sana shem wako hatukupanga kuishi pamoja kwa wakati huu!" Amani aliongea kama vile ananilalamikia.

" Kwaiyo ndugu yangu wee unataka nifanye nini!?" Nilimuhoji Amani ili nimpe ushauri anaoutaka.
"Tom nimeshakueleza kila kitu wee si mtu wa kuniuliza swali hilo!" Amani aling'aka.
" Je utaridhia nnachotaka kukifanya!?" Nilimuhoji tena naye akanijibu ndio kwa kutikisa kichwa baada ya kufikiri kwa muda.

" Si yupo nyumbani saivi?" Tena niliuliza naye Amani akanajibu ndio.Tukasimama pamoja na kuelekea kwake.Kuna usemi usemao ukitaka kuonekana mjinga basi ingilia mapenzi ya watu siku hii sikuujali usemi huo nnaouzingatia kila mara ili kumuokoa rafiki yangu Amani.

" Mambo vipi shem!?" Nilimsalimu mpenzi wake Amani aliyekuwa kajilaza kwenye sofa naye akaitikia poa bila kunitizama.

"Unaweza kutupisha dakika sifuri tafadhali!" Nilimuomba Amani kwa kumnong'oneza naye akatuacha sebuleni peke yetu.

"Japo umenijibu poa lakini naamini si poa unaeza kuniambia nini kimetokea mpenzi wangu!?" Nilianzisha mazungumzo na shem wangu ambaye tumezoeana kuitana majina yote ya kimapenzi na huenda yupo huru kwangu zaidi kunieleza mambo yake kuliko afanyavyo kwa Amani.

Baada ya kumuuliza swali hilo alikaa kitako na kunieleza yote yaliyotokea hadi yeye kuchukua maamuzi hayo ya kukimbia kwao na kuhamia hapo.Kesi yake haikuwa kubwa sana ila nadhani aliondoka kwa kuwa alikuwa na pakwenda.

"Hivi unampenda Amani kweli!?" Nilimuuliza shem naye akajibu ndio.

"Me nadhani humpendi! Na kama unampenda kweli basi usingemsababishia matatizo yasiyo na lazima.……hivi unadhani wazazi wako wakisikia umekuja kwake na umezinguana nao watampenda kweli? Si ndio wataona yeye anakupa kiburi na kukufanya uwadharau wao.

Ukiachana na hilo ili mfanikiwe kimaisha na kuwa na maisha bora ni lazima muwe na baraka za wazazi hebu nambie maisha yenu yatakuwaje iwapo kila siku wazazi wako wanawalaani juu ya mlichokifanya……unadhani maisha yenu yatakuwa vipi zaidi ya mifarakano isiyoisha kila kukicha na kuandamwa na mabalaa.

Kitu pekee nnachokushauri mpenzi wangu rudi nyumbani, mtoto akinyea mkono haukatwi wazazi watakusamehe na watafurahi pia.Kinyume na hapo neno langu sio sheria lakini hamtakuwa na kesho nzuri."

Tuliongea mengi na shemeji yangu huyo na mwisho wa siku alinielewa na akakubali kurudi nyumbani kwa roho moja.Hivyo nikawa hakimu mzuri kwenye kesi hiyo hakuna nilichokuwa nimebakiza zaidi ya kurudi nyumbani huku nikimuacha Amani amsindikize mpenzi wake kwao.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA KWENYE APPLICATION YETU HIVYO UKIYAONA NAOMBA BONYEZA HAPO NDIO UNANIPA SAPOTI MIMI, UKIBONYEZA UNAWEZA KUCANCEL SIO LAZIMA UENDELE ULIKOPELEKWA, KIKUBWA UBONYEZE HATA MARA 2-3 KILA UKIFUNGUA APP YETU

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

TAZAMA KICHEKESHO HIKI KISHA BONYEZA SUBSCRIBE ILIYOPO CHINI YAKE WAKATI TUKIELEKEA KWENYE MUENDELEZO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni