UZOEFU (3) - CnZ Media

CnZ Media

Jisomee Simulizi Mpya Kila Siku

Alhamisi, 1 Aprili 2021

UZOEFU (3)

Je unajua kwamba Simulizi zote unazozipata hapa zipo kwenye app ya CnZ Media?

Humo Pia Utakuta:
πŸ“– KUSOMA SIMULIZI
🎬 FILAMU na TAMTHILIA za KITANZANIA
πŸ˜‚ VIDEO za KUCHEKESHA
πŸ“‘ MAKALA za AFYA na MAPENZI

Install app hii GUSA HAPA utavipata vyote hivyo bure kabisa

JINA: UZOEFU
Mwandishi: Elisha Msafiri

SEHEMU YA TATU
ILIPOISHIA...
Nikataka kumkoromea juu ya hilo lakini isingesaidia kitu hasa ukizingatia sikio halizidi kichwa,Nilielekea chumbani kwangu muda huo huku machozi yakinilenga,sikumbuki kama kabla ya siku hiyo nilishawahi kupokea habari mbaya namna hiyo.

SASA ENDELEA...
Hadi muda huo nilikuwa bado na uwezo wa kwenda kwao Lisa na kumuaga.Lakini nilisita kufanya hivyo,nilivuta picha jinsi ambavyo Lisa angeipokea habari hiyo kwa masikitiko tele na huzuni kuu.Nikajikuta nakosa ujasiri wa kwenda kusimama mbele ya msichana mzuri kama Lisa kisha mdomo wangu kufunguka na kutamka maneno ambayo yangemtoa chozi,naam sikupenda kumuona Lisa akihuzunika na kulia mbele yangu.

Nikaamua nitaondoka bila kumuaga japo nilijua kuwa angeumia sana baadae akijua lakini maumivu yake yasingekuwa makubwa kama ningeenda kumwambia mimi mwenyewe.

Kama mimi mwenyewe mwanaume nimehuzunika na kughafilika kiasi hiki vipi kuhusu yeye mtoto wa kike?

Yale niliyoambiwa siku iliyopita na kuyachukulia kama ndoto.Hatimaye alfajiri siku iliyofuata ile ndoto ikawa kweli.

Mapema kabla ya mapambazuko ilikuja gari kubwa na kisha kupakia vitu kadhaa huku vingine baba akiahidi kuvinunulia huko huko Dar es salaam.Zoezi la kupaki vitu halikuchukua nusu saa kutokana na uhodari wa wapakiaji.Sisi nasi tulipanda kwenye gari ndogo kisha safari ya kuelekea jijini Dar es salaam ikaanza.

Kwa mara ya kwanza chozi lilinidondoka kwajili ya Lisa,niliposoma kibao kilichoandikwa KWAHERI TABORA.maandishi niliyoweza kuyasoma kutokana na kibao hicho kumulikwa na taa za gari.Japo paliandikwa Kwaheri Tabora na macho yangu kusoma hivyo lakini moyo wangu ulikuwa tofauti kidogo wenyewe ulisoma kwaheri Lisa.

Nitamuona tena lini Lisa? hilo ni swali lililouchafya ubongo wangu na kunipa maumivu ya kichwa ambapo hata hedex hazikunifaa kitu.

Hatimaye tulifika Dar salama salimini japo maumivu bado yalisalia kumtima sikuwa na budi kuikubali hali hiyo na kuzoea maisha hayo mapya bila Lisa.

Hata pawe na shida kubwa namna gani tumaini huwa halikosekani.Ingawa nilikuwa nimetengana na Lisa,bado nilikuwa na tumaini la kumuona tena.Je nitamuona vipi? hilo lilikuwa ni swali rahisi sana.Matokeo yangu ya Darasa la saba ndio ilikuwa muhimili wangu mkuu wa kumuona tena Lisa.

Nilikuwa nikimuomba Mungu usiku na mchana kuchaguliwa kujiunga na shule za Sekondari zilizopo palepale Tabora.Sala ambazo niliamini Mungu amezisikia na atanijibu.

Hadi muda huo nilikuwa nimeshaweza kuwashawishi baba na mama kuwa iwapo matokeo yangetoka basi ningerudi kusoma Tabora na wao walionekana kuniekewa hasa ukizingatia kuwa mji huo kulikuwa na ndugu zetu wengi.

Muda ukaenda na masaa yakasogea.Hatimaye ule msemo usemao kuwa Binadamu wanapanga na Mungu anapanga ukatimia kwangu.Kwani licha ya kupanga kwangu kurudi tena Tabora kwa gea ya kusoma na kujiandaa kwa hilo.Mungu hakupanga hivyo,Alipanga nikasomee Moshi.

Naam,matokeo niliyoyasubiri kwa ghamu na hamu yanikomboe.Yakanipiga tena teke,teke lililokuwa na maumivu makuu kuliko yale ya kwanza.Ama kweli ukitegemea kwendmbele hatua mbili na usiende basi unaweza kurudi nyuma hatua kumi.ndicho kilichonikuta na safari hii sikutaka tena kuumia moyo hivyo sikujiwekea mpango wowote ule wa kuonana na Lisa.

Ingawa mtoto akifaulu nnje ya mkoa huwa ni sifa kubwa kwa familia yake na heshima kwake pia lakini wazazi wangu walishangaa kuniona bado sina raha.Nini kinachonisibu? jibu lilibaki moyoni mwangu.

Hatimaye muda wa kwenda shule ulifika.Na mimi nikaelekea Mkoani kilimamjaro kwajili ya masomo yangu.Mji niliouona kama gereza huku shule nikiiona kama selo halikazalika walimu sikuwatofautisha hata kidogo na askari magereza,naam vyote hivyo niliviona katika mtazamo huo kwa kuwa vilikuwa vimenitenganisha na Lisa.Kipenzi cha moyo wangu,japo alikuwa maili nyingi na upeo wa macho yangu lakini daima aliishi moyoni mwangu.

Miaka minne ambayo ningesoma shuleni hapo kwangu ilikuwa kama miaka minne ya kifungo changu katika jela ya mapenzi jela ya kutomuona Lisa.

Nakumbuka siku moja katika kipindi cha likizo nilipokuwa nyumbani Dar es saalam alikuja ndugu yetu mmoja toka Tabora.Ndugu huyu ndiye aliyeamsha tena hamasa ya mimi kutaka kuweka mipango upya ya kurudi Tabora.

Katika mazungumzo yetu mafupi niliweza kumdodosa juu ya habari za Lisa naye bila hiyana hakunificha jambo,alinieleza jinsi Lisa alivyokuwa na kunawiri mara elfu.Kichwani mwangu nilijaribu kuivuta picha lakini haikuja,naam ilitakiwa tena mimi niende kwa miguu yangu mwenyewe ili nimuone Lisa kwa jicho langu mwenyewe.

Tangu hapo nilishi nikiisubiri kwa hamu ifike tena siku ya kurudi Tabora.

Kama ilivyo kwa siku hazigandi ndivyo ilivyo kwa masaa yanavyosogea,Hatimaye nilimaliza kifungo changu cha miaka minne mkoani Kilimanjaro na sikutaka kubaki jijini Dar es salaam sasa nilikuwa mjini Tabora.Mji wa ahadi ya moyo wangu kuwa nitarudi tena kwajili ya Lisa,kipenzi cha moyo wangu.

"Tom!....Tom!..wee Tom?" Sauti hiyo ya Mama mdogo ndiyo iliyonitoa katika dunia ya kumbukumbu nzito zilizopita kichwani mwangu kama movie na kuniacha nimeduwaa.

"Namalizia mamdogo nakuja!" niliongea kwa sauti isiyosikika vizuri kutokana na uwepo wa mswaki kinywani mwangu kisha nikaongeza juhudi za mkono kumalizia kibarua hicho kilichonichukua dakika chungu mzima.

Baada ya kumaliza kusafisha kinywa nilielekea moja kwa moja hadi chumba cha chakula (dining room).Hapa nilikuta mamdogo kaandaa chai nzuri ya maziwa pamoja na chapati za kumimina,Tukaendelea kunywa chai huku mamdogo akinipigia hadithi kadha wa kadha za mji huo tangu tulipouhama.

Nani kaondoka!,nani kaja!,nani kaolewa!,nani kaoa!,nani kafilisika!,nani katajirika,nani mzima na nani kaukwaa!,Hadithi zote hizo za uongo na kweli mamdogo alinisimulia bila kubakiza neno.Masikini,Mamdogo pamoja na kukazana kwake kunisimulia hakuna lililokuwa likiniingia kichwani,japo nilikuwa nikimsikia akiongea,sikuwa naelewa haswa anasema nini,Akili yangu haikuwa pale,nilikuwa nikimuwaza sana Lisa na kitendo cha kuiona nyumba yao nilikuwa kama vile nimejiloga mwenyewe.

Japo nilijitahidi kumsikiliza mamdogo kwa makini,hakuna nililokuwa nikiambulia na mara nyingi nilikuwa nikiitika itika,kumaanisha kuwa arudie alichosema hali iliyomfanya abaini kuwa hatuko pamoja.

Kadri muda ulivyozidi kwenda kuna jambo niligundua.Niligundua mamdogo ameanza kununa,labda alihisi kuwa namdharau kwa yale anayosema.Kumbe mimi masikini ya Mungu nilijitahidi kweli kuenendananaye lakini fikra zikanizidi nguvu.

Heri nusu shari kuliko shari kamili.Ingawa mamdogo alikuwa ameshaanza kununa,sikutaka anune kamili.Na ili asinune kabisa ilikuwa ni lazima nimuonyeshe ushirikiano wa hali ya juu kwa kile anachosimulia.

"Enhee!..hivi mzee Shaka yupo kweli!?" Hatimaye nilimuuliza swali mamdogo ambapo nilijua majibu yake yatanifanya nimsikilize kwa makini.Mzee Shaka ndiye baba yake na Lisa.Mamdogo hakushangaa hata kidogo mimi kumuulizia mzee huyo kwani alikuwa ni moja kati ya watu maarufu mtaani hapo haswa kutokana na umashuhuri wa biashara zake.

Taratibu mamdogo alianza kunipa habari (Michapo) ya mzee huyo, habari zilizoniwia tamu zaidi ya sukari niliyoweka kwenye chai ya maziwa ambayo nilikuwa nikiinywa muda huo.Na mamdogo hakuweza kujua kuwa janja yangu ilikuwa ni kuanzia kwa baba kuelekea kwa mwana.

"Mmhh hivi na yule mtoto wake wa kike yupo kweli...anaitwa nani vilee!?" Hatimaye nilifikia nilipopataka na nikamuuliza swali hilo kiujanja nikijifanya simjui Lisa jina ili kumpoteza mamdogo maboyaa.

"Nani Lisa!?!" Mamdogo naye alinijibu kwa namna ya kuuliza na mimi nikaitika kama vile sina uhakika.Laiti angejua jina hilo lilivyonikaa kichwani wala hata asingehangaika kunijibu.

"Ah jamani alivyokuwa rafiki yako vilee umemsahau na jina!" 

Hatimaye mamdogo alinishushua bila yeye mwenyewe kujua.Ama kweli duniani hamna siri hadi mamdogo aliujua urafiki wangu na Lisa! Nilijiwazia moyoni mwangu huku nikiona haya kiasi kutokana na kushushuliwa.

"Lisa yupo,amekuwa mzuri huyoo sema siku hizi anasomea Moshi!"

"Arrghhh!!" Nilijikuta nimeghafilika ghafla na kushindwa kujizuia,niliitandika meza ngumi kali ali manusura nimwage chai yote.Nikamwacha mamdogo katika hali ya sintofahamu na mshangao wa hali ya juu.Na bahati nzuri meza ile ilitengenezwa kwa mbao imara ya mninga la sivyo ingevunjwa kwa konde lile.

"Khaa vipi tena!?" Hatimaye mamdogo aliniuliza kwa kifupi huku sura yake ikionyesha kuwa ana swali refu.

"Aaah samahani mama unajua ulivyonitajia Moshi,nimekumbuka na mimi nimesahau leaving certificate (cheti cha kuhitimu) yangu shule! Yaani hata sijui itakuwaje maana baba alinisisitiza sana nisiiache!" 

Nilijikuta nime jitetea kwa maneno mengi ya uongo ambayo hata sikujua nimeyatoa wapi,mamdogo akaungana na mimi katika hali ya kusikitika huku akijaribu kinishauri njia za kuweza kukipata.Masikini hakujua,usilolijua litakusumbua.

Mimi kwa wakati huo nilikuwa nikimuwaza Lisa tu.Yaani nimejitahidi kung'ang'ana na kulazimisha safari hii ili nije nimuone kipenzi cha moyo wangu Lisa alafu leo hii naambiwa yupo Moshi.

Mji ambao nilikuwa nikiwaza usiku na mchana nitaondoka lini ili nirudi Tabora,nije nimuone mpenzi wangu.Kumbe mji huo nilioukimbia ndio uliokuwa ukimuhifadhi mpenzi wangu.

Ama kwa hakika ilikuwa ni habari mbaya kwangu sikuwa na tofauti na mtu aliyeitupa almasi na kufwata kipande cha chupa kinachong'ara juani.Na laiti kama nisingeipiga meza ile kupoza hasira yangu iliyonikaba koo ghafla huenda hasira hiyo ingeniua usiku usingizini.

Hadi kufikia muda huo si chapati laini za kumimina tu bali hata chai niliyokuwa nakunywa haikuwezs kupita tena kooni.

"Mamdogo asante sana kwa chai!"
"Ah jamani malizia hiyo iliyobaki bwana!"
"Yaani mama nimeshiba kweli ntakunywa tena badae!" Nilijaribu kumshawishi mamdogo lakini hakunielewa ikabidi niimalizie ile chai iliyobaki nikiwa nimekunja sura mithili ya mtu anayekunywa pombe kali.

"Sasa mama mie nataka niusabahi mtaa kidogo unajua siku nyingi sana nimeondoka!" Hatimaye niliaga na kukubaliwa kutoka kwa sharti la kuwahi kurudi.

Nilitembea kwa haraka kuelekea kwa kina Lisa.Sikujali ningemkuta nani huko lakini kitu pekee nilichojali muda huo ni kupata habari kamili za Lisa,Kwani si ndicho kilichonileta mji huo!?.

Nilipiga hatua za haraka haraka hadi nilipofikia geti na kugonga mlango.Niliugonga mlango kama mara tatu hivi kwa mkupuo kisha nikasimama pembeni kusubiri ni nani atakayekuja kunifungulia.Ingawa nilisimama imara lakini kamoyo kalidunda dunda,Ukweni si parahisi hata kidogo haswa kama hujapata uhakika.

Nikiwa bado nawaza hiki na kile nilisikia hatua za mtu kuja hapo getini nilipo.Nikaweka sawa kola ya shati yangu kisha nikajitazama tena muonekano wangu juu mpaka chini,naam,nilikuwa vizuri na baada ya kujirizia nilikohoa kidogo kusafisha koo langu tayari kwa mazungumzo na huyo anayekuja.

"Habari yako!?" Baada ya mlango kufunguliwa kilitokeza kichwa cha binti mmoja ambaye hakuruhusu mlango kufunguka wote.Alinisalimia na kunitzama kwa makini binti yule ambaye kwa mtazamo wangu wa haraka nilihisi atakuwa mfanyakazi wa ndani (housegirl) ama ndugu yao kutoka kijijini.

"Safi!...Mzee nimemkuta!?" Huwa sinaga nidhamu ya uoga mbele ya watu wenye wasiwasi kama yeye.Nilijibu salam yake kwa kujiamini ni sikutaka aniulize shida yangu moja kwa moja nikamuulizia baba mwenye nyumba kama vile nilikuwa namtafuta kwa udi na uvumba lakini rohoni mwangu nilipiga dua ya kimya kimya asiwepo.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA KWENYE APPLICATION YETU HIVYO UKIYAONA NAOMBA BONYEZA HAPO NDIO UNANIPA SAPOTI MIMI, UKIBONYEZA UNAWEZA KUCANCEL SIO LAZIMA UENDELE ULIKOPELEKWA, KIKUBWA UBONYEZE HATA MARA 2-3 KILA UKIFUNGUA APP YETU

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

TAZAMA KICHEKESHO HIKI KISHA BONYEZA SUBSCRIBE ILIYOPO CHINI YAKE WAKATI TUKIELEKEA KWENYE MUENDELEZO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni