KUTI KAVU (11) - CnZ Media

CnZ Media

Jisomee Simulizi Mpya Kila Siku

Alhamisi, 9 Februari 2023

KUTI KAVU (11)

Je unajua kwamba Simulizi zote unazozipata hapa zipo kwenye app ya CnZ Media?

Humo Pia Utakuta:
๐Ÿ“– KUSOMA SIMULIZI
๐ŸŽฌ FILAMU na TAMTHILIA za KITANZANIA
๐Ÿ˜‚ VIDEO za KUCHEKESHA
๐Ÿ“‘ MAKALA za AFYA na MAPENZI

Install app hii GUSA HAPA utavipata vyote hivyo bure kabisa

Jina: KUTI KAVU

SEHEMU YA KUMI NA MOJA
ILIPOISHIA...
Alijiinua kutoka katika mkao wake ule, na safari hii alijiegemeza kwenye mgongo wa kiti halafu akaendelea, “…. Ilikuwa ni wakati ambao nilikuwa mahakama ya mwanzo ya Temeke kwenye mafunzo kwa vitendo. Mara tu baada ya shughuli za mahakama kuisha, nilielekea kwenye kituo cha daladala tayari kuelekea nyumbani kwa mapumziko.

WAKATI UNAFUNGUA KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE WALAU KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
KAMA UPO NJE YA APP INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KWA WAKATI

SASA ENDELEA...
Watu walikuwa ni wengi sana kituoni na kusababisha kila gari lilokuja pale kuonekana lulu machoni pa wasafiri kwa sababu ya mahitaji yao ya huduma ya usafiri. Yalikuja magari kadhaa kituoni, lakini yote yalikuwa yamejaa kiasi cha kutokuwa hata na nafasi ya kusimamisha abiria ndani yake. Nilikaa pale kituoni nikiendelea kusubiri gari lenye nafasi angalau ya kusimama ili niwahi nyumbani nikapumzike. Ikawa kama nilivyotarajia. Lilikuja gari aina ya Toyota Coaster likiwa na abiria wachache, nikajitoma ndani.

Humo nilielekea mpaka kwenye siti za upande wa kulia, siti ambazo huwa na viti maaalum kwa ajili ya abiria wawili, nikakaaa kwenye siti ya dirishani, siti ambayo ilifuatia baada ya siti ya nyuma, ambayo hukaliwa na abiria wanne na pengine hata watano kutokana na shida ya usafiri iliyopo.

Nikiwa nimekaa pale kwenye siti, alikuja dada mmoja mrefu wa wastani, ambaye ama hakika alikuwa ni mrembo wa haja! Alikuwa ndani ya gauni refu la rangi ya kijani iliyochanganyika na weusi. Gauni lile aina ya dila lilimfanya mrembo yule avutie, nami nikavutika naye.

Nilitamani akae kwenye siti niliyopo, ikawa kama vile aliyasoma mawazo yangu. Alikuja tukajumuika naye kwenye siti ile, “Mungu anipe nini tena!” nilijisemea.

Wakati pua zangu zikipokea burudani ya manukato mazuri aliyojipulizia mrembo yule, mara masikio yangu yakajiwa na sauti yake laini, “Habari yako kaka?”

“Salama tu, sijui wewe?” nilimjibu na kumtaka hali, lengo likiwa ni kuziteka hisia zake.

“Njema tu,” alijibu huku akijaribu kujiweka sawa pale kitini tulipokuwa. Wakati huo gari lilikuwa katika mwendo kwa safari ya kuelekea Mbagala na vitongoji vyake na mwiso wake ulitarajiwa kuwa Mbagala Rangi tatu.

Shauku ya kutaka kuendeleza mazungumzo na mrembo yule ikazidi kuzitwaa fikra zangu, niligeuka na kumtizama kwa mara nyingine.

Naweza kusema safari hii uzuri wake uliongezeka maradufu. Wakati bado naendelea kumtizama, wasiwasi ambao sijui ulikotokea uliuvamia moyo wangu na kuyabadiri mapigo yake kutoka kwenye mwendo wa kawaida na kuufanya udunde kwa kasi zaidi.

Alikuwa pilikani huku mkono wake mmoja ukiwa ndani ya mkoba na mwingine uliobaki ulikuwa umeshikilia mkoba aliokuwa nao. Punde mkono uliokuwa ndani ya mkoba uliibuka na ‘Earphone’ ambazo alizichomeka kwenye simu yake ya mkononi aliyokuwa nayo na baadaye aliziweka zile Earphone kwenye Masikio yake kisha akaruhusu muziki ucheze kutokea kwenye simu yake.

Nadhani haikuwa kama alivyopanga, kwani badala ya muziki kusikika kupitia kwenye zile spika ndogo alizoweka masikioni mwake, ulisikika kupitia spika ya simu! Licha ya sauti kusikika kupitia spika ya simu, sauti ile haikuweza kuvuka mipaka ya eneo tulilopo, kwa maana ya kusikika na watu walio nyuma au mbele yetu isipokuwa mimi na yeye.

Naam, ulikuwa ni wimbo wa ‘hero’ ulioimbwa na Enrique Egliasis.

Kitendo kile cha mambo kwenda kinyume na matarajio yake kilimfanya mrembo yule ahisi kupatwa na aibu, mara ghafla akaanza kuhangaika kuusimamisha muziki uliokuwa ukiendelea kusikika kupita spika za simu. Niliushika mkono wake kama ishara ya kumzuia asifanye alichokusudia huku nikifuatisha baadhi ya mashairi ya wimbo ule, “… I can be your hero…. Now I stand by you forever….” Aligeuka kunitazama na mara macho yetu yalipokutana aliachia tabasamu pana lililozidi kuukonga mtima wangu.

“Who is the lucky guy?” nilimuuliza lakini hakujibu chochote zaidi ya kuchanua tena tabasamu lililozidi kumpamba na kumfanya aonekane mrembo zaidi, hasa kwa vile vijishimo vilivyojiunda mashavui mwake ‘Dimpozi’.

Sikuishia pale, nilimuuliza tena, lakini safari hii kwa lugha ya Kiswahili, “Ni nani mwenye bahati?”

“Una maana gani?” aliuliza.

“Namaanisha kuwa; ni nani huyo mwenye bahati ya kuwa na mrembo kama wewe?”

Hakujibu kitu, alizidi kutabasamu huku wimbo ule wa ‘hero’ ukiendelea kucheza kwenye simu yake.

Sikuona sababu ya kumlazia damu, nikaendelea, “Naitwa Dominic Masaka. Ila wengi hulifupisha jina langu kwa kuniita Domi. Je wewe mwenzangu waitwa nani?”

“Naitwa Doi,” alijibu.

“Sabasaba wa kushuka, sabasabaa..” sauti ya tandiboi ilisikika kuwakumbusha watu vituo wanavyopaswa kushukia ili wasije wakavushwa kwenye vituo husika.

Ni sauti hiyo ya konda ndiyo iliyonikumbusha kuwa ndani ya muda mfupi ujao tutatenganishwa na Doi.

Japo safari yangu ilikuwa bado ni ndefu, sikutaka kujiaminisha kuwa angedumu kwenye gari lile mpaka nitakapokuwa tayari kushuka baada ya kuwa nimefika. “Yawezekana akashuka kituo kinachofuata.” Niliwaza.

Nikaona ule ndiyo wasaa pekee nilionao, wasaa wa kuandaa mazingira yatakayonifanya nizidi kuonana na Doi. Sikutaka kushuhudia nikipotezana na mrembo yule katika hali ya uzembe namna ile. “Sina budi kufanya jambo....” niliwaza.

Nilimtazama tena Doi ambaye alikuwa ametulia kimya, sijui kama alikuwa amezama kufuatilia mashairi ya wimbo ule ama lah!

“Doi,” nilimuita.

Aliitika na kunitazama, tukawa tunatazamana kwa hisia tofauti. Wakati nafikiria maneno mwafaka ya kuzungumza kwake, yeye alikuwa makini akisubiri nimueleze sababu ya kumuita.

“Nisingependa kuona kuwa, huu unakuwa mwisho wa mimi na wewe kuonana. Natamani tukutane tena na tena,”

“Mh!” aliguna na kubetua mabega yake juu kisha akasema, “Unaenda kwenu… sijui kwako, nami naenda kwetu, ni vipi tutaonana tena?”

“Ipo namna Doi,”

“Namna ipi hiyo?”

“Nipe namba yako ya simu na wewe uchukue yangu.” Nilisema.

“Lakini….” Alisita kidogo kabla hajaniuliza, “kuna nini cha mno?”

Swali lake lilikuwa gumu kwa mimi kulijibu ghfla. Nilituliza akili yangu, nikafikiri kwa nidhamu kisha nikasema, “Maisha yana namna ya ajabu sana Doi, leo tumekutana kwenye daladala kama wasafiri. Huwezi jua kesho tutakutana wapi tukiwa katika hali gani… tafadhali tubadilishane namba zetu za simu”

Ombi langu la namba ya simu kwa Doi lilikubaliwa, tukabadilishana namba. Wakati huo gari lilikuwa limekaribia kizuiani, kondakta aliwakumbusha tena abiria wake wanaoshukia kizuiani wajiandae.

Doi alikuwa ni mmoja wao. Tuliagana huku akijiandaa kushuka na mara gari lilipofika Kizuiani alishuka sanjari na abiria wengine ambao walikuwemo garini.

Baada ya gari kuwa limewashusha watu kizuiani liliendelea na safari yake na lilipofika Zakhem nilishuka na kuliacha gari likiendelea na safari yake ya kuelekea Rangi tatu. Hiyo ikawa ni siku ya kwanza.

Utitiri wa majukumu ulinifanya nitingwe na shughuli kwa muda mwingi. Licha ya kujitahidi kuyapunguza kwa bidii kubwa, majukumu hayo hayakuisha. Wingi huo wa shughuli ulinifanya nikamsahau kabisa Doi. Siku ile iliisha bila kumbukumbu yoyote kuhusu Doi akilini mwangu!

Siku iliyofuata nayo iliisha, na siku nyingine tena hatimaye wiki ya kwanza, ya pili na ya tatu. Mwezi ukaisha bila kumkumbuka Doi kwa namna yoyote ile.

Kwa kuwa likizo yangu ilikuwa ikielekea ukingoni, nilianza kufanya maandalizi kwa ajili safari yangu ya kurejea chuoni Iringa ambako nilikuwa nikisoma.

Siku moja jioni, yapata majira kama ya saa 12 hivi, nilikuwa nimejipumzisha chumbani kwangu huku nikichezea simu yangu kwenye orodha ya majina. Nilianza na majina yanayoanza na herufi ‘A’, yalipoisha niliingia kwenye herufi ‘B’, ‘C’ na baadaye ‘D’ ambapo nilipitia jina moja baada ya jingine, mpaka nilipofika kwenye jina lililonikumbusha siku kadhaa nyuma. Nilikumbuka siku ile nilipokutana na Doi kwa mara ya kwanza kwenye daladala.

Sura ya Doi ilinirejea akilini. Uzuri wa sura yake pamoja na sauti vilinifanya nipatwe na pumbao pale kitandani nilipokuwa. Shauku ya kutaka kuisikia tena sauti ya Doi ikanijia, hamu ya kutaka kumtia tena machoni pangu ikanivaa, nikaamua kumpigia simu ili kumshawishi tuonane kabla likizo yangu haijasha na kurejea chuoni, Iringa.

uWakati najiandaa kubonyeza kitufe cha kijani, ambacho ni kitufe cha kupigia simu, mara mtetemo ukasikika kwenye simu yangu ukifuatiwa na mlio ulioashiria kuwa kuna ujumbe mfupi wa maandishi umeingia. Niliupuuza ujumbe ule kwa lengo la kutimiza kwanza jambo nililolikusudia, kumpigia Doi simu.

Nilibonyeza kitufe cha kijani na mara simu ya Doi ikaanza kuita.

Mapigo ya moyo wangu yalianza kwenda mbio sambamba na msululu wa maswali ambayo nilihisi ningekumbana nayo baada ya kuwa amepokea simu. Kwanza; niliomba namba yake ya nini, ikiwa sikuwa na umuhimu nayo? Pili; nina lipi la kumueleza, ikiwa ni mwezi sasa tangu niichukue namba yake. Nimekumbuka nini?

Wakati bado nasumbuliwa na msululu huo wa maswali, mara sauti ikasikika, “Hallow….” hakika ilikuwa ni sauti yake, “Hallow Doi, mambo?” nilijibu na kumjulia hali kwa kumsalimia.

“Safi tu, za siku?”

“Salama wangu, wajionaje na hali?”

“Kwema tu, ina maana nisingekutumia huo ujumbe ndiyo ingekuwa jiii…?” Doi aliuliza kwa sauti iliyojaa mzaha, na hapo ndiyo nikajua kuwa, kumbe ule ujumbe mfupi ulioingia ameutuma yeye! Mara ghafla nikapatwa na hangaiko la akili. Shauku ya kutaka kujua ameandika nini kwenye ujumbe alioutuma ikauvaa moyo wangu. Nikajaribu kubashiri kile alichokiandika bila mafanikio na wakati huohuo sauti yake laini iliendelea kunishitaki. Nikajitetea.

“Hapana Doi…. Siyo hivyo….” Kabla sijamaliza kauli yangu aliuliza, “kumbe je?”

Ilinibidi nianze kujitetea, “Nilitingwa na majukumu wangu, na siku zote nimekuwa nikiutafuta wasaa wa kuzungumza na wewe bila mafanikio. Najua huwezi kuniamini nikisema kuwa hata huo ujumbe ulioutuma sijausoma kwa sababu umeingia nikiwa nimekwisha ruhusu simu ije kwako,”

“Unasema kweli Domi?” Doi aliuliza.

“Kwa nini nikudanganye?” nikalijibu swali lake kwa kumuuliza swali jingine.

“Nhuu.. Basi makubwa hayo! Ina maana unataka kuniambia kuwa umenikumbuka wakati ambao mimi nimekukumbuka?” aliuliza.

Kwa haraka sikujua nimjibu nini. Nilijitahidi niendelee kubaki kwenye mhimili wa staha ili niongee naye kwa uwekevu, lakini haikuwezekana. Nilijikuta nimetamka, “Haswaa…”

“Kwa nini?” aliuliza tena.

“Nahisi kuna kitu kati yetu Doi…. Kuna kitu”

Nilitarajia aseme neno baada ya mimi kusema hayo lakini haikuwa, Doi alikuwa kimya!

Sikutaka kuruhusu ukimya ule ushike hatamu kati yetu. Hivyo baada ya yeye kuwa kimya niliamua kumuuliza, “Samahani Doi, tunaweza kuonana kabla wiki hii haijaisha?”

“Tunaweza. Lakini iwe weekend,”

“Haina shida, nadhani Jumamosi itakuwa ni siku nzuri”

Tulikubaliana kuwa tuonane siku ya Jumamosi, tukapanga mahali na muda. Hiyo ikawa ni siku ya pili.

USIIKOSE SIMULIZI INAYOFUATA

Kama Una Channel Youtube Haupati Watazamaji Karibu Tuzisambaze Video Zako, Utagharamia Tsh 10 kwa Kila View(Mtazamaji) 1
Wasiliana Nami Kwa WhatsApp +255718274413

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni