KUTI KAVU (12) - CnZ Media

CnZ Media

Jisomee Simulizi Mpya Kila Siku

Alhamisi, 9 Februari 2023

KUTI KAVU (12)

Je unajua kwamba Simulizi zote unazozipata hapa zipo kwenye app ya CnZ Media?

Humo Pia Utakuta:
๐Ÿ“– KUSOMA SIMULIZI
๐ŸŽฌ FILAMU na TAMTHILIA za KITANZANIA
๐Ÿ˜‚ VIDEO za KUCHEKESHA
๐Ÿ“‘ MAKALA za AFYA na MAPENZI

Install app hii GUSA HAPA utavipata vyote hivyo bure kabisa

Jina: KUTI KAVU

SEHEMU YA KUMI NA MBILI
ILIPOISHIA...
Sikutaka kuruhusu ukimya ule ushike hatamu kati yetu. Hivyo baada ya yeye kuwa kimya niliamua kumuuliza, “Samahani Doi, tunaweza kuonana kabla wiki hii haijaisha?”

“Tunaweza. Lakini iwe weekend,”

“Haina shida, nadhani Jumamosi itakuwa ni siku nzuri”

Tulikubaliana kuwa tuonane siku ya Jumamosi, tukapanga mahali na muda. Hiyo ikawa ni siku ya pili.

WAKATI UNAFUNGUA KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE WALAU KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
KAMA UPO NJE YA APP INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KWA WAKATI

SASA ENDELEA...
Siku ya Jumamosi ilifika. Niliamua kuelekea maeneo ya fukwe za Coco saa moja kabla ya muda wa miadi ambao tulikuwa tumekubaliana na Doi haujafika. Lengo la kuwahi eneo lile lilikua ni kwa ajili ya kuandaa sehemu nzuri katika ufukwe ule, ili tuwe na faragha katika mazungumzo yetu. Sababu nyingine ilikuwa ni kuepuka uswahili wa kutokulinda muda, hasa zaidi ukizingatia ile ilikuwa ni siku ya kwanza kuonana na Doi baada ya kuwa tumepanga miadi.

Niliwasili Coco majira ya saa 6:00 mchana kwa usafiri wa Bhajaji, nilishuka na kumlipa dereva ujira wake. Niliangaza kushoto na kulia katika ufukwe ule, watu walikuwa wamesheheni kila upande… naweza kusema tangu nianze kuhudhuria kwenye ufukwe ule, siku hiyo idadi ya watu ilikuwa ni kubwa kuliko siku nyingine zote nilizowahi kuhudhuria eneo lile.

Taratibu nilianza kupiga hatua kuelekea upande wa kulia, upande ambao niliamini ninaweza kupata mahali ambapo pangetupa faragha.

Nikiwa katika hatua ya tatu tangu nilipokata shauri kuelekea upande wa kulia, alikuja mtu nyuma yangu na kuniziba macho kwa viganja vya mikono yake. Sikuweza kujua ni nani kwa sababu; moja, sikutarajia kukutana na mtu ninayefahamiana naye mahali pale kwa sababu, marafiki zangu karibia wote si wapenzi wa maeneo kama haya. Mbili, ni kweli nilikuwa nimeahidiana na Doi kuwa tuonane naye mahali pale, lakini akili yangu haikunituma kuamini kuwa huyo angekuwa ni Doi kwa sababu muda wa miadi yetu ambao ulikuwa saa moja mbele ulikuwa haujafika. Ni nani sasa awezaye kufanya mzaha wa namna hii?

Shauku ya kutaka kumjua ikanizidi moyoni! Niliunyoosha mkono wangu wa kulia kuelekea nyuma, kule alikosimama aliyeniziba macho kwa viganja vyake. Wakati naunyoosha mkono ule wa kulia yeye alihama na kuelekea kushoto, wakati naunyoosha wa kushoto alihama tena na kurudi upande wa kulia, nikawa sina jinsi.

Ulaini wa mikono iliyoyaziba macho yangu sanjari na uzuri wa manukato yaliyotuama kwenye pua zangu, vilinifanya kubashiri ni nani aliyeniziba macho baada ya kuwa njia niliyodhani ingenisaidia kumtambua kushindikana. Nilipiga upatu wangu kwa kulitaja jina la Doi huku akili yangu ikijiandaa kukabiliana na aibu ambayo ingenipata endapo jina nililolitaja si la yule niliyedhani kuwa ndiye.

Mara baada ya kulitaja jina Doi, ile mikono iliyaacha macho yangu huru. Kile kitendo cha viganja vilivyoyaziba macho yangu kuyaacha huru kilifuatiwa na sauti ya kicheko ambacho kilinifanya nitambue fika kuwa aliyeniziba macho yangu alikuwa ni Doi.

Niligeuka kumtizama, naam, alikuwa ni yeye!

“Doi!” nilijikuta nimelitaja tena jina hili baada ya kuwa nimemuona Doi akiwa amesimama mbele yangu. Alikuwa amejifunga kikoi kilichouufunika mwili wake tangu kiunoni mpaka sehemu ya juu kidogo ya magoti na juu alikuwa amevaa kijiblauzi cha kubana kilichoyaziba matiti yake tu, na kuiacha sehemu kubwa ya tumbo lake ikiwa nje!

Nilijisogeza kidogo kuelekea mahali alipokuwa, kasha nikaitanua mikono yangu naye akajibu mapigo kwa kujaa ndani ya mikono ile, tukawa tumekumbatiana!

Tukiwa katika hali ile ya kumbato, nilihisi mabadiriko yaliyoufanya mwili wangu kusisimka kwa namna ya pekee, namna ambayo siwezi kuieleza kwa misamiati ya lugha za binadamu, ulikuwa ni msisimko wa ajabu.

Kwa upande wa Doi, naye pumzi zake zilibadiri mwelekeo na hapo ndipo kikatokea kile ambacho sidhani kama kuna hata mmoja kati yetu alidhani kuwa kitatokea. Kwa pamoja sauti zilisikika zikitamka neno moja, “Nakupenda!”

Sikutaka kuyaamini masikio yangu kwa kile yalichokisikia, lakini ilinibidi kuamini baada ya kuisikia tene sauti ya Doi ikilirudia neno lile kwa sauti iliyosheheni mahaba, sauti yenye kusisitiza kile kilichotamkwa. Sauti ile laini ilisema, “Nakupenda Domi”

Sikuwa na la kusema zaidi ya kujibu, “Nakupenda pia Doi… nakupenda sana,”

Sikujua hasa ni lini na ni wapi ndimi zetu zilipata kufahamiana. Kwani mpaka wakati huo vinywa vyetu vilikuwa vimeumana huku ndimi zetu zikizungumza kwa lugha yao. Ilanza kama mzaha katika siku ile ya tatu.
****
Ukurasa wa kwanza wa mapenzi baina yetu ulifunguliwa katika siku ile ya tatu katika fukwe za Coco beach. Wasaa uliofuata ulikuwa ni wa kufahamiana juu ya taarifa zetu binafsi, ambapo aliniambia kuwa; yeye ni mtoto wa kwanza kwenye familia yao yenye watoto wawili, na mdogo wake anayemfuata ni wa jinsia ya kiume.

Elimu yake ya kidato cha nne haikumruhusu kuendelea zaidi na masomo baada ya kuwa amefeli vibaya kwenye mitihani yake ya taifa. Hivyo hakuwa na weledi wowote ambao ungemsaidia kupata ajira. Kwa sababu hiyo alilazimika kuwa nyumbani akisaidiana na wazazi wake shughuli za hapa na.

Likizo yangu ilipoisha nilielekea chuoni kumalizia ngwe ya mwisho ya masomo yangu ya shahada ya kwanza ya sheria. Na wakati wote ambao niliokuwa chuoni, mawasiliano baina yangu na Doi yaliendelea kupitia simu.

Maneno yake matamu yalinifanya niamini kuwa kuna pendo pevu baina yetu. Kwa sababu Doi alionesha wazi kuwa anayo nia ya dhati ya kuishi nami kama mwenzi wake baada ya kuniahidi kuwa yuko tayari kuishi nami katika hali yoyote ile ya maisha; yawe ya shida ama ya raha! Ni nani wa kuipinga ahadi adhimu kama hiyo?

Wingu zito la mapenzi likatanda juu yetu huku tukiendelea kuunganishwa kwa mawasiliano ya simu mpaka nilipomaliza masomo yangu na kurudi tena Dar es salaam.

Niliporudi Dar es salaam, Doi alihamia rasmi nyumbani kwangu licha ya pingamizi kutoka kwa nduguze.

Hali ya uchumi kwa upande wangu haikuwa njema, lakini hiyo haikutosha kuwa kikwazo cha Doi kunivumilia. Siku zote alinitia moyo… jambo lililonifanya nihisi kuwa na mimi ni miongoni mwa watu wapendwao chini ya jua.

Hapo niliielewa aina ya upendo wa Doi kwangu, japo sikuwa naelewa nini maana halisi ya mapenzi! Ikiwa tajiri na masikini wote wana nafasi ya kupendwa, nini hasa sababu ya upendo?

Nililewa kwa penzi Doi, nililewa hasa! Naweza kusema hiyo ni miongoni mwa sababu zilizonifanya niongeze bidii ya kutafuta kazi mara baada ya kuhitimu mafunzo yangu ya uwakili.

Nilitafuta kazi kwa muda mrefu bila mafanikio, hapo likanijia wazo la kutafuta ufadhili wa kuchapisha hadithi zangu katika makampuni mbalimbali yaliyojishughulisha na uchapishaji. Huko pia niliziandika barua nyingi bila kupata majibu huku ugumu wa maisha ukizidi kushika hatamu.

Katika kuyafanya yote haya, nilikuwa sambamba na Doi ambaye alinitia moyo na kunifariji kuwa nisikate tamaa kwani mafanikio yapo kwa ajili ya wale wayatafutao.

Maisha yalikuwa magumu, na hata ikafika mahali nikayaona machungu. Mara nyingi sana kula yetu ilikuwa ni ya shida. Usishangae nikikwambia kuwa kuna wakati siku iliisha bila kutia chochote mdomoni isipokuwa maji. Kama ujuavyo jiji hili huwezi kupata chochote kama huna pesa, cha bure ni hewa tu, labda na salamu mara mojamoja.

Maisha yaliendelea kwa matumaini kuwa; mafanikio yamo mbioni kuja. Niliamini hivyo kwa sababu alikuwepo wa kunifariji, yule ambaye nilimuona kama sehemu ya mwili wangu… kumbe lah! Doi alikuwa na hila.… Doi alikuwa na hilaa…” alisema Domi huku machozi yakimtoka.

Ilibidi Makeke achukue jukumu jipya, jukumu la kubembeleza Domi ambaye alikuwa hajiwezi kwa kilio.

“Nyamaza Dominic… wewe ni mwanaume jikaze. Ndivyo maisha yalivyo. Maisha yako katika uwili usiokwepeka. Kuna wakati wa furaha na wakati wa huzuni… jikaze Domi,” alisema Makeke.

Wakati Makeke na Domi wakiendelea na mazungumzo katika ofisi ile ndogo iliyopo nyumbani kwa Makeke, mke wa Makeke alibisha hodi akakaribishwa.

Alipoufungua mlango kuingia chumbani mule, sauti ya muziki kutoka sebuleni ilipenya na kuingia mule ofisini amabako kulikuwa kimya. Muziki ule ulisikika barabara masikioni mwa Domi na kumpa wakati mgumu zaidi kwa sababu mashairi ya wimbo uliosikika yaliendana kabisa na kile kilichomtekea. Ulikuwa ni wimbo wa Daz Nundaz, wimbo wa barua ambao ulisikika hivi:

“…..katika mahaba tulishazama dimbwini,

Lakini barua niliyopokea nashindwa hata kuamini,

Ua la moyo wangu halipo tena na mimi,

Barua hii shika mwenye usome,

Barua hii….”

Yalikuwa ni maneno yaliyouchoma moyo wake kama mkuki.

Mke wa Makeke aliwakaribisha chakula kisha akaondoka.
*****
SIKU ya Jumatatu, majira ya saa tatu asubuhi, Doi alikuwa amejikunyata katika moja ya vyumba vya mahabusu vilivyopo katika gereza la Keko. Alikuwa amejitenga peke yake akijaribu kutafakari hatma yake, kwani tangu afikishwe hapo gerezani hakuna hata mmoja kati ya watu aliowajua na aliyekuja kumjulia hali.

Akiwa katika lindi la mawazo, Doi alisikia sauti ikiliita jina lake, alinyanyua macho kuangalia kule sauti ilikotokea akamuona askari wa kike akiwa amesimama mlangoni huku akichezesha funguo zilizokuwa mkononi mwake.

Askari Yule aliyekuwa nadhifu ndani ya sare za jeshi la magereza, shati jeupe na sketi ya rangi ya ugoro alimuita, “Doi Vioja, kuna wageni wako”

Doi aliisikia vyema sauti ya askari yule, alitii kwa kusimamana kuelekea mlangoni alipokuwa amesimama yule askari huku akili yake ikiwa imetekwa na utitiri wa maswali.

Alijiuliza juu ya ugeni alioitiwa. Alijiuliza ni wageni gani hao ambao wamekuja kumjulia hali. “Watakuwa ni baba na mama” Doi aliwaza huku akichapua hatua kuelekea mahali alipokuwa amesimama askari ambaye alimpokea kwa kumfunga pingu, kisha akamtanguliza mbele kuelekea kule walipo wageni wake.
****
Koplo Mwalo Mlekwa, alikuwa ni binti wa umri wa miaka 28. Mrefu na mwenye umbo la wastani, mzuri wa sura na hodari katika kazi. Alikuwa ni wakala wa usalama wa taifa katika idara ya magereza, hasa zaidi magereza ya kike kwa sababu ya jinsia yake. Yeye ndiye aliyekuwa amekabidhiwa jukumu la kumlinda Doi, jukumu alilopewa na mkurugenzi wa usalama wa taifa kupitia kwa wakala aliye karibu yake kiutendaji katika idara ya magereza. Mwalo alipewa jukumu hilo kwa sababu ya imani kubwa waliyokuwa nayo waajiri wake hasa katika ufuatiliaji wa mambo nyeti.

Wakiwa kwenye korido ya gereza la Keko, wakielekea kwenye chumba cha mazungumzo, koplo Mwalo nyuma, na Doi akiwa mbele, koplo Mwalo aliuliza, “Unamfahamu vipi Makeke?”

Lilikuwa ni swali gumu sana kwa Doi, kwa sababu katika maisha yake hakuwahi kulisikia jina hilo la Makeke. Alijaribu kuvuta kumbukumbu zake ni wapi amewahi kulisikia ama kuliona bila mafanikio.

“Makeke?” Doi aliuliza baada ya kushindwa kulitambua jina hilo.

USIIKOSE SIMULIZI INAYOFUATA

Kama Una Channel Youtube Haupati Watazamaji Karibu Tuzisambaze Video Zako, Utagharamia Tsh 10 kwa Kila View(Mtazamaji) 1
Wasiliana Nami Kwa WhatsApp +255718274413

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni