SITOISAHAU FACEBOOK (18)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mwandishi: Emmy John Pearson
SEHEMU YA KUMI NA NANE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Alikuwa akikimbia kwa juhudi zote lakini hakuwa akikimbia bure kuna kitu ama mtu alikuwa anamfukuza.Nikajaribu kupiga kelele. RIP na mwenzake hawakunisikia.Maria alikuwa anakimbizwa na nyoka. Nyoka mkubwa alikuwaanang’ara sana. Nashangaa wenzangu hakumuona.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
Nikajikuta natimua mbio uchi. Na nilikuwa kitendo cha sekunde chache yule nyoka akavamia eneo lile. Sikushuhudia sana kilichowatokea wenzangu. Sasa nikaanza kuhangaika huku na huko katika pori hilo ambalo sikuwa nalifahamu.Mguu mmoja ukiwa umekufa ganzi. Ningeweza vipi kukimbia mbio ndefu. Isabela mimi nikaanguka chini. Sasa nikawa najivuta kama nyoka. Nalia kama mtoto. Sikuwa na uelewa bado kwa nini mguu wangu ulikufa ganzi. Lakini kumbukumbu za kuchomwa sindano ile kali zilikuwa kichwani mwangu.
Nikiwa bado sijapata jibu sahihi. Lile joka la maajabu sasa likatokeza mbele yangu. Mdomoni likiwa na kipande cha nyama. Nyama ile yenye namba 666.Nikajiinamia kwa uchungu. Nikafanya dua fupi. Nikajilaani kwa kila hatua ya maisha yangu niliyopitia. Nikatamani ningekuwa na nguvu niweze kutimua mbio. Lakini tayari nilikuwa nimelegea. Macho yakazidi kuhesabu hatua za yule nyoka kunifikia. Sijawahi kuona nyoka mkubwa kama huyu!!! Nakufa kwa kumezwa na nyoka. Inauma sana!!Joka likazidi kusogea!! Joka kuu likawa linatambaa!!!
Kabla joka halijanifikia. Lilibadilisha uelekeo. Ni kama kuna kitu lilikuwa limehisi. Likaanza kutambaa kuelekea upande mwingine.Joka linatoka mara sasa namuona John. John yule mpenzi wangu ambaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha pale chuoni.“John…John!!” nilianza kumuita. Sauti ilikuwa imekauka. Haikutoka.Joooooh!!! Nikajaribu tena, nikawa kama ninafanya mnong’ono. John akawa anaenda zake. Nikalia sana kuikosa nafasi hii hadimu ya kusikiwa na John!! Huenda angeweza kuwa msaada mkubwa kwangu.
Ubaridi ulipenya katika mwili wangu. Mwanzoni niliuhisi kuwa wa kawaida lakini baadaye nikahisi kama maumivu hivi. Nikajipapasa. Nilipoutazama mkono wangu ulikuwa na damu. Nikageuka kujitazama sehemu zangu za nyuma.Maajabu!! Nilikuwa na kovu kubwa sana!! Na palikuwa pamechimbika. He! Ina maana nilikatwa nyama yangu ya…..!! niliduwaa.Maumivu yakazidi. Na sasa giza likazidi kuchukua nafasi yake baada ya mbalamwezi kutoweka. Giza nene!! Hapo bado nilikuwa sijaweza kunyanyuka imara. Nikajaribu kujikunjua nisimame.
Maumivu makali katika makalio. Nikaanguka kama mzigo. Nilipoanguka palikuwa na kisu kipya, kikiwa na damu.Nikaendelea kulia. Sauti haitoki.!! Nilikuwa katika jaribio kuu maishani.Ikiwa bado sijaweza kusimama. Lile joka lililopotea njia sasa lilionekana tena. Safari hii lilikuwa linakuja kwangu tena.Bora nife!! Nilijiapiza. Sasa nikaanza kutambaa kumfuata huyo nyoka. Mkononi nikiwa na kisu ambacho nilikiokota, bila shaka ni kile kilichotumika kunikata nyama.
Nikawa natambaa kama joka lile linavyotambaa. Sikuwa naijua nia yangu. Lakini nilihisi ni vyema kufa kuliko mateso haya.Lile joka likazidi kunisogelea, macho yake makali yakiangaza huku na huko. Urefu wa joka lile la dhahabu likiwa na kipande cha nyama mdomoni ulinitia kwenye hofu. Nikajiuliza iwapo kisu changu kinaweza kupenya katika ngozi yake, nikajipuuza maana kisu changu kilikuwa kidogo sana. Nikasita kutambaa. Nikatulia tuli, huku nikiamini kuwa ni heri linimeze kistaarabu kuliko kunimeza likiwa na hasira baada ya mimi kujaribu kupambana nalo. Nikafumba macho nikakitupa kisu changu chini, nikajinyoosha tayari kwa kumezwa.
Haikuwa ndoto kwamba nikifumbua macho nikutane na mashuka yangu masafi ya kuvutia yakinibembeleza kulala badala yake nilipofumbua macho. Joka kuu hili hapa!!Ubaridi wake ukapenyeza sasa, lilikuwa juu ya mwili wangu, pumzi zikawa zinaniishia. Ndio ninamezwa au? Nilijiuliza.Nikaanza kugalagazwa kadri lilivyokuwa linajivuta. Sasa ile hamu ya kufa ikatoweka baada ya lile kovu langu makalioni kupatwa maumivu makali. Maumivu yaliyosimamisha misuli yangu. Nilipogeuka kujitazama nikakuta kuna mwiba umezama nikajivika ujasiri nikauchomoa. Sikuwa navutwa tena. Nilitazama mbele nikalishuhudia lile joka likienda zake.
Inamaana huyu nyoka hakuniona ama!! Nilitafakari. Nikashangaa.Damu zilikuwa zikinitoka tena, sasa haikuwa katika kovu tu, bali na sehemu nyingine. Lile joka lilikuwa limenivuta hadi katika mti wa miiba na ni hapo nilipojitonesha.Pori likatulia kimya, kimya kikawa kirefu sana. Nikawa nahisi kiu kikali. Lakini hapakuwa na maji. Usingizi ukanisaidia kuikwepa karaha hii. Nikasinzia.Mwanga wa jua ndio ulionishtua. Nikakurupuka. Ni uchi!! Nikajishangaa kisha nikawahi kujiziba lakini bahati mbaya hakuwepo ambaye alikuwa ananichungulia. Nilikuwa peke yangu katika pori lile.Hakuna mnyama, hakuna mmea ninaoufahamu, hakuna hata mdudu!! Lilikuwa pori la maajabu, pori la mateso makali kwa kiumbe hai.
Nilisimama wima, nikajisikia dhaifu sana lakini sikutakiwa kuendelea kuwa lelemama, nikiwa nachechemea nilianza kuzunguka huku na kule niangalie uwezekano wa kupata msaada. Harakati zangu sasa zikazaa matunda, kwa mbali nilimuona mtu akiwa analima. Alhamdulilah!!Lilikuwa jambo maalumu kwa wakati maalumu. Nikajongea kwa kujikaza hadi nikalifikia lile shamba. Hakika mtu huyu alikuwa mchapakazi. Alikuwa peke yake na shamba lilikuwa kubwa sana.“Kaka!!….Kaka…” Sauti ilitoka kwa taabu, nadhani hakuweza kunisikia.
Nikataka nimsogelee. Lakini ghafla akageuka. Ni kama aliuhisi uwepo wangu pale.Japo alikuwa amechakaa sana. Nguo zikiwa zimeraruka, lakini niliweza kumtambua. Huyu mtu alikuwa ni marehemu. Zaidi ya kuwa marehemu, kifo chake niliwahi kukiota. Basu!!Hakusema neno alipogeuka na wala hakunitazama, ni mimi niliyeiona alama ya 666 kifuani pake. He! Anamilikiwa!! Nilitafakari. Nikatimua mbio. Mbio za kuchecheme ziliniumiza lakini nitafanyaje??
Akili yangu ilikuwa sawa kabisa. Nilikuwa namkumbuka vyema Davis. Nilijuta kukutana na bwana huyu katika mtandao na kumuamini sana. Nilijutia na pesa alizokuwa akinipatia.Mara nikaanguka!! Nilikuwa nimegongana na kitu kigumu. Ajabu na kweli haukuwa mti bali mtu. Jesca! Jesca na urembo wake alikuwa amebeba ndoo kubwa ya maji, alikuwa peku na alikuwa amepauka sana. Hata Jesca naye hakunitazama, badala yake aliendelea na safari zake huku akinipa nafasi ya kuitazama alama ya 666 katika mkono wake.“Jesca!! Jesca!!” hakunijibu na dhani hakunisikia. Akatoweka.Sasa sikukimbia tena, ina maana hawa watu hawanioni. Na kamahawanioni hata lile joka halinioni. Nilijiuliza.
Kwani kuna kitu gani sifanani nao? Nilipojiuliza hivyo. Nikaikumbuka alama ya ‘666’ iliyokuwa imetolewa katika upande mmoja wa makalio yangu.Alama hii ni ile ninayoijua ama kuna utofauti? Nilitafakari. Jesca huyo akawa ametoweka. Nilipoendelea mbele kidogo nikakutana na kile kisu nilichokitupa. Nikakitwaa. Nikazunguka huku na huko nikiwa uchi nikaipata ile kanga yangu, nikaivaa, wakati naivaa ndipo nilikumbuka juu ya watu wawili niliokuja nao huku katika kujisafisha na alama hiyo mbaya.
Nilipowakumbuka nikalikumbuka na kaburi lililokuwa wazi. Nikazungukazunguka na sasa nilikumbana nalo. Huenda walikuwa wamejichimbia kaburi hili. R.I.P na mwenzake walikuwa wamejizika huko.Amakweli wewe ni Roho Iliyo Potea!!! Nilikiri kimoyomoyo baada ya kugundua kuwa sasa RIP amepotea kweli. Nilisikitika kuwa hakuwa amenieleza mambo mengi juu ya alama hizi za maajabu.Jambo moja la muhimu alilonieleza ni kwamba nilikuwa namilikiwa. Kuna mtu alikuwa ananimiliki. Ili nisimilikiwe ilikuwa lazima alama hiyo ifutwe.
Sasa nilikuwa nimekatwa kipande cha nyama. Damu ya hedhi hainitoki tena na sihisi kichefuchefu cha mimba. Ina maana ndio similikiwi tena? Na mimba nayo imetoka. Nilishangaa.Lakini sasa mbona siwezi kutoka humu porini? Nilijiuliza sikupata jawabu.Mawazo yangu yalikatishwa na sura ya mtu mwingine aliyekatisha mbele yangu. Huyu alikuwa ni marehemu mwingine ambaye tulisoma chuo kimoja enzi za uhai wake.Hivi niko peponi ama jehanamu? Kwa nini sasa nakutana na maiti tu.
Huyu naye hakuonekana kunifahamu. Alikuwa na alama yake sikioni. Nikakumbwa na moyo wa kujaribu. Kama mimi nimekatwa kipande cha nyama na alama imetoweka, nikaamua kujaribu kutumia mbinu ya RIP ambaye sasa ni marehemu.Nikamnyatia yule binti. Nikakiweka kisu changu tayari nikamkaba. Bila kukumbuka maumivu atakayoyapata nikafyeka sikio lake. Nikasisimuka lakini katika nafsi nikikiri kuwa kile kisu kilikuwa kikali sana. Sikio chini!! Yule binti naye chini, akawa anatoa kilio kikubwa sana. Kitu cha ajabu hakuna msaada alioupata. Mimi nikajiweka mbali niweze kuwa shahidi wa nini kitakachotokea.
Mara upepo mkali ukaanza kuvuma. Miti ikayumba, pori likatulia na sasa alitokeza nyoka mkubwa, ni yule yule wa awali. Nikataka kukimbia, nikakosa ujasiri nikaendelea kujificha, joka lile likatambaa hadi katika ule mwili unaogalagala, kisha likakwapua lile sikio na kisha kuanza kuzurura huku na huko hadi lilipotoweka ndipo nilipomsogelea yule binti. Alikuwa ametulia tuli na damu haikuwa ikivuja sana.Nikamgusa. Akajigeuza, akanitazama. Mungu wangu!! Tiba inafanya kazi ile. Aliniita jina langu. Akakaa kitako.Sikuwa nikiamini lakini sasa nikampongeza RIP yule tahira niliyemdharau sasa alikuwa njia.“Na wewe umejiua?” “Nimejiua?” nilimuuliza.
“Isabela kwa nini uliniua?” alinihoji. Nikashangaa.“Mimi nilikuua wewe.”Yule binti alinieleza kila kitu, akanisimulia alivyouwawa akiwa ndotoni. Akakiri kuniona mimi nikimmaliza huku ninacheka. Akanielezea juu ya sauti alizozisikia. Ni sauti zile zile na mimi nilizisikia katika kifo chake na pia katika mazishi ya yake, hata Jesca alipokufa zilisikika.Niliamini tena kauli ya RIP kuwa kuna mtu ananimiliki na ananifanya anavyotaka yeye kwa wakati wake. Huyu mtu ni nani? Nilijiuliza huku tuhuma za kwanza nikizitupia kwa Dokta Davis.
(OPARESHENI UKOMBOZI)Jenipher alinieleza mambo mengi huku akinisaidia kupata chakula na maji. Chakula kilikuwa kizuri na maji yalikuwa safi lakini namna ya kuvipata ilikuwa ya namna yake. Wakati huo na yeye hakuweza kuonekana.Chakula na maji pekee havikuwa vitu tulivyokuwa tukihitaji. Kikubwa tuliuhitaji ukombozi wetu na wanadamu wengine wanaomilikiwa na watu wabaya.
Sasa ilikuwa ni lazima kuuvaa moyo wa ujasiri ili kufanya harakati za ukombozi. Tuliwahitaji wanaume wenye nguvu waweze kuungana nasi.Basu akawa chaguo la kwanza! Tulimtegea siku akiwa katika kulima shamba kubwa lisilotoa mazao.Tulifanikiwa kumpata kwa wakati. Huku tukiwa tunajiamini kabisa. Tulimvaa kwa nguvu akaanguka chini huku akiwa haoni lolote.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni