Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA THELATHINI NA SITA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Bahati nzuri Kilingo nae alikuwa amewasili tena kituoni baada ya kuondoka na gari muda mrefu uliopita, aliyelekea Ofisini kwao alikohitajika kwa dharura punde baada ya kufukuzwa na Insp Kenjah, akawachukua wazee na kuianza tena safari ya kurejea Hospitalini kumwangalia Mgonjwa wao waliemuacha akiwa kitandani
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Mawindo yakaendelea..
Mzee Sufian anamwinda Komando Takadir wakati nae(Takadiri) anawawinda Mzee Sufian, Suhail, na Shekhia huku akiwa amedhamiria kupambana na kila mmoja kwa mtindo wake tofauti.. wakati huo Silaha hatari ya Khatam Budha ikiwa Kituoni Polisi..
Muda huohuo Joram Ndege(Meno ya Dhahabu) naye anawawinda wabaya wake ambao kwa namna moja ama nyingine wanatishia usalama wa kambi yao ya Black Scopion kwa kutoa siri zao ama kwa kuwachunguza mambo yao..
Huku nako Insp Kenjah, Koplo Marando na Sajent Bangi wakiwawinda kila watakaohisiwa kuhusika na kadhia hiyo inayoendelea, kuanzia na Joram Ndege mwenyewe, Sajent Rwehumbiza, na afande Chanzi
Ulikuwa ni Mchezo mtamu
*****
Mzee Kusekwa na Fungameza wakaingia ndani ya gari wakifuatiwa na wake zao kisha safari ya kuelekea hospitali ikaanza huku Kilingo Mkude akiwa nyuma ya usukuni. Safari ilielemewa na foleni ndefu ya magari iliyotanda barabarani lakini mpaka wanaingia Hospitalini hakuna aliyegundua kuwa kulikuwa na foleni kubwa kutokana na mlundikano wa mawazo vichwani mwao. Wakateremka garini baada ya kuegesha katika eneo maalum hapo hospitalini kisha wakaongozana mpaka Wodini.
Ule mfadhaiko uliomkumba Suhail baada ya kumwona mkewe Sharifa akiwa mzima kabisa sasa ulihamia kwa wazee hawa pamoja na Kilingo, hakuna aliyeamini utendaji kazi wa macho yake pindi walipomwona Sharifa akiwa Bukheri wa Afya ndani ya wodi.. ilikuwa ni furaha na hofu vilivyowakumba kwa wakati mmoja maana mgonjwa mliyemwacha akiwa taabani kumkuta katika hali ile ilikuwa si jambo dogo japo hilo halikuwafanya wamkimbie au wamwogope mtoto wao bali lilizidi kuwapa hamasa ya kumsogelea kwa kasi wakistaajabishwa na hali ile.
Baada ya kuketi, hawakupata muda wa kusalimiana, ikawa ni maswali juu ya maswali.. Sharifa akaanza kuwaelezea mkasa mzima ulivyokuwa, ilikuwa ni mkasa wa ajabu na vioja! Mkasa uliowastaajabisha wote mle Wodini
Hali ya mshangao ikazidi pale Sharifa alipowaeleza kuwa Suhail aliwasili Hospitalini pale muda uliopita na ameahidi kurejea tena baadaye
“Unasema?! Suhail alikuwa hapa?” Aliuliza kwa mshangao Mama Suhail, na si yeye tu pekee aliyekumbwa na mshangao huo bali wote walibutwaika! kila walipojaribu kuyapanga matukio hayakuwaingia akilini, kubwa zaidi ni muda ambao Suhail alitoweka na kurejea kule kituoni usingetosha kwake kuja mpaka huku Hospitali na kurejea tena, na hata kama angeweza kwanini afanye vile hasa? Hakuna mwenye majibu!
“Ndiyo alikuwa hapa na nimekaa naye sana hapa”
“Ama!”
“Mbona siwaelewi kwani kuna nini kinachoendelea?” Hatimaye Sharifa aliingiwa na hofu kufuatia hali wanayoonekana nayo wazazi wake ikabidi sasa awasaili kwa umakini zaidi, Wakajaribu kumlaghai kwa kuuficha ukweli lakini nyuso zao zilizotahayari zilionesha dhahir bin Shahir kuwa hali haikuwa shwari hata chembe.. Sharifa alilisoma hilo ndipo akawakazania wamweleze tu kila kitu bila kumficha, hatimae Mzee Fungameza akampasulia jipu ‘Pwaa!’
Akamweleza kila kitu nukta kwa nukta jinsi mkasa mzima ulivyokuwa mpaka kuhisishwa kwa mumewe katika saga lile la mauaji ya Mwandishi wa habari
“Suhail ameuwa? NOO! Haiwezekani..” aliongea kwa kasi mpaka akapaliwa na mate, akashusha pumzi na kuzipandisha tena kama mzani, Akaendelea “..Mbona amekuja hapa hana dalili yoyote ya kukabiliwa na kesi?.. Mmesema yuko wapi kwa sasa?”
“Tumemwacha Polisi kwa sasa, ila hakuna haja ya kupaniki Mama yangu maana suala lake linashughulikiwa vizuri tu” alijibu Mama Sharifa
“Hapana mama, hapa kuna jambo tu si bure!.. Wamekuwa wakimfutafuta sana itakuwa wamembambikia kesi tu” Kikapita kimya cha muda kidogo kila mmoja akiwa amezama katika tafakuri kivyake, ndipo tena Sharifa akaibuka na swala jingine lililozuwa mjadala mpya
“Ni huyo aliyeuawa ni nani? Mmeshamjuwa?”
“Aliyeuawa ni yule mwandishi wa habari aliyemchafua kwenye magazeti… Msigwa,” Alijibu Kilingo Mkude
“NANI? Umesema?!..” Sharifa alizidi kuchanganyikiwa maana alimjua vyema Msigwa na alikuwa akijuwa kila kinachoendelea baina yao, na japo aliondokea kumchukia sana kijana yule lakini kwa hili la kuuawa lilimshituwa sana ukizingatia anayehusishwa kuuwa ni mumewe kipenzi, jasho lilimtoka “Msigwa ameuawa? Oooh.. Mungu wangu!” Sharifa aliendelea kuuliza huku macho yakimtembea huku na kule kama saa mbovu!
Huku nako Mzee Kusekwa aliposikia jina la Msigwa hapohapo Kengere ya hatari ikagonga kichwani mwake, alilikumbuka vizuri jina hilo na punde taswira ya kijana Msigwa akimdhihirikia, akashindwa kujizuwia akaropoka
“Mmesema nani, Msigwa?.. Msigwa ameuawa? Sitaki kuamini..”
“Kwani mnamjuwa huyo Msigwa?” Aliuliza kwa hofu Mzee Fungameza lakini hakujibiwa zaidi ya kuishia kuwasikia wenzie wakilalama tu, Mama Suhail naye akamkumbuka kijana yule waliyemlea kwa upendo kipindi kile akiwa Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora, Walimtambuwa Msigwa kuwa ni rafiki kipenzi wa Suhail tangu walipokuwa shule na hata baada ya kuhitimu sasa iweje tena Suhail amwue mwenzie? Habari zile za magazetini walizisoma lakini hawakujua kua ni Msigwa aliyekua akiziandika kumchafua Suhail japo walitambua kuwa kwa sasa Msigwa ni Mwandishi wa habari
“Kumbe Msigwa ndiye aliyekuwa akimchafuwa Suhail magazetini! Kwanini hasa?” Mzee Kusekwa alijiuliza mwenyewe kwa Sauti! Hakika ilikuwa ni habari mpya na mbaya kwao. Mzee Kusekwa akamgeukia Mzee Fungameza na kuanza kumpa historia ya Suhail na Msigwa tangu walipokuwa shuleni, ilikuwa ni historia yenye kumbukumbu tamu iliyoingiwa na shubiri. Baada ya majadiliano yahapa na pale Mzee Kusekwa akamuuliza Kilingo kama itawezekana waende kwa Msigwa ambapo bila shaka wataonana na wazazi wa marehemu ambao yeye alikuwa akiwasiliana nao mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kutumiana zawadi tangu walipounganishwa na urafiki wa vijana wao
“Walikuja hao wazazi wake, lakini tayari wameshachukua maiti na kwenda kuzika kwao huko Iringa” Jibu la Kilingo likakata hamu ya Mzee Kusekwa
“Kama umesema una mawasiliano nao hebu wapigie simu labda utawapata,” alipendekeza Mama Sharifa lakini simu ilipopigwa majibu ni kuwa haikuwa ikipatikana.. wakatazamana!
Mjadala ukaanza upya mle Wodini kuhusu mtungo wa matatizo yanayoendelea, hapakuwa na suluhu la matatizo hayo zaidi ya kila mmoja kutoa mawazo yanaoonekana kuchagizwa na Mchoko wa akili, Ndipo Mzee Fungameza akatoa rai kuwa waree kwanza nyumbani wakapumzike ili wavute akili mpya, wakaafikiana! Sharifa naye akagoma tena kuendelea kubaki pale Hospitalini.. Wakaondoka naye mpaka Ilala, nyumbani kwa Suhail na Sharifa
*****
Huko Kituo cha Polisi nako Inspekta Kenjah alikuwa amezungukwa na vijana wake wa kazi akiwapa mpango mkakati wa kukabiliana na kesi iliyo mbele yao ambapo alipanga vikosi kazi; Cha kwanza kikapangiwa kuweka ulinzi kule Hopitalini alipolazwa yule Mhariri aliyepigwa Risasi, kikosi hiki kilikuwa chini ya Koplo Marando. Cha pili kikapangiwa kuzifuatilia zile gari zinazotumiwa na akina ‘Meno ya dhahabu’ ili wafahamike nyenendo zao, kikosi hiki kikawa chini ya Sajent Malumbo. Na kikosi cha mwisho kilikuwa ni kikosi maalum kinachozuru eneo lolote muda wowote, hiki kilikuwa chini ya Inpektah Kenjah.
Baada ya kuhakikisha wamejipanga vya kutosha wakaahidiana kuwa wakapumzike maana usiku ulikwishaingia, ili kesho yake ndipo kazi ianze!
*****
Giza likatanda na kufunika anga, Usiku ukaingia!
Kila mmoja alikuwa nyumbani kwake amepumzika, lakini si kwa Mzee Sufian Bin Shamhurish wala Komando Takadir Al-harabi ambao wao walikuwa wakiendelea kuwindana kwa ustadi wa hali ya juu lakini hakuna aliyefanikiwa kumnasa mwenzie.
Wakiwa katika hali hiyo ndipo tena Miale ya Pete(Khatam Budha) ikamjia waziwazi Komando Takadir Al-harabi, akaachana na kumwinda hasimu wake na sasa akaanza kuifuta miale ile, ilikuwa ikitokea kulekule katika kituo cha Polisi.. Akaifuata mpaka kituoni,
Alipofika pale Kituoni kwa kutumia uwezo wake wa kijini akamwona sasa Suhail akiwa amejilaza ndani kabisa ya Selo, akajibadili kidogo tu kisha akaingia mpaka pale Kaunta, akawapita wale Askari wakiwa na majukumu yao bila ya wao kumwona akaingia mpaka kule alipolala Suhail.. alipoingia tu akajirejesha katika lile umbile lake la mwanzo kabisa ambalo Suhail alipata kuliona walipokuwa wakipambana kule Yemeni..
Ghafla Suhail akashituka kutoka usingizini na kukutana uso kwa macho na Komandoo Takadir, Suhail akahamanika maana haraka alimng’amua Komando yule.. Jicho likamtoka kama Sorokoto kabanwa na mlango.. akataka kupiga kelele lakini kabla hajafanya hivyo Takadir akamuwahi kumsemesha
“Bwana Suhail, usithubutu kufanya ujanja wowote ule nitakuangamiza hata maiti yako isionekane..” Komando Takadir alikuwa akiongea Kiswahili fasaha kama Mkwere wa Bagamoyo, Suhail akasimama na kurudi nyuma ili awe mbali na Takadiri lakini haikufaa kitu maana ukuta ulimpokea na kumzuwia.. Takadir akamsogelea mpaka karibu yake ksha akaendelea
“..Leo nitaondoka na kimoja kati ya viwili au ikibidi vyote.. kama si Pete(Khatam Budha) basi roho yako! naomba uchaguwe moja”
“Wewe ni nani, Na unataka Pete gani? Mbona sikumbuki kupewa pete na wewe!” Suhail alijibu huku Mdomo ukimtetemeka kama mtoto aliyekamatwa akilamba sukari, Jibu hilo lilitosha kuzichokoza hasira za Takadiri, Kelbu moja alilotandikwa Suhail lilimrusha mithili ya mtu aliyepigwa shoti ya umeme, kabla hajapumua akafuatwa tena akapigigwa ngumi kama kumi mfululizo mpaka akawa anaona nyotanyota tu, kisha akainuliwa akiwa anatweta.. Miale ya Pete ilikuwa ikionesha kuwa iko maeneo hayohayo lakini Takadir hakuiona, akamwangalia Suhail kidoleni hakuona kitu
Kaiweka wapi Pete huyu? Alijiuliza Takadir! hakupata majibu.
“Utanionesha Pete au hautanionesha?”
“Mimi sina Pete utaniuwa bure kaka” Hapohapo akapokea kichapo kingine cha haja mpaka akatapakaa damu mwili mzima.. Suhail akawa hatamaniki! Sasa maumivu yakamtia ujasiri wa ajabu akajikuta anainuka kwa hasira na kumrukia Tajadir ili amshambulie lakini ilikuwa ni sawa na ‘Kukitoa kinu juani’ hakitanenepa wala kukushukuru, na hata ungekiacha juani kisingeungua.. Kazi bure! Akapokea kichapa kingine cha nguvu mpaka akaishiwa nguvu akaanza kupiga kelele sasa! Kelele hizo zilikuwa ni za maumivu yaliyochanganyika na kukata tamaa!
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi