SALAMU KUTOKA KUZIMU (1)

0
Mtunzi: ___

SEHEMU YA KWANZA
KIFO kaja duniani kwa kazi moja tu. Akikukuta umekwisha… Akikusalimia umekwisha… Hana mdhaha. Lakini sasa huyu anataka watu mashuhuri, watu wakubwa zaidi. Anataka kuifanya Afrika nzima iangue kilio na maombolezo ambayo hayajapata kutokea duniani. Na anataka hilo litokee siku moja, saa moja… “Bendera zote duniani zipepee nusu mlingoti”, anasema huku akichekelea. “Sijawahi kushindwa…” Jasho linawatoka watu mashuhuri. Damu inamwagika kama mchezo. Inspekta Kombora machozi yanamtoka. Joram Kiango anabaki kaduwaa.

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

TUENDELEE...
“Bado nasisitiza kuwa tusithubutu wala kujaribu kufanya lolote kabla ya kuhakikisha kuwa Joram Kiango yu marehemu”, ilidai sauti moja nzito.

“Naam, lazima afe”, sauti nyingine iliunga mkono. “Afe kabla hatujainua mikono kufanya lolote tulilokusudia. Hakuna asiyefahamu jinsi kijana huyu alivyo hatari anusaye shari na kuingilia kati kuharibu harakati zote. Hajasahaulika alivyowakorofisha wale mashujaa waliotaka kuuangusha utawala wa nchi ya Ngoko katika tukio lile lililoitwa Dimbwi la damu. Kadhalika bado hatujasahau alivyosababisha vifo na kuharibu mipango ya majasusi waliotaka kuiharibu nchi hii katika mkasa ambao mtu mmoja aliuandikia kitabu na kuuita Najisikia kuua tena. Kwa kila hali Joram Kiango ni mtu hatari zaidi ya hatari zote zinazoweza kutokea, Hana budi kufa”.

Kicheko kikavu kikasikika kidogo, kikafuatwa na sauti iliyokwaruza ikisema.

“Atakufa. Lazima afe. Na atakufa kifo cha kisayansi kabisa. Mpango huu tumeuandaa kwa uangalifu mkubwa, Na watekelezaji wake pia ni watu ambao wamehitimu vizuri katika nyanja zote zinazohusika na kazi hii, Tuondoe shaka kabisa. Mpango huu utafanikiwa kwa asilimia mia”.

“Kwa hiyo ndugu Mwemyekiti”, ilisema sauti ya mtu wa kwanza. “Niwie radhi kwa kukukata kauli. Ninachokuomba ni kuuahilisha mkutano huu na tusisubutu kukutana tena hadi hapo Joram Kiango atakapokuwa kaburini, Pengine mtaniona mwoga kupindukia, Lakni mimi sipedi kabisa kufanya jambo lolote wakati kijana yule akiwa hai. Mnajua jinsi alivyo na miujiza. Anaweza kuwa hapa akisikiliza mazungumzo yetu, kesho tukajikuta mahakamani bila kutegemea”.

Ilizuka minong’ono, sauti mbili tatu zilimuunga mkono msemaji aliyemaliza kusema. Jina la Joram liliamsha hofu katika mioyo yao. Wakatazamana…

Walipenda pia kumwona Mwenyekiti wao uso kwa uso. Kwa bahati mbaya, hawakuweza kuona uso wake isipokuwa kiwiliwili tu, ambacho kilifunikwa kwa mavazi ya thamani kama walivyokuwa wamevaa wao. Mwanga mkali uliotokana na taa ya umeme iliyowekwa kwa namna iliwachoma macho kila walipotamani kumtazama Mwenyekiti usoni. Ni yeye tu aliyekuwa na nafasi nzuri ya kuwatazama wote mmoja baada ya mwinginge kikamilifu na kuwasoma nyuso zao. Wakati wa kumtambua Mwenyekiti ulikuwa bado haujawadia hivyo hawakupaswa kumuona kabisa isipokuwa sauti yake tu.

Mkutano huo ulifanyika katika chumba cha siri, chini ya ardhi katika mojawapo ya majumba ya kifahari yaliyoko Jijini Dar es salaam.

Kila aina ya tahadhari iliwekwa kuhakikisha usalama wa mkutano huu wa awali. Mkutano ambao ulikuwa umeitishwa ghafla, kwa njia za kutatanisha, hata wajumbe hao walijikuta wamefika kwenye mkutano bila kufahamu kilichowaleta hapo.

Mwenyekiti akaufungua mkutano huo kwa maneno machache akisema: “Tunataka kuitetemesha Afrika na kuishangaza dunia. Tunataka kuachia pigo ambalo halitafutika katika historia ya Ulimwengu”. Wajumbe wakaelewa kinachoendelea. Ndipo mjume mmoja alipotoa rai ya kumaliza kikao hadi watakaposikia Joram Kiango amekuwa marehemu.
Tahadhari kubwa ilikuwa imechukuliwa wakati wa kuandaa mkutano huo. Wajumbe waliingia kwa siri kubwa wakipita milango tofauti, katika eneo hilo vilitegwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhakikisha kila mshiriki wa mkutano huo wa siri anahusika kwa njia moja ama nyingine. Walihakikisha pia hakuna kifaa au chombo chochote cha kunasa sauti ama kusikiliza maongezi hayo ya siri. Vinginevyo chumba hicho kingeweza kutoweka kisayansi kisionekane mlango wowote zaidi ya kuta za kawaida. Zaidi ya yote silaha za kisasa, hewa za sumu, buduki zisizotoa mlio, madawa ya kulevya na mbinu zingine zilikuwa tayari kutumika endapo lolote lingetokea. Kwa bahati mbaya, ni Mwenyekiti peke yake ndiye aliyejua mpango mzima kuhusu mkanda huo.

Kulikuwa na kila sababu ya kuweka tahadhari au uangalifu huo. Watu waliokutana katika mkutano huu hawakuwa watu wenye njaa ya pesa wala kiu ya utajiri. Ni watu mashuhuri walioshiba na kudhamiria kulinda shibe yao. Wote walikuwa na hadhi mitaani, nyadhifa serikalini, na heshima katika chama. Waliokutana hapa wote walikuwa na matarajio ya kuvuna matunda matamu. Matunda ambayo yangetokana na mkutano huo. Hakuna mjumbe aliyependa kukosa utamu wa matunda hayo. Hivyo wote walikuwa na dhamira moja.

“Inaonyesha kuwa Joram ni tishio kwa kila mtu hapa”, Sauti nzito ya Mwenyekiti ilisema. “Hilo linanifanya nizidi kuwa na imani juu ya dhamira yenu. Joram anaogopwa kuliko Polisi na jeshi zima la nchi hii, Kwanini? Wanajeshi mko hapa, polisi mko hapa, Chama tawala kiko hapa. Serikali iko hapa. Anayekosekana hapa ni mtu huyo anayejiita Joram Kiango. Mtu mtundu sana, ambaye utundu wake ni madhara kwa watu wenye dhamira maalumu. Hakuna atakayeshuku kuwa kauawa. Daktari atampima na kuona kafa kwa kansa ya moyo. Atauawa kitaalamu na kufa kistaarabu. Msiwe na shaka”.

Kimya kifupi kikafuata. Wajumbe wakatazamana usoni. Kimya kilimezwa na sauti ya Mwenyekiti alipoongeza maneno.

“Kwa hiyo, naahirisha kikao hiki kama alivyoshauri mjumbe. Tutakutana tena hapa baada ya wiki mbili, siku na saa kama za leo, kwa njia zetu zile zile, bila kusahau kuwa joram Kiango hatakuwa Joram tena ila hayati Joram Kiango. Na ifahamike kuwa kuitoa nje siri hii ni sawa na kujiwekea saini ya kifo chako mwenyewe”.

“Ni kweli Mwenyekiti”, sauti mbili tatu za wajumbe wenye hofu, ziliitikia.

Nyumba mbovu zilizojengwa bila utaratibu katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam ambazo huishi kina mama kutoka sehemu mbalimbali nchini ambao humudu kupanga katika nyumba hizi kwa ajili ya makazi na biashara isiyosemekana wala kuitamka. Biashara ambayo ni aibu kubwa kuitaja hadharani, japokuwa inafanyika hadharani bila kificho. Biashara ya kuuza miili kwa pesa chache za matumizi.

Tupo Mburahati, mbele ya moja ya majumba ya aina hii. Kaketi mwanamke ambaye umri wake haujaruhusu kumwita mwanamke. Yu msichana mwenye sura nzuri, mwendo mzuri na kila kitu kizuri, Hata mavazi yake si duni kama wenzake walioketi hatua chache karibu yake, mbele ya milango ya nyumba zao, Kwa jina msichana huyu anaitwa Waridi.

Ni juzi tu Waridi alipotokea hapa Mburahati na kujipatia chumba. Sifa na uzuri wake zilizagaa haraka haraka zikawafikia hata wale ambao si wateja wa biashara hii. Kwamba kaja msichana mzuri.Hakuna aliyetaka kujua katokea wapi, Hakuna aliyetaka kujua kwanini binti mzuri kama huyu aamue kutouthamini uzuri wake ambao ungemfanya aishi vizuri zaidi, akila na kunywa pesa za walionazo. Hakuna aliyejali.

Leo Waridi alikuwa katika hali yake ya kawaida. Hali ya ukimya na majonzi pamoja na kwamba alionekana akiwachekea mara kwa mara wateja wake. Hakuna aliyejua jeraha kubwa lililokuwa moyoni mwake. Jeraha ambalo lilikuwa siri yake na alipenda liendelee kuwa siri. Kutunza siri ni kazi kubwa kama kubeba mzigo mzito usiobanduka kichwani. Mzigo aliobeba kwa dhiki sana. lakini alistahamili kwanki maisha yake yenyewe yalitegemea utunzaji wa siri hii.

Mara akatokea mteja ambaye sura yake, mwendo wake na mavazi yake vilimtofautisha na wateja wa kawaida. Huyu alimtaka Waridi afunge biashara yake siku hiyo ili wafuatane wote nyumbani kwake.

“Haiwezekani. Ninaye bwana wangu ambaye huja kulala hapa”.

“Twende kwangu halafu nitakurejesha hapa haraka iwezekanavyo”.

“Haiwezekani vilevile”.

“Ziko pesa nyingi kwa ajili yako kama utakubali kwenda nyumbani kwangu”.

“Nimesema hapana”. Ghafla hasira zikampanda Waridi. AKashangaa kwanini kamchukia mtu huyu. “Toka kama hutaki”, alifoka na kumwacha mtu huyo kakalia kitanda chake.
Mteja huyu akatabasamu. Kwa waridi lilikuwa tabasamu la kebehi ambalo halikumshitua kuliko alivyotegemea. Swali fupi likaulizwa kwa sauti ndogo. “Huendi na mimi? Hata nikisema kuwa marehemu Bomba ni ndugu yangu pia nafahamu mpaka mahali alikozikwa?”.

Hilo lilimshitua kidogo Waridi. Mshituko ulipomtoweka yalifuata machozi mengi yaliyomtoka katika macho yake yaliyoduaa kwa hofu yakimtazama mteja huyo. Mwili wake ulikuwa umemlegea kiasi cha kumfanya ashindwe hata kusimama kikamilifu.

Waridi hakuwa na uwezo wa kufanya lolote. Ndipo mteja huyu alipomsukuma Waridi na kuanguka chali kitandani, akampambua mavazi yote na kumtenda kikatili yote aliyojisikia kumtendea.

Baada ya hapo mteja alimwamru Waridi kufuatana naye. “Tutatoka mara moja. Ukiendelea kukataa nami nitashindwa kutunza siri yako. Twende zetu. Nitakupa kazi ndogo tu, unisaidie. Kuna mtu anahitaji kufa. Utamsaidia wewe. Haitakuwa kazi kubwa kuua mtu wa pili mama. Au vipi? Tofauti pekee ni kwamba yule aliitwa Bomba na huyu anaitwa Joram”.

Waridi alimfuata kikondoo.

                   **********************************
Huyu hakuwa mwingine zaidi ya Jodor Prosper kama alivyojiita katika ule mkutano wa siri uliofanyika usiku wa juzi. Yeye akiwa Mwenyekiti.

Jina hilo lilikuwa moja miongoni mwa majina yake kadha wa kadha ambayo huyatumia wakati tofauti na kwa dhamira tofauti. Kadhalika alikuwa mtu mwenye sura mbalimbali na miondoko aina aina. Kila jamii ilimfahamu Prosper yule yule katika jina na sura tofauti. Vivyo hivyo, tabia zake kubadilika mara kwa mara kama kinyonga anavyojibadili rangi. Katika kundi la wahuni Prosper yu mhuni mkubwa, katika jamii ya waungwana yu muungwana halisi, katika familia ya masikini Prosper alikuwa mmoja wao, na miongoni mwa matajiri yeye ni kama wao.

Huyo ndiye Prosper. Mswahili aliyezaliwa mahali fulani katika Pwani ya Bahari ya Hindi. Akiwa na miaka kumi na miwili, alitoweka numbani kwao kwa kudandia meli moja iliyotia nanga katika Bandari ya Tanga.

Meli hiyo iliyokuwa na mabaharia katili kupita kiasi. Walimpokea Prosper kwa ukatili usiosemekana. walimtendea mengi maovu, akitukanwa na kusimangwa.

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)