Mtunzi: ___
SEHEMU YA NANE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Kisha aligusa waya fulani ambao hakutarajia kuuona hapo. Aliutazama waya huo kwa mshangao. Mshangao ambao ulikatizwa na mlipuko mkali uliomfanya apae juu na kutua chini akiwa tayari ametawanyika vipande mfano wa nyama za kopo, zinazoandaliwa kwa ajili ya kusindikwa.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
Mlipiko huo ulimkuta Joram Kiango akiwa amesimama wima, fimbo mkononi. Aliduwaa alipoona ghafla mtu akizuka mbele yake na kupaa angani ambako alitawanyika vipande vipande. Lakini hakupata muda wa kuendelea kuduwaa, kwani wakati huo huo kila kitu kilikuwa kikipaa na kutua huku na huko kwa kishindo cha kutisha.
Kila kitu pamoja na Joram mwenyewe. Alijikuta angani kisha akajibwaga chini akifuatwa na lundo kubwa la vitu vizito ambavyo vilimfunika juu.
Joram hakuwa na muda wa kusikia maumivu pia. Alihisi kama mtu aliyepoteza kichwa au ubongo. Fahamu zikamtoka na nafsi yake kuchukuliwa na kiza kinachotisha.
******************************
Kifo cha kusikitisha! Joram aliwaza hivyo, karibu kila mtu kati ya umati mkubwa uliosimama kando kuizingira nyumba hiyo. Macho yenye hofu na huzuni yalikuwa yakiwatazama askari ambao walikuwa wakiviokota viungo vya marehemu kimoja baada ya kingine na kuvitia katika sanduku. Ni watu wachache sana walioweza kutazama tukio hili kwa muda mrefu. Wengi walitupa jicho kwa sekunde kadhaa na kisha kugeuza nyuso zao upande mwingine huku wakiguna na kufuta machozi. Mama mmoja alisikika akilia kwa sauti.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa wengi wao kushuhudia tukio la mtu aliyepoteza maisha kwa njia hii ya kutisha.
Miongoni mwa walioshuhudia tukio hilo alikuwwepo Jodor Proper. Alikuwa mmoja wa watu waliofika mapema katika eneo hilo. Lakini alimkuta mtu wake aliyetega bomu hilo akijifuta vumbi baada ya ule mweleka alioupata kutokana na tofali lililomponda kichwani. Yeye alikuwa mmoja kati ya ‘wapita njia’ wanne waliojeruhiwa katika ajali hii. Proper alimsaidia mtu huyu kama asiyemfahamu. Walipopata mwanya walinong’onezana: “Kazi nzuri sana, Sasa nenda zako…”
Mtu huyo alipoondoka. Proper aliendelea kutazama ‘ajali’ huku akijitia kunung’unika. Lakini ndani ya moyo wake alikuwa akisherehekea na kushangilia sana tukio hilo. ‘Kifo kinachomstahili kabisa’ Aliwaza kwa furaha. “Mnofu mmoja mmoja! Na ajiunge basi tuuone huo ushujaa wake”.
Wazo la kwamba huenda huyu akawa si adui yake mkubwa Joram Kiango halikumjia akilini. Ingawa haikuwa njia rahisi ya kuthibitisha mabaki hayo ya marehemu, lakini katika uchunguzi wake Proper alifanikiwa kuiona ile fimbo ya Joram na madevu yake ya bandia ambayo yaliokotwa na askari mmoja na kumwonyesha Inspekta wao ambaye alibabaika kama mtu aliyeguswa na simba. Kitendo hicho kilimfanya Proper ajisikie kucheka huku akijituliza. Wangetangaza nini tena wakati dunia nzima imefahamishwa zamani kuwa Joram Kiago amefariki dunia?.
Proper alipotoka katika eneo hilo kwa tabasamu, alikuwa na wazo moja tu la kuendelea na mipango yao bila kuwa na hofu yoyote. Kikwazo pekee alichoogopa yaani Joram Kiango kilikuwa tayari kimeingia kuzimu, kikiwasalimia babu zake huko.
Mmoja wa maofisa wa polisi alipendekeza wafanye uchunguzi wa kina ili kuhakiki kama eneo hili lilikuwa na maiti ama mareruhi wengine zaidi waliokandamizwa na kifusi. Lakini majirani wa eneo hilo waliwahakikishia polisi kuwa nyumba hiyo haikuwa na watu. Wakaondoka haraka haraka kwani kazi ya kufukua vifudi ilikuwa nzito, ambayo hakika ingewatoa jasho. Wakaondoka na mwili wa marehemu wakiuacha umati wa watu ukiendelea kufika katika eneo hilo kutazama kilichotokea.
Usiku ulipoingia, giza liliwaondoa watu katika eneo hilo likabaki katika hali yake ya kawaida.
Unono, huyu alikuwa mwanamke wa makamo, mfupi kiasi, mnene wa kutosha, mweusi kupindukia, mama huyu alikuwa mmoja kati ya watu wengi walioshuhudia ajali hii ya mtu kuuawa kwa bomu. Mama huyu alikuwa miongoni mwa umati huo, kama wananchi wengine alisema hili na kusikiliza lile, macho yake yakifanya kazi ya kutazama kwa hofu tukio hilo pamoja na polisi kadhaa, ambao walikuwa katika pilika pilika za kukusanya mabaki ya marehemu huyo.
Kichwani Unono alikuwa na mawazo tofauti, nje kabisa ya tukio la msiba huo uliotokea eneo hilo. Alikuwa na mawazo mchanganyiko wa matatizo ya kiuchumi na mapenzi. Mama huyu alihisi kuwa sehemu hiyo ingeweza kumfanya apate ufumbuzi wa tatizo lake moja ama yote mawili yanayomtatiza.
“Usiku…” aliwaza moyoni mwake.
Kimaumbile, Unono hakuwa na umbo la kuridhisha wala hakuwahi kujidanganya kuwa ana sura nzuri. Ukweli huo alikuwa ameubaini tangu enzi za usichana wake alipojiona akikua miongoni mwa vijana wa kiume ambao walionekana kumwepuka kama jini na kumtazama kama jinamizi. Wakati huo huo aliambulia kuwaona wenzake wakifuatwa na vijana wa kiume na kubembelezwa kama malaika, wakipewa lugha tamu na matendo ya kimapenzi. Ndipo alipoanza kujitathimini katika kioo.
Akagundua kuwa pamoja na kuwa na sura mbaya, Alitisha na kuchukiza kwa jinsi alivyojengeka kama kilema ingawa hakuwa na kasoro yoyote kimaumbile. Hivyo maisha yake yaliyofuata aliishi akifahamu kabisa kuwa tunu ya kuzaliwa mwanamke yeye isingemsaidia kama wanawake wengine. Aliamini kuwa katika maisha yake lazima atoe jasho ili aweze kuishi.
Jasho lake alilitoa kwenye vilabu akiwauzia wanywaji makongoro ya ng’ombe ambayo aliyanunua machinjioni na kuyachemsha kwa maji na chumvi. Sura yake haikumtendea wema katika biashara yake. Mwanamke huyo aliyekuwa na tama zote za kike, alipata mume wa kufariji kwa kwa bahati. Na alipompata, ilikuwa mhali mwanaume huyo kumrudia. Naye Unono hilo halikumshangaza kamwe kwani hilo lilikuwa jambo la kawaida katika maisha yake. Hayo yalimtokea kwa nadra sana. Hivyo siku nyingi Unono alikuwa mhitaji. Ndipo akabuni mbinu za kutembea sehemu fulani fulani usiku, sehemu ambazo alikuwa na matumaoni ya kukutana na wanaume ambao nafsi na hali zisingewaruhusu kuchunguza. Walevi wachelewao kurejea majumbani kwao usiku, wazururaji wasio na makazi maalumu, na walinzi wanaokesha wakilinda nje usiku, hawa ni miongoni mwa wateja ambao Unono aliwahi kuwapata ili kutimiza haja zake. Baadhi waliwahi hata kumpatia pesa.
Kwa hivyo Unono akakusudia kujaribu bahati yake kwenye eneo hili lililolipuliwa na bomu. Hangekosa kufua dafu pale. Askari mmoja ama wawili wasingekosa kuwekwa hapa kwa ajili ya kulinda mazingira. mmoja wao asingekosa kumtupia maneno iwapo angecheza vema karata yake. Na hata wawe wote wawili angebabaishwa na nini angestahimili. Eti kakosa mapenzi ya mume kwa muda mrefu sasa. Ni mawazo hayo yaliyomfanya Unono afunge biashara mapema na kurejea nyumbani. Aliogaa, akajipaka mafuta yake yenye harufu nzuri, mafuta ambayo aliyanunua kwa shingo upande. Alivaa baibui lake jeusi bila vazi lingine lolote mwilini.
Alijikuta akiingiwa na wasiwasi. Alikuwa peke yake, katikati ya kiza katika eneo ambalo mchana huo lilikuwa la maafa. Akawaza kurudi, lakini alijikongoja hadi alipofika kando ya vifusi vya jumba hilo. Alitupa macho kila upande, hakuonana dalili yoyote ya mlinzi. Baada ya mizunguko kadhaa, aliamini kuwa sehemu hiyo haikuwa ikilindwa. Akasononeka moyoni.
Mara likamjia wazo jingine. Yawezekana katika jumba hili mlikuwa na vitu vya thamani ambavyo angevichukua na kuviuza! Wazo hili likamtuma Unono kuanza kuchungulia, akashika kile na kujipenyeza pale. Alipata mwanya ambao ulimwingiza ndani ya kifusi hicho. Mikono yake iliendelea kupeleleza kwa makini, macho yakifanya juhudi kutazama.
Ghafla Unono aligusa kitu ambacho kilimshitua. Kitu chenye dalili ya uhai. Nyoka? alijiuliza baada ya kuutoa haraka mkono wake. Baada ya kutulia kwa makini, aligundua kuwa alichogusa ni mwili wa binadamu. Ugunduzi wake ulimshitua zaidi. Maiti nyingine! aliwaza akiinuka na kuanza kuondoka.
Kisha ushujaa ukamwingia na kumfanya ahairishe safari yake na kuuinamia mwili huo kwa uchunguzi zaidi.
Inspekta Kombora alikuwa mgonjwa mahututi, ingawa hakuwa tayari kumweleza daktari wake kuhusu kuumwa kwake wala hakutaka kujieleza mwenyewe ni maradhi gani yanamsumbua. Alijiona tu yu hoi bin taaban, hali ambayo ilimtokea ghafla baada ya kuviona vile vipande vya mwili wa binadamu vilivyotawanywa kwa bomu. Lakini kilichomuuguza zaidi ni kuokotwa zile ndevu za bandia alizokuwa amevaa Joram Kiango.
Joram kafa! lilikuwa wazo lililomtesa zaidi ya ukweli Inspekta Kombora. Joram ambaye jina lake lilikuwa tishio kwa waovu wote wenye nia mbaya kwa nchi na wananchi wake! Joram ambaye alikubali kuiweka roho yake hatarini mara kwa mara kwa lengo la kuwakabiri maadui wenye nguvu na uwezo wa kutisha! Joram, kijana mwenye moyo wa jiwe na mwili wa chuma! Joram amekufa?…
Miaka mingi ilikuwa imepita, kiasi kwamba Inspekta Kombora hakumbuki siku gani aliyotokwa na machozi. Leo hii, akiwa peke yake ofidini, akiitazama meza yake, alihisi chozi likipenya kwenye vipingamizi vyote na kuelea juu ya mashavu yake, jambo ambalo lilimshangaza zaidi. Mshangao ambao ulimezwa na hasira kali za ghafla. Akaupiga mkono wake mezani kwa nguvu nyingi na kuvifanya vifaa kadhaa vilivyokuwa mezani hapo vidondoke sakafuni. Hakujishughulisha kuviokota.
“Joeam kafa!… aliendelea kuwaza kwa machungu.
Mara swali la kutisha likamjia akilini, Ataitangazia nini dunia iliyoamini kuwa Joram alikufa siku nyingi, atasema nini badala ya ule uongo wa kifo kilichosababishwa na sumu. Dunia ingemwelewa vipi mzee huyu mwenye dhamana kubwa serikalini.
Halafu akajikuta akitetemeka ghafla lilipomjia swali la kutisha zaidi. Nani hawa wauaji na wanakusudia kufanya nini? Kwamba, hawa si adui wa mzaha, Hakuwa na shaka na swali lake hilo. Yeyote aliyehusika kumwua Joram na hasa aliyemwua kikatili kiasi kile, hawezi kuwa mtu wa mzaha hata chembe. Wala hakuwa mtu anayecheza isipokuwa aliyedhamiria kufanya jambo baya mno ambalo hakutaka Joram Kiango aliingilie kama walivyofanya majuzi kwa kuwavunja uti wa mgongo wale waroho waliokuwa katika hatua za mwisho za kupindua nchi na kuiuza kwa mabepari. Hawa ambao wameshawishika kumwua Joram kwa bei yoyote ile wanakusudia kufanya nini?.
Ilimuumiza zaidi kujiona yeye kama mkuu wa usalama akae kimya wakati akijua kuwa kuna uovu uliojificha kando ukinyemelea, wakati huo huo akiwa hajui ni uovu gani na utatokea upande gani. Alikuwa amekwisha fanya mengi. Tangu jana wakati akitazama mabaki ya marehemu wakati yakikusanywa, alikwisha chukua hatua zote za upelelezi dhidi ya mauaji hayo. Kikosi cha askari kilikwisha teuliwa kitambo, kikifuatilia kila kichochoro ambacho kingeweza kuwafikisha mbele ya adui, Maswali mengi pia yalikuwa yakiulizwa.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)