Mtunzi: ___
SEHEMU YA TISA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Tangu jana wakati akitazama mabaki ya marehemu wakati yakikusanywa, alikwisha chukua hatua zote za upelelezi dhidi ya mauaji hayo. Kikosi cha askari kilikwisha teuliwa kitambo, kikifuatilia kila kichochoro ambacho kingeweza kuwafikisha mbele ya adui, Maswali mengi pia yalikuwa yakiulizwa.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
Lakini yawezekana kabisa maswali hayo yangeweza kuulizwa kwa miaka bila majibu kupatikana. Mtu pekee ambaye ama alikuwa na jibu tayari, ama angeweza kulipata mapema zaidi, sasa alikuwa marehemu.
Hata hivyo afanye nini? Aendelee kusubiri mtu au watu hawa wafanye yote waliyokusudia wakati yeye akiendelea kustarehe juu ya kiti hiki kama Ofisa wa Polisi alijiuliza. Afanye nini kuongeza nguvu ya mkono kuwatafuta maadui hao? Nani anaweza kuwa na walau fununu ya kinachotokea?.
Ni katika kujiuliza maswali hayo alipomkumbuka Katibu Mahsusi ya Joram Kiango, yule msichana mzuri, Neema Iddy. Akajilaumu kwa uamzi wake wa kumpinga msaidizi wake mmoja ambaye alipendekeza Neema aletwe ili amthibitishie marehemu.
“Ataonyeshwa nini? Huone kama tunaweza kumpata msichana wa watu ndoto za kutisha katika maisha yake yote au hata wazimu kwa kumuonyesha haya mabaki ya mtu aliyekuwa mwenzi na mpenzi wake?”. Kombora alikuwa amemjibu hivyo askari huyo. “Hapana”, aliongeza. “Mwacheni”.
Zaidi ya hayo, nadhani mnakumbuka kuwa hii ni siri ya watu wachache sana, watakaowajibika kufahamu aliyefariki ni Joram Kiango. Wengine wote lazima waendelee kuamini kuwa alifariki ghafla kabla ya kifo hiki.
“Sasa aliuona umuhimu mkubwa wa kumuona Neema. Hivyo bila ya kuaga wapi aendako, alipanda gari na kuielekeza iliko ofisi ya Joram.
Aliikuta ofisi hii imefungwa. Akajielekeza Temeke, ambako alifahamu jina, mtaa na namba ya nyumba ya Neema.
******************************
Ilikuwa siku ndefu kwa Neema Iddy. Ingawa kila siku ni kama siku nyingine lakini siku hii aliiona hivyo kutokana na ile harara kubwa iliyomkaria rohoni ikimtia shauku ya kumwona Joram Kiango na kutaka kufahamu hicho alichokuwa akikishughulikia safari hii, hata akaweza kujibadili na kuwa mkongwe kiasi kile, na kutangazwa uongo kuwa amekufa. Neema alihisi kuwa mkasa huu bila shaka ni wa kutisha na wa hatari kuliko yote iliyotangulia, au sivyo, Joram asingechukua hashari kiasi kile, wala polisi wasingeafiki kutangaza uongo. Ilimsikitisha Neema alipomkumbuka Joram alivyomnyima siri hiyo kwa madai ya kwamba, ni “Hatari” kumhusisha.
Siku ya jana nzima, Neema alikuwa ameshinda katika hali hiyo. Akihesabu dakika na masaa, akisubiri wakati ambao ingetanagzwa upya redioni: “Joram yu hai… Na amesababisha kukamatwa kwa wahujumu ambao…” Ni hapo alipokuwa akiishia Neema. Na ni swali hilo ambalo lilikuwa likimweka roho juu. Hamu ya kujua safari hii adui ni nani na walikusudia kufanya nini.
Neema alitabasamu, akakumbuka sifa ambayo Joram aliipata kwa kusuluhisha mambo magumu magumu. Mara hii, akawaza atailetea nchi yake gani? Wazo kuwa angetokea mtu, amshinde Joram, hasa baada ya kutangazwa kuwa amekufa, kama walivyotaka wao, swali hili halikuwa na nafasi katika fikra za Neema. Akawa mtu ambaye anasikia sifa za wapelelezi hodari duniani, pamoja na kusoma hadithi za kubuni juu ya upelelezi, Bado Neema alikuwa hakumbuki kama alikwisha tokea yeyote mwingine ambaye alikuwa na mtindo wa aina ya Joram Kiango. Mtu asiyeogopa wala kutishiwa, mtu asiyekata tamaa, mtu anayejua kila anachofanya! Neema alihisi furaha na faraja kubwa kuona kuwa yeye ni msichana pekee ambaye amepata fursa ya kushirikiana na mtu huyu shujaa. Hadhi iliyoje!.
Ni mawazo hayo yaliyokuwa yakimfanya Neema atabasamu. Lakini alihitahidi kuificha tabasamu hilo kwa huzuni ya uongo kila alipotokea mtu wa kumpa pole kwa kifo cha ‘mwajiri’ wake. Ilikuwa ni wajibu wake kujifanya yumo katika msiba.
“AMekufa kijana yule mzuri? Siamini” angesema kijana mmoja. Neema bila ya kumtazama ya kumtazama usoni angemjibu kwa masikitiko.
“Amekufa… ndiyo hali ya dunia.
Kifo cha ghafla! Wamempa sumu.
“Haijajulikana”.
“Ama kweli ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu”.
Angeondoka huyo, aje mwingine. Kila mmoja alisema hili au lile.
Neema aliwasikiliza wote na kuwafanya waondoke wakiwa wameamini kile ambacho hawakutaka kukiamini, kuwa Joram Kiango amefariki.
Neema akiwa katika hali hiyo, tabasamu rohoni, huzuni moyoni, alisikia gari likisimama mlangoni mwao na baadaye mlango wa chumba chake ukagongwa. Aliingia Inspekta Mkwaju Kombora.
Macho ya Inspekta Kombora yalimfanya Neema ahisi jambo mara moja kuwa hakukuwa na habari njema. Neema akiwa si mgeni kwa Inspekta Kombora baada ya kuzungumza naye mara kwa mara kuhusu harakati na mipango ya Joram, Neema alimjua Inspekta huyu vizuri, alifahamu wakati gani yuko katika hali mbaya kimawazo na wakati gani anajisingizia hali mbaya. Leo ilikuwa dhahiri kuwa kuna kitu kikubwa kimemkaria rohoni.
“Kuna nini Inspekta?”, Neema alihoji baada ya kumaribisha kiti.
“Joram amekufa!” Inspekta Kombora alimwambia.
“Najua”, Neema alijibu kwa tabasamu.
“Nadhani bado hujanielewa. A-me-ku-fa”, alisisitiza,
Kidogo Neema akashangaa. “Ndiyo mzee! Nadhani hata wewe unajua. Imebidi ujifanye hivyo kwa ajili ya watu hawa ambao wanamtafuta Joram. Muda si mrefu atafufuka na jambo ambalo naamini litakusisimua Inspekta”.
Kombora akamkatisha kwa kumweleza kuhusu tukio zima la bomu lililosababisha kutawanyika kwa viungo vya marehemu. “Nimeona nitakutia katika msiba na simanzi iwapo nitakuonyesha mabaki hayo ya Joram. Ama kweli kilikuwa kifo cha kusikitisha sana dada yangu. Sikuona kama ungestahili kumwona mtu uliyempenda sana akiwa katika hali kama ile”.
Ndipo Neema alipopata ukweli wa mambo ulivyo. Aliduwaa kwa muda, Macho kayatoa akimtazama Kombora wakati hamuoni. Neema alihisi damu yake imesimama kabisa na fikra kukwama. Joram kufa! Fahamu zilipomrejea, alinong’ona maneno fulani ambayo Kombora hakuyasikia. Kisha akaondoka mbio hadi chumbani kwake. Alifunua mto na kutoa bastola yake ndogo aliyozawadiwa na Joram katika moja ya sherehe zake za kuzaliwa. Akaishika imara na kuitingisha huku akipiga kelele: “Nitamwua yeyote aliyekuua Joram…” alifoka Neema, lakini sauti ilitoka ikinong’ona hata isiyafikie masikio yake mwenyewe. Alipokumbuka kuwa alikuwa hamjui mwuaji huyo, aliirejesha silaha hiy katika maficho yake ya siri na kubaki ameduwaa katikati ya chumba chake. Kisha akarejea ukumbini na kuketi chini.
“Samahani Inspekta”, Neema alisema polepole, “Kwa muda mrefu sijapata habari mbaya ya kuumiza kama hii”,
“Si habari ya kupendeza hata kidogo. Mimi pia imenitia homa. Pole sana”.
Baada ya kutafakari kwa muda, Inspekta Kombora akayarejesha maongezi yake kikazi. Alimsihi Neema kumweleza chochote anachofahamu ambacho kingeweza kupatikana kwa mwuaji au wauaji hao mapema iwezekanavyo. Hata hivyo Inspekta Kombora alivunjika moyo baada ya kugundua kuwa Neema hajui lolote la maana. Hivyo akaondoka kimya kimya kurejea ofisini kwake baada ya kumkumbusha Neema kuwa kifo cha Joram kiendelee kuaminika kuwa alifariki ghafla kwa maradhi ambayo hayajafahamika.
Neema alibaki katika hali ile ile ya butwaa, moyo ukiwa kama uliokufa ganzi na ubongo kudumaa. Alihisi kama mtu aliyefika ukingoni katika safari yake ya maisha. Kwake Joram alikuwa kila kitu. Alikuwa furaha na faraja katika maisha yake, heri na neema yake. Hakuona vipi angeweza kuyahimili maisha bila tabasam la Koram mbele yake. Hakujua vipi ataweza kusisimukwa bila harakati za Joram dhidi ya adui zake.
Mapenzi ya Neema na Joram hayakuwa yale ya kimwili kati ya msichana na mvulana. Lakini Neema aliyaona kuwa ni makubwa zaidi ya uhusiano wa aina hiyo. Makubwa yaliyojengeka katika misingi mikubwa zaidi. Ni kweli kuwa zipo nyakati ambazo Neema alijikuta akimhitaji Joram kimwili kwa tamaa kali kuliko alivyowahi kuhitaji kitu chochote. Siku kama hizo alikesha kitandani akisali kuomba Joram atokee, amkumbatie. Ni kweli pia kuwa kuna siku ambazo aliwahi kuona tamaa hiyo ikiwaka katika macho ya Joram kwa nguvu kiasi kwamba ilitokea kama mwujiza alipofaulu kutotamka kile ambacho alitamani kukitamka. Kitu ambacho jibu la Neema lisingekuwa zaidi. “Sawa tu”.
Wote walifanikiwa kuzitawala nafsi zao. Kama alivyowahi kusema Joram: “Akili isipoutawala mwili ni sawa na gari kuacha barabara na matokeo yake hakuna asiyefahamu”, Joram! ambaye sasa ni marehemu!
Bado haikukubalika kichwani mwa Neema kuwa Joram amekufa. Ilimrudia akilini siku ile ambayo alimwona Joram kwa mara ya kwanza.
Wakati huo Neema akiwa mwandishi wa habari katika gazeti moja hapa nchini. Siku hiyo alipata barua kutoka kwa mtu asiyejulikana, ikimdokeza kuwa mtu mmoja mkubwa serikalini alikuwa amehusishwa katika mauaji ya watu watatu ambao maitiza zao ziliokotwa huko Manzese. Habari hii ilikuwa imeishitua sana nchi. Neema akiwa mwandishi anayependa kuripoti habari kubwa kama hii, aliamua kwenda kutafuta ukweli na kuandika habari hii kwa undani ili kuligusa kila jicho la msomaji.
Ilibidi Neema ajifanye kuwa mwanamke kahaba ili aweze kuingia ndani ya jumba la kigogo huyo. Huko ndani Neema alifanya kila mbinu hadi kuteka mawazo ya mtumishi wa mkubwa huyo wa serikali, ambaye bila kufahamu aliweza kueleza habari zote za siri zinazofanywa na kigogo huyo. Neema alipofanikiwa kuujua udani wa mauaji hayo alitumia mlango wa uwani kutoka katika jumba hilo na kurejea ofisini kuwahi nafasi katika gazeti la kesho. Lakini hakuweza kufika mbali baada ya kujikuta akiwa katikati ya watu wanne wenye bastola ambao walimpiga na kitako kichwani Neema akapoteza fahamu. Fahamu zilipomrejea alijikuta yuko baharini, katika jahazi, mmoja wa majambazi hao akiwa amemshika kichwani na mwingine miguuni wakijiandaa wakijiandaa kumtosa majini. Alilia kwa nguvu zake zote lakini majambazi hayakuonyesha dalili yoyote ya kumuonea huruma. Mmoja wao alikuwa akisema kwa kebehi.
“Kamlilie mama aliyekuzaa na hao bwana zako waliokutuma kuchunguza mambo yasiyokuhusu”.
“Sikieni, mimi si mpelelezi…” alijaribu kusema. hakuna aliyemsikia. Wakamwinua juu na kumchezesha bembea ili wamtupe kwa urahisi. Neema alikoma kulia. Badala yake akayafumba macho yake akisubiri kifo. Ni hapo lilipotokea jambo ambalo hakuna aliyelitegemea. Mtu aliibuka ghafla kutoka mahali fulani katika jahazi hilo na kuwashambulia watu hao kwa mtindo wa upiganaji ambao Neema aliwahi kuuona katika michezo ya sinema tu. Dakika chache baadaye maadui wote walikuwa wamelala chini wakigalagala kwa maumivu. Mtu huyo alimwunua Neema na kuanza kumkumbatia huku akimtazama kwa tabasamu.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)