Mtunzi: ___
SEHEMU YA KUMI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Mtu aliibuka ghafla kutoka mahali fulani katika jahazi hilo na kuwashambulia watu hao kwa mtindo wa upiganaji ambao Neema aliwahi kuuona katika michezo ya sinema tu. Dakika chache baadaye maadui wote walikuwa wamelala chini wakigalagala kwa maumivu. Mtu huyo alimwunua Neema na kuanza kumkumbatia huku akimtazama kwa tabasamu.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
“Pole sana mpenzi”, alitamka mtu huyo baada ya kuona mshangao hauyaachi macho ya Neema.
“Umeyaokoa maisha yangu… Asante sana”, Neema alisema kwa sauti ya unyenyekevu. “U nani wewe?”.
“Naitwa Joram Kiango”.
“Joram!”, Neema alifoka kwa mshangao. Alikuwa amepata kusikia jina jilo likihusishwa sana katika kuwakabiri majambazi, wahaini na wahalifu wengine. Alikuwa amelisoma mara kadhaa magazetini. Lakini hakupata kumtia machoni. Ndio kwanza akaona hawakukosea sana wale walioandika kuwa yu kijana mzuri. Walichosahau ni kutoweka neno ‘sana’ katika sifa zake. Kwa keli Neema hakutegemea kama mtu mwenye tabia zile za kupambana na maadui wengi ana kwa ana bila hofu angeweza kuwa hivi; mzuri sana, mtaratibu sana, macho yenye upole, sauti… “Joram Kiango!” akaita tena. “Umeniokoa lakini sijui namna ya kukushukuru”.
“Huna haja”, Joram alimjibu. “Ni mimi mwenye haki ya kukushukuru. Siku zote nilimshuku mkubwa yule kuhusika katika yale mauaji lakini sikuwa na ushahidi wa kutosha. Wewe umefanya kazi nzuri Neema. Umeniwezesha kupata ushahidi mzuri. Hawa wauaji watasema ukweli watakapofika mahakamani…”
“Ni wewe uliyeandika ile barua?”, Neema aliropoka ghafla.
“Ndio”, Joram alijibu baada ya kutabasamu. Nadhani utaniwia radhi kwa kukufanya chambo. Nilikufahamu siku nyingi na kujua kuwa u msichana shujaa. Nilijua kuwa ungefanya vizuri, na umefanya vizuri… vitu vyote viwili ambavyo nilivihitaji unavyo, ushujaa na uzuri…”
Neema alijikuta akimkumbatia Joram. Walitulia kwa muda na tena kwa faraja. walipoachana Joram aliiwasha mashine ya jahazi na kuiendesha hadi pwani ya bahari ambapo aliwakabidhi majambazi hao kwa polisi. Siku chache baadaye mahakama ilitoa adhabu kali kwa ‘mkubwa’ huyo kitanzi na majamazi kufungwa kifungo cha maisha jela. Neema alipotoka mahakamani alimsaka Joram bila mafanikio. Ilikuwa baada ya wiki kadhaa walipokutana bila kutegemea. Hawakutengana tena.
Na sasa Joram amekufa, Neema aliwaza. “Yeyote aliyemwua nitahakikisha anamfuata”, Neema alifoka kimya kimya. “Naapa”.
Usiku ulipoingia ulimkuta Neema akiwa bado kaduwaa pale pale alipokuwa. Alikuwa hajatia chochote mdomoni ingawa jirani zake walimfuata mara kadhaa wakimshawishi kula. Aliinuka na kuwasha taa ya umeme. Wakati wa kulala ulipowadia, alijilaza kitandani kama kawaida na kuyafumba macho yake, lakini usingizi haukumjia. Hadi asubuhi alikuwa hajatongoa walao lepe.
Kisha mlango uligongwa na kufunguliwa polepole. Neema alikuwa amesahau kuufunga kutokana na kuzongwa na mawazo. Aliyeingia ni mtu ambaye Neema hakupata kumwona katika maisha yake yote. Mtu huyu aliyarejesha mawazo ya Neema katika ulimwengu wa kawaida, Dunia ya mtu kushutuka, kushangaa, kucheka na kukasirika. Mtu huyu angeweza kumfanya yeyote amtazamaye afanye lolote kati ya hayo. Lakini Neema alishangaa tu.
Hiyo ilitokana na umbo la mtu huyo. Neema alifahamu kuwa yu mwanamke kutokana na mavazi na matiti yake manene, ambayo badala ya kukaa kama ilivyo kawaida ya matiti katika kifua cha mwanamke haya yalikuwa kama matuta yaliyolimwa shambani pasi na mpangilio maalumu. Sura yake haikuwa na chochote kinachofaa kuitwa ‘uzuri’ Macho yake hayakupendeza kutazamwa! Pua lake! Midomo!… Neema akajikuta anatokwa na mshangao na kujikuta akiingiwa na mshituko. “Mwenzetu huyu kweli aliumbika”, Neema akajisemea.
“Naitwa Unono”, mgeni alianza kujieleza akisimama kando ya kitanda. Hakujishughulisha kujaribu kutabasamu. Wala Neema hakuona kitu kinachoitwa tabasamu kiliwahi kuupitia uso huo, Wala hakuona kama tabasamu lingewezekana kwa hali ipi. “Wewe ndiye Neema Iddy?”, aliuliza.
“Ndiyo”, Neema alijibu.
“Unamfahamu Joram Kiango?”.
Neema alibadilika na kuonekana mnyonge zaidi. “Wewe ni nani?”, Neema akahoji. Unono hakujishughulisha kujibu. Badala yake akasukuma swali lingine.
“Unajua kuwa Joram amekufa?”.
“Na… Najua. Wewe ni nani? Neema aliendelea kuhoji.
“Huna haja ya kunifahamu. Naona dhahiri kuwa u mpenzi wake. Au siyo?” Neema alipochelewa kujibu Unono akaendelea, “Unampenda kweli?”
Mbali na ubaya wa sauti ya mwanamke huyu, na ubaya wa macho yake. Neema aliona kitu kingine pia. Naam, aliona wivu. Naam, mkabala wa mwanamke huyu ulionyesha hisia fulani, wivu. Mwanamke huyu wa ajabu anamwonea wivu kwa Joram Kiango.
|Ni mpenzi wangu”, Neema akajikuta akifoka. “Ndiyo nampenda. Hata kwa kifo chake nitaendelea kumpenda. Wewe u nani na unahusika vipi baina yangu na mwandani wangu?”.
Unono hakujibu upesi. Aliutia mkono kifuani mwake na kuutoa ukiwa umeshika picha ndogo. “Kama kweli unampenda. Kama kweli utaendelea kumpenda, jitahidi umjue huyu ni nani, na anaishi wapi ili leo jioni nikija hapa uniambie wapi anapatikana”.
“Umepata wapi picha hii?” Neema aliuliza baada ya kuipokea na kuitazama kidogo, “Na picha hii inahusikaje na kifo cha Joram?”.
“Inahusika… Niliipata kwenye mifuko ya marehemu dakika chache baada ya kifo chake . Naamini mwenye picha hii anahusika. Pata maelezo kamili ya picha hiyo. Nikirudi hapa nitakueleza nini zaidi cha kufanya. “Baada ya maelezo hayo Unono aligeuka na kuanza kuondoka zake kwa mwendo wa kuchekesha.
Neema aliitazama tena picha hiyo. Ilikuwa sura ya mwanaume mwenye dalili ya heri kimaisha na kimadaraka. Lakini picha hii ilionekana kama muhusika hakujiandaa kupigwa picha hiyo. Ilikuwa sura ambayo haikuonekana ngeni sana machoni mwa Neema. “Huyu anahusika vipi na kifo cha Joram?”, Neema alijiuliza. Na mwanamke yule, Unono analijua asemalo? Akajiuliza kwanza amewezaje kumpata yeye (Neema) kirahisi hivyo katika jiji kubwa kama hili? Lazima kuna jambo hapa. Mawazo haya yakamfanya Neema aamue kufuata maelekezo ya Unono. Kwa kuwa alikuwa bado msichana tena aliyepitia taaluma ya uandishi wa habari, alifahamu wapi angeweza kupata habari za mtu huyu.
Muda mfupi baadaye Neema alikuwa njiani akielekea kituo cha mabasi. Alipanda UDA ambalo lilimfikisha mjini, Akatelemka na kuiendea ofisi yake ya awali, katika shirika moja la habari. Baada ya kupewa pole nyingi na rafiki zake kufuatia kifo cha Joram, aliomba ruhusa ya kutumia maktaba ya picha. Humo alitafuta picha ambayo inafanana na ile aliyokuwa nayo mikononi. Hakuipata, Alipokaribia kukata tamaa akawauliza wengine kijanja kama wanamfahamu mtu huyo.
Mtu wa kwanza kuitazama picha hiyo alicheka na kisha kumtazama Neema kwa mshangao. “Umeipata wapi picha hii Neema?”.
“Unamfahamu?”, Neema aliuliza kwa msisitizo akiwa na matumaini.
“Wewe Neema, yaani humfahamu huyu?” Alijibiwa kwa swali lingine. “Huyu siyo Profesa Kimara? Karibu kila mtu anamfahamu”.
“Kimara yupi?”.
“Chain Kimara. Yule Profesa ambaye anaandika kitabu juu ya uwezekano kuifanya mimea aina ya wanga inayolimwa hapa nchini iweze kukua na kukomaa haraka katika kipindi cha nusu ya muda wake wa kawaida. Huwa anakuja hapa ofisini mara kwa mara kueleza jinsi anavyoendelea na utafiti wake”,
Ilikuwa habari njema kwa Neema, Anapatikana wapi?”, aliuliza Neema.
“Nani anajua?” alijibiwa. Kwani unamhitaji kwa ajili gani Neema?”
Neema alijitahidi kumlaghai alivyoweza. Kisha akachukua kitabu cha orodha za simu na kulitafuta jina la Profesa Kimara. Haikumchukua muda kulipata, Anuani ilionyesha kuwa anapatikana katika mtaa wa India katika nyumba za msajili wa majumba namba 107. Taarifa hizo Neema akazinakiri nyuma ya picha hiyo na kisha kuanza safari ya kutoka akimshukuru mkutubi. Moyoni Neema alijaa furaha. Ilikuwa rahisi kuliko alivyotegemea.
Alirejea haraka nyumbani kumsubiri yule mwanamke aliyeleta picha hiyo. Alipoitazama saa yake aliona ni mapema mno, ingempasa kusubiri kwa masaa mengi zaidi kabla hajatokea. Neema asingeweza kusubiri kwa muda mrefu kiasi kile. Alikuwa na kiu kali ya kumpata mwuaji wa Joram. Huyu Profesa anahusikaje? Pengine anaweza kuwa na fununu fulani ya haja? Hamu ya kuyapata majibu ya maswali hayo ikaushinda nguvu wajibu wake wa kumsubiri Unono kama alivyoelezwa. Badala yake aliisoma tena anuani ile akaiweka picha mezani na kisha akatoka nje kuendea kituo cha mabasi.
Mara akahisi kitu fulani kikimnong’oneza achukue bastola yake. Akarejea ndani katika chumba chake na kuichukua bastola. Baada ya kuhakikisha kuwa bastola hii ilikuwa na risasi zake zote kwenye magazinei, akaiweka kwenye mkoba wake wa kawaida na kuanza safari upya kuelekea mtaa wa India, anakoishi Profesa Kimara.
Proper alikuwa ameketi katika chumba chake cha kusomea aliposikia kengere ya mlango ikilia akashituka. Akainua kichwa kwa mshangao. Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kugongewa mlango akiwa chumbani. Majirani zake walifanya ujirani wao wote nje. Rafiki zake ‘bandia’ aliwakaribisha nje kabisa ya nyumba hii.
Muda mfupi kabla ya mlango kugongwa, alikuwa akimalizia kuandika mpango wake kabambe ili baadaye auhariri, na kisha kuuingiza katika mtandao maalumu ambao ungeyrsafirisha maandishi hayo hadi mahali fulani katika nchi fulani huko Ulaya, kwa wakubwa zake. Mpango huo alikuwa ameubuni yeye binafsi, akauhakiki na kuona kuwa lazima utafanikiwa. Yangekuwa mafanikio makubwa ambayo yangeitetemisha Afrika na kuitikisa dunia nzima.
Kwa kuwa hili litakuwa pigo la aina yake, ambalo halijapata kuitokea dunia kwa muda mrefu. Pigo zito kama lile lililotokea wakati wa gharika lililoua watu wote na kumwacha Mungu na familia yake tu. Au kama lile bomu la Atomic lililopigwa na Mwamerika ambalo liliua maelfu ya Wajapani kule Hiloshima. Hili lake pia ingawa alikusudia kuziteketeza baadhi ya nchi, lakini litafanya machozi mengi yamwagike kiasi cha kufanya lisifutike katika kurasa za matukio ya kihistoria duniani.
Mafanikio lazima. Hakukiona kipingamizi chochote. Polisi walikuwa gizani wakitetemeka na kusubiri kwa hofu bila kufahamu wanachosubiri. Watakapotanabai, kazi itakuwa imekamilika. joram Kiango, ambaye alihofiwa kama tishio, ingawa yeye proper hakuona vipi angeweza kumletea vipingamizi, sasa yuko kuzimu. Wafu wenzake watamsimulia ilivyotokea.
Pengine tatizo lingetokana na viongozi wake huko Ugaibuni. Labda ni wao wangeweza kumpinga kutokana na woga wao. Lakini mpango huo ulikuwa wake binafisi, ameubuni, ameuandaa na lazima autekeleze. Imekwisha mgharimu muda na pesa nyingi, zake binafsi wakati akiuhakiki.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)