
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA KUMI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Alipokuja muhudumu akamuagiza amletee kinywaji kisichokuwa na kilevi cha Malta Guness, na yule muhudumu akadai pesa yake kabisa, na Inspekta Jamila akamlipa kabisa muhudumu yule.
Kiroja kilikuja yule muhudumu alipokuja, alileta chupa tatu badala ya ile moja aliyoagizwa!
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
Inspekta Jamila alifikiri labda ni “Order” ya watu wengine wameagiza. Lakini tofauti na mawazo yake, muhudumu yule aliweka mezani kwake zote zile chupa tatu! Na akasema.
“Dada uliagiza chupa moja ya Malta Guness, ila kuna Buzi moja pale limejipendekeza limekupa ofa hizi chupa mbili hivyo usilaze damu.”
Inspekta jamila alishangaa sana kwa kitendo kile, pia akichukia kufikiriwa labda ni Malaya aliekwenda pale kutafuta wanaume!
“Poh, mungu anipishie mbali”, alisema Inspekta Jamila huku akimalizia kwa msonyo hafifu.
Inspekta Jamila akiwa anapata kinywaji chake taratibu mara wakaingia watu wanne wanaume katika Hoteli ile na mara moja moyo wa Inspekta Jamila ukapiga chemba kifuani mwake!
Kwani aliweza kumuona Dokta Masawe akiwa na jamaa wengine watatu, moja kwa moja wakatafuta sehemu wakakaa.
Inspekta Jamila alipowaangalia wale jamaa kwa makini zaidi ndipo sasa alipopigwa na Butwaa zaidi!
Kwani katika wale jamaa watatu waliongozana na Dokta Masawe, kuna jamaa mmoja sura yake ilikuwa si ngeni machoni mwa Inspekta Jamila, alimtambua kuwa ni Geradi Mwaipopo! Yule mtu aliyepata kuwa askari katika Jeshi la Polisi kisha akafukuzwa kazi!
“Ndiyo yeye huyu,” alijikuta akiongea mwenyewe huku akiwaangalia wale watu kwa macho maalum!
“Hawa jamaa wana uhusiano na Dokta Masawe bila shaka Dokta Masawe atakuwa anahusika katika maswala yao,” alijikuta bado akiongea peke yake Inspekta Jamila!
“Sasa huyu Dokta Masawe nimfuate pale alipo au nimuache kusudi niwafatilie watakapoondoka ili nijue nyendo zao?!”
Alikuwa anapanga na kupangua Inspekta Jamila kwani aliona kuwa mambo sasa yameiva!
Na hata pale alipokuwa anaongea kimoyomoyo, aliangalia saa yake nakuona ni saa sita kasoro dakika kumi! Ikiwa ni tofauti ya dakika kumi tu iliyosalia ili kutimia ahadi ya kuonana na Dokta Masawe pale FRIENDS CORNER HOTEL kama alivyopendekeza Dokta Masawe!
Inspekta Jamila akajipongeza kwa kuweza kuificha namba yake ya simu alipompigia Dokta Masawe, kwani sasa hatoweza kumtambua kwa kuwa hawajawahi kukutana ana kwa ana kabla ya sehemu ile, ila yeye anamtambua Dokta Masawe kutokana na tukio moja la ajali iliyotokea pale Kibaha, na jopo la madaktari kutoka Muhimbili na hospitali zingine walipokwenda kutoa msaada ili kuokoa maisha ya watu, Dokta Masawe ndiyo alikuwa kiongozi wa msafala ule wa Madaktari!
Hivyo mara kwa mara alipokuwa anaongea kupitia vyombo vya habari, kuelezea maendeleo ya wagonjwa, Inspekta Jamila alikuwa anamuona kupitia kwenye Luninga!
Ndiyo maana hata alipoiona picha yake katika Albam ya marehemu Hamida, mara moja alimtambua!
Lakini kabla hajaongea na Dokta Masawe, kimaajabu na kiulaini anamuona pia Geradi Mwaipopo ambaye yeye alikuwa akimtafuta kwa Udi na Uvumba! Ambaye picha ya sura yake ilinaswa kwenye macho ya marehemu Kiyarwenda Mwemezi Baada ya kufanyika vipimo vya kitaalam.
Hakika Mungu ni Mkubwa kwani hakutegemea watu wale kama wangekuwa na uhusiano! Duh ama kweli usilolijua ni kama usiku wa kiza!
Inspekta Jamila akiwa pale alipo, alimuona yule Dada aliyemletea vinywaji, akiwahudumia Dokta Masawe na kundi lake, akaangalia saa yake na kuona ni saa sita kasoro dakika tano za mchana.
Dokta Masawe aliangalia saa yake kisha akawa anaongea jambo na wenzake, ambalo Inspekta Jamila kwa umbali aliokaa, hakuweza kuwasikia wanachoongea.
Mara bila ya kutarajia Inspekta Jamila alimuita yule Dada Muhudumu, na alipofika pale akamtuma akamwambie Dokta Masawe kuwa, yule mgeni wake wa saa sita ameishafika kitambo yupo pale anamuhitaji! Na yule dada kama umeme akawasilisha ujumbe ule kwenye meza ya Dokta Masawe walioijaza kwa nyama za kuchoma na pombe! Na wote waliokuwa wamekaa katika meza ile wakageuka kumtazama Inspekta Jamila.
ndipo Inspekta Jamila alipoiona sura ya Geradi Mwaipopo kwa ufasaha na uwazi kabisa, kwa haraka haraka aliwatupia macho na wale jamaa wawili lakini hakuambua kitu, kwani hakuweza kumtambua hata mmoja kati ya wale wawili!
Na nukta chache baadae Dokta Masawe alikuwa amehamia katika meza ya Inspekta Jamila wakawa wanatazamana uso kwa uso mdomo kwa mdomo!
“Ndiyo Bi Jenipha habari za tokea muda ule?” alianzisha mazungumzo Dokta Masawe, huku akilikariri lile jina la Jenifa!
Inspekta Jamila ilibakia kidogo tu aangue kicheko, kwani yeye alishasahahu lile jina alilomuongopea Dokta Masawe.
“Nzuri tu Dokta Masawe, pole na kikao. Je! wale waheshimiwa uliokuwa nao, ni miongoni mwa wajumbe katika kikao chako?”
Inspekta Jamila aliongea huku akijichekesha.
“Wewe umejuaje? Watu hawa ndiyo wanaoniweka mjini na muda huu nikawa napata kilaji hapa!”
Alijibu Dokta Masawe, na Inspekta Jamila akatambua kuwa mtu anayeongea nae , ni mualifu anaejiweka katika kivuli cha udaktari.
Ila ana kazi nyingine ya ziada tena ya haramu, inayompa pesa nyingi zinazomfanya awe jeuri na kulewa wakati wa kazi!
“Kumbe nimepatia, basi nipe zawadi yangu.”
Inspekta Jamila akazidi kujizoesha kwa Dokta Masawe ili awe naye Karibu, na hatimaye aendeleze kazi yake iliyomfanya awe pale wakati ule.
“Ehee Lete habari zako, kwani sina muda mrefu nataka kutoka, kuna sehemu nakwenda kumuhudumia mgonjwa.”
Dokta Masawe alianzisha Mazungumzo.
Inspekta Jamila, bila ya kupanga alijikuta akiongea hivi.
“Dokta Masawe Samahani sana tena sana, kwani nina mdogo wangu, amepatwa na matatizo amekuja yupo nyumbani kwangu, hivyo ninahitaji msaada wako umuhudumie!”
Inspekta Jamila aliongea kwa sauti ya upole, huku akiwa macho yake ameyalegeza, na kwa kuwa macho ya Inspekta Jamila tokea asili yake tayari yasharembuliwa! Basi alivyoyalegeza, loo Salale utadhani macho ya mtoto mchanga aliepatwa na ugonjwa wa Degedege!
Na hata kama ungekuwa mgumu kiasi gani, kwa macho yale uzalendo ungekushinda lazima!
Na ndivyo ilivyotokea kwa Dokta Masawe! Akaingia katika mtego wa Inspekta Jamila.
“Do pole sana bibie, je huyo ndugu yako amepatwa na matatizo gani?”
Aliuliza Dokta Masawe huku akionyesha huruma na moyo wakusaidia!
“Yeye amepigwa Risasi na Polisi na risasi imebaki mwilini kwake! Lakini pia imemvunja bega alikuwa katika harakati za kutafuta maisha unajua tena vijana Dokta, hivyo akiwa na wenzake, wameshafanikiwa kupora pesa, wakatokea askari wa doria na kuanza kutupiana risasi, na yeye ikampata risasi ya bega, lakini alifanikiwa kuwatoroka polisi na kuondoka!”
Inspekta Jamila, alisema maneno hayo huku akimtazama Dokta Masawe usoni mwake, na kuendelea.
“Hivyo tafadhali sana Dokta Masawe nakuomba nisaidie kama itawezekana, nitakupa kiasi chochote cha pesa ukiweza kufanikisha jambo hili tafadhali Dokta, tafadhali. Niokoe katika kadhia hii!”
Inspekta Jamila sasa aliuwa kabisa, kwani mtego huo ukinasa, moja kwa moja atakuwa analipigia mstari jibu lake tu kwamba, Dokta Masawe ana uhusiano na wahalifu, wakiwemo Geradi Mwaipopo na wenzake!
Hivyo inawezekana, majambazi kuwa wanamtumia Dokta Masawe katika maswala kama haya, kwani majambazi wanapopigwa risasi, hawaendi katika hospitali za Serikali kwa kuhofia kukamatwa na polisi, Lakini huwa wanatibiwa katika hospitali za watu binafsi au madaktari huenda na vifaa vyao katika nyumba za majambazi hao, na kuwatibia kisha kupewa pesa nyingi sana kwa kitendo hicho!
“Duh Dada unanitisha kidogo, kwani hatujazoeana kabisa, unawezaje kuniambia kitu kama hicho, na wewe nani kakwambia kama mimi nashughulika na vitu hivyo! Yaani unaniweka katika wakati mgumu na sina amani hata kidogo!”
Dokta Masawe alikuwa yupo njia panda, Pesa anaitaka, lakini pia anaogopa kwani hamtambui huyu Dada asije akawa ni askari akaingia katika matatizo, ukizingatia leo hiyo hiyo alitembelewa na askari tena wa kike!
Inspekta Jamila muda wote tokea afike Dokta Masawe alikuwa haishi kuchezeachezea simu yake mara kwa mara kama mtu aliekuwa limbukeni wa simu!
Dokta Masawe baada ya kujiumauma, mwisho wa yote akamwambia yule mwanamke mrembo aliyekuwa mbele ya macho yake, mwenye pua ya upanga iliyochongoka mithili ya pua ya kisomali, ambaye akimwita kwa jina la Jenipha akasema.
“Sawa nimekuelewa na kwa sababu yako nitaifanya kazi hiyo kwa moyo mmoja, na kijana atarejea katika hali yake ya kawaida! Je umeniandalia kiasi gani?”
“Kwa kweli Dokta Masawe kwanza nakushukuru sana kwa moyo wako wa huruma, kuhusu pesa inabidi utaje wewe Dokta, kwani wewe ndiyo mtendaji ila usinigonge sana kwani ndugu yangu atakuletea Tenda kutoka kwa jamaa zake ili nao uwe unawatibia wanapopatwa na matatizo kama yake!”
Inspekta Jamila alizidi kumtega yule Dokta dhalimu ambaye hadi kufikia pale, alikuwa anamchukia vibaya sana!
“Kwanini Dokta unafikiria kunitajia bei, inamaana hujawahi kuwatibu wagonjwa wa namna hiyo?! Kama umeshawahi wewe nipe bei kama hao ulizowapa siku za nyuma!”
Inspekta Jamila aliyasema hayo huku akiendelea kuchezea simu yake!
Dokta Masawe alikohoa kidogo kisha akasema.
“Nakuwa mzito kusema kiasi cha pesa kwa sababu sijamuona mgonjwa mwenyewe nikaweza kumkagua, ili kwanza nijue hiyo risasi imemchuna tu, au imeingia kwenye nyama, lakini pia nijue risasi ya bunduki gani iliyomuathili ndiyo ningeweza kukwambia bei kwa urahisi. Hao ambao tayari nimekwisha watibia Hospitalini kwangu na wengine majumbani mwao wote kwanza niliwaona kisha baada yakuwafanyia uchunguzi, nikawapa bei na kuwashughulikia!”
Dokta Masawe alikuwa anaeleza kitaalam namna anavyofanya kazi yake kwa ufasaha, na kuendelea.
“Labda kwako tuseme hivi, itabidi tukubaliane moja kwa moja hata kama mgonjwa sijamuona kwa kiasi cha shilingi Laki Tano!”
Inspekta Jamila alishusha pumzi nzito kwa jibu lile kwani Dokta Masawe alimthibitishia kuwa ndiyo zake, hivyo kwa kuwa yeye alikuwa yupo kazini, alikubali bila hata kulilia hali!
“Sawa Dokta nimekubali, kwani pesa kitu gani bwana, pesa zinatafutwa! Hasara Roho pesa makaratasi!”
“Thatha Bwana Mathawe ndiyo umehamia moja kwa moja kwa huyu bibie hadi jamaa dhako umetuthahau?!”
Ilikuwa ni kauli ya mmoja kati ya wale jamaa alioingia nao Dokta Masawe, na mara moja Inspekta Jamila mapigo ya moyo yakaanza kumwenda mbio!
Kwani aliikumbuka kauli ya Bwana Masudi, yule jirani yake Mwaduga, alipomwambia kuwa.
“Nilimsikia akiongea kwa kithethe, tunatho Elfu tatu tupeleke kwa macheni”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media