BARUA KUTOKA JELA (12)

Zephiline F Ezekiel
0
Mtunzi: Ibrahim Gama

SEHEMU YA KUMI NA MBILI
ILIPOISHIA...
Yule jambazi alietaka kutoroka na gari,baada yakuona wamedhibitiwa, alikuwa anatolewa chini ya uangalizi wa askari polisi, kwani alikuwa amenaswa na usukani wa gari ile.

Inspekta Jamila akamuendea yule Jambazi aliepambana nae pale alipolala ndani ya gari ya polisi na kumwambia.

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
“Kabla hatujaendelea na safari yetu, itabidi upelekwe

hospitali kwanza,ukishapata uzima safari yetu kama kazi

itakuwepo!”

Dakika tano baadae Inspekta Jamila aliondoka eneo lile

akielekea ofisini kwake, huku zile Gari mbili za askari polisi

moja ikiwa imebeba majeruhi wawili ikiwakimbiza katika

hospitali ya taifa ya muhimbili na nyingine ikimsindikiza Afande jamila!

Namna gari zile zilivyokuwa zikiondoka, na wale askari

walivyokuwa wananing’inia huku bunduki zao aina ya SMG walivyozidhibiti mikononi mwao,raia walijikuta wakishangilia kama wapo mpirani vile!

Huku nyuma magari matatu aina ya Land Rover 109

yalikuwa yanakuja kwa kasi eneo lile ili kuwahi Tenda ya

kuinua na kuivuta ile gari iliyopata ajali,zilikuwa ni ‘Break Down!’ Na hiyo ilikuwa ni saa nane na robo ya mchana mbuzi anakula majani.

*******

Saa kumi na moja ya jioni, Inspekta Jamila alikuwa ameketi

katika kiti ofisini kwa IGP akimpa maelezo ya kazi yake

kama alivyoelekezwa na bosi wake huyo.

“Afande kuna jambo linaniumiza kichwa,kwani leo ikiwa ni siku ya kwanza tu kuanza rasmi kufatilia kesi hii

nimegundua kwamba kuna watu ambao tayari wana taarifa ya mimi kuishika kesi hii! Na wanajaribu kunitisha

nisiendelee kuifanya kazi hii, kazi ambayo ina heshima

kubwa kwangu katika maisha yangu ya uaskari.”

Inspekta Jamila alikuwa anaongea kwa hisia ya hali ya juu sana,huku akionekana mzuka kumpanda.

“Hasa yule bwege aliepelekwa hospitali,yule anajua kila kitu kwani ameshanithibitishia mimi mwenyewe pale alipojaribu kuniteka!”

IGP alikuwa kimya akimsikiliza kijana wake,lakini bado akiendelea kumshangaa!

Kwani Inspekta Jamila alikuwa anajiamini na nimtendaji mzuri.

“Sasa Inspekta,hebu nipe taarifa kwanza namna

ilivyokuwa,kisha kujulikana kuwa wewe ndiyo mwenye

kesi hii tutajadili mwisho wa ripoti yako.”

IGP alimwambia Inspekta Jamila.

Nae Inspekta Jamila akamuhadithia kila kitu,toka asubuhi matukio ya kikazi aliyopambana nayo, hadi kufikia wakati ule walipokuwa wamekaa katika ofisi ile!

IGP alikuwa akimsikiliza kijana wake huku akisisimkwa na damu katika baadhi ya maelezo ya kijana wake.

Inspekta Jamila baada ya kumaliza kutoa ripoti yake,IGP alikuwa katika tafakari nzito,kisha akasema.

“Umesema ulikuwa ukiwarekodi kupitia simu yako yenye uwezo wakupiga picha za video,na wale wahalifu wote umepata sura zao, kazi nzuri sana kijana.”

IGP alimpongeza Inspekta Jamila kwa ujasiri na kuweza

kufanikisha kuwatambua wahalifu wale, lakini pia wale

aliowatia mbaroni!

“Sasa kuna kitu kimoja nataka uwelewe kutoka sasa kuwa,kwa vyovyote vile,wale wahalifu wameshakugundua kuwa wewe ni askari,tena hatari kwao!

Hivyo hata Dokta Masawe kwa kuwa ana mawasiliano na wale jamaa,kuna uwezekano mkubwa tukampoteza,hivyo

itabadi leo usiku atiwe mbaroni ili tuweze kuwakamata na wahalifu wenzake!”

IGP alikuwa anachangia mawazo yake baada yakupata ripoti kutoka kwa kijana wake.

“Sawa kabisa mkuu,pia naomba afande,yule kijana aliopo mahabusu Mwaduga Dingo,ufanyike mpango wa haraka aachiwe ili aje kuwatambua wale jamaa niliowapiga picha.”

Inspekta Jamila alitoa pendekezo kwa mkuu wake wa kazi.

“Kijana Mwaduga nilishaongea na mkurugenzi wa mashtaka kila kitu,na kesho kutwa siku ya jumatano,mkurugenzi amenambia,atamuondolea mashtaka yanayomkabili,hivyo ataachiwa huru.”

-

“IGP” alihitimisha suala la Mwaduga Dingo.

Inspekta Jamila na mkuu wake wa kazi walipanga mikakati ya namna ya kushinda kesi ile kwa ushahidi usio na chembe ya shaka, kisha wakaletewa chakula mlemle ofisini wakala, walipomaliza kula ilikuwa imeshatimu saa mbili za asiku!

“Sasa wewe nenda ukapumzike kazi nzuri sana uliyoifanya katika siku ya leo, na kama ulivyopendekeza katika ripoti yako, Afande Kubuta awe ndiyo askari utakaeshirikiana nae, hilo litakamilika na usiku huu yeye ndiye atakaekwenda kumkamata Dokta Masawe nyumbani kwake.”

“IGP” akaagana na Inspekta Jamila ambae alikuwa amechafuka na amechoka, huku yeye akiinua simu na kumtafuta Afande Kubuta na kumwita ofisini kwake usiku uleule!

Afande Kubuta alipofika alipewa mikakati yote ya kazi inayotakiwa kufanyika usiku ule, pia atafanya kazi ile akiwa chini ya Inspekta Jamila, na atatoa ripoti ya kazi yake kwa Inspekta Jamila, huku akisisitiziwa kwamba kwa kipindi hiki chote watakachokuwa wanashughulikia kesi ile, hatakiwi kujihusisha na kesi nyingine yoyote, na mkuu wake wa kituo atafahamishwa suala lile.

Inspekta Jamila alipofika nyumbani kwake alikwenda kuoga ili kupunguza uchovu, kisha akavaa kaptula na fulana nyepesi, akaisogelea Compyuta yake nakuchukua simu yake akachomeka waya kwenye simu, na upande mwingine akachomeka kwenye Compyuta.

Akawasha Compyuta na kufungua faili maalum, na baada ya muda picha za video zikawa zinaonekana.

Zilikuwa ni zile picha alizokuwa akiwarekodi Dokta Masawe na wenzake bila wao kutambua, kiasi alikuwa akionekana kama limbukeni wa simu!

Alihamisha picha zile za video kutoka kwenye simu, nakuingiza kweye Compyuta kisha hakuishia hapo, alizitoa zile picha kutoka kwenye Compyuta akazituma kwenye FLASH DISC kisha akazifuta kutoka kwenye simu yake ya mkononi.

Mara simu yake ikawa inaita alipoitazama namba ya simu ile, ilikuwa ni namba ya Dokta Zahala.

“Vipi shoga upo Nyumbani?”

Dokta Zahala aliuliza baada ya kupokelewa ile simu.

“Ndiyo Dokta vipi una habari nyingine, manaake shoga wishi habari kama Idara ya habari maelezo!”

Inspekta Jamila alianzisha utani kwa rafiki yake kipenzi.

“Nitakosa wapi habari wakati mie ni Salatul Habari? Washa sasa hivi TV stesheni ya ITV uone vitu!”

Inspekta Jamila akafanya kama alivyoambiwa na shoga yake, akaona taarifa ya habari ya saa nne usiku ikiendelea, ikionyesha lile gari lililoanguka baada ya Inspekta Jamila kulishambulia, katika lile tukio la pale Friends Corner Hotel.

Pia baadhi ya watu wakihojiwa tukio lilivyotokea, huku kila mtu akisema lake!

Jambo lile lilimchukiza sana Inspekta Jamila, kwani litaharibu upelelezi wa kesi hasa wale majambazi watakapoona taarifa ile au usikia.

*******

Dokta Masawe akiwa nyumbani kwake, aliangalia habari ile kwa makini, huku moyo ukimuenda mbio! Kwani hakuamini hata kidogo kama yule mwanamke aliekuwa akiongea nae ni Askari polisi.

“Mimi nilikuwa mle hotelini nakunywa, yule dada alipoingia pale nilimuagiza muhudumu ampe ofa ya chupa mbili, za kinywaji alichokuwa anakunywa! Alipotoka nilikuwa namfatilia kule nje, ndiyo nikakutana na kasheshe aisee! Yule dada anapiga Karate bwa shee usisikie!”

Alikuwa ni jamaa aliekuepo eneo la tukio akitoa ushuhuda kwa aliyoyaona. Na ndiye aliemfungua macho Dokta Masawe, lakini akimuudhi Inspekta Jamila!

Kwani alijua kuwa kwa vyovyote vile wale majambazi wanaweza kuona taarifa ile waka kimbia!

*******

Saa tisa kamili ya usiku, Afande Kubuta alikuwa na askari wengine saba, walikuwa katika Gari yao ya polisi aina ya Land Rover 110 Defender.

Walikuwa wameiegesha gari yao katika Baa ya Patchoto pale Kinondoni, wakiwa jirani kabisa na nyumba ya Dokta Masawe.

Wale askari wakiwa na silaha aina ya SMG walitelemka katika gari ile, na kwenda kuizingira nyumba ya Dokta Masawe!

Afande Kubuta yeye alikuwa anamuhoji mlinzi wa Baa ile, ili amtajie anapoishi, mjumbe wa Shina wa mtaa ule.

Yule mlinzi akamuelekeza katika nyumba moja ya kota iliyokarabatiwa vizuri, na Afande Kubuta bila ya kupoteza muda, alikwenda kubisha hodi katika nyumba ile.

“Ndugu Mjube mimi ni Mwana Usalama, naomba utoke nje ili tuzungumze.”

Afande Kubuta alijitambulisha, na baada ya muda yule mjumbe aliekuwa anatambulika kwa jina la Mohamedi Mwinyi Kheri alitoka huku akiwa na mashaka!

“Vipi mbona usiku jamani! Kumetokea nini katika Mtaa wangu?”

Mjumbe Bwana Mohamedi Mwinyi Kheri alimuuliza yule afande aliekuwa amevaa koti la kipolisi.

“Samahani Ndugu mjumbe kwa kukusumbua saa hizi ukiwa umepumzika, ila tunakuhitaji kwani katika mtaa huu, tunataka kuingia kwenye nyumba ya Dokta Masawe ili tumpekuwe katika nyumba yake, lakini pia twende nae kituoni kwa mahojiano zaidi, hivyo nataka uwe shahidi tutapokuwa tunafanya hivyo.”

Afande Kubuta alimwambia Mjumbe wa nyumba kumi Bwana Mohamed Mwinyi Kheri. Na dakika tatu baadaye wanaume wale walikuwa ndani ya nyumba ya Dokta Masawe.

Dokta Masawe hakuwemo mle ndani toka saa nne na nusu ya usiku!

“Alipokwisha kuangalia taarifa ya habari, walikuja wenzie wakamfuata!”

Yalikuwa ni majibu ya Mke wa Dokta Masawe ambayo yalimwacha hoi bin taabani Afande Kubuta na vijana alioongozana nao!

“Je alikuaga kuwa anakwenda wapi?” Afande Kubuta alimuuliza yule Mama wa kichaga mke wa Dokta Masawe.

“Hapana kwa kweli Babangu, hakusema anakwenda wa..wapi kweli. Yeye alisema anatoka mara moja hatochelewa kurudi ila sisi tufunge milango, atakaporudi atatugongea!”

Mke wa Dokta Masawe, alikuwa akiongea kwa lafudhi ya kichaga, alikuwa anajibu akiwa na uhakika na majibu yake.

Afande Kubuta alikuwa amehemewa! Kwani sasa mambo yote yalikuwa yameelekea kwenda kombo.

“Sasa?!”

“Hakuna cha sasa, hapa tutamsubiri hadi asubuhi, mjumbe wewe nenda kapumzike, huyu bwana atakaporudi tutakwita!”

Yalikuwa ni majibu ya Afande Kubuta alipokuwa anamjibu mke wa Dokta Masawe aliposema sasa, akiwa anataka kujua kinachoendelea!

“Humu ndani ya nyumba yangu hamtosubiri peke yenu, labda awepo na mjumbe, kwani pia mtu mliyemfata hamkumkuta, hata mlipoingia vyumbani kumtazama hamkumuona sasa mtabakiaje humu?!”

Mke wa Dokta Masawe alikuja juu akiwa amekasirika, asionyeshe woga hata kidogo!

“Samahani jamani sio kama naingilia kazi yenu, ila huyu mkewe ampigie simu mumewe amuulize alipo nasi tutajua chakufanya!”

Mjumbe alitoa rai na mke wa Dokta Masawe akajibu mara moja

“Simu yangu haina Dola mzee!”

Afande Kubuta akatoa simu yake akataka namba ya simu ya Dokta Masawe, Mke wa Dokta Masawe alichukua Business Card pale sebuleni walipokuwa wamekaa nakumpa Afande Kubuta.

Afande Kubuta aliipiga namba ile zaidi ya mara tano lakini ilikuwa haipatikani ilikuwa imefungwa!

“Lakini kwani mume wangu amefanya nini?”

Mke wa Dokta Masawe alitaka kujua, kwani mumewe haijawahi kutokea hata mara moja akafatwa na polisi namna vile, kwake kilikuwa ni kitu cha ajabu sana.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

 Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)