
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA KUMI NA TATU
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Lakini kwani mume wangu amefanya nini?”
Mke wa Dokta Masawe alitaka kujua, kwani mumewe haijawahi kutokea hata mara moja akafatwa na polisi namna vile, kwake kilikuwa ni kitu cha ajabu sana.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
Lakini hakuna askari yeyote kati ya wale sita waliokuwa mle ndani, nadhani hata askari wa saba aliebaki kwenye gari ambae ni Dereva kama angeweza kumueleza yule mama, mumewe alichofanya!
Hata Mjumbe Bwana Mohamed Mwinyi Kheri alipoamua kubaki na wale askari nyumbani kwa jirani yake, hakuwa Dokta Masawe wala simu yake aliepatikana mpaka jua likawapambazukia.
Wana Usalama wale wakaondoka na mjumbe wa shina huku wakiwa patupu!
Siku ya jumanne saa mbili asubuhi Inspekta Jamila alikuwa yupo Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kwa mambo mawili.
Kwanza kuchukua maelezo ya wagonjwa wake!
Pili kumkamata Dokta Masawe kwa mikono yake, baada ya Afande Kubuta kumpa taarifa kwa ufupi kupitia njia ya simu kuwa hawakufanikiwa kumtia mbaloni, kwani hakulala nyumbani kwake!
Dokta Masawe huwa ana Clinic siku ya jumanne pale muhimbili, kitengo cha MOI.
Hivyo kwa vyovyote vile angekwenda kazini tu, na yeye angemtia mikononi kiulaini!
Akaamua aanzie katika wodi ya Kibasila walipokuwa wale majeruhi wake waliolala na pingu mikononi mwao.
Jibu alilolipata huko lilimrudisha nyuma hatua hamsini kikazi!
“Ninasikitika Afande tumejaribu kuokoa maisha ya hawa wagojwa bila mafanikio, kwani huyu mmoja moyo wake ulikuwa umepasuka na kumwaga damu nyingi ndani kwa ndani. Lakini hata katika kichwa chake amepata athali kubwa, kwani ubongo wake wa nyuma katika kisogo MEDULA OBLANGATA ulivurugika na damu, hivyo katika hali kama hiyo mtu hawezi kuishi; huyu alifariki dakika ishirini toka kufikishwa hapa!”
Daktari aliekuwa anawatibia wale jamaa wawili alikuwa anamfahamisha Inspekta Jamila namna ya yule jamaa aliepambana nae namna alivyokuwa ameumia na kupelekea kifo chake, akalikumbuka teke lake aina ya MAIGERI, lilivyotua usawa wa kifua na jinsi yule jamaa alivyoangukia kisogo.
Mara moja akatambua Medula Oblangata pale ndipo ilipochokozwa!
“Dah nimekuelewa Daktari je na yule mwenzake nae vipi?”
Inspekta Jamila alitaka kujua kuhusu yule jambazi aliyepinduka na gari baada ya yeye kupiga mipira yote miwili ya nyuma ya gari ile kwa risasi na kupelekea kupinduka kwa gari ile.
“Yule nae alifariki saa mbili baadae tangu alipofikishwa hapa. Yule alikuwa na tatizo la kukosa hewa kwani mbavu zake sita zilivunjika, tatu kila upande na hata kama angepona asingefanya kazi yoyote yule!”
Hiyo ilikuwa ni ripoti ya Daktari aliekuwa akiwahudumia wagonjwa wale toka walipofikishwa Hospitalini pale jana yake.
Inspekta Jamila alipelekwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti pale Muhimbili na kuonyeshwa maiti zile, na akawatambua na akawapiga picha katika nyuso zao!
Kiasi Roho ya Inspekta Jamila iliingia simanzi kidogo alipoiona ile maiti ya yule jamaa aliemwambia “UHAI WAKO NIMEUSHIKA UPO MKONONI MWANGU”
Inspekta Jamila alitoka katika wodi ya Kibasila na kuelekea Moi, ofisini kwa Dokta Masawe, alisubiri sana, sasa akiwa yupo katika benchi walilokalia wagonjwa waliokuwa wanasubiri huduma ya Dokta Masawe, lakini hadi inatimu saa nne kulikuwa hakuna dalili za Dokta Masawe bali daktari mwingine aliingia kwa dharula na kuwahudumia wagonjwa!
-
Inspekta Jamila akakata shauri kuwa, kwa kuwa waliahidiana wakutane pale Amana Ilala, basi akaandae mtego wake. Alitoka nakuiendea gari yake akiwa yupo katika mawazo tele na mwendo wa haraka mara, simu yake ya mkononi ilikuwa inaita. Ilikuwa ni namba iliyopigwa katika mfumo wa Private namba!
Inspekta Jamila akasita pale alipo, kisha kabla hajapokea simu ile aligeuka na kuangalia sehemu yote ile ili kuangalia kama kuna mtu yoyote anaepiga simu, akaona patupu!
Akaendelea kuifata gari yake huku simu ile ikiendelea kuita, akafungua mlango wa gari na kuingia ndani!
Na ile simu ikakatika wala na yeye asihangaike tena na simu ile,kwani alikumbuka yeye alivyomcheza shere Dokta Masawe, akachelea na yeye asije fanywa hivyo!
Inspekta Jamila alikuwa akiendesha gari yake kuelekea ofisini kwake walipokubaliana na Afande Kubuta wakutane ili ikiwezekana leo wafunge kazi, kwa kuwakamata wahalifu wale wanaotoa roho za watu kwa sababu ya mali ambayo hawakuitolea hata jasho katika kuichuma. Kwani mwenye mali masikini ya mungu huangaika kwa miaka na miaka, kisha hawa madhalimu wanakuja kuchukua kwa siku moja, lakini pia wanakutoa na roho yako au wakuache majeruhi! Udhalimu wa hali ya juu kabisa huu.
Inspekta Jamila aliendesha gari yake akitokea Muhimbili, akaingia Mtaa wa Malik, alipofika Makutano ya Malik na Umoja wa Mataifa, aliacha barabara ya Mtaa wa Malik na kupinda kushoto kuchukua barabara ya Umoja wa Mataifa. Asubuhi ile kulikuwa na foleni kidogo hivyo alitembea na gari taratibu kiasi, hadi akafika Makutano ya Barabara ya Ally Hassan Mwinyi na Umoja wa Mataifa, akakata kulia kushika njia ya Ally Hassan Mwinyi akaendesha gari yake kwa kasi kidogo kwa kuwa askari aliyesimama pale kwenye taa za Makutano ya barabara inayokwenda AGA KHAN HOSPITAL na ALLY KHAN ROAD, alikuwa anazivuta sana, gari zinazotoka daraja la Salender katika barabara ile ya Ally Hassani Mwinyi.
Katika makutano ya barabara ya Ohio na Ally Hassan Mwinyi , alichepuka kushoto kuelekea Mtaa wa Ohio na kabla hajafika Jengo la PPF akakata kulia kuingia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, akapitiliza hadi nyuma katika ofisi za mbao ambapo ndipo ofisi yake ilipo, akaiegesha gari yake katika maegesho, na kushuka kuelekea ofisini kwake ambapo baada ya kuingia tu alimkuta Afande Kubuta ameshajaa tele kama pishi ya mchele akimsubiri!
Baada ya salaam za utii za itifaki walikaa kujadili namna ya kuendelea na upelelezi kutoka pale walipofikia.
Afande Kubuta alitoa taarifa kwa kirefu namna walivyokwenda kwa Dokta Masawe kwani alishampa ripoti ya jambo hili, ila alimpa kwa muhtasari tu, sasa akamweleza A – Z.
“Hadi ninakuja hapa askari tuliembakiza kuangalia kila anayeingia na kutoka kwa Dokta Masawe bila yeye kujulikana amenipigia simu muda si mrefu kuwa Dokta Masawe hajarudi nyumbani kwake!”
Afande Kubuta alikuwa anampa ripoti yake Inspekta Jamila.
“Sawa Afande kazi nzuri, sasa mimi nina simu ambayo jana niliongea na Dokta Masawe baada ile ya Voda kumkosa, hivyo nataka tumpigie kutumia simu namba ile.”
Inspekta Jamila alimwambia Afande Kubuta, na Afande Kubuta akashangaa aliposikia neno hilo, akashindwa kujizuia na akasema.
“Afande tunachelewa tumpigie sasa hivi.” Alisema Afande Kubuta!
“Hapana Afande Kubuta, huyu tunatakiwa tumpigie simu tukiwa Computer Room, na kama atapokea simu wakati huo, basi atakuwa anatusogeza hatua thelathini mbele.”
Inspekta Jamila alimwambia Afande Kubuta, na hata alipokwisha kusema maneno yale, Afande Kubuta alikuwa anatabasamu huku akimpa tano Inspekta Jamila.
Wote kwa pamoja Inspekta Jamila na Afande Kubuta walinyanyuka vitini wakaelekea katika chumba cha mawasiliano kilichosheheni Computer, wakaeleza shida yao kwa mtu wa mawasiliano anaeitwa Dihenga ambaye pia ni askari.
baada ya kuweka mambo sawa Inspekta Jamila akampigia simu Dokta Masawe huku akiomba mungu simu ile isiwe imezimwa.
Na baada ya sekunde kadhaa simu ya Dokta Masawe ikawa inaita.
“Hollow nani mwenzangu?!”
Dokta Masawe alipokea simu huku akiwa anahema ile mbaya.
Wakati huohuo Dihenga bila kufanya ajizi akafanya vitu vyake!
“Jenifa hapa Dokta nilikuwa nakukumbusha kuhusu ahadi yetu.”
Inspekta Jamila alianzisha mazungumzo mara moja.
“Dah! Afadhali nimekuona, Aha Samahani afadhali nimekusikia, kwani nilikuwa natafuta namna ya kukupata nikawa nashindwa kwani namba yako ya simu hukunipa. Nimepatwa na dharura nimesafiri toka jana usiku hapa nipo Moshi. Sasa ile kazi yako sitoweza kuifanya kwa kweli. Kwani sitarajii kurudi siku za hivi karibuni. Hivyo tafuta Daktari mwingine.”
Dokta Masawe huku akibabaika kweli kweli, alisema kisha akakata simu, kabla Inspekta Jamila hajaongeza neno lolote, kwani alishambaini kuwa yule ni askari kanzu na wala hana mgonjwa!
Inspekta Jamila ilipokatwa ile simu, akamgeukia afande Dihenga, kama mtu aliekuwa anataka kuelezwa kitu!
Afande Dihenga, akiwa anavua vifaa vya mawasiliano masikioni mwake, alimnyooshea alama ya kidole gumba Inspekta Jamila.
Inspekta Jamila, kwa wahka mkubwa akamwambia afande Dihenga.
“Nipe uelekeo tafadhali.”
“Tabata Segerea, Bs motel”
Afande Dihenga alijibu huku akitazama compyuta ilyokuwa mbele ya macho yake.
Bila ya kupoteza muda, Inspekta Jamila alimpa tano afande Dihenga, akatoka na afande Kubuta, wakiwa tayari kuelekea Tabata Segerea.
Askari wale wakiwa katika gari lenye namba za kiraia, mali ya Jeshi la Polisi gari aina ya Toyota Soluna walikuwa wanaitafuta Tabata Segerea.
Dakika arobaini baadae gari ile waliiegesha nje ya jengo la Hotel ya BS, pale eneo la Segerea.
Afande Kubuta na Inspekta Jamila wakateremka ndani ya gari ile wakionekana kama Bibi na Bwana wakajichoma ndani ya Hoteli ile.
Walipoingia tu pale ndani katika sehemu ya kupatia vinywaji, walikutana uso kwa uso na Dokta Masawe akiwa anapata kilevi.
Hali aliyokuwa nayo Dokta Masawe baada ya kumuona Inspekta Jamila, pombe yote ilimtumbukia nyongo!
Kwani alitahayari kama mtu aliyefumaniwa akiwa katika ugoni.
Inspekta Jamila na Afande Kubuta wakakaa katika viti vitupu vilivyokuwa katika meza ya Dokta Masawe na Inspekta Jamila akamsalimia Dokta Masawe.
“Habari ya safari ya Moshi Dokta vipi umerudi kwa concord?!”
Ilikuwa ni salamu ya uzushi na dharau kutoka kwa Inspekta Jamila.
Dokta Masawe hakuweza kusema chochote bali alikuwa amejiinania huku akiwa na wasiwasi na hofu.
Kitendo bila ya kuchelewa Afande Kubuta alitoa pingu akamfunga nazo mikononi Dokta Masawe.
“Kwa nini mnanifunga pingu hali sijakataa kwenda huko mnapotaka kunipeleka. Hii siyo sheria bwana, nitawashitaki kwa kitendo hiki cha kunidhalilisha!”
Dokta Masawe alikuwa anatatalika kama bisi kikaangoni.
Lakini wapi bwana alichukuliwa kituuteni hadi ndani ya gari na safari ya mjini ikaanza.
Dokta Masawe hakika alikuwa amepatikana kweli kweli, ikawa hana jinsi ila kuyakubali matokeo, akawa muumini mtiifu wa ule msemo usemao, kubali yaishe!
Wakati Afande Kubuta alikuwa anaendesha gari, Inpekta Jamila alikuwa anamchunga Dokta Masawe aliyekaa naye katika kiti cha nyuma ya gari ile, huku akiiperuzi simu ya Dokta Masawe.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media