
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA KUMI NA TANO
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Inspekta Jamila na Afande Kubuta walikuwa wanatingisha vichwa kwa huzuni ,wakimsikitikia marehemu Bartazal kwani niya yake njema, imemtoa roho yake
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
Dokta Masawe alifuta machozi kisha akaendelea.
*Nilipomkubalia alinipiga busu zito, akaniachia na pesa shilingi Elfu hamsini tasilimu, akaniaga nakutoka. Baada ya kama wiki tatu baadae Hamida alikuja na mumewe ili kuja kupima ujauzito, nami nikajua mchezo umeshaanza! Nilimchukua vipimo vya damu ya mshipa pamoja na mkojo wake nikajifungia navyo maabara, nilipotoka nilimpa Hongera Bwana Bartazal na atarajie mtoto wa kiume!
Kwa kweli Bwana Bartazal alionyesha furaha isiyo kifani, kwani alimkumbatia mkewe na kumbusu mbele yangu, huku akiniambia, Dokta niliwahi kuahidi mbele yako kuwa mke wangu akipata ujauzito, nitamuandikisha mali zangu zote, kwa kuwa hili limetimia, basi na mimi sina budi ila kutimiza ahadi yangu kwani Ahadi ni deni!*
*Bwana Bartazal alimuandikisha mali zake zote mkewe.
Ilipofika miezi mitatu Hamida akanijia nakuniambia, sasa umefika wakati wakupata Robo ya mali yangu, kama tulivyokubaliana, na ili jambo hilo litimie, bado juhudi zangu zinahitajika!
Nazo nikumpa mbinu ya kumuuwa mume wake mpendwa Bwana Bartazal Halim.
Nikifanikisha hilo, muda si mrefu nitafungua Hospitali kabisa, badala ya Zahanati! Nami kwa kuwa Shetani alikuwa anatawala mbele yangu, nikampa vidonge vya SALBUTAMOL kumi ili amtilie kwenye Juice. Nakweli Hamida alivichukua vidonge vile nakumtilia mumewe vyote kwenye Juice kama nilivyomuagiza, na mara yule bwana alipokunywa Juice ile, saa moja baadae akawa marehemu Baltazar!*
Inspekta Jamila na Afande Kubuta walikuwa wanatingisha vichwa kwa huzuni ,wakimsikitikia marehemu Bartazal kwani niya yake njema, imemtoa roho yake.
Ama kwa hakika Mbega hufa kwa uzuri wake!
Dokta Masawe alikuwa anafuta machozi pamoja na uharamia wake alioufanya lakini alikuwa anaijutia nafsi yake, ama kweli Damu nzito kuliko maji.
*Okey nini kikaendelea?*
Afande Kubuta akamuuliza Dokta Masawe.
*Kilichoendelea Hamida saa moja baadae alipohakikisha kuwa mumewe amekwisha fariki, alikwenda kuimwaga ile juisi iliyobaki, na akatungua kilio kikubwa ili kujaza watu, na kweli majirani zake wakajaa nyumba tele nakuuliza kulikoni, akawaambia kilichojiri ni kwamba, yeye Hamida alikuwa amelala akamuacha mumewe anaangalia Tv, sasa baada yakugeuka nakuona mumewe hajarudi kitandani, akatoka sebuleni ndipo alipomkuta mumewe yupo katika hali hiyo wanayomuona nayo, huku akisisitiza kuwa ameshamuamsha sana bila mafanikio!
Na hapo wale majirani wakatoa wazo la mwili ule kupelekwa Hospitali ili ukachunguzwe kilichomsibu bwana Bartazal, lakini pia Daktari ndiyo akathibitishe kama Bartaza amekufa!
Hapo Hamida akashauri mwili ule uletwe kwangu kwakuwa mimi ndiyo Daktari wao, na hata waliponipigia simu kunifahamisha kilichojiri, mimi niliwaambia nitakwenda mwenyewe pale kwake ili nikamchunguze na kumchukua vipimo!
Hata nilipofika pale na kumchunguza yule Bwana ukweli ulibaki palepale kuwa yule bwana alikwisha fariki!
Niliwathibitishia kwamba mwili ule ni wa marehemu, na amekufa kiasi cha saa moja nyuma, na kilichosababisha kifo chake ni Presha! Iliyosababishwa na mshtuko wa kuona au kusikia jambo lililompa mshtuko nakupelekea kifo chake!*
*Sawa Dokta Masawe hadi sasa tumeelewa Makoko na Matandu ya kifo cha Bwana Bartazal Halim, je na kifo cha Hamida nini kilikuwa chanzo kwa jinsi unavyoelewa, kumbuka kutuambia ukweli kwako kunaweza kusababisha tusichukue hata senti tano yako, na wewe tukakuachia huru!*
Inspekta Jamila alikuwa anatumia DIPLOMASIA zaidi ili kumlegeza Dokta Masawe, kuliko kutumia nguvu isiyokuwa na lazima.
Kama wafanyavyo baadhi ya askari wenzake, wanapotaka kujua jambo Fulani kwa mtuhumiwa!
*Kifo cha Hamida kwa kweli kilitokana na yeye kunizima mafao yangu. Baada yakumkamilishia kazi yake, kwani alikuwa ananikimbia akabadilisha mpaka namba ya simu, kwa kuwa Mshahara wa dhambi ni mauti, nami sikukubali kupata Dhambi za kuua bure bileshi, hivyo nikawatuma majambazi wakenda kummaliza Hamida ili tukose sote. Nalitote tugawane mbao!*
Dokta Masawe kwakadiri alivyokuwa akisema ukweli, alijuwa baadae atakuwa huru hivyo hakuona sababu ya kupindisha maelezo!
Afande Kubuta akamuuliza Dokta Masawe. *Hao Majambazi uliowatuma uliwapataje?*
*Majambazi walio wengi ninawafahamu. Kwani wanapopambana na polisi,na kujeruhiwa na risasi huja katika Zahanati yangu nami huwatibia kwa siri, kisha hunipa pesa nyingi sana, ambapo mgonjwa wa kawaida hawezi kutoa pesa hiyo hata kwa nini, na kwa kiasi kikubwa ukiwa na watu wale kazi ya Udaktari utaiona inalipa sana, ingawa kuanzia sasa sitaki tena kufanya biashara ile!*
Inspekta Jamila akamuangalia Dokta Masawe kutoka chini hadi juu, kisha akatingisha kichwa na akasema.
*Unazo taarifa kama Dereva wa Taxi anaeitwa Mwaduga Dingo, yupo ndani mahabusu kwa kosa la mauaji ya Hamida? Na Je! Unamfahamu kijana huyo, na anahusika na chochote katika mauwaji yale, kwani wewe ndiyo ulieyapanga mauaji ya Hamida na unawajuwa watu waliofanya mauwaji yale!*
*Hapana yule Chalii hausiki hata kidogo, kwani yule aliwapakia kina Baajuni siku ile wakitokea Zahanati kwangu kuchukua malipo ya kazi yao, na walikuwa wanakwenda Baa ya Macheni ili kukutana na Kiongozi wao, ambae mimi sijawahi kukutana nae hata siku moja.
Sasa walipofika pale wakawaona askari wa Doria, na wao kwa mapepe yao wakakimbia bila sababu, wakidhani kuwa bosi wao ameshakamatwa, na pale walikuwa wanasubiriwa wao, kumbe sivyo!*
Dokta Masawe alikuwa akimkataa Mwaduga Dingo kwamba hamfahamu ila bahati mbaya tu imemkumba kwani LILILOKUWA LA KUKUPATA, HALIKUWA LA KUKUKOSA NA LAKUVUNDA HALINA UBANI!
Na mara simu ya Inspekta Jamila ikaita. Alipoangalia saa yake ilikuwa inaonyesha ni saa tisa na robo!
*Duh kumbe muda umekwenda hivi!* aliwaza kisha akaipokea simu, mambo aliyoelezwa kwenye simu kamwe hakuyaamini masikio yake, lakini ndivyo ukweli ulivyotokea.
Wale askari walioagizwa na Inspekta Jamila kwenda kule Baracuda, wamempigia simu wakimueleza kuwa; Jambazi Geradi Mwaipopo limevunja mtego wa polisi, nakufanikiwa kutoroka, lakini pia amejeruhi askari wawili kwa risasi!
Taarifa hiyo ilimpa wakati mgumu sana Inspekta Jamila na hakutaka kusema taarifa ile kumwambia Afande Kubuta mbele ya Dokta Masawe, hivyo wakaendelea kunyonya taarifa kutoka kwa Dokta Masawe mpaka waliporizika kwa yale waliyoyapata!
Ila kitu ambacho sio Dokta Masawe, wala Afande kubuta alichokuwa anajuwa kuwa mazungumzo yale Inspekta Jamila alikuwa Anaya record kupitia Simu yake kwa njia ya Video na Audio!
*Haya sasa jamani yote mliokuwa mnayataka kutoka kwangu, nimewaeleza,na hata aliyonihadithia Marehemu Hamida nimewaambia, basi tumalizane ndugu zangu na nawaahidi sitofanya tena jambo kama lile Yesu na Maria!*
Dokta Masawe alikuwa anataka msamaha kwa gharama yoyote ile!
*Sawa Dokta Masawe tumekuelewa, lakini bado hujatupeleka au kutuelekeza wanapo patikana wale watu tunaowatafuta, hivyo kuwa kwako nje kutatufanya tuharibu upelelezi, au kwa njia rahisi tu niseme, sisi askari polisi, hatuna mamlaka ya kumaliza kesi kienyeji, hivyo fanya subira ili sheria ichukue mkondo wake, kwani hadi hapa tulipo una mashitaka mawili yakujibu tena yote ya mauaji, yaliyotokea katika nyumba moja na yanawahusu Mke na mume!*
Inspekta Jamila aliposema maneno haya, Dokta Masawe alikuwa analia kama mtoto mdogo aliekimbiwa na mzazi wake!
****
Siku ya jumatano katika jiji la Dar es salaam, upepo ulikuwa unavuma kutoka mashariki kwenda magharibi, hivyo kufanya eneo lile la Mwambao wa pwani, kuwa na hewa safi.
Watu walikuwa wengi katika eneo la Mahakama ya Mkoa wa Dar es salaam, Maarufu kwa jina la Mahakama ya Kisutu.
Mahabusu walikuwa wameshaletwa kutoka magerezani na vituo vya Polisi, miongoni mwao alikuwepo mtuhumiwa wa kesi ya Mauaji, dereva wa Taxi, Mwaduga Dingo aliekuwa ameshika tama muda wote toka waliposhushwa kutoka katika basi la magereza wakitokea Gereza la Keko, wakikutana na watuhumiwa kutoka katika gereza la mahabusu la Segerea.
Nje ya mahakama walikuwepo watu wengi waliokuwa wakiwafuatilia ndugu zao, walikuwepo waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali, na katika pembe moja ya eneo lile alikuwepo Eshe Muhidini mke wa Mwaduga Dingo, na jirani yao Bwana Masudi pamoja na mkewe.
mtoto wa Mwaduga anaeitwa Marijani, anaepata miaka mitatu na nusu au mine akiwa amekaa chini katika kivuli cha mti, jirani na mama yake akichezea kokoto wala hana habari na dunia inavyokwenda. Mara ikasikika sauti ikisema
*Mahakama karibu inaanza, hivyo wale wote waliokuja katika mashauri ya kesi, waingie mahakamani na muhakikishe mnazima simu zenu*
Lilipokwisha tangazo lile, Eshe alimbeba mtoto wake na akajongea Karibu huku akiwa ana kiherehere cha hali ya juu sana.
*COOOOOOOOOOOORT*
Sauti ya askari mkakamavu ilikuwa inaashiria kuwa Muheshimiwa Hakimu alikuwa akiingia mahakamani hivyo pia kuashiria watu wote wasimame ili kumpa heshima muheshimiwa.
Muheshimiwa Hakimu mkazi alikaa katika sehemu yake, na mara moja taratibu za kimahakama zikaanza.
Kesi ya tatu kutajwa ilikuwa inamuhusu Mwaduga Dingo,na ilipotajwa namba ya kesi yake na karani wa Mahakama, Mwendesha mashtaka wa serikali akasimama baada ya karani kukaa katika kiti chake, akiwa na faili la kesi ile akasema.
*Niipendeze Mahakama yako Muheshimiwa, naitwa Mabewa wakili wa Serikali naiwakilisha Jamhuri, Shauri hili lilikuja kwa kutajwa upelelezi wake bado unaendelea, ila kutoka kwa mkurugenzi wa mashitaka kanda ya Dar es salaam nina NOLLE PROSEQUI UNDER SECTION 91(1) OF CRIMINAL PROCEDURE ACT, 1985 (CAP 20 R.E 2002)*
Ilikuwa ni kauli ya muendesha mashtaka Wakili wa Serikali akiifahamisha Mahakama hatua ya kesi ya Mwaduga ilipofikia wakati huo huo alifungua Jalada la Kesi ile na kutoa Ganda gumu la njano na kumkabizi Karani wa Mahakama ili ampe Muheshimiwa Hakimu kwa uthibitisho, na hatimae kutoa maamuzi.
*Mshitakiwa Mwaduga Dingo kuanzia sasa Mahakama yangu imekuachia huru unaweza kwenda.*
Muheshimiwa hakimu baada ya kuipitia ile karatasi ya njano, alitoa maamuzi.
Ama kwa hakika Mwaduga Dingo aliiona nyota ya Jaha!
Furaha iliyochanganyika na huzuni ilitawala katika kichwa chake, akashindwa kuamini ukweli kwamba yupo huru,alihisi yupo ndotoni.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media