
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA KUMI NA SITA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Ama kwa hakika Mwaduga Dingo aliiona nyota ya Jaha!
Furaha iliyochanganyika na huzuni ilitawala katika kichwa chake, akashindwa kuamini ukweli kwamba yupo huru,alihisi yupo ndotoni.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
Machozi yakambubujika mfululizo, huku akiwa anateremka kutoka kizimbani, akawa anajisemea ndani ya moyo wake.
*Yote yalionifika, namuachia manani
Ni yeye alietaka, mimi kuwa gerezani
Tabu dhiki na mashaka, nivijuwe kwa undani
Katu sidai fidia, mola atanilipia!*
*Mke wangu mtukuka, na mwanangu Marijani
Sameheni bila shaka, mtaingia peponi
Kila linalokufika, mja kwako mtihani
Katu sidai fidia, mola atanilipia!*
*Kusamehe kwa hakika, ndiyo bora duniani
Kwa dhati ninatamka, sina kinyongo moyoni
Ila hayatafutika, hadi niwe kaburini
Katu sidai fidia, mola atanilipia!*
Eshe akiwa na mtoto mgongoni, alishindwa kujizuia alipomuona mumewe anatoka nje ya Mahakama ile akiwa huru, alilia kilio cha furaha huku mke wa Masudi akimbembeleza.
Mwaduga alipotoka tu pale nje ya mahakama waandishi wa habari walimzonga, huku Camera zao zikichukua picha kwa ajili ya magazeti na picha za Televisheni.
Wakiwa katika mahojiano. Mara walitokea polisi na kutimua watu kisha wakamkamata Mwaduga na kumtia ndani ya gari ya polisi aina ya Land Rover Difender 110 na kuondoka nae kituuteni, hadi kituo cha kati cha polisi mkabala na Relwe Stesheni.
-
Huku nyuma yakaachwa maswali kadhaa, huku wale waandishi wakifanikiwa kupiga picha za video tukio lile!
Eshe sasa alikuwa hajitambui kwa kilio, kwani alikuwa anagalagala chini kama mtoto mdogo!
Mwanae analilia huku na yeye analia kule, kukawa kati ya mama na mtoto hakuna wakumnyamazisha mwenzie, tafrani moja kwa moja!
Masudi alikuwa haamini macho yake kwa kitu kilichotokea, kwani rafiki yake ameshaachiliwa huru na mahakama,sasa anakamatwa tena kwa kosa gani?!
Eshe akajizoazoa pale chini akamwambia shemeji yake masudi;
“Shemeji kama simu yako ina pesa tafadhali naiomba ili nimpigie simu Inspekta Jamila.”
Masudi akampa simu yake iliyokuwa na pesa yakuweza kuongea, na Eshe akampigia simu Inspekta Jamila huku akiwa analia kwa kwikwi.
Inspekta Jamila aliipokea ile simu ,Eshe alijitambulisha kwake na kumpa tukio lililotokea muda mfupi uliopita.
majibu aliyoyapata kutoka kwa yule askari wa kike yalimshangaza. Kwani Inspekta Jamila alimjibu kwa mkato kwamba.
“MBWA HAFI MAJI, AKIUONA UFUKWE.” Kisha akamtaka aende ofisini kwake anamsubiri!
*******
Mwaduga Dingo alipelekwa kituo cha polisi cha kati, akaingizwa ndani huku akiwa ametaharuki kwa kiasi kikubwa, akiwa haamini na haelewi kipi kilichomsibu! Akawauliza wale askari waliomkamata.
“Mnanikamata kwa kosa lipi, wakati kesi mlionibambikizia, nimeshaachiwa huru?!”
Wale askari wakamwambia.
“Hapa hatuna shitaka na wewe, ila tumetumwa tukukamate na sisi tumetekeleza amri, hivyo subiri mpaka tupate maelekezo mengine!”
Mwaduga alichoka choko kwa kauli ile ya wale wana usalama, alichofanya ni kumuachia mungu, akapiga moyo konde akangoja kitakachotokea ili akabiliane nacho.
Dakika ishirini baadae aliingia Afande Kubuta nakumchukua Mwaduga.
Kitu kilichompa tofauti Mwaduga, ni kwamba askari huyu alimtesa sana siku alipokuwa anamuhoji ili amtajie wahalifu aliodhaniwa kuwa ni wenzie, ila sasa anamchukua kama rafiki yake!
Alitoka nae nje ya kituo kisha akapandishwa ndani ya gari ileile iliyokwenda kumchukua Dokta Masawe, Toyota Soluna yenye vioo vya kiza.{Tinted}
Huku akiwa anapulizwa na kiyoyozi ndani ya gari ile, Mwaduga alipelekwa ofisini kwa Inspekta Jamila, bila ya kufungwa pingu mikononi!
Alipofika katika ofisi ile Mwaduga alishangaa kumkuta mkewe na mtoto wake, rafiki yake Masudi na mkewe wakiwa na Inspekta Jamila wote kwa pamoja wakiwa wanapata vinywaji vya soda huku nyuso zao zikiwa zimekunjuka, zenye bashasha na tabasamu tele!
Na bila yakujifahamu, Mwaduga nae alijikuta akitabasamu.
“Pole sana Mwaduga, Karibu tena uraiani na sahau yaliyopita kwani, yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo, na yajayo.”
Maneno hayo alikuwa anayasema Afande Kubuta, huku akimfungulia soda Mwaduga!
Kitendo kile kilikuwa kimepangwa na Inspekta Jamila ili Mwaduga asiweke chuki kwa Afande Kubuta katika yale yaliotokea siku za nyuma.
Mwaduga alitingisha kichwa kwa kukubali yale anayoambiwa huku akiipokea chupa yenye soda akasema;
“Kidonda kinapopona, lisalialo ni kovu
Kila unapoliona, ijapo liwe chakavu
Kumbukumbu huja tena, hata kama yakivivu
Yoye nimeyasamehe, ila sitoyasahau!”
Mwaduga aliposema maneno haya akamkumbatia Afande Kubuta, kisha akamkumbatia Inspekta Jamila, alipomkumbatia mkewe na mwanae, machozi ya furaha, yakachukua nafasi yake.
Mwisho akamkumbatia Masudi na mkewe, wote kwa pamoja akawaambia.
“Ndugu zangu nashukuru, kwa kuwa nasi pamoja
Kwani mlijikusuru, mkaacha yenye tija
Atawalipa ghafuru, moja kwa kumi na moja
Sina kubwa la kuwapa, zaidi ya shukurani.”
Alipokwisha kuwashukuru wote kwa pamoja akambeba mwanae akakaa nae kitini, na Inspekta Jamila akamwambia Mwaduga.
“Kwanza pole kwa kizaazaa ulichokipata leo mahakamani, ila halikuwa jambo la bahati mbaya hata kidogo, bali ni mpango wetu jeshi la polisi kwa sababu ya usalama wako ilibidi tufanye vile! Kwani tuna hakika kuwa vyombo vya habari vingetangaza kuwa umeachiwa huru, ni dhahiri maisha yako yangekuwa katika hatihati, kwani wale majambazi wangesikia au kuona kupitia vyombo hivyo wangefanya Ima fa ima wakahakikisha wanakudhuru, au kukuondosha duniani ili usije kuwatambua, ikitokezea kuitwa kufanya hivyo!
Kwani kutoka sasa vyombo vya habari bila shaka vitatangaza kwamba umechiwa huru na kukamatwa tena!
Ingawa najua kwamba utajiuliza kuwa si bado watu watakuona ukiwa nyumbani kwako na labda kazini kwako pale Kituo cha Taxi cha magomeni usalama?!
Hilo tumejipanga nalo na tutakupa mikakati nini cha kufanya, pia wapo watu ambao tutataka uwatambue na baada ya hapo utaambiwa kitakachoendelea.”
Inspekta Jamila akawageukia Masudi na mkewe, nao akawapa mikakati, mambo ya kuzingatia kwa kipindi hiki.
Baada ya hapo Masudi na mkewe wakaaga na kuondoka wakimuacha Mwaduga na Familia yake na wale askari wawili.
Huku nyuma Mwaduga alipewa mikakati ya jeshi la polisi linavyotaka afanye katika kipindi hiki.
Inspekta Jamila alizitoa zile picha alizokuwa amezichukua kwa njia ya video pale Friends Coner Hotel akaziweka mbele ya macho ya mwaduga Dingo, kisha akamwambia.
“Kuna yeyote unaemtambua katika picha hizi?”
Mwaduga alizitazama zile picha kwa makini, na wakati huohuo Inspekta Jamila na Afande Kubuta, wao walikuwa wakimtazama usoni Mwaduga.
“Hapa nawakumbuka hawa jamaa wawili.”
Mwaduga alisema vile huku, akionyeshea kidole zile picha alizozikumbuka.
“Unawakumbukaje hawa jamaa, uliwahi kukutana nao wapi?”
Afande Kubuta alimtupia swali la haraka Mwaduga.
“Hawa jamaa, hakika ndiyo walionikodi siku ile kule Sinza, na huyu bwana huyu, ndiyo alienambia kuwa wanazo elfu tatu, niwapeleke kwa Macheni. Tena huyu bwana anaongea kwa kithethe huyu.”
Mwaduga kama mtu aliepagawa, alikuwa ana hasira na wale watu kwelikweli.
“Na huyo mwengine?”
Afande Kubuta alimrudisha Mwaduga katika utambuzi, kwani tayari alikuwa keshapandwa na hasira.
“Huyu mwingine, alikuwa amepanda nyuma namkumbuka pia, tena huyu jamaa mwepesi kweli, kwani ndiye alieshuka mwanzo pale kwa macheni. Huku gari ikiwa bado haijasimama sawasawa!”
Mwaduga Dingo alikuwa anaichambua picha ya Jeradi Mwaipopo.
Baada ya utambuzi ule, Mwaduga Dingo pamoja na familia yake, walihamishiwa nje ya mji kwa muda, mpaka itakavyoamriwa vinginevyo, huku gharama za chakula, malazi na matibabu ikibidi, jeshi la polisi limechukua jukumu hilo!
*******
Siku ya Alhamisi saa nne ya asubuhi, ofisini kwa “IGP” kulikuwa na kikao cha dharula kujadili namna kesi ile ilipofikia, na inavyo endelea.
Miongoni mwa waliokuwemo katika kikao kile ni “IGP” mwenyewe, Kamanda wa kanda maalum, Kamanda wa mkoa wa kipolisi wa kinondoni, Mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini “DCI”, Inspekta Jamila na Afande Kubuta.
Kikao kile kilikaliwa kiasi ya saa nzima wakubwa wale walitoa uzoefu wao, kwa vijana wao ilimradi mambo yaende sawa.
Mikakati ikakamilika mipango ikawekwa ili ndani ya wiki moja waweze kumaliza swala lile ili washughulike na mambo mengine!
“IGP” alikifunga kikao kile huku akiwa na matumaini makubwa kwa jinsi vijana wake wanavyochapa kazi kwa mwendo kasi.
Ruhusa ilitolewa na kila mmoja akarudi katika eneo lake la kazi.
Inspekta Jamila akiwa na Afande Kubuta wakiwa ofisini kwao, mara aliingia Mke wa Dokta Masawe na akataka kuongea na Afande Kubuta.
Yule Mwanamke jeuri wa Kichaga, tofauti na siku alipokuwa nyumbani kwake, wakati Afande kubuta akiwa na maaskari wenzake walipokwenda kwa minajili yakumkamata Dokta Masawe, leo alikuwa mpole na mwenye heshima kubwa!
Afande Kubuta na Inspekta Jamila walitazamana kisha, Afande Kubuta akamkaribisha mwanamke yule.
Baada ya kuketi akamuuliza.
“Nikusaidie nini Mrs Masawe?”
Mke wa Dokta Masawe akasema.
“Aksante nimekaribia, nimepigiwa simu na Mume wangu akiwa kituo cha polisi cha kati, nakuniambia kwamba amekamatwa, hivyo akanielekeza mahali hapa kwenu ili tuje kuongea ili tuyamalize!”
Maaskari wale wawili wakatazamana tena na safari hii akajibu Inspekta Jamila.
“Ndiyo mumeo amekamatwa jana kwa makosa ya mauaji, na kula njama kwa kushirikiana na majambazi katika kufanya uhalifu nchini, hivyo tumemkamata na baada ya kumuhoji mumeo amekili shutuma hizo, hivyo ni kweli yupo kituo cha kati, baada ya kuwatia mbaloni washirika wenzake, itabidi wakasimame mahakamani, kujibu mashitaka.”
Mke wa Dokta Masawe katika kitu alichosisitiziwa na mumewe, katika simu aliyoomba kwa askari pale kituoni, na akiongea katika lugha ya kichaga pekee ni kwamba,
Swala lile ahakikishe linaishia polisi, kwani kwa ushahidi uliopo akipanda mahakamani, hanusuriki na kifungo cha maisha, au kunyongwa kabisa hadi kufa!
Mke wa Dokta Masawe kwa majibu aliyoyapata kutoka kwa yule Askari wa kike yalimtisha na kumkatisha tamaa sana, hivyo akawaambia askari wale.
“Ndugu zangu naomba msaada wenu, yaliyotokea ndiyo yashatokea, hivyo nipo tayari kujisaidia naomba na nyie mnisaidie!”
Kwa mara ya tatu askari wale walitazamana katika siku ile, ikiwa kama hawaelewi alichokikusudia mke wa Dokta Masawe, wote kwa kauli moja wakasema.
“Tukusaidieje?!”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media