BARUA KUTOKA JELA (17)

Zephiline F Ezekiel
0
Mtunzi: Ibrahim Gama

SEHEMU YA KUMI NA SABA
ILIPOISHIA...
Kwa mara ya tatu askari wale walitazamana katika siku ile, ikiwa kama hawaelewi alichokikusudia mke wa Dokta Masawe, wote kwa kauli moja wakasema.

“Tukusaidieje?!”

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
Na mke wa Dokta Masawe akasema huku akifungua mkoba wake.

“Nimekuja na Milioni mbili, naomba mchukue ili mnisaidie kulimaliza jambo hili likiwa polisi. Baada ya mume wangu kutoka tutawapa pesa nyingine!”

Mke wa Dokta Masawe alisema maneno yale na kutoa bulungutu la Fedha akaliweka juu ya meza ile, huku akiwatizama wale maaskari usoni mmoja baada ya mwingine.

Kilichotokea Mke wa Dokta Masawe hakukitegemea kabisa katika mawazo yake kama kingeweza kutokea!

Inspekta Jamila aliangaliwa na Afande Kubuta usoni, na Inspekta Jamila akakilaza kichwa chake kidogo pembeni ikiwa ni ishara ya kuruhusu jambo fulani kutendeka, hivyo kufumba na kufumbua Mke wa Dokta Masawe alikuwa ana Pingu mikononi mwake, huku Afande Kubuta akimwambia.

“Nakufungulia shitaka la kutoa Rushwa, ili kutaka kupindisha sheria huku ukiwa unafahamu kuwa ni kosa la Jinai katika Serikali ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania!”

“Ama kwa hakika huu ni mtego wa panya.”

Inspekta Jamila alijisemea kimoyomoyo huku akiihakiki kama simu yake yenye Video Camera kama ilikuwa inafanya kazi yake sawasawa, na akathibitisha kuwa kweli alichokuwa akikirecodi kimeingia barabara.

Mke wa Dokta Masawe alipokuja kutanabahi, alikuwa yumo ndani ya gari ya polisi akiwa na pingu mikononi, akipelekwa kituo cha Polisi cha Daraja la Salenda akawekwe Rumande.

Inspekta Jamila na Afande Kubuta walikuwa hawana Msalie mtume, katika kufanya kazi yao.

*******

-.

*******

Kijana mrefu wa wastani aliejengeka kimazoezi, mweye misuli imara iliyotokeza anapotembea.

Alikuwa pahala ambapo mwenyewe hupendelea kupaita Chimbo, akimaanisha ni sehemu iliyojificha.

Alikuwa yupo katika himaya yake kule maeneo ya Vingunguti nyuma ya kiwanda cha kutengeneza kandambili cha Fida Hussein, akiwa anatafakari namna alivyowaacha wale maaskari kule maeneo ya Tabata Baracuda.

Alijipongeza kwa kitendo chake cha kuchelewa kufika katika eneo alilopanga kukutana na Dokta Masawe kwa dakika takribani kumi tu, lau kama angewahi kufika kama kawaida yake anapokuwa na ahadi na mtu, pengine siku ile angekuwa “Amelosti” (angekamatwa) kama watu wa Jamii yake wanavyopenda kulitamka neno lile!

Lakini kilichokuwa kinamuumiza kichwa zaidi ni pale kila anapoipiga simu ya Dokta Masawe, ilikuwa haipatikani kitu ambacho kilimtia mashaka zaidi.

Kupitia simu maalum ya Dokta Masawe ilikuwa haikosekani kwa siku zote zinazokwenda kwa Mungu.

Lakini leo nayo kila anapoipigia simu ile, ikawa pia haipatikani!

Akafikiri mambo mengi, yakiingia na kutoka, mara akasikia simu yake ikiita,na alipoitazama namba ya mpigaji alipatwa na kihoro, na wahka wa hali ya juu sana.

Akaipokea simu ile, ilikuwa ni simu ya Dokta Masawe!

Kwa sauti ya kunong’ona, Dokta Masawe alisema.

“Haloo JM, njoo ‘faster’ tukutane pale bar ya Y2K Buguruni ili tufanye mpango wa kuondoka leo hii hii, kabla ya kesho!”

Jm akamuuliza kwa makini Dokta Masawe.

“Nije ‘faster’, au nisije?!”

Dokta Masawe akasisitiza.

“Njoo faster bwana, fanya faster!”

Na Jeradi Mwaipopo au kwa kifupi JM, alijibu kwa maneno yasiyozidi matatu kisha akakata simu, alijibu;

“Itabidi iwe hivyo!”

Jeradi Mwaipopo baada ya kukata simu, alitingisha kichwa kwa masikitiko kisha akachomoa Bastola yake na kuibusu, na alipofanya kitendo kile macho yake yalikuwa yamemuiva kwa huzuni, na sekunde chache baadae machozi yalianza kumlengalenga!

Ama ukiona mtu mzima analia, basi ujue kuna jambo ni kweli.

Jeradi Mwaipopo ingawa aliambiwa maneno yale na alietokea kuwa Swahiba wake mpenzi, kwa siku za hivi karibuni Dokta Masawe, alipatwa na simanzi siyo kwa maneno yale laa hasha!

Bali kwa wito wa Dokta Masawe anapomtaka aende faster!

“Ama kwa yakini mimi sipajui, anapokaa Mwaipopo, ila kama mnataka apatikane, nipeni simu yangu ili nimpigie, kwangu yule kama pipa na mfuniko vile, atakuja tu kama Ng’ombe na zizi lake vile kisha nanyi mtamkamata!”

Wale askari wawili wakaona lile ni wazo lililokwenda shule, na bila ajizi Inspekta Jamila akawasha simu ya Dokta Masawe aliyokuwa nayo katika droo za ofisi yake, kisha akaitafuta namba ya Mwaipopo na kuipiga na baada ya sekunde chache simu ile ikawa inaita akaiweka katika ‘Loud speker’, ndipo alipompa Dokta Masawe ili amvute Jerdi Mwaipopo.

Na Dokta Masawe hakufanya makosa, akaenda hewani na kumtaka JM aende pale Y2K Bar Buguruni.

Hiyo ikiwa ni saa nne asubuhi siku ya Ijumaa.

Wingu zito jeusi lilitanda angani, kuashiria mvua inaweza kunyesha muda si mrefu.

Maafande wale walishauriana namna ya mtego wao jinsi utakavyokuwa, wakajipanga nani ake wapi, na afanye nini.

kisha akapakiwa Dokta Masawe, ndani ya gari ya polisi yenye namba za kiraia, isiyoonyesha vioo vyake kwa mtu alie nje kumuona wa ndani, bali wa ndani anaweza kumsanifu mtu wa nje kwa namna anavyotaka!

Safari ya kwenda Buguruni Y2K, ikaanza bila kuchelewa, kwani chelewa chelewa, utamkuta mwana si wako!

Inspekta Jamila, Afande Kubuta na Dokta Masawe, walikuwa ndani ya gari moja, na nyuma ya gari yao, kama gari ya tatu hivi kutoka katika gari yao, kulikuwa kuna gari nyingine ikiwafata!

Walitoka katika jengo la Wizara ya mambo ya ndani, wakachukua mtaa wa Azikiwe hadi Sokoine Drive wakapinda kulia, na kuendelea hadi yalipokutana maungio ya Mtaa wa Sokoine Drive na Barabara ya Uhuru, wakakata kulia kushika njia ya Barabara ya Uhuru waliyonyoosha nayo moja kwa moja hadi Buguruni, na kabla ya kituo cha mafuta cha Buguruni wakapinda kulia, na baada ya mwendo kidogo, wakawa katika Baa ya Y2K Buguruni, na kila mmoja akachukua nafasi yake, kama walivyokubaliana.

Katika kiti cha peke yake pale nje, Dokta Masawe aliletewa Bia aina ya Ndovu akapewa ajiburudishe nayo.

jamaa watatu waliokuwa wanaifatilia kwa nyuma gari aliyopandiswa Dokta Masawe, walishuka pale pia na moja kwa moja wakaenda katika meza ya mchezo wa Pool, wakawa wanajiburudisha kwa mchezo ule, wakiwa hawapo mbali sana na meza aliyokaa Dokta Masawe!

Afande Kubuta alikaa upande wa kaskazini, akiangalia upande wa kusini, walipotokea na gari yao.

Inspekta Jamila hakuwepo kabisa katika Baa ile ingawa alikuja pamoja wakiwa katika gari moja na Dokta masawe na Afande Kubuta, kwani kukaa pale kungeweza kuharibu mtego wao, kwa kuwa Jeradi Mwaipopo, alishamuona na anamfahamu!

*******

Jeradi Mwaipopo baada kuongea na simu ya Dokta Masawe, aliingia chumbani kwake huku bastola yake akiwa sasa ameichomeka kiunoni kwakwe, alitumia kiasi ya dakika ishirini hivi mle ndani, kisha akatoka huku akiwa anatabasamu!

Aliziendea Taxi zinazoegesha pale kiwandani kwa Fida Hussein akapanda katika gari moja iliyo makini, na kumwambia Dereva wa Taxi.

“Nipeleke Buguruni Sheli haraka iwezekanavyo”.

Yule dereva wa taxi, hakutaka kupatana, aliwasha gari na safari ya Buguruni ikaanza.

Na walipofika Pale Buguruni Sheli, JM akamlipa pesa zake dereva yule na wakaagana.

Akaanza kupiga hatua kuelekea katika Baa ya Y2K pale Buguruni.

Watu wachache waliokuwa katika Baa ile kulipafanya eneo lile kuwe na utulivu wa namna yake, Afande Kubuta akiwa na chupa yake ya soda ya Coca Cola, alikuwa ametulia kimya akinywa funda mojamoja, huku akiwa hana raha hata kidogo.

kwani muda unakwenda na Mwaipopo hakuwa na dalili kama angetokea!

Huku akiwa makini na kila anaeingia na kutoka katika Baa ile. Mara alimuona mzee mmoja mwenye kibyongo alievaa kanzu iliyochakaa na kofia chakavu miguuni mwake akiwa amevaa viatu vya kubazi,akiwa anaombaomba pesa.

Afande Kubuta akakumbuka kumbe leo ni siku ya Ijumaa, hivyo akayaondosha macho na mawazo yake kwa yule mzee masikini wa kutupwa. Nakuendelea kuangalia watu ambao anaweza kumuona mtu anaemuhitaji.

Muda ukawa unakatika dalili za kumuona Mwaipopo zilikuwa finyu sana.

Yule mzee ombaomba alikuwa katika meza ya Dokta Masawe, akiendelea kuombaomba kwa watu waliokuwa katika eneo lile.

Dokta Masawe alitazamana na yule mzee uso kwa uso na kisha yule mzee akaelekea uani kwenye Baa ile, akashika njia inayokwenda msalani.

Dokta Masawe kwa ishara maalum aliyoelekezwa na Afande Kubuta akaifanya, na mara moja Afande Kubuta akang’amua kwamba Dokta Masawe anataka kwenda chooni, akanyanyuka pale alipo kisha akakaa!

Hiyo ilikuwa ni ishara kwamba imetolewa ruhusa ya Dokta Masawe aende msalani.

Dokta Masawe akainuka,

na kuelekea katika vyoo vya wanaume.

Huku nyuma yake akiwa na mtu aliekuwa anamsubiri nje ya mlango wa vyoo vile, akiwa anaongea na simu yake!

Nyuma nje ya choo kile, pia alikuwapo mtu mmoja akiwa na sigara yake mdomoni akichukua doria!

Kiasi eneo lile lilikuwa na ulinzi wa kutosha.

Kiasi cha kama dakika mbili hivi yule mzee ombaomba alitoka chooni mle akatoka nje ya Baa ile na kuondoka zake.

Zikapita kiasi ya Dakika tano Dokta Masawe alikuwa bado hajatoka chooni, yule askari aliekuwa akiongea na simu, akamgongea mlango atoke kwani muda umekwenda sana na wao hawakwenda kwenye Baa ile kwaajili ya kustarehe, bali walikuwa na kazi maalum,

Lakini hata alipoendelea kugonga na kugonga, hakupata jibu lolote kutoka kule chooni alikokuwa Dokta Masawe!

Akaamua kuusukuma ule mlango wa choo ili amtoe Dokta Masawe chooni mle akaendelee kuwa chambo kule nje, katika mtego wao wa kumnasa Jeradi Mwaipopo.

Yule askari aliusukuma mlango kwa nguvu na kuingia mle chooni, Hamadi?!

Hakuyaamini macho yake kwani alimkuta Dokta Masawe alikuwa amelala mle ndani chooni akiwa hana dalili za uhai, macho yamemtoka pima, huku damu zikiwa zinamvuja pembeni ya sikio lake!

“Shit” Yule askari alisema maneno hayo kisha akasonya na kutoka nje mbio huku akiwa hakuugusa popote mwili wa marehemu Dokta Masawe!

Afande Kubuta alipomuona yule askari ametoka mbio kule uani huku akiangaza huku na kule kwa fadhaa, yeye akakimbilia kule uani,akapitiliza hadi chooni nakumshuhudia Dokta Masawe akiwa sasa ameshabadilika jina kwa kuongezewa jina la Marehemu Dokta Masawe!

Afande Kubuta alipatwa na mshangao usiosemeka, kwani wamezidiwa maarifa ingawa hakuelewa ni nani aliefanya vile!

Dokta Masawe hakuwa na silaha hivyo isingekuwa rahisi kujiuwa! Kwa kuwa shimo lililokuwa linaonekana chini ya sikio la Dokta Masawe, au Marehemu Dokta Masawe, lilikuwa ni tundu la risasi!

Kitu kilichomuumiza kichwa zaidi ni kuwa, silaha iliyotumika katika mauaji yale haikusikika mlio, kwa hiyo ilikuwa imewekwa kiwambo chakuzuia sauti isitoke!

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

 Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)