
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA KUMI NA NANE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Kitu kilichomuumiza kichwa zaidi ni kuwa, silaha iliyotumika katika mauaji yale haikusikika mlio, kwa hiyo ilikuwa imewekwa kiwambo cha kuzuia sauti isitoke!
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
Jasho likamtoka Afande Kubuta nae akatoka nje kwa haraka na kumfata askari ambae alipewa jukumu la kumlinda Dokta Masawe akiwa chooni, nakutaka maelezo ya kina ya nani aliefanya mauaji yale, na namna yalivyotokea!
“Mimi kama mpango ulivyokuwa, nilimsindikiza hadi chooni huku nikiwa sionyeshi kama nipo nae, alipoingia chooni mimi nilibaki nje ya choo kile nikijifanya naongea na simu, huku macho na masikio yangu nikiyaelekeza katika kazi iliyonileta.
mara akatoka mzee mmoja ombaomba mle chooni, mimi nikaendelea kumsubiri Dokta Masawe nikaona muda unakwenda nikaanza kumuhimiza Dokta Masawe atoke ili tuendelee na zoezi letu, lakini hakunipatiliza kwa chochote, nikaamua kuusukuma mlango ambao kumbe ulikuwa haujafungwa.
Ndipo nilipomkuta Dokta Masawe katika hali ile, na mle chooni zaidi ya yule babu ombaomba, hakuwemo mtu mwingine!”
Yule askari aliekuwa na jukumu la kumlinda Dokta Masawe alikuwa anaeleza vile ilivyotokea.
Wale jamaa waliokuwa wanacheza Pool, mara moja wakaungana na Afande Kubuta, na wakapewa maelezo ya kumtafuta yule ombaomba maeneo yale haraka iwezekanavyo!
Na mara moja kazi ikaanza huku yeye na yule askari wakirudi tena kule chooni kufanya upekuzi, na katika kutafuta tafuta mle chooni wakiwa wamevaa “gloves” mikononi mwao, Afande Kubuta akaokota ganda la risasi iliyotumika kumuua Dokta Masawe.
Na alipoliangalia vyema lile ganda, Afande Kubuta akatingisha kichwa kwa masikitiko.
Afande Kubuta, alibaini kuwa silaha iliyotumika kumuua Dokta Masawe, kwa mujibu wa ganda lake la risasi, ndiyo silaha ileile iliyotumika siku moja nyuma kule maeneo ya Tabata Baracuda!
-
Mara moja akang”amua kwamba Jeradi Mwaipopo alikuwa pale muda si mrefu, huku akijibadilisha na kujifanya ni ombaomba!
Afande Kubuta, akakumbuka jinsi Yule mtu, aliemdhania kuwa ni ombaomba, alivyokwenda katika meza ya Dokta Masawe akijifanya kuomba hela, kumbe ilikuwa ni geresha kwani alipotoka tu na kwenda chooni, haikupita hata dakika mbili, na Dokta Masawe akainua mikono yake juu huku akivifunganisha vidole vyake kule juu, ikiwa ni ishara aliyopewa na yeye mwenyewe Afande Kubuta, ikiwa kama atabanwa na mkojo.
kufikia hapo akaamini kwamba kweli Geradi Mwaipopo au JM alikuwa ni askari mwenye mbinu za kujihami[MK]na mbinu za medani[MM].
Watu waliokuwa wanataka kwenda chooni kwa wakati ule, walizuiliwa kuingia chooni mle huku wakielezwa kuna mtu amekufa chooni mle!
Mara muda si mrefu Afande Kubuta alitoka nje na kumuacha askari mwenzake kushika doria ili kuhakikisha haingii mtu yeyote chooni mle.
Afande Kubuta haraka alikwenda pale walipoiegesha gari yao na Inspekta Jamila, alipofika pale sehemu walipokuwa wameegesha gari yao, akakuta papo peupe!
Siyo gari wala Inspekta Jamila aliekuwa katika eneo lile, na Afande Kubuta akashika kiuno kwa kuchoka na mambo yaliyokuwa yanamuumiza kichwa kwa siku ile.
Akatoa simu yake ya mkononi, na kumpigia Inspekta Jamila ili ajue alipo,lakini pia ampe kilichojiri.
kitendo kilichozidi kumchosha kwani simu yake ilimwambia;
“Namba unayoipigia haipatikani kwa sasa, tafadhali jaribu tena baadae.”
Afande Kubuta sasa akawa kama mtu aliepagawa vile, akaangalia maeneo yote ya jirani na Baa ile lakini mambo yalikuwa kama anavyoyaona, hakuna gari ya Inspekta Jamila, wala yeye mwenyewe! ikambidi akate shauri.
Mara akaona kundi la watu wanawake kwa wanaume, wakikimbia katika barabara ya Uhuru kuelekea upande wa kulia kule kwenye taa za kuongozea magari pale Buguruni sheli.
Afande Kubuta akiwa anatafakari, ukasikika mlio wa Risasi! Na sasa akaona watu wengi zaidi wakikimbilia kule kulikosikika mlio wa Risasi.
******
Inspekta Jamila akiwa ametulia ndani ya gari pale nje kwenye Baa ile ya Y2K pale Buguruni, alivutiwa sana na yule Ombaomba!
Kwani alipokwenda kwenye meza iliyokuwa na kinywaji cha Dokta Masawe, hakuonyesha mkono kama ishara ya kuomba pesa, aliyokuwa anaifanya katika meza za watu wengine!
Inspekta Jamila alimuona yule Ombaomba akimtazama kwa makini Dokta Masawe, na kisha kichwa cha yule Ombaomba kililazwa upande kidogo sana, kikielekeza upande wa uwani wa Baa ile!
Baada ya kufanya vile, yule Ombaomba akaelekea uwani mwa Baa ile, na katika muda usiozidi dakika mbili Dokta Masawe alifanya ishara iliyoashiria kwamba anataka kwenda chooni.
Inspekta Jamila moyo ulimripuka Ripu na damu yake ikaanza kuchemka! Huku mapigo ya moyo yakiongeza kasi katika mapigo yake!
Inspekta Jamila akiwa mle ndani ya gari alimshuhudia Afande Kubuta, akimruhusu Dokta Masawe aende chooni. Na Dokta Masawe akaelekea uwani mwa Baa ile ambapo vyoo vyake ndipo vilipokuwa.
Inspekta Jamila akaongeza umakini mara dufu, na hapo akamuona Afande Michael Chazza aliekuwa ameshika mti maalum wa kuchezea mchezo wa pool Table, akiuweka ule mti pale juu ya meza na kuelekea uwani sanjari na Dokta Masawe.
Na baada ya kama dakika nne hivi, Inspekta Jamila alimuona yule Ombaomba akitoka na kuondoka zake eneo lile akiifata ile barabara ya Uhuru kwa mwendo wa haraka kidogo.
Inspekta Jamila alimshuhudia yule Ombaomba akiipita gari aliyokuwemo yeye mle ndani, na aliporudisha macho yake kule kwenye Baa ya Y2K Dokta Masawe alikuwa bado hajarudi katika meza yake!
Kitendo bila kuchelewa, Inspekta Jamila aliwasha gari nakumfatilia yule Ombaomba kwa mwendo wa taratibu.
yule Ombaomba alikuwa ameshachanganya mwendo, na sasa alikuwa ameshaikaribia ile barabara ya Uhuru, akageuka nyuma kutazama kule kwenye Baa ya Y2K, huku akiwa anatembea kwa mwendo wa haraka, akaiona gari ndogo yenye vioo vya kiza ikija taratibu.
Hamadi! Yule ombaomba akagongana na Dada mmoja hivi aliekuwa anaelekea kule wenye bar ya Y2K.
Yule Ombaomba akakutanisha viganja vyake vya mikono kifuani kwake, na kuinama kidogo kama ishara yakumtaka radhi yule dada aliegongana nae. Lakini yule dada badala yakupokea samahani ile, alitoa msonyo mrefu kisha akashika Hamsini zake.
yule Ombaomba akapinda kulia kuelekea Buguruni Sheli.
Inspekta Jamila alipofika pale kwenye barabara ya Uhuru alisimama na kumfatilia kwa macho yule Ombaomba aliekuwa anazidisha hatua.
Inspekta Jamila akaiingiza gari katika barabara ya Uhuru akapinda kulia katika ile barabara inayoelekea Buguruni Sheli, huku macho yake yakiwa hayampotezi yule Ombaomba.
Yule Ombaomba alikuwa nae akiitazama ile gari ya Inspekta Jamila kwa makini na kituo, ambayo sasa alikuwa nayo sanjari yeye akiwa upande wa kulia katika njia ya watembea kwa miguu, na ile gari ikiwa upande wa kushoto katika njia ya gari kwenye ile barabara ya Uhuru.
Yule Ombaomba mara akasimama ghafla na kuingia katika duka moja la kuuza Vipuri vya magari, lakini pia akitaka kuthibitisha kwamba ile gari ilikuwa inamfata yeye au ilikuwa na safari zake!
Akiwa pale dukani aliishuhudia ile gari ikiegeshwa pembeni, na hata baada ya kuegeshwa kulikuwa hakuna mtu alietelemka kutoka katika gari ile, wala aliepanda!
Yule Ombaomba akiwa anabawabu muelekeo, mara akaja Bwana mmoja akiwa na pikipiki aina ya Honda 750 GL, akashuka na kutaka kuingia dukani mle.
kilifanywa kitendo ambacho hata Inspekta Jamila hakukitarajia kama kingeweza kufanyika, tena kwa wepesi wa ajabu namna ile!
Yule Ombaomba aliingiza mikono mifukoni mwake, alipoitoa mikono ile ilikuwa imekamata bastola iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti, na kuifanya bastola ile ionekane ndefu kiasi!
Akamnyooshea bastola ile yule bwana aliekuja na pikipiki, huku akimtaka ampe funguo za pikipiki ile bila ya kuchelewa, na yule bwana aliekuja na pikipiki huku akigwaya kwa kitendo cha kuonyeshewa silaha ya moto namna ile, alimrushia zile funguo yule Ombaomba ambae kwake yule bwana mwenye ile pikipiki alimuona kama mtu mzima aliechanganyikiwa, Lakini pia dhalili na masikini wa kutupwa!
Yule Ombaomba alizidaka zile funguo na kuirukia ile pikipiki iliyokuwa inaangalia mjini, akaipiga stati na ile pikipiki bila hiyana, ikawaka ikisubiri safari!
Yule Ombaomba bila kufanya ajizi, kitendo bila kuchelewa akaigeuza kwa kupiga msele pikipiki ile. ikawa inatazama Buguruni Sheli!
Kila mtu ambae ameiona ile pikipiki ilipogeuzwa angeamini kuwa ni pikipiki yake yule mzee namna alivyoimiliki.
Aliingiza barabarani kiufundi katika barabara ile ya Uhuru akawa anatembelea barabara inayoruhusu kupita magari yanayotoka buguruni kwenda mjini! yaani alikuwa anatembelea barabara “NO ENTRY”
Bahati njema kwake ni kwamba, kulikuwa hakuna magari yanayokuja upande ule kwani taa za pale katika makutano ya barabara ya Uhuru na Mandela ilikuwa imeziruhusu gari kutoka Ilala kwenda Tabata, na usawa wa Tazara na hakukuwa na gari ilyokuwa inakata kuelekea Ilala.
Inspekta Jamila alipoona kitendo kile nae akaiingiza gari barabarani katika mwendo uliowaacha hoi watu wote walioiona namna gari ile ikichimba huku ikitoa mlio wa tairi zilizokuwa zikisuguana na barabara, na kusababisha vumbi kubwa sana sehemu ile.
Ikawa sasa upande wa kulia kulikuwa na pikipiki aina ya Honda 750 GL, na upande wa kushoto kulikuwa na gari aina ya Toyota Soluna XL zote kwa pamoja zikiiwahi sehemu ya maungio ya barabara ile pale kwenye kituo cha mafuta pale Buguruni.
Pikipiki iliongwezwa mwendo kwa mkono, na gari iliongezwa mwendo kwa mguu!
Kiasi kulikuwa hapatoshi eneo lile la Buguruni, kwani watu waliokuwa wanatokea Buguruni upande wa sokoni, na wale waliokuwa wanatokea upande wa Buguruni chama na kwa Mnyamani na kule upande wa sheli wote walikuwa wanakimbilia upande ule kulipotokea kizazaa cha pikipiki kelele zake lilipogeuzwa uelekeo, na kule kulipotokea kelele za gari alilokuwa anaendesha Inspekta Jamila.
Kwa kweli ilikuwa ni hatari tupu kukimbilia jambo kama lile.
Pikipiki ndiyo iliyowahi kufika katika maungio yale ikaingia, huku Inspekta Jamila akiwa amezuiliwa na gari iliyokuwa ikisuasua mbele yake, akaipita gari ile mkweche aina ya Datsun Nissan Old Model yakubebea mizigo, na sasa akawa yeye nyuma ya Pikipiki iliyokuwa imeibiwa na yule Ombaomba wa ajabu!
Mara Inspekta Jamila akamshuhudia yule Ombaomba akigeuza uso wake kumtazama, huku mkono wake wa kushoto ukiwa na bastola iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti isisikike {Silence} akimnyooshea pale upande wake usawa wa dereva.
Mara akaona kidole kikigusa kile kifyatulio cha risasi {Trigger}
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media