
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA ISHIRINI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Wote kwa pamoja walikuwa wamepigwa chenga ya Mwili.
Baadae wakapata taarifa zilizowafanya wakunje uso kwa ghadhabu, kwani taarifa ile kupitia Radio Call zao ilisema;
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
“Jambazi Sugu Geradi Mwaipopo anaetafutwa na Polisi, kwa makosa ya mauwaji na uhalifu wa kutumia silaha, amepora Pikipiki aina ya Honda 750 GL ya Ndugu Majidi Ndosho katika maeneo ya Buguruni, na kuelekea Maeneo ya Tazara.
Hivyo askari wote watakaoiona Pikipiki au mtu anaeiendesha, anaeonekana kama mtu mzima, mtu huyo, awekwe chini ya Ulinzi mara moja Ova”
-
Ilipomaliza taarifa ile, wale askari wakasambaa kuanza msako mkali wa kumtafuta Jambazi yule.
Eneo lote la Tazara kuanzia mchicha, hadi katika maeneo ya Viwandani, yalikuwa katika mshikemshike wa hali ya juu kabisa, akitafutwa Jeradi Mwaipopo.
Katika kona ile ya mchicha kwenda Kiwalani kabla ya kufika ile pacha ya Vingunguti na Viwandani, ilitiliwa mashaka kuwa huenda Jeradi Mwaipopo, akawa amechepukia pale, kwa kuwa Pikipiki ile haikuonekana kupita katika njia panda ya Vingunguti, Bombom!
Hivyo nguvu kubwa ikaelekezwa pale, askari wa doria kenda, pamoja na askari wa pikipiki, walilizunguka eneo lile, wakawa wanamsaka Jeradi Mwaipopo!
Wacheza kamari wa maeneo yale, hawakuwa na raha kabisa siku ile, wala walevi wa Pombe ya Gongo, kwani kila walipowaona askari Wakitayaya, wao walikuwa nusura wavunje miguu yao kwa mbio!
Msako ule uliendelea katika eneo lote la Kiwalani lakini muda ulikuwa unakwenda, Jeradi Mwaipopo alikuwa haonekani hata vumbi lake!
Wale askari waliotoka tazara wakiwa na pikipiki walifanikiwa kuziona alama za Tairi za Pikipiki ile, wakaanza kuifata taratibu.
Walifanikiwa kuzifata alama zile za Tairi kwa robo kilometa!
Lile wingu zito jeusi lilokuwa limetanda angani, likaanza kunyesha Mvua kubwa, ikaharibu mwenendo mzima wa kuzifatilia alama za tairi za Pikipiki aliyokuwa akiiendesha Jeradi Mwaipopo, kiasi wale askari walimuhusisha Jeradi Mwaipopo na kutumia pia, nguvu za Kiza!
Dakika ishirini baadae, ilipatikana taarifa kupitia Radio Call ,kwamba Pikipiki aina ya Honda 750 GL, iliyokuwa inaendeshwa na Jambazi Jeradi Mwaipopo, imekutwa imetelekezwa katika eneo la makazi ya Walemavu kule Kiwalani!
*******
Afande Kubuta, akiwa na Inspekta Jamila akaendesha gari ile huku akiwa hajui wanakwenda wapi, akamuuliza Inspekta Jamila aliekuwa ameinama kwa mawazo, yaliokuwa yanatembea kichwani mwake.
“Sasa afande tunaelekea wapi?”
Inspekta Jamila aliinua kichwa chake akatazama nje, akaona walikuwa katika Taa za kuongozea magari za Tazara, zinapokutana barabara zenye majina ya viongozi mashuhuri Barani Africa, Barabara ya Mandela, na Barabara ya Mwalimu Juliasi Kambarage Nyerere.
Inspekta Jamila akasema;
“Turudi ofisini tukajipange upya, mradi taarifa ya kutafutwa yule Gaidi tumeshaitoa askari wa doria watamtafuta.”
Afande Kubuta akapinda kushoto gari ile na chombo kikawa kinatazama mjini, huku askari wale wakiwa wamelowana ndembendembe kwa namna Jambazi Jeradi Mwaipopo alivyowafanza!
Inspekta Jamila mara baada ya kufika ofisini kwao, akamwambia Afande Kubuta kwamba;
“Kuna mtu mmoja yupo Kijitonyama, tunatakiwa tumfikie na tumuhoji ili tubaini kama nae anahusika, kwa namna moja au nyingine katika kadhia hii!”
Afande Kubuta akiwa bado hajamuelewa Inspekta Jamila akamuuliza;
“Ni mtu gani huyo Afande unaemaanisha ambae kwamba, atakuwa anaweza akawa anahusika na kesi hii?!”
Inspekta Jamila alivuta mtoto wa meza yake nakutoa picha, aliyokuwa ameihifadhi mle, picha ambayo ameichukua katika Albam ya Marehemu Hamida, katika zile picha tatu ambazo mbili tayari ameshazifanyia kazi na tayari majibu yake yameshapatikana!
.
Ilikuwa ni Picha ya Bitozi, ambayo bado hajajuwa kama itampa jibu gani.
Akaichukua picha ile na kumpa Afande Kubuta.
Afande Kubuta aliipokea picha ile na kuitazama kwa makini, kisha akaipindua upande wa pili akaona maandishi yalioandikwa kwa mkono katika picha ile kwa kalamu ya wino yaliokuwa yakisomeka BITOZI.
Afande Kubuta alimtazama usoni Inspekta Jamila, akamuona nae anamtazama kwa makini sana! Afande Kubuta akasema;
“Huyu Predeshee namfahamu huyu mie, ni muuza magari maarufu sana, na ni mgonjwa kwa wanawake huyu!”
Inspekta Jamila huku akiwa anatabasamu akamuuliza Afande Kubuta;
“Wewe unamfahamu kivipi huyo Bitozi, au Predeshee kama ulivyomwita?”
“Nina jamaa zangu kama wawili hivi, wamenunua magari kwake na mara zote mbili nilionana nae, sidhani kama anaweza kuwa na mahusiano yoyote na Genge lile!”
Afande Kubuta alikuwa anamjibu kiongozi wake huku akiondosha kabisa Dhana kama jamaa anaweza kuwa na uhusiano na kesi ile.
Inspekta Jamila alicheka huku akionyesha mshangao kwa majibu ya Afande Kubuta, akamwambia;
“Kwani Afande unataka kuniambia kwamba, ukimtazama mtu tu unaweza kumjuwa matendo anayofanya? Hivi uliwahi kufikiri kuwa Dokta Masawe anaweza kuhusika na kesi hii?, Na akawa ndiyo chanzo cha Mauwaji yaliyotokea?!”
Afande Kubuta aligwaya kwelikweli, na Inspekta Jamila akaendelea kwa kusema;
“Mimi sijasema kama huyo Predeshee anahusika hata kidogo, bali ninachotaka kujuwa alikuwa na mahusiano gani na Marehemu Hamida, hadi akapiga nae picha! Na hakuna mtu mwingine anaeweza kutupa ukweli wa jambo hili bali ni Bitozi mwenyewe, lakini pia kuchunguza ndiyo kazi yetu!”
Afande kubuta akatikisa kichwa chini juu, kuonyesha kuwa ameelewa. Kisha akasema;
“Kwa kuwa huyu jamaa ni Mkwale, nashauri bora uwende wewe kiongozi, kwani jamaa lazima atatoa ushirikiano unaopaswa! Lakini pia Bosi wangu nasema kidhati kuwa Mungu amekupa upendeleo maalum, kiasi hata mwanaume angekuwa mgumu kiasi gani, basi kwako atakuwa laini kama Pamba!”
Inspekta Jamila alimtazama Afande Kubuta kwa macho ya aina yake kisha huku akimwemwesa akasema;
“Nashukuru kwa Mungu kunipa huo upendeleo kama upo, pia asante kwa kunisifia.”
Alipokuwa anamwemwesa mashavu ya Inspekta Jamila yalikuwa yana vishimo maalum vilivyokuwa vinabonyea kwa kuingia ndani.
Mashaallah Inspekta Jamila alikuwa ni mrembo sana, kitu kilichokuwa kinampa tabu Afande Kubuta ni kule kuona kuwa, pamoja na uzuri wa sura, umbo, na tabia, lakini bado alikuwa hajaolewa!
Akawa hajuwi kama wanaume walikuwa wanamuogopa kumtokea, au mwanamke yule hana bahati ya kuolewa, au alikuwa hataki kuolewa!
Ilimradi Afande Kubuta alikuwa amehemewa kwa uchu wa mapenzi kwa bosi wake, lakini pia nayeye alikuwa anamuogopa kumwambia!
Akawa anaishia kusema kimoyomoyo, kuchukua mwanamke kama yule ni kujipa presha za bure!
Ama kweli hakuna kizuri kikakosa kasoro.
Inspekta Jamila akasema;
“Sawa sasa tuweke masihara pembeni na turudi katika kazi, hivi sasa ni saa saba za mchana, itabidi tukapate chakula cha mchana, na ikifika saa nane kamili tukutane hapa ofisini, kwa kuendelea na zoezi letu ili tuone leo tunaimaliza siku kwa jibu gani.”
Alipokwisha kusema hayo Inspekta Jamila aliichukua ile picha ya Bitozi na kuirudisha ndani ya mtoto wa meza, na kutoa chaja ya simu, na kuichaji simu yake.
Afande Kubuta aliinuka nakutoka nje kwenda kupata chakula cha mchana.
Inspekta Jamila alipotaka kufunga yule mtoto wa meza, akaiona simu ya Marehemu Dokta Masawe aliyokuwa ameihifadhi mle ndani, na hapo akawa kama mtu aliekumbuka jambo fulani!
Aliitoa simu ile mle ndani nakuiwasha, na baada ya kuwaka aliibonyeza namba ya mwisho kuipiga simu ile na kuipiga.
Akasubiri kwa muda kidogo huku moyo ukimuenda mbio kama saa mbovu, na kwa mastaajabu makubwa simu ile ikawa inaita upande wa pili!
Kwani hakutarajia kuisikia simu ile ikiita katika muda ule, matarajio yake nikusikia kwamba simu ile imezimwa.
“Halow Jm mambo vipi?”
Inspekta Jamila alitamka kifupi cha jina la Jerard Mwipopo baada ya simu ile kupokelewa.
Kwa mshangao wa ajabu, alisikia upande wa pili ukimjibu tena bila ya wasiwasi wala kutetemeka!
“Muongeaji ni Inspekta Jamila, nipe habari.”
Ama kwa hakika kitendo kile hakukitarajia kabisa, akajikuta anamuuliza Jeradi Mwaipopo;
“Umejuaje kama Inspekta Jamila ndiyo unaeongea nae, hali ya kuwa simu niliyoitumia kukupigia ni ya rafiki yako Dokta Masawe?!”
Kwa swali lile alisikia upande wa pili wa simu ile, Jeradi Mwaipopo akicheka sana kisha akajibu kwamba;
“Mimi ni askari Afande, hivyo kutambua jambo hilo na zaidi, ya hilo sio kitu cha kushangaza kabisa!”
Inspekta Jamila alitingisha kichwa juu chini karibu mara tatu!
Akiwafiki maneno yale ya Jeradi Mwaipopo, kisha akarudi katika hali yake ya kawida na kumwambia.
“Hapana JM, ulikuwa Askari hapo mwanzoni, ila sasa ni jambazi hatari sana wewe, na hilo ndilo lililokufanya ufukuzwe kazi katika Jeshi la polisi.”
Jeradi Mwaipopo huku akiendelea kucheka, alijibu kwa kusema.
“Baadhi ya watu wengi sana wanaelewa hivyo, ulivyoelezwa wewe kuhusu mimi, ila ninachokwambia ni kwamba hizo ni taarifa za uzushi mtupu, huku sababu za kweli za kuachishwa kazi kwangu haziwekwi wazi!”
Inspekta Jamila akajilaumu kwa nini asingetumia simu yake kuongea na JM – kwani angeweza kuyarecodi mazungumzo yale, lakini simu ya Marehemu Dokta Masawe haina uwezo wa kurekodi!
Ingawa yale mazungumzo yalikuwa yanamgusa sana, kwani alikuwa anapata maelezo ya kwanini Jeradi Mwaipopo amefukuzwa kazi.
Ingawa Jeradi Mwaipopo anakana tuhuma za kufukuzwa kazi kwa sababu ya uhalifu, lakini picha yake imeonekana katika vipimo vya kitaalamu alivyowekewa machoni marehemu Kiyarwenda Mwemezi, lakini pia aliwajeruhi Askari kwa risasi siku moja nyuma pale Barakuda Bar na leo hii amemuua Dokta Masawe!
“Hapana huyu ni Jambazi anavunga tu, kwani wezi wachache sana hukubali kuwa wameiba!”
Inspekta Jamila baada ya kupita mawazo hayo kichwani mwake, akamtupia swali linguine.
“Kama wewe hukufukuzwa kazi kwa sababu za kujihusisha na uhalifu, lakini upo ushahidi wa kutosha, kuwa wewe ni muhalifu, lakini pia unashirikiana na wahalifu, ambao baadhi yao tumewakamata na wanatuthibitishia kila kitu kuwa wewe ni muhalifu!”
Jeradi Mwaipopo aliacha kucheka, na akasema;
“Acha kutumia simu ya marehemu, kwani sheria haikuruhusu kufanya hivyo, huo pia ni uhalifu!”
Inspekta Jamila alichukia, kwa maneno ya kiburi ya Jeradi Mwaipopo, akamjibu huku akimuuliza swali.
“Kwa taarifa yako, Dokta hukumuua kama ulivyokusudia! Lakini Jeradi kama wewe ni mwanaume kweli, unaejiamini, niambie upo wapi nikufate?”
“Ukiwa wewe ni askari, unatakiwa unitafute unikamate, ili utambue ukweli wa mimi kufukuzwa kwangu kazi, na tumetambua vipi kama wewe ndiyo unayefatilia kesi hii, hata siku yako ya kwanza tu ya kuanza kazi hii, tukakuachia ujumbe kule katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili!”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media