BARUA KUTOKA JELA (21)

Zephiline F Ezekiel
0
Mtunzi: Ibrahim Gama

SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA
ILIPOISHIA...
“Ukiwa wewe ni askari, unatakiwa unitafute unikamate, ili utambue ukweli wa mimi kufukuzwa kwangu kazi, na tumetambua vipi kama wewe ndiyo unayefatilia kesi hii, hata siku yako ya kwanza tu ya kuanza kazi hii, tukakuachia ujumbe kule katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili!”

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
Inspekta Jamila alipagawa kweli kweli kwa maelezo yale, akamwambia Jeradi Mwaipopo kwamba.

“Basi Jeradi kwa nini tusipange sehemu tukakutana na tukaongea kwa kirefu kiurafiki?!”

Jeradi Mwaipopo alitungua kicheko kama mwehu vile kisha akamjibu Inspekta Jamila.

“Hata mimi nilipokuwa upande huo, nilikuwa nawalaghai watu hivyo hivyo, na hatimaye niliwatia nguvuni. Sasa kitanda hicho nimeisha kilalia, na nawajua kunguni wake! Ila zingatia kwamba huu ni mtego wa panya Inspekta Jamila wa Ilala Mtaa wa Songea nyumba namb………!”

Simu ile ilikatika na Inspekta Jamila akaingia kiwewe akapiga ngumi katika meza yake!

-

-

Akaipiga tena namba ile ya simu iliyokatika.

Akasikia ujumbe kutoka kwenye simu ile ya Marehemu Dokta Masawe, ikimwambia;

“Salio lako halitoshi kupiga simu hii, tafadhali ongeza pesa katika simu yako kabla hujajaribu kupiga simu nyingine!”

“Shabashi” Inspekta Jamila alisema maneno hayo huku sasa akiwa amesimama na akawa anatembea kwenye ofisi ile toka kwenye kona moja kwenda kwenye kona nyingine, huku akitafakari mazungumzo ya Jeradi Mwaipopo, kwani alimtajia hadi Mtaa anaoishi bila shaka hadi namba ya nyumba alikuwa aitaje kwani kama si kukatika kwa simu ile pengine angesikia namba ya nyumba yake ikitajwa!

Kitu kilichomtia hofu zaidi ni kwamba, watu anaowatafuta wao wanamfahamu vizuri hadi katika nyumba anayoishi, kitu ambacho ni hatari kubwa sana kwa maisha yake kwani angewezwa kuviziwa na kupigwa hata risasi na majambazi wale!

“Ama kweli huu ni mtego wa panya.”

Inspekta Jamila alijikuta akitamka maneno hayo, mara kama mtu aliyegutuka, akakumbuka jambo Fulani, akaenda hadi sehemu alikochomeka simu yake kwenye chaja akaichomoa.

Akaichukua simu ya Marehemu Dokta Masawe, pamoja na simu yake, kwa mwendo wa haraka, akaelekea katika chumba cha mawasiliano ‘Computer Room.’

Akamfuata afande Dihenga na kumpa mkadima mzima.

Vyombo vikawekwa sawa na baada ya kusetiwa mitambo ile, simu ya Jeradi Mwaipopo ikapigwa, na ikasikika sauti katika simu ile;

“Simu unayopiga kwa sasa haipatikani, tafadhali jaribu tena baadae”

“Oh shit” Inspekta Jamila alitamka maneno hayo huku akikunja ngumi katika mikono yake yote miwili kwa hasira.

Walijaribu kuipiga namba ile zaidi ya mara tano, ulipatikana ujumbe ule ule kutoka kwenye simu ile, hii ikimaanisha kwamba simu waliyokuwa wanaipigia imezimwa!

Inspekta Jamila akazichukua simu zile mbili pamoja na chaja yake na kurudi navyo ofisini kwake huku akiwa hoi bin taabani kwani Jeradi Mwaipopo aliiharibu kabisa siku yake kwa maneno aliyomwambia.

Lakini akapiga moyo konde huku akisema kimoyomoyo.

“Vilima Havikutani bali wanadamu wanakutana, hivyo ipo siku nitakutana na Jeradi Mwaipopo uso kwa uso, na mimi mwenyewe nitahakikisha ninamfunga pingu!”

Kichwa cha Inspekta Jamila kilijaa mawazo lukuki, kiasi kwamba akaanza kuhisi uchovu na njaa, huku akili yake ikishindwa kabisa kufanya kazi kwa wakati ule.

Akaangalia saa yake na kuona imetimia saa nane kasorobo.

Robo saa tu ndiyo iliyosalia ili wakutane tena na Afande Kubuta wapate kuendelea na ratiba yao.

Inspekta Jamila alikuwa amechoka sana kiasi hawezi kufanya kazi kwa ufanisi.

Aliiweka simu yake katika chaja huku ikiwa inachajiwa, akampigia simu Dokta Zahala.

“Shoga nakuja nyumbani kwako mchana huu kwa mambo makuu mawili. Jambo la kwanza ni kuja kula chakula cha mchana, na la pili ni kuja kupumzika. Kwani kwako ni mahali salama kwa kazi yangu na maisha yangu kuliko nyumbani kwangu kwa hivi sasa!”.

Dokta Zahala akiwa hakumuelewa vizuri shoga yake, akamuuliza.

“Mbona sikuelewi shoga, yaani leo nyumbani kwangu kuwe pahali salama kwa maisha na kazi yako kuliko nyumbani kwako ki vipi?!”

Inspekta Jamila akamwambia shoga yake

“Punguza Wahka shoga, mimi ninakuja huko huko kwako maswali mengi ya nini?”

Wote wakatungua kicheko kirefu kwani watu wale kila wanapokutana, walikuwa wanapendana kama watoto mapacha.

Baada ya muda Afande Kubuta aliingia ofisini mle, akiwa ameshikilia chupa ya maji safi iliyokuwa shinda.

Akamuona Inspekta Jamila akimaliza kuongea na simu.

Afande Kubuta alistaajabu, kwani kiongozi wake hakuonekana kama ametoka nje kwenda kula. Akamuuliza.

“Vipi kiongozi wangu mbona wewe bado hujaenda kupata chakula hadi muda huu, kumezuka jambo jipya au umeagiza viazi?!”

“Hapana sijala chochote toka wewe uondoke, wala sijaagiza kitu ila kazi zilikuwa zimenibana, sasa kwa kuwa wewe tayari umekwisha pata chakula cha mchana, itakubidi muda huu uende Kijitonyama kwa Bitozi ili ukamchukulie maelezo.

Mimi nakwenda kupata chakula cha mchana nyumbani kwangu, lakini pia ndiyo tutakuwa tumeagana, kwani nikiondoka ofisini hapa sitarajii kurudi tena hadi kesho.

Hivyo asubuhi tutakapokutana kwa majaaliwa ya mungu, tutapeana taarifa kamili na matokeao ya kazi yako huko uendako.”

Afande Kubuta alipatwa na bumbuazi au mzubao kwani yeye alidhani kuwa Inspekta Jamila ndiyo angekwenda kule Kijitonyama lakini pia yeye ndiye aliyesema kwa muda ule wakapate chakula cha mchana.

Sasa iweje tena yeye asiende na kusema kwamba anakwenda kula kwake! Lakini afanye nini na kiongozi wake ndiyo kasema hivyo.

Akageuka na kutoka nje ya ofisi ile na kuelekea katika sehemu ya maegesho ya magari akachukua gari ile yenye namba za kiraia na kufungua mlango na kujipakia mle ndani.

Akawasha gari na kutoka eneo la jengo lile kuelekea Kijitonyama kwa Bwana Bitozi au Predeshee.

Inspekta Jamila akafunga mtoto wake wa meza kwa funguo baada ya kuweka vitu vyake muhimu ndani yake, pia alizima computer na kiyoyozi kilichokuwa kinafanya kazi muda wote.

Kisha akaichukua simu ya Marehemu Dokta Masawe aina ya Siemens MC 60 na simu yake aina ya NOKIA 6230i pamoja na chaja yake, akafunga ofisi na kutoka nje katika maegesho ya magari, akaiendea gari yake na kufungua mlango na kujipakia ndani kisha akawasha gari na kutoka nje ya eneo lile na kuitafuta Wilaya ya Temeke katika maeneo ya Keko Bora nyumbani kwa Dokta Zahala.

10.

Inspekta Jamila, alishituka kutoka katika usingizi mzito,akawa bado anatafakari katika fikra zake kilichomuamsha muda ule.

Alisikia mlio wa simu, ukihanikiza katika chumba cha wageni alipokuwa amelala, pale kwa shoga yake dokta Zahara. Akatazama saa yake ya mkononi, aliyolala nayo, ilimuonesha kuwa ni saa nane za usiku!

Akanyoosha mkono wake, kivivu akachukua simu yake, akaitazama namba ya mtu aliekuwa akimpigia simu, usiku ule wa manane! Moyo wake ukawa unakwenda mbio kwa furaha, huku akiipokea ile simu na kutamka majina matatu, yalioonekana katika simu ile “SHANY KARAMA RASHIDI” Huku akiitikia kwa madaha “Halow sweety?”

Aliongea kwa mbwembwe nyigi,mizaha, na zihaka, ilitawala mazungumzo yao, huku Bwana Shany aliekuwa nje ya nc

hi kwa mambo yake ya biashara, akimtaka aende kumpokea katika uwanja wa ndege wakimataifa wa mwalimu Nyerere, akamwambia muda atakaotua Tanzania kutoka ughaibuni.

Inspekta Jamila, usingizi ulimpaa akaanza kufikiri mambo mengi kumuhusu Shany, tangu siku ya kwanza walipokutana, hadi kuanzisha mahusiano. Alipokuja kutoka katika mawazo, alisikia majogoo yanawika!

Aliinuka kutoka kitandani, akafanya mazoezi ya viungo kidogo, kisha akaingia bafuni, alipotoka hakujipodoa sana, alitaka kuwahi nyumbani kwake kabla hakujapambazuka, ili kukagua usalama, kisha awahi kazini, kwake kwa utendaji zaidi.

Alipotoka Sebuleni, akamkuta shoga yake Dokta Zahara, ameshaamka muda mrefu, anapata kifungua kinywa.

“Shoga hulali umekuwa kama kolokoloni?”

Inspekta jamila alimtania shoga yake, na Dokta Zahara kwa utani akamjibu.

“Mimi nakulinda wewe, siwezi kulala, kwani wewe ni mtu muhimu sana!”

Wote kwa pamoja, waliangua vicheko huku wakikutanisha, mikono yao hewani (Wakagonga) Baada ya kupata kifungua kinywa, Inspekta jamila, akaagana na Dokta Zahara, akaiendea gari yake, na safari ya nyumbani kwake, ikaanza huku akiwa na shauku, ya kutaka kujua usalama wa nyumbani kwake.

Inspekta Jamila aliendesha gari yake huku akiwa makini, hadi akawa umbali wa alipo na nyumbani kwake, ni takribani nyumba kumi hivi, akaegesha gari yake pembeni, kisha hakushuka ndani ya gari yake, akawa anatazama nyumbani kwake, kama kuna mtu anaetoka au kuingia! Lakini mtaa ule wa Songea pale Ilala, ulikuwa tulivu, na watu wengi walikuwa bado wamelala.

Inspekta jamila, alibakia mle ndani ya gari yake, kwa zaidi ya dakika kumi, lakini hakuambulia kitu cha maana, zaidi ya kumuona mtu mmoja mwembamba mrefu,akiwa katika mavazi machafu na chakavu, akiwa amebeba mfuko aina ya kiroba,kikiwa kichafu, akihangaika eneo lile, kuokota chupa za plastiki, na vyuma chakavu!

Inspekta jamila, alitazama saa yake, na kuona kuwa ilikuwa imeshatimu, saa kumi na mbili na robo, akajisemea kimoyomoyo, “Hawa mateja hawalali?” Kisha baada ya kusema hayo, aliteremka ndani ya gari yake, na kutembea hatua za taratibu, kuelekea nyumbani kwake.

Akiwa yupo karibu na nyumba yake, kwa tofauti ya nyumba mbili, akapishana na Yule muokota chupa. Inspekta Jamila alimtazama Yule bwana,akashangaa kiasi,kwani yeye alishazoea kuwaona vijana walioathirika na madawa ya kulevya, ndiyo, wanaookota chupa za plastiki na vyuma chakavu, lakini huyu jamaa anaepishana nae, hakuonekana sura yake, kama inachembe ya ujana!

Walipopishana, Inspekta Jamila aligeuka kumtizama kwa nyuma Yule bwana, lakini Yule bwana wala hakuwa kabisa na habari na yeye. Inspekta Jamila akafika nyumbani kwake,akawa makini mara dufu, na kila kitu anachokitazama. Akakijaribu kitasa cha mlango wake kama kimefungwa kama alivyo kiacha, naam kitasa kikawa salama! Akatazama katika kipande cha zulia la kufutia miguu pale mlangoni, naam hapo mapigo ya moyo, yakamuenda mbio kama saa mbovu!

Bahasha nyeupe ilikuwa imewekwa pale kwenye futio la miguu, kwa chini. Robo tatu ya bahasha ile ikiwa imefunikwa haionekani na kile kipande cha zulia, na robo ya bahasha ile ikiwa inaonekana dhahiri, shahiri.

Inspekta jamila, aliinama huku akiongeza umakini zaidi, akaiokota bahasha ile.Akatizama huku na huko,asimuone mtu yeyote mahala pale, hata Yule “mteja mtu mzima”hakuonekana eneo lile!

Akatoa fungua za mlango, akafungua akaingia ndani.Alikagua kila kitu muhimu mle ndani kwake,akaviona vimekaa, kama alivyoviweka,hakukuwa na badiliko lolote.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

 Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)