
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Akatoa fungua za mlango, akafungua akaingia ndani.Alikagua kila kitu muhimu mle ndani kwake,akaviona vimekaa, kama alivyoviweka,hakukuwa na badiliko lolote.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
Inspekta Jamila,aliifungua ile bahasha, akakutana na kipande cha karatasi, kilichoandikwa kwa mkono, tena kwa maandishi mekungu, kilichoandikwa “SHANKARA!” Alikisoma tena na tena, lakini hakuelewa maana yake,sasa akawa yupo katika tafakari nzito, akazama katika dimbwi la mawazo, akagutushwa na mlio wa simu yake.
“Halow Dokta?”
Ilikuwa ni simu ya Shoga yake Dokta Zahara.
“Vipi mbona kimya hunambii kama huko ni salama? Kwani roho yangu nimeitundika hapa kama mkungu wa ndizi sina amani?!”
“Mmmmh shoga, sijui niseme salama, au nisemeje, manaake hapa nimepagawa kwelikweli, kifupi nipo salama, ila kuna jambo halipo sawa!”
“Duuuh pole sana shoga, kama huko hakuko sawa beba nguo zako, uje ukae huku, hao wanaharamu wasije kukutoa roho bure!”
“Nikifa kazini,itakuwa heshima kubwa kwangu na familia yangu, ila sitorudi nyuma Dokta, nitapambana hadi hatua ya mwisho, mimi ni askari niliepasi chuoni kwa nadharia na vitendo, sikupita kule kwa njia mkato!”
Inspekta Jamila alijibu majibu ya kishujaa, akakata simu, akabadilisha nguo na kutoka, kuelekea kazini kwake, tayari kwa majukumu, ya siku ile!
Asubuhi ile, bado foleni ilikuwa haijachanganya, hivyo ilimchukua dakika ishirini tu hadi kufika ofisini kwake.
Ilipotimu saa mbili kamili juu ya alama Afande Kubuta nae aliwasili, ofisini kwao, akiwa yupo tayari kwa maelezo ya kazi aliyokuwa ameifatilia.
“Ndiyo Afande, lete taarifa!”
Inspekta Jamila, alianzisha mazungumzo yale, huku akitaka kujua kilichojili.
“Kiongozi kama nilivyowahi kusema, Bitoz alikuwa mpenzi wake Hamida, ila hajui chochote kuhusu kesi hii, tunayoifatilia, kwani nimetumia mbinu, zote za kuhoji, lakini jamaa hakuonyesha maelezo tofauti yenye shaka hata kidogo!”
Inspekta Jamila, alimsikiliza Afande Kubuta kwa umakini, kisha akatingisha kichwa chake kukubaliana, na maelezo yale.
“Sasa leo ni jumaamosi, hivyo andaa jalada la mke wa Dokta Masawe, ili jumatatu apande kizimbani, hatuna sababu ya kukaa nae!”
Inpekta Jamila, baada ya kusema maneno yale, alitoa ule waraka alioukuta nyumbani kwake asubuhi ile, na kumpa Afande Kubuta kisha akamwambia.
“Unaelewa nini juu ya neon hilo?”
“SHANKARA?!”
Alisema Afande kubuta, kwa mfumo wa kuuliza, na kushangaa!
Inspekta Jamila, yeye alikuwa ametulia makini, akimtazama usoni msaidizi wake,katika namna ya kumsoma!
Sasa ikawa zamu ya Afande Kubuta,kuzama katika lindi la mawazo.
“Nini hii?! Na umeipata wapi?” Sasa ikawa zamu ya Afande Kubuta kuuliza.
“Huo waraka, nimeukuta leo mlangoni kwangu! Alieuweka simjui, wala una maana gani vilevile sitambui, ila lazima kuna maana, tena ni kubwa sana!”
Inspekta Jamila, alimueleza msaidizi wake kutokulala kwake ile jana, kwa simu ya Geradi Mwaipopo, hadi asubuhi alipokwenda kukagua nyumba yake, alipoukuta huo waraka, ila hakuthubutu kumweleza mahali, alipolala!
-
Askari wale wakapanga na kupangua, hadi saa nane mchana. Walipeana mikakati ya kufanya, ili kushinda kesi ile kwa kishindo.
“Sasa naona leo hapa tulipofika,siyo pabaya sana, itabidi tufunge kazi kwa leo, ila kama ujuavyo, askari muda wote yupo kazini! Hivyo tunaweza kuitana muda wowote ule!” Inpekta Jamila alimwambia msaidizi wake, kasha ule waraka akaufungia katika droo ya meza yake, akaendelea kusema.
“Leo usiku nina mgeni anaingia kutoka ughaibuni, ambae ndiye dakitari wa mwili wangu, nyonda mkalia ini wangu, kipenzi cha roho yangu!” Inspekta Jamila alikuwa akizungumza huku akitabasamu, na kumfanya Afande kubuta nae kuwa katika hali ile ya kutabasamu!
“Haya sasa mie nifanyeje Afande?” Afande Kubuta alisema maneno hayo huku nae akiwa anatabasamu.
“Nataka uniambie duka, wifi yangu anaponunulia Msio, kwani nataka kumsinga Bwana,najua ameyakosa mambo haya muda mrefu”
“Hahaha Afande Msio ndiyo nini? Kwani ndiyo kwanza nakusikia wewe hilo neno!”
“Heee makubwa haya, wewe hujui msio?! Tuseme huyo wifi yangu huko nyumbani kwako, hajawahi kukusinga?!” Inspekta Jamila alimuuliza msaidizi wake, huku akimshangaa!
“Hawa wanawake wenzangu,baadhi yao wamezidi, yaani unakaa na mume au bwana, hujawahi kumsinga hata siku moja, ukamwimbia nyimbo za mahaba, ukamtuliza ndani, hakika unyago ni kitu muhimu sana kwa wanawake!”
“Basi niletee huyo wifi yangu, nikaenae walau siku tatu tu, atabadilika huyo!” Wote wakaangua kicheko kisha wakaagana.
……………
Ilikuwa saa nne za usiku, Inspekta Jamila, alikuwa anakaribia uwanja wa ndege wa kimataifa wa JULIUS KAMBARAGE NYERERE,alipokuwa akikata kona ya kuingia katika uwanja wa ndege, akiiacha ile barabara ya Pugu, mara macho yake yakamvuta kumtiza muokota chupa na vyuma chakavu, aliekuwa amesimama pale kona katika njia ya kutokea uwanjani, akiwa na kiroba na nguo chakavu!
Inpekta Jamila akasimamisha gari ili amtizame sawasawa, akasikia kelele za tairi kutoka nyuma, zilizokuwa zinasuguana kwa breki,iliyokanyagwa ghafla!
Inspekta Jamila, haraka alikanyaga mafuta gari yake, nakuokoa ajali ambayo angeisababisha yeye, kwa kusimama ghafla
Barabarani.
Ile gari ya nyuma ilitanua kulia, ikasimama sawasawa na gari yake. Dereva wa ile gari alishusha kioo, akatazamana na Inspekta Jamila, huku dereva Yule akiwa amefura kwa hasira, alimuonyesha vidole vya kati vya mikono yake yote miwili, kisha akapandisha kioo akaondoa gari,kuelekea kwenye geti na kuchukua kadi maalum, akaiingiza gari yake katika maegesho akaiegesha na kushuka, akaendelea na hamsini zake!
Inpekta Jamila, pale alipo aliishuhudia ile gari dereva wake aliemtusi,ikiondoka mbele yake, akaiandika namba ya gari ile. Nae akasogeza gari yake hadi pale kwenye lile geti, akachukua kadi nakwenda kuiegesha gari yake, kisha kwa mwendo wa haraka, alitembea ili kumuwahi Yule muokota chupa na vyuma chakavu.
Inspekta Jamila, alitazama eneo lote la pale alipomuona Yule bwana muokota chupa na vyuma chakavu, alipokuwa amesimama awali, lakini hakumuona! Akavuka barabara hadi pale kituo cha basi, chakuendea mjini, pia hakumuona, kichwa chake kikaanza kuchanganyikiwa!
Kinachanganyikiwa kwa sababu, hakuna waokota vyupa na vyuma chakavu, wanapokuwa kazini, wakapanda gari, kwani hivyo vitu wanavyookota watavipataje? Pia hakuna waokota vyupa na vyuma chakavu, wanaofanya kazi zao usiku kama ule! Lakini pia Muokota vyupa na vyuma chakavu huyu, aliemuona muda mfupi uliopita, ndiye aliemuona asubuhi, maeneo ya nyumbani kwake Ilala mtaa wa Songea!
Inspekta Jamila, alirudi uwanja wa ndege ili kuendelea na jambo lililompeleka pale, lakini fikira zake, zikianza kumtilia mashaka Yule bwana.
Alikwenda mpaka katika maegesho lilipokuwa gari lake, akaikagua gari yake, ikawa ipo salama kabisa.
Akaelekea pale wanapokaa watu kuwasubiri abiria, mara wakasikia tangazo kupitia vipaza sauti vilivyokuwa pale uwanjani kuwa, ndege iliyotarajiwa kufika muda ule, imefika salama, na watu wakaanza kujongea, karibu na mlango ule mkuu wa kutokea wageni, ili kuwapokea wageni wao, huku wengine wakiwa na mabango madogomadogo, yaliyoandikwa majina ya wageni wao, ili mgeni iwe rahisi kwake, kumtambua mwenyeji wake, hasa ikiwa hawajawahi kuonana ana kwa ana!
Inspekta Jamila, alikuwa makini na kila aliekuwa akitoka katika mlango ule, na mara, akamuona mtu wake aliekwenda kumpokea, akamkumbatia na kumbusu, kasha akamwambia “Karibu nyumbani mpenzi wangu.”
“Asante nishakaribia mpenzi” Alijibu mgeni Yule,Shani Karama Rashidi.
Inspekta Jamila, alisaidiana mizigo na mpenzi wake, wakaenda kwenye gari yake, akapakia mizigo ndani ya gari yake, akajipakia upande wa dereva, na Shani upande wa abiria, safari ikaanza kuelekea mjini. Baada ya gari ya Inspekta Jamila, kuondoka eneo lile, huku nyuma gari ndogo nyeupe, ilikuwa ikimfatilia kwa mbali!
“Sweety nimekodi hotel,ya Kibodya ile ya mtaa wa Nkruma, ili tupumzike mahala pale!” Inspekta Jamila, alimwambia mpenzi wake, huku akiwa makini katika usukani.
“Alaa kama umeamua hivyo, hakuna tatizo, kwani mfungwa hachagui gereza, nami kwako ni kama mfungwa wa mapenzi kwako!”
Walitabasamu kwa pamoja, huku wakiwa wameshafika katika taa za Tazara. Usiku ule barabara zilikuwa hazina foleni.
Hatimae wakafika Kibodya Hotel,wakateremka na mizigo baadhi, wakaingia hotelini, Inspekta Jamila, alichukua funguo mapokezi, na kwenda hadi katika chumba alichopanga, akafungua mlango huku akitamka “Karibu waukweli, mimi nashuka chini, kumalizia mizigo kwenye gari.” Inspekta Jamila, alimbusu mdomoni mpenzi wake, akashusha ngazi, kuelekea nje ya Hotel ile.
Inpekta Jamila, alifungua mlango wa gari ili atoe mizigo iliyobakia, mara akajihisi hakuwa peke yake mahala pale!
Akageuka nyuma ili ajiridhishe fikira zake, lakini hakuweza kumaliza mzunguko wa shingo yake, kwani kitu chenye ugumu kama wa ubao, kilitua usawa wa kichogoni kwa pigo moja, lililopigwa kiufundi na mpigaji, na Inspekta Jamila, alianguka mle ndani ya gari kama mzigo, akapoteza fahamu.
Inspekta Jamila, alipokuja kutanabahi, alijikuta amefungwa kamba katika kiti cha chuma, akiwa amezingiliswa kamba kutoka mabegani hadi kiunoni, huku mikono yake ikiwa imefungwa kwa nyuma na kamba zile, bila kusahau miguu yake, ambayo pia ilitatalizwa kwa kamba zile za nyloni, huku akiwa amekalishwa katika kiti kile! Ama kwa hakika alikuwa amepatikana khaswa.
“Thatha mkubwa,huyu dem tumalidhe, au tumtie ulemavu wa maisha, kwani huyu mpumbavu thana.”
Inspekta Jamila, aliyasikia mazungumzo yale, ya Yule mtu aliekuwa akizungumza na simu, ili kupata maelekezo, kutoka kwa huyo aliekuwa akizungumza nae. Ila kitu kilichomfanya sasa ainue kichwa chake na kumtizama Yule mtu aliekuwa akizungumza na simu,ni ile lafidhi ya Kithethe!
Alitazamana na mtu Yule, kisha akaona pia na watu wengine wawili, wakiwa mle. Nao pia walikuwa wakimtazama, ingawa wale jamaa, wao walimtazama kwa dharau na kedi ya hali ya juu!
Inspekta Jamila, akiwa pale kitini alipofungwa kamba, aligeuza uso wake, na kutazama kulia na kushoto kwake, hakuona watu wengine zaidi ya hawa watatu, waliokuwa wamesimama mbele yake.
Alikuwa katika chumba kikubwa, ambacho hakikuwa na kitu chochote zaidi ya kile kiti cha chuma, alichofungwa nacho!
“Nimekuelewa bothi, thithi tunamalidha kabitha.” Yule bwana anaezungumza kwa kithethe, alihitimisha mazungumzo yake, akakata simu.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media