BARUA KUTOKA JELA (25)

Zephiline F Ezekiel
0
Mtunzi: Ibrahim Gama

SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO
ILIPOISHIA...
JM na Shankara,na mke wa marehemu Dokta Masawe,siyo muda mrefu,watafikishwa mahakamani,mara baada ya Shankara kupata nafuu majeraha ya risasi na Jm kifua

chake kimepata matatizo,nae yupo hospitali,wote wakipata nafuu,watafikishwa katika vyombo vya sheria,ili wakajibu mashitaka yao!”

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
IGP alinyamaza kimya ili kutoa nafasi kama kuna swali,alipoona kimya,akaendelea.

“Kuanzia kesho mmepata likizo,ya mwezi mmoja,leo hii

mtapata pesa yenu ya likizo,na kesho nitakuwa na

Mwaduga Dingo,ili nimpe majukumu mapya.”

IGP aliposema maneno yale kabla hajaagana na vijana

wake, kupitia simu yake ya upepo, ilisikika taarifa

iliyowafanya waume meno kwa ghazabu.Taarifa ile ilisema hivi.

“Jambazi sugu,Jeradi Mwaipopo,ametoroka katika ulinzi wa polisi,pingu alizofungwa,zimekutwa chini ya uvungu wa kitanda,na askari wawili waliokuwa wakimlinda,wamekutwa wamezirai”!

“Kuanzia sasa, kila kitu kimevurugika, Likizo nimeifuta na mtarudi tena kazini, mpaka huyu Jeradi Mwaipopo, tuwe nae mikononi!”

IGP alisema maneno hayo huku akiwa amekasirika vibaya sana.

Na wote askari wale,Inspekta Jamila, na Sajenti Kubuta kwa pamoja wakasema.

“Sawa afande!”

IGP akawataka askari wake aende nao Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ili akajionee mwenyewe, kilichotokea.

Bila kuchelewa, safari ya Hospitali ya Muhimbili ikaanza!

IGP Kupitia kifaa chake cha mawasiliano, akatoa amri kwa wakuu wa polisi wa kanda zote za Dar es salaam, wahakikishe, vituo vya mabasi, uwanja wa ndege, bandari ya kwenda Zanzibar, vyote vinakuwa na ulinzi mara moja, ili kumzuia Jeradi Mwaipopo, asitoroke nje ya Mkoa huu!

Picha za Jeradi Mwaipopo zikasambazwa katika vyombo vya habari, ikiwemo magazeti na Luninga, kuwa anatafutwa na Polisi, na mtu yeyote atakae fanikisha kukamatwa kwake, Donge nono limeandaliwa kwa ajili yake!

IGP, pamoja na vijana wake wakaelekea katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, na wakajionea hali halisi ilivyokuwa!

Askari wawili walikuwa wapo hoi, hawajitambui kwa usingizi! Lakini pia povu jeupe likiwa katika vinywa vyao! Ulimi ukiwa umetoka nje kwa kiasi kikubwa sana!

Walikuwa wakipumua kwa tabu, mithili ya mtu aliekuwa katika ‘Sakalatilmauti’Yaani hatua za mwisho anazozipitia mwanaadam, kabla hajafikwa na umauti.

Pingu zilikuwa chini ya kitanda sakafuni, zikiwa zimefunguliwa!

IGP, alitikisa kichwa kwa masikitiko, nakuwataka askari aliokwenda nao pale hospitali, kuhakikisha kwa gharama yoyote, Jeradi Mwaipopo, anatiwa katika mkono wa sheria, tena haraka iwezekanavyo!

Inspekta Jamila na Sajenti Kubuta, waliitikia “Sawa Afande.” Huku wakisaluti

Inspekta Jamila, alivaa glovu na kuanza kuikagua miili ya askari wale,waliokuwa hawana fahamu.

Akagundua walikuwa hawana simu zao za mikononi, akashangaa!

Akakikagua chumba kizima kwa umakini mkubwa, hatimae macho yake yakakutana na mfuko laini mweusi wa plastiki, uliokuwa pembeni ya chumba kile.

Akauwendea ule mfuko, na alipoufikia akachuchumaa na kuutazama kwa makini. Ule mfuko ulikuwa haukufungwa juu yake, hivyo uliweza kuonesha kitu kilichokuwamo ndani yake!

Inspekta Jamila akiwa pale alipo, aliushuhudia mfuko ule ndani yake, kulikuwa kuna mabaki ya chakula.

Viazi vilivyokaangwa pamoja na mayai, maarufu huitwa chipsi, nyama ya kuku wa kukaanga na mifupa ya kuku iliyokwishaliwa tayari!

Inspekta Jamila, aliuchukua ule mfuko kwa umakini mkubwa, kisha akamgeukia bosi wake na kumwambia. “Afande nahisi hiki chakula watakuwa wamekula askari wetu, na bila shaka kinaweza kikawa ndiyo sababu ya haya matokeo tunayoyaona!” Alisimama kuzungumza Inspekta Jamila, na IGP kwa haraka akadakia.

“Kwa nini unahisi hivyo Inspekta!”

Inspekta jamila huku akiwaoneshea vidole wale askari waliokuwa mahututi, alimjibu kiongozi wake kwa unyenyekevu mkubwa.”Afande, hao askari mikono yao inaonesha walikula chakula hiki na hawakunawa baada ya kula! kwani mafuta yapo katika vidole vya mikono yao na mabaki ya tomato !”

“Inspekta unamaanisha chakula hicho kinaweza kikawa na sumu?!” IGP aliuliza kwa mshangao kisha akaendelea “Itabidi haraka kikapimwe ili tujiridhishe, na kama itathibitika ni kweli, swali hili litahitaji majibu, nani alieiweka sumu hiyo, na atakuwa ametumwa na nani?!”

Tafakari na ukimya ulitanda kwa muda, kisha Inspekta Jamila akasema kumwambia IGP.

“Afande mie naona, hawa askari tufanye kila tuwezalo, ili kuokoa maisha yao, kwani wao pekee kwa sasa ndiyo watakaokuwa na majibu sahihi, ya waliponunua au mtu aliewaletea chakula hiki, au chochote kilichopelekea kikaingia humu ndani chakula hiki!”

Mara moja aliitwa mganga mkuu pale hospitali, na kutakiwa kuzipima zile chipsi zilizosalia kama zipo salama, huku askari wale baada, ya kuwafanyia uchunguzi wa kina askari wenzao, waliokumbwa na masahibu yale, wakakabidhiwa madakitari ili kujaribu kuokoa maisha yao.

Na dakika arubaini baadae, Mganga mkuu aliwapa ripoti ya chakula kile!

“Vipimo vimeonesha kuwa, chakula hiki kimewekwa dawa za usingizi kwa kiasi kikubwa aina ya LAGACTIL, dawa tunazozitumia kuwapa wagonjwa wa akili, ili kupata usingizi! Kama mwendawazimu amezapo dawa hizi hupata usingizi, basi alapo mtu asiekuwa mgonjwa wa fahamu, anaweza kupata madhara makubwa sana katika ubongo wake, kama kulala kwa muda mrefu zaidi, kulewa, kutokwa na ulimi kama mbwa,na hata kufa, ikiwa atakuwa amekula au kulishwa dawa hizo kwa kiasi kikubwa.”

Alihitimisha mganga mkuu taarifa yake kwa askari wale, na wao wakawa wanamaswali mengi yaliokosa majibu sahihi, nani alieweka dawa zile katika chakula kile?! Na je mtandao wa genge la uhalifu lakina JM bado halijamalizika?! Fadhaa, hasira, chuki na sintofahamu, ikawakumba askari wale na kiongozi wao mkuu kabisa!

*******

Jeradi Mwaipopo, akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi wawili, katika chumba maalum pale hospitali ya taifa ya Muhimbili, alikuwa amefungwa pingu za miguu, na pia pingu za mikono! Ingawa katika mikono, alifungwa pingu mkono mmoja, na sehemu nyingine ya pingu ile, ilikuwa imefungwa katika kitanda cha chuma alichokuwa amelazwa.

Jeradi mwaipopo alikuwa katika maumivu makali, lakini akiwa katika fahamu zake kamili!

Alijizoazoa katika kitanda kile na kutaka kukaa kitako,akashindwa. Akawaambia askari wale. “Ndugu zangu nataka kwenda chooni.”

Askari aliekuwa na funguo za pingu, alizofungwa nazo JM, akamsogelea na kumfungua pingu za miguu zenye nyororo ndefu kiasi, kisha akamfungua pingu ya mkononi, ili waende nae chooni.

Jeradi Mwaipopo au kifupi JM, akawatazama askari wale, kisha akawaambia huku akiwatazama usoni moja kwa moja! “Ndugu zangu mnajuwa kuwa mie ni mwenzenu? Mbona mnanifanyia hivi?!”

Askari aliemfungua pingu akamjibu. “JM wewe ulikuwa askari, ila sasa siyo askari, lakini hata kama bado ungalikuwa ni askari, sie tunatekeleza wajibu wetu.”

JM, alitafakari kidogo, kisha akainuka na kuelekea katika choo, huku akifatwa kwa karibu na askari wale.

JM, aliingia chooni akiwa anatembea kwa kuburuza miguu yake, kutokana na pingu alizokuwa amefungwa nazo miguuni mwake muda mrefu, na kukazwa kumpa maumivu.

Alijisaidia haja kubwa na ndogo, huku akiwa akili yake ikifanya kazi kwa haraka na kubawabu hiki na kile, hadi alipomaliza haja zake, akawa amekwisha pata maarifa yakufanya! Akajisafisha na kurudi kitandani kwake, katika mwendo kama ule wa awali. Akakaa kitandani, na kunyoosha mikono yake, ili afungwe pingu kama awali, naam alifanyiwa huduma hiyo, iliyokuwa imemstahili kwa wakati ule, huku askari mwingine akimfunga zile pingu za miguu, JM sasa akiwa amelala chali, akasema kuwaambia askari wale.

“Ngugu zangu, naomba msaada mmoja kwenu, nina ndugu yangu anaishi jirani na hapa, naomba mnifanyie huduma ya simu, kumwambia kama nipo hapa, ili aniletee chakula, lakini pia nitamwambia awawekee vocha simu zenu, tafadhalini sana.”

Wale askari wakatizamana, kisha mmoja akamjibu JM kwa kumwambia. “Huo siyo utaratibu wa kazi yetu JM, wewe upo chini ya ulinzi, hivyo kukuitia watu ni kuhatarisha usalama wako na wetu, hilo halitowezekana, labda isubiri zamu itakayokuja, sie hapana JM!”

JM akiwa ametoa macho kwa jibu lile, akamjibu askari Yule, kwa kumwambia.

“Hiyo ni haki yangu ya msingi askari, sheria inaniruhusu kufanya hivyo! Kisha mie sijahukumiwa bado, bali ninatuhumiwa tu, hivyo nina haki ya msingi kwa mujibu wa sheria, kumbuka mie pia ni askari hivyo ninatambua haki zangu za kimsingi. Pia hiyo zamu ijayo sidhani kama haifanyi kazi kwa mujibu wa sheria. Naomba bwana nisaidie, au kama unataka nikulipe kwa jambo hilo, basi nitajie kima!”

Sasa ikawa zamu ya wale askari kufikiri, huku JM akiombea akubaliwe ili atimize azma yake, aliyoikusudia wakati ule!

“Unataka msaada JM, burebure tu, watu tupo kazini bwana, kama unaweza kutupa elfu hamsini, mie nitakupa simu yangu umpigie huyo jamaa yako, kama huna pesa, basi endelea kuugulia maumivu yako!”

Alisema askari mmoja aliekuwa na funguo za pingu za JM, ambae ndiye aliekuwa kiongozi.

JM,alitabasamu huku akichezesha kichwa chake kushoto kulia, kisha akasema. “Mie kama mnionavyo hapa nilipo, sina pesa hata kidogo, ila huyo ndugu yangu, naweza kuzungumza nae, akawaletea pesa hata elfu hamsini kila mmoja, wachilia mbali wewe kutaka elfu hamsini mgawane, mie natambua kuwa, mbuzi anakula kwa urefu wa kamba yake!”

Naam mjadala ule ukapata muafaka kuwa, JM azungumze na ndugu yake.

Jeradi Mwaipopo, alipewa simu, akabonyeza namba kadhaa kwa ule mkono wake mmoja uliokuwa huru, kwani mkono mmoja wa kulia, ulikuwa umefungwa pingu, pamoja na kitanda! Mkono wa shoto, uliwachwa kusudi, ili aweze kujikuna na kumpa huduma zingine!

JM alizipiga namba zile, na upande wa pili, ikawa inaita simu ile. Ama kweli, penye udhia, penyeza rupia.

“Halow…” JM alisema baada ya kupokelewa ile simu upande wa pili, na kuendelea. “…JM hapa, nipo hospitali ya muhimbili, huku karibu na Moi,nikiwa chini ya ulinzi. Hii simu ya askari nimeiomba hapa ili niwasiliane na wewe uje kunifaa nduguyo, naomba uje na Shilingi laki moja ili niwape viongozi wangu bwana, hawa ni watu muhimu sana kwangu, nakaa nao vizuri tu, kisha niletee……” JM akasimama kuzungumza na simu, akawauliwa wale askari.

“Mtakula nini awaletee, semeheni tu, kwani mchana unaingia!”

Wale askari walitazamana kisha mmoja akatabasamu, akasema .

“Mwambie atuletee chipi yai, na kuku aweke pilipili nyingi.”

JM huku akishusha pumzi ndefu akarejea katika simu na kumwambia mtu aliemuita ndugu yake. “……niletee chipsi mayai, na kuku sahani mbili, weka pilipili nyingi, watengenezee vizuri sana. Mie niletee maziwa fresh yananitosha, ukiniletea na pesa kidogo, utakuwa umenifaa sana!”

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

 Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)