
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA TANO
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Mbona mmeshituka sana, ina maana hamna taarifa za picha hizo kufika ofisini kwenu? Mimi nimejua mmekuja kuchukua nyingine ili mkamilishe huo upelelezi wenu!”
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
Neema badala ya kurudia kauli yake, akatoa maneno yalioonyesha kumshangaza, kwa namna kesi ile inavyoshughulikiwa!
Hatimaye akairudia tena kauli yake, sasa akiwa makini zaidi ya mwanzo.
“Juna alikuja afande mwenzenu wa kike, aliyejitambulisha kwa jina la afande Jamila. Amechukua picha tatu kutoka katika albam hizo, na ameahidi kuzirudisha mara baada ya kukamilisha upelelezi wenu.”
Neema alirudia kauli ile huku akiwatazama machoni maafande wale wawili waliopigwa butwaa ya mwaka!
“Samahani dada, huyo afande Jamila alipokuja alikwambia anatokea Kituo gani?”
Aliuliza afande Kubuta. “Na alikuonyesha Kitambulisho?” Akaongeza swali afande Magane.
Sasa ilikuwa zamu ya Neema kupigwa na butwaa.
“Yaani mnataka kuniambia, kwamba afande Jamila hamumtambui?” Aliuliza Neema huku akivuta tafakari na kuwa makini zaidi.
“Jibu swali mwanamke”, afande Kubuta akasema huku akiwa amechanganyikiwa kwa kauli ya neema.
“Jibu maswali mwanamke.” Afande Magane akadakia na huku akiendelea kusema. “Hii ni kesi ya mauaji hivyo usije kuleta mzaha umesikia?”
Neema aliitikia kwa kutikisa kichwa. Kisha akajibu, “Alipokuja hapa jana alijitambulisha yeye ni askari polisi na akatoa kitambulisho chake kama nyinyi mlivyofanya. Ila hakusema ametokea kituo gani cha polisi! Akataka “photo albam” kama nyinyi mlivyotaka, nami nikampa na baada ya kuzipekua, akachomoa picha tatu akatia kwenye mfuko wake kama nyinyi mlivyochukua hizo albam na kutia katika mfuko wenu. Ila yeye hakutaka kitabu cha kumbukumbu, baada ya kupata picha zile akaaga na kuondoka.”
Afande Kubuta akamuuliza “je alikuonyesha picha alizochukua?”
“Hapana” Neema akajibu.
“Ila unazitambua picha zilizokosekana katika albam hizo?”
Afande Magane akamuuliza Neema huku akimkazia macho.
“Hapana kwani mimi nimekuja hapa ulipotokea msiba, kabla ya hapo nilikuwa siishi hapa, hivyo picha za marehemu dada zote alizopiga ukiondoa za harusi yake ambazo nimeziona nyingine zote sizijui.” Akamaliza Neema huku akifuta machozi yaliyoanza kumtoka, labda baada ya kukumbuka picha zilizomuonyesha dada yake akiwa katika maisha yake ya ndoa!
“Sawa alikuachia namba za simu huyo afande Jamila?” Hatimaye akauliza afande Kubuta.
“Hapana hakuacha, ila alichukua namba yangu ya simu na kusema angenipigia pindi ambapo angelihitaji msaada kutoka kwangu.”
Ama kwa hakika askari wale walichanganyikiwa sana kwani kila kitu walichokitarajia kuwasaidia kumtambua huyo afande Jamila waliambulia jibu la hapana! Ama kweli walikuwa wamepigwa bao la kisigino. Mwisho wa yote wakaacha namba zao za simu na kumwambia Neema.
“kama atakuja tena huyo afande Jamila muulize anatokea kituo gani, na unipigie simu mara moja. kwani mimi ndiye mpelelezi katika kesi hii. Hivyo mtu yeyote atakayejihusisha na kesi hii, lazima mimi nimtambue.”
Mwisho wakaaga na kuondoka.
Afande Kubuta alibisha hodi Ofisini kwa Bosi wake na kutoa heshima za kijeshi kama inavyotakiwa na kuketi kitini baada ya IGP kumuashiria kufanya hivyo.
IGP akanyoosha mkono kuchukua vitu alivyoagiza kutoka kwa afande Kubuta na kitu cha kwanza kuanza kuangalia zilikuwa ni zile albam nne zilizokuwa mbele yake.
Aliangalia moja baada ya nyingine huku akiangalia hadi zile picha zilizokuwa zimewekwa nyuma ya picha, mwisho akazimaliza zote albam nne bila kuona kitu alichokikusudia!
Akainua uso na kumtazama usoni kijana wake afande Kubuta. Na kwa mara ya kwanza akanyanyua mdomo wake kusema.
“Kuna picha humu ambazo zimetolewa! Kwani zipo sehemu zilizokuwa tupu kuonyesha kwamba kulikuwa na picha! Kwani si kama picha zilizomo humu hazitoshi kuijaza albam kwani kuna picha nyingi hadi nyingine zimewekwa picha tatu katika sehemu moja! Je picha hizo umezitoa wewe? Na kwa sababu gani wakati nilikwambia ulete kama utakavyozichukua?”
Akauliza IGP huku akiwa amechukia na amefula kwa hasira!
“Hapana Mkuu, kama ulivyoagiza ndivyo nilivyotekeleza. Ila picha zilizopungua, nimeambiwa kwamba amekwenda afande Jamila amezichukua na kuahidi angezirudisha baada ya upelelezi kukamilika!”
Sasa ikawa zamu ya IGP kufadhaika, aliinuka kwenye kiti chake na kusimama huku akiwa ametoa macho pima! Kitu ambacho hata afande Kubuta naye alishangaa. Kwani alidhani labda huyo afande Jamila, alitumwa na Bosi huyo kama yeye alivyotumwa kwenda kuchukua zile albam. Sasa kama naye anashangaa je kuna nini kinachoendelea. Na je hizo picha ni za nini? Hatimaye IGP akauliza.
“Huyo afande Jamila nani kampa kesi hii?!” Sasa IGP alionekana kama ana hofu katika sura yake lakini pia jazba ilimtawala vile vile.
Afande Kubuta akaisoma hali ya Bosi wake akawa makini sana.
“Sielewi mkuu, lakini pia katika kituo chetu cha Magomeni hatuna jina la afande Jamila, achilia mbali kuwa mpelelezi. Pia nilidhani labda amri hii imetoka juu, katika kuweka askari mwingine bila mimi kujua! Ili naye afatilie mwenendo mzima wa kesi hii. Sasa kama mkuu hujui lolote kuhusu afande Jamila, nini kinaendelea katika kesi hii?”
Afande Kubuta aliuliza huku akiwa amechanganyikiwa kwa mawazo. Pia baada ya maelezo yake “IGP” akagundua mchezo wote atakuwa anaufahamu huyo afande Jamila, lakini yeye kwa nini asifahamishwe alipohitaji kujua mpelelezi anayeendesha kesi ya marehemu Hamida?!
Ila yeye alipewa jina la afande Kubuta, nambari ya faili na nambari ya simu ya afande Kubuta. Sasa huyo afande Jamila anafanya kazi kwa kutumwa na nani na kwa faida ipi hatimaye “IGP” aliwaza na kuinua mkono wa simu kisha kubonyeza nambari kadhaa na simu ikawa inaita upande wa pili.
*******
Madereva Taxi katika Kituo cha Taxi Magomeni Usalama, walikuwa katika harakati za kazi yao. Wapo waliokuwa wakifuta magari, wengine kuyaosha kabisa. Pia wapo waliokaa juu ya Boneti na wapo waliokaa juu ya Buti. Wapo waliokuwa ndani ya magari yao wakisinzia ili mradi kila mtu alikuwa na harakati zake.
“Karibu dada, hii hapa pamba nyepesi full kiyoyozi na bei sina, ngoma full tank siyo mafuta ya kidebe.”
Dereva wa taxi alijinasibu kwa kuipamba gari yake, na kumshawishi Yule abiria ili apande kwenye gari yake. Huku akifungua mlango wa nyuma wa gari yake, ili abiria aweze kuingia, kisha watapatania ndani bei ya sehemu atakayompeleka.
Yule abiria aliekaribishwa bila kujishauri wala kusita, akazama ndani ya gari ile.
Dereva badala ya kuingia ili waanze safari, akaanza kupiga honi mfululizo! Mara kijana mmoja mfupi mweupe alikuja mbio alitokea upande wa kushoto wa gari lile ambalo walikuwa wamekaa vijana wengine kadhaa wakicheza draft.
“Mpeleke huyo Dada sijaongea naye kitu chochote mtaelewana.”
Aliongea yule kijana aliyemkaribisha yule abiria.
Alipopanda yule dereva na kuwasha gari, yule abiria akatambua kwamba, yule kijana wa mwanzo alikuwa ni shanta, huyu sasa ndiye Dereva.
“Samahani Dada tunaelekea wapi?” Yule Dereva Taxi aliuliza huku akiondosha gari.
“Nipeleke Kimara Suka, itakuwa shilingi ngapi?”
“Ahaa Kimara Suka kubwa dada yangu, unakwenda pale pale kituoni, au kule shule, au kule Golan au kwa yule Mwandishi maarufu wa riwaya Hussein Tuwa?”
“Nakwenda Kimara Suka Hotel utanichaji shilingi ngapi?”
“Alaa kama pale ni shilingi elfu nane tu Dada yangu!” Alijibu yule dereva wa Taxi huku akigeuza Gari na kuanza safari.
“Wewe una bei sana kwani nilikuwa nikimchukua yule kijana Mwaduga, alikuwa akinipeleka kwa shilingi Elfu sita tu! Sijui leo kapakia, kwani sijamuona yeye wala gari yake!”
Yule abiria alimwambia Yule dereva wake kwa upole.
“Usinikumbushe sister Bwana. Mshikaji wetu jumba bovu limemdondokea! Jamaa ana bahati mbaya sana Yule.”
Dereva alimwambia abiria wake kwa masikitiko huku akionyesha huzuni usoni mwake!
“Umesema jamaa kaangukiwa na jumba bovu siatakuwa ameumia sana?!”
“Sio hivyo unavyofikiria, jamaa yetu kapatwa na matatizo. Kapewa msala wa mauaji hivi hivi, majambazi na wauaji wanaachwa wanatembea mitaani tu!”
Alijibu Yule taxi dereva, katika lugha yao ya kijiweni, ambayo ilimpa wakati mgumu, abiria wake kumuelewa kwa urahisi, maana ya baadhi ya maneno!
“Aaaaaa Bwana usiniambie!”
Yule abiria aliuliza swali kwa mfadhaiko, na fadhaa kubwa.
“Kweli sister wangu, jamaa ana miezi miwili na kitu, sasa yupo katika maisha mabovu mahabusu. Yaani kama alikupakia basi ni siku nyingi kidogo. Sasa bei zimebadilika mafuta yamepanda bei sana.”
Alijibu yule dereva Taxi nakutoa ufafanuzi huku akibadilisha gia, sasa wakiwa maeneo ya Aljentina Manzese.
“Kwani kilimpata nini jamani kaka wa watu duh kama namuona vile!?”
Yule abiria aliuliza kwa masikitiko, na kuonyesha sura ya huruma na kuendelea kueleza.
“Mimi nilikuwa Chuoni nimekuja pale kituoni kwenu kama miezi mitatu iliyopita, na Mwaduga ndiye alikuwa ananizungusha katika mizunguko yangu!”
“Yaani sister we acha tu, kwani kesi ya mshikaji imekaa vibaya sana!”
Dereva Taxi akaongeza msisitizo wa jambo lile.
“Umesema kesi ya Mwaduga imekaa vibaya sana, kwa sababu gani, wakati umesema ni jumba bovu tu limemwangukia, yaani yeye hakufanya jambo lile?”
“Dada, yule mshikaji keshapotea yule kwani amepewa soo nne. Mauaji, kukutwa na silaha, kula njama ya kutenda kosa na wizi wa kutumia silaha. Haya yote anaweza kuchomoa, lakini kosa lakukutwa na silaha, jamaa si washamuachia msala?! Huwezi kuamini sister lakini nakuambia yule Demu alieuliwa ni mali ya wakubwa, kwani Bosi wa polisi wa cheo cha juu kabisa, ndiyo alikuwa anaburuza ule mzigo”
“Ha ha haa, sasa kaka unafika mbali sana, yaani wewe unajua pia kuwa huyo marehemu, anaeshitakiwa Mwaduga kuwa alimuua, kuwa ni kimada wa mkubwa wa jeshi la polisi!?”
Yule abiria alionyesha kutaharuki kupita kiasi, lakini pia alijiona ni mwenye bahati kubwa kuichagua gari ile, kwani dereva wake ni mtu mropokaji! Kwani anatoa taarifa nyeti kwa gharama nafuu sana!
“Siyo mzaha sister wangu, mimi nina mshikaji wangu anapaki Town yeye ndiyo ilikuwa kazi yake! Ameisha mpakia sana yule Demu kumpelekea Bosi wa polisi, karibu mara tatu! Na yule Bosi alikuwa anamlipa pesa nzuri sana! Yaani jamaa anaweza kumchukua yule Demu Mikocheni nyumbani kwake, na kumpeleka labda bwalo la polisi ostabey akalipwa shilingi elfu ishirini! Au siku nyingine humpeleka Bagamoyo na kumuacha kwenye hoteli za kitalii siku za mwisho wa wiki, akalipwa laki moja!
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media