
Mtunzi: Ibrahim Gama
SEHEMU YA SABA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Sasa nimewaita hapa, baada yakuona maelezo yaliyopo katika faili hili hayatoshelezi, na hayaridhishi katika kuiendesha kesi hii, lakini pia kuna jambo lisilo la kawaida limejitokeza!”
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
ENDELEA...
“IGP” alisema maneno hayo huku akiwaangalia maafande wale walivyokuwa makini na utulivu wa hali ya juu, wakienda sanjari na ukakamavu!
“Kesi hii amepewa kijana hapo!”
Alisema “IGP”, huku akimnyooshea mkono ulioshika faili Afande Kubuta, kisha akaendelea.
“Kuna mtu amejiingiza katikati, nae akifanya upelelezi wa kesi hii! Ambapo ni kinyume na utaratibu wa Jeshi la Polisi. Kwani askari asipotambulika na Mkuu wake kama anafanya nini kwa wakati gani kuna “Risk” nyingi sana zinazoweza kupatikana, kama vile Rushwa, askari kuuwawa au kuumia wakati akiwa hayupo kazini kisheria. Pia anaweza kuharibu upelelezi wa kesi, hivyo ni lazima atafutwe mara moja na aletwe kwangu ili anipe maelezo yatakayoniridhisha. Vinginevyo atapoteza kazi yake, ikiwa kweli ni askari halali wa jeshi la polisi, na atakaa selo.”
“IGP” alisema maneno hayo huku akiwa amefura kwa hasira. Mwisho wa yote “IGP” akaagiza kesho saa mbili asubuhi wahakikishe huyo afande Jamila anakuwa ofisini kwake!
Baada ya kikao kile, maafande wale wakaanza kazi ya kumtafuta afande Jamila, baada ya afande Kubuta kumpigia simu ndugu wa marehemu Hamida na kutaka kufahamishwa umbile la huyo Jamila, na baada ya kama dakika 40 tu hivi mara moja wakawa wanachambuliwa maaskari wenye majina ya Jamila walioko katika Mkoa wa Kinondoni, na wakakosa mwenye sifa au wasifu unaomfanana huyo afande Jamila, alieelezwa na Neema, ndugu wa marehemu Hamida ambae alimuona!
Mara moja Kamanda wa Kanda Maalum akawasiliana na Makamanda wa Mikoa ya kipolisi ya Ilala na Temeke, ili wawasiliane na wakuu wa vituo katika sehemu zao za kazi, ili atambuliwe huyo Afande Jamila, ambaye wasifu wake umeelezwa kuwa ni mweusi wa chokoleti, mrefu wa wastani, mwenye umbo namba nane, ana hipsi kubwa na makalio yaliotokeza, miguu minene, meno meupe sana na lipsi nene katika midomo yake, na macho manene yanayoonekana muda wote kama yamerembuliwa mithili ya mwanamke aliyekula kungu manga! Na anapotabasamu hubonyea mashavuni!
Lakini pia majibu yaliyotoka kutoka Temeke na Ilala ni kama yale ya Kinondoni.
Hakuna afande mwenye jina la Jamila mwenye sifa hizo!
Sasa maafande wale walichanganyikiwa vibaya sana, kiasi wakahisi labda kuna mtu aliyejifanya ni askari akaenda kwa marehemu Hamida ili akaharibu ushahidi wowote uliopo!
“Sasa hii nini”, alijikuta akisema Kamanda wa Kanda Maalum!
“Kuna sehemu moja bado hatujaiangali.”
Alisema Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini, na wale askari wengine wakawa wamemtumbulia macho.
Yeye akaendelea. “Ni hapa Makao Makuu kwenyewe!”
Wote wakatamka, “Yes” na kazi ikaanza tena na mara moja Inspekta Jamila akapatikana kuwa ndiye mwenye sifa zilizotajwa.
Kamanda wa Kanda Maalum akawa anasoma namba ya simu ya Inspekta Jamila kutoka katika orodha ya majina iliyobandikwa ukutani pale makao makuu, Cheo chake na nambari yake ya kazi, alipoziweka kichwani akaenda hewani moja kwa moja akiwasiliana na Inspekta Jamila.
“Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya D’Salaam, popote ulipo kesho unahitajika ofisini kwangu saa moja na nusu asubuhi bila kukosa! Kumbuka hii ni amri, hivyo ufanye hivyo haraka iwezekanavyo”.
Baada ya kusema hayo kamanda wa kanda maalum akakata simu bila ya kutaka kusikiliza upande wa pili utajibu nini.
Bila shaka Inspekta Jamila alikuwa katika wakati mgumu sana. Hivyo akajikaza na kuahidi kwenda kusikiliza wito wa mkuu wake ili akajue mbichi na mbivu!
********
-
********
Saa moja na nusu juu ya alama, Inspekta Jamila alikuwa amekaa katika kochi akitazamana na Kamanda wa Kanda Maalum, huku akiwa katika ukakamavu mkubwa.
“Binti nimekuita hapa kwa mahojiano na wewe”. Alinza kwa kusema Kamanda wa Kanda Maalum, kisha akaendelea.
“Hivyo nataka kujua nani aliyekupa idhini yakufatilia kesi ya Marehemu Hamida inayomkabili yule Dereva wa Taxi Mwaduga Dingo?! Kwa nini umefanya upelelezi katika kesi mbayo uongozi wako umempa mtu aliyeonekana anafaa kufanya kazi hiyo! Na pia nataka kufahamu ulipofikia katika huo upelelezi wako!”
Kamanda Kanda Maalum alihoji maswali hayo huku akiwa amechukia vibaya sana. Kabla Inspekta Jamila hajajibu chochote akiwa bado anasubiri mkuu wake amalize ili yeye aanze kujitetea, simu ikawa inaita ya Kamanda wa Kanda Maalum.
“Nakusoma mkuu”, akaitikia Kamanda wa Kanda Maalum. “Ndiyo afande, sawa afande” Kamanda wa kanda maalum alikuwa anapokea maagizo kutoka kwa mkuu wake “IGP”.
Baada ya kumaliza kuongea na simu,Kamanda wa kanda maalum alimuangalia Inspekta Jamila na kumwambia.
“Okey sasa maelezo yako utakwenda kuyatoa mbele ya “IGP”, Ofisini kwake sasa hivi. Inuka twende ofisini kwake.”
wote wakainuka wakaelekea katika ofisi za “IGP”, zilizopo palepale katika jengo la Wizara ya Mambo ya ndani.
Kamanda wa Kanda Maalum aliingia ofisini kwa “IGP” akiwa na Inspekta Jamila.
Baada ya kumtolea heshima ya kijeshi, “IGP” aliwaelekeza kukaa vitini. Walipokwisha kuketi, Kamanda wa Kanda Maalum akaanza kwa kusema;
“Afande yule kijana ni huyu nilimwita ofisini kwangu asubuhi hii ili anipe maelezo ya kina kabla hujakutana naye, ili niweze kuyachekecha, lakini kwa ulivyoniamrisha uonane naye sasa hivi ndio nimemleta, huyu ndiye Inspekta Jamila”.
“Sawa Afande kazi nzuri, sasa niachie nimuhoji mimi mwenyewe, wewe kaendelee na kazi yako”.
Kamanda wa kanda maalum aliinuka na kupiga Saluti, kisha akatoka nje ya ofisi ile na kuelekea ofisini kwake.
Tofauti na Kamanda wa Kanda Maalum alivyokuwa mbogo kwa Inspekta Jamila, “IGP” alikuwa anaongea katika hali ya utulivu kama anayeongea na wakuu wenzake!
Hali ile ilimshangaza sana Inspekta Jamila kwani alitarajia kukutana na ukali, ukifatiwa na Amri nyingi kama sio kuwekwa lumande!
Basi hali ile ilimfanya awe mpole na mwenye kujiamini. Pia akishukuru kuongea na “IGP” moja kwa moja, ingawa angeweza kuhojiwa na Askari wa chini yake.
Lakini kitendo cha kumuhoji yeye mwenyewe, Inspekta Jamila alielewa ni ile picha ya “IGP” aliyokuwa nayo yeye wakati ule na si kitu kingine!
“Afande nataka kufahamu upelelezi wako umefikia wapi, umegundua vitu gani vyenye maana na bila shaka utanambia au kutaka kujua juu ya picha yangu uliyoichukua kutoka katika albam ya Marehemu Hamida.”
“IGP” aliongea kwa utulivu mkubwa huku akitambua anachokifanya!!!
Inspekta Jamila alikuwa ametulia kama kawaida yake, kisha akajibu.
“Afande kwanza sina budi kukushukuru kwa kuweza kunita na kukaa na wewe kama hivi, na tukawa tunazunguza, kwani ni nafasi adhimu sana! Lakini pia nilihitaji kupata nafasi kama hii kwa wakati huu ili nikupe taarifa ambazo yawezekana huna, au unazo juu juu si kwa undani”.
Kisha akaanza kumhadithia toka alipopewa jambo lile na mke wa Mwaduga, na namna alivyolishughulikia hadi kufikia muda ule! Alimwambia kila kitu alichokutana nacho katika upelelezi wake, ikiwemo picha yake “IGP”. Dereva Taxi aliemkodi kwenda nae Kimara suka, na taarifa za mahusiano ya kimapenzi kati yake na marehemu Hamida, bila kusahau taarifa ya ajali ya jirani wa Marehemu Hamida, Bwana Kiyarwenda Mwemezi kwa kina, pamoja na picha za wahalifu waliohusika katika ajali ya kutengenezwa, iliyogharimu maisha ya Bwana Kiyarwenda Mwemezi!
“IGP” alikuwa anamsikiliza Inspekta Jamila kwa makini na kushangaa ujasiri aliouonyesha kijana wake yule, lakini pia utendaji wake! Na kuona kuwa tayari ameshafahamu uhusiano wake na marehemu Hamida!
Waliweza kuongea kwa muda mrefu, hatimaye “IGP” aliamua kumkabidhi faili la kesi ya marehemu Hamida, na kumwambia.
“Upelelezi wako umejua mambo mengi sana kwa muda mfupi wa wiki moja tu, kiasi aliyekuwa akiiendesha kesi hii toka awali hakufika hata robo ya ulipofika wewe, ingawa yeye ana zaidi ya siku sitini!”
“Hivyo nitaongea na mwanasheria Mkuu ili kuliondosha suala la kijana Mwaduga Dingo Mahakamani ili awe huru, ili aweze kukusaidia kwa upelelezi wako kwa kuwatambua waalifu wale! Kwani akiwa nje atakuwa na imani na jeshi la polisi, pia atakuwa mkweli na muwazi kuliko akiwa mahabusu. Lakini pia kutokana na upelelezi wako, nami pia naungama ya kwamba yule kijana Mwaduga Dingo hana hatia!”
Mkuu wa jeshi la polisi, alikuwa mtulivu sana, akitawaliwa na hekima na busara, akiwa ameiweka mbali sana jazba.
“Hivyo hatuna muda wa kupoteza, picha hizo za sura za watu wawili alizokupa Dokta Zahala, utazipeleka kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai ili azifanyie kazi. Na suala hili kutoka sasa utakuwa ukiliripoti kwangu moja kwa moja!”
Inspekta Jamila alifurahi kupita kiasi, kwani kuweza kufanikisha yule dereva wa Taxi kuachiwa huru, kwake ulikuwa ni ushindi mkubwa. Lakini pia kupewa kazi rasmi na “IGP” na kuiripoti kazi hiyo moja kwa moja kwake pia ulikuwa ni ushindi mwingine.
Hivyo alimshukuru”IGP” na kumhakikishia kwamba ataifanya kazi hiyo kwa uaminifu na kwa utii.
Kisha Inspekta Jamila alitoa picha ya “IGP” aliyopiga na marehemu Hamida akamkabidhi “IGP”.
“IGP” akaipokea picha ile huku akitabasamu na kumwambia Inspekta Jamila.
“Nakuaminia askari wangu!”
Kisha wote wakatabasamu kwa pamoja. Na “IGP” akamalizia kwa kusema.
“Nakutakia kazi njema yenye mafanikio tele.” Kisha wakaagana.
Inspekta Jamila aliporudi ofisini kwake akiwa na furaha tele huku mkononi akiwa na faili la kesi ya Mwaduga, alimkuta Eshe Muhidini mke wa Mwaduga Dingo akiwa ameketi anamsubiri.
“Karibu mgeni upo muda mrefu?”
Inspekta Jamila alimkaribisha Eshe Muhidini na kumuuliza.
“Hapana afande nina kama dakika tatu toka kufika hapa.”
Eshe alijibu, kisha akaendelea, “leo ni Jumamosi nimekuja kukuona katika ile ahadi yetu ili nijue ulipofikia.”
“Ohoo! sawa nakumbuka kwani nilikwambia uje leo ili kwanza niwe nimefatilia ili nione nawezaje kukusaidia.
Na hapa nilipo nimepata namna ya kukusaidia, na haitachukua muda mrefu kutoka sasa mumeo utakuwa naye uraiani akiwa huru kabisa!”
Alijibu Inspekta Jamila kwa kujiamini. Jibu hilo lilimfanya Eshe atoe machozi ya furaha na kutoamini alichokuwa anakisikia.
“Afande umesema haitachukua muda mrefu mume wangu atatoka?!”
Aliuliza Eshe kwa fadhaa kama kwamba hakumsikia pale awali alipojibiwa.
Inspekta Jamila alipa jibu, kama lile la awali huku akiongeza neon.
“Sasa hivi tutakwenda wote gerezani tukamuone Mwaduga ili pia nizungumze naye suala hili, na vitu fulanifulani.”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media