BARUA KUTOKA JELA (8)

Zephiline F Ezekiel
0
Mtunzi: Ibrahim Gama

SEHEMU YA NANE
ILIPOISHIA...
Inspekta Jamila alipa jibu, kama lile la awali huku akiongeza neon.

“Sasa hivi tutakwenda wote gerezani tukamuone Mwaduga ili pia nizungumze naye suala hili, na vitu fulanifulani.”

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
Eshe alikuwa katika mshangao mkubwa sana, kwani aliona kama anaota ndoto za mchana. jambo kama lile ambalo hakutoa pesa hata senti tano ya hongo, kama baadhi ya watu wanavyodhani kwamba, huwezi kumaliza kesi bila kuwa na pesa! Sasa yeye hajatoa chochote kisha ndani ya wiki moja suala lile anaambiwa halina muda mrefu litakuwa limetatuliwa.

Jambo alilohenyeka nalo kwa zaidi ya miezi miwili!.

Eshe alimshukuru mwenyezi Mungu, Dokta Zahala na Inspekta Jamila kwa kuweza kumsaidia.

Aliinuka katika kiti alichokuwa amekaa na kwenda kumkumbatia Inspekta Jamila huku akilia kwa kwikwi na machozi yakilowanisha mashavu yake.

Inspekta Jamila alimtuliza na kumnyamazisha, kisha wakatoka wote wakitumia gari ya Inspekta Jamila wakaelekea Gereza la Keko.

*******

Siku ya Jumamosi jiji la Dar es Salaam huwa na foleni za magari sana, hivyo iliwachukua kama saa moja kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani hadi Gereza la Keko.

Baada ya kufika pale na kufanya taratibu za kiofisi, Mwaduga aliitwa katika chumba maalum akaweza kumuona mkewe na Inspekta Jamila, yule afande aliyemuhoji wiki moja iliyopita. Askari magereza aliekuwa amewasimamia ili kusikiliza mazungumzo yale ikiwa ni taratibu za kawaida za jeshi la Magereza.

Baada ya kumjulia hali, Inspekta Jamila akamwambia Mwaduga.

“Nipo hapa ili kukufahamisha jambo moja kuwa, huna muda mrefu kutoka sasa utakuwa raia huru. Jeshi la polisi limefanya uchunguzi wa kina na kuridhika kuwa huusiki kwa namna yoyote katika kesi zinazokukabili, hivyo jeshi nalo linataka ulisaidie katika mambo fulani fulani!”

Alisema Inspekta Jamila huku akimuona Mwaduga macho yamemtoka pima na kuacha kinywa wazi kwa mshangao, huku machozi yakimlengalenga machoni mwake.

Afande Jamila hakumpa nafasi Mwaduga ya kusema neno akaendelea.

“Kwa kuanzia, jeshi la polisi linataka ututajie wasifu wa wale jamaa watatu waliokodisha gari yako namna walivyo. Na je ikitokezea kuziona picha zao au wao wenyewe kwa mara nyingine tena utaweza kuwatambua?”

Inspekta Jamila alimwambia Mwaduga taarifa ile muhimu zaidi ya sana, na Mwaduga Dingo sasa akiwa na nguvu mwilini, mwake na matumaini mapya katika moyo wake alijibu.

“Afande nakushukuru sana, kwanza wewe binafsi kwa juhudi zako za kuweza kulifikisha hapa suala hili, na jeshi la polisi kwa ujumla. Pili kwa mke wangu Eshe kuweza kulifikisha kwako jambo hili! Yaani siamini naona kama nipo ndotoni, kwani kwa zaidi ya miezi miwili hivi sasa, mimi nimekuwa katika maisha mabovu. Hali ya kuwa sijawahi kukamatwa na kuwekwa kituo chochote cha polisi tangu nimezaliwa. wachilia mbali kuletwa gerezani kama mahabusu. Hivyo nimejifunza mambo mengi sana na sasa ninaamini kuwa si wote wanaofungwa jela kwamba wana hatia. Na ama hujafa hujaumbika! Kwani jambo hili haliwezi kusahaulika katika maisha yangu, hadi naingia kaburini.”

Mwaduga Dingo badala ya kujibu maswali aliyoulizwa, yeye alianza kutoa risala, yenye wingi wa shukurani.

“Nikiwa huku jela kama mahabusu nimeiweka nadhiri ya kwamba, ikiwa nitashinda kesi hii na kuachiwa huru, basi nitauandika mkasa huu uwe filamu. Ili wale wote waliodhani kuwa mimi ni jambazi na Jamii yote ya Tanzani kwa ujumla wapate somo kutokana na filamu hiyo. Lakini pia kuielimisha Jamii yetu ijue kwamba serikali ipo na inawajali raia zake.

Na pia watambue wapo maaskari wanaojali haki za raia na kuthamini ubinaadamu, ambao hawafanyi kazi kwa nguvu ya rushwa, kama wewe Inspekta Jamila!”

Alipofika hapa Mwaduga sasa akawa analia kwa sauti akiwa hawezi kuongea kwa vile donge la uchungu lilivyomkaa rohoni.

-

Inspekta Jamila na Eshe walimnyamazisha Mwaduga na Eshe akampa mkono wa pole mumewe huku akimpa moyo.

“Hakuna lenye mwanzo lisilokuwa na mwisho, lakini pia likiwapo la kuchukiza lipo na la kupendeza. Hivyo usilie sana, kwani tambua ya kwamba, Mbwa hafi maji akiuona ufukwe!”

Inspekta Jamila akafungua mkoba wake na kutoa picha nne alizokuwa nazo, akaziweka mbele ya macho ya Mwaduga Dingo na kumwambia!

“Je kuna yeyote katika picha hizi unayemfahamu?”

Zilikuwa ni zile picha ambazo mbili kati ya tatu alizozichukua nyumbani kwa Marehemu Hamida, na mbili ni zile picha alizopewa na Dokta Zahala.

Zile picha mbili alizochukua kwa marehemu Hamida, moja alishaifahamu ni ya Dr. Masawe. Zile nyingine bado hajazitambua.

Mwaduga akaziangalia picha zile, kwa umakini mkubwa kisha akasema.

“Hapa nimeitambua picha moja tu”

Mwaduga alisema maneno hayo huku akionyesha picha aliyoitambua.

Ilikuwa ni ile picha aliyoipata kwa marehemu Hamida iliyomuonyesha marehemu Hamida akinyweshwa kinywaji na kijana mmoja aliyeonekana mtanashati.

Mwaduga akasema “huyu jamaa anaitwa Bitozi ni muuzaji magari maarufu kule Kijitonyama. Hata gari nililokuwa ninaendesha, aliyekuwa tajiri yangu Bwana Shaame aliinunua kwenye Show Room yake.”

Inspekta Jamila aliandika neno Bitozi nyuma ya ile picha iliyotambuliwa.

Baada ya mahojiano ya hapa na pale kuhusu ofisi ya bwana Bitoz ilipo, Inspekta Jamila alipata taarifa za kutosha, na wakaagana na Mwaduga. Yeye na Eshe wakaondoka, wakimuacha yule askari Magereza na Mwaduga akiwa na matumaini tele.

*****

Siku ya Jumatatu Inspekta Jamila alikuwa amekaa ofisini kwake akifuatilia ripoti ya picha zile alizozipeleka kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, ili kuzifanyia kazi.

Picha zile za watu wawili moja kati ya picha zile ilitambuliwa!

Na ile picha nyingine haikuwepo kumbukubu yoyote ya sura ile katika ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.

Hivyo majibu ya picha zile yalikuwa kama ifuatavyo.

Picha ya mwanaume aliyevaa fulana nyeupe anatambulika kwa jina la Geradi Mwaipopo, kabila Mnyakyusa, aliwahi kuwa askari wa Jeshi la Polisi aliyekuwa na cheo cha Staf Sajent ambaye alifukuzwa kazi katika Jeshi la Polisi, baada ya kugundulika kufanya vitendo vya uhalifu katika kivuli cha Jeshi la Polisi.

Alipobainika aliachishwa kazi mara moja. Kiasi miaka miwili iliyopita! Wakati huo alikuwa anaishi Magomeni Mwembechai, Mtaa wa Mengo, Nyumba Namba 8. Hupendelea kutembelea Mikoa ya Mbeya, Songea, Tanga, Arusha,Pwani na Dar es Salaam. Kwa sasa haijulikani anaishi wapi wala anafanya nini. Ni mrefu wa futi 6 na inchi 3, rangi ya mwili wake ni nyeusi ya asili. ilimalizia ripoti ile. Na nyuma ya picha ile liliandikwa jina kamili la mwenye picha na kufuatiwa na maandishi “WANTED”.

Inspekta Jamila alitingisha kichwa kwa taarifa ile, kwani aliona askari anafukuzwa kazi hali ya kuwa ana ujuzi wa kutumia silaha, lakini pia mbinu mbali mbali za kijeshi halafu hajulikani anaishi wapi na anafanya nini, hii ni hatari kubwa kwa taifa letu.

Inspekta Jamila baada ya kuipitia ripoti ile kwa kina, akaiendea gari yake aina ya Toyota RAV 4 maarufu kwa jina la “Kitchen Party” yenye milango mitatu, akafungua mlango wa gari na kuingia ndani ya gari. Kisha akatoa simu na kumpigia Dokta Zahala akitaka kujua kama yuko kazini muda ule.

Alipopata jibu la ndiyo akamwambia.

“Nipo njiani nakuja Muhimbili ofisini kwako”

Inspekta Jamila akakata simu.

Baada ya dakika kumi Inspekta Jamila alifunga breki katika Hospitali ya Muhimbili nje ya jengo la ofisi ya Dokta Zahala.

Akatia lock milango ya gari yake, akahakikisha vioo vimefunga vyote, na kuelekea ofisini kwa Dokta Zahala.

“Dokta nashukuru kwa msaada wote ulionipa tangu unipe kazi hii! Ila sasa siifanyi kwa siri tena kwani sasa nimekabidhiwa faili rasmi kwa ajili ya kufuatilia kesi hii.”

Alisema Inspekta Jamila akimshukuru shoga yake wakiwa wawili katika ofisi ile na kuendelea.

“Hivyo basi sikuja hapa kwa ajili ya kukushukuru peke yake laa! Ila bado ninahitaji msaada wako mwingine.”

Inspekta Jamila alisema huku akimwangalia shoga yake ambaye alikuwa kimya muda wote akiwa anamtazama.

“Wee! Hongera shoga kwa kupewa rasmi kazi hiyo, sasa msaada upi huo unaouhitaji kutoka kwangu?”

Aliuliza Dokta Zahala.

“Nataka unifahamishe kwa Dokta Masawe ofisini kwake na hata nyumbani kwake ikibidi.”

Alijibu Inspekta Jamila.

“Ahaa sawa shoga, Dokta Masawe ni Daktari Bingwa, hapa huwa kazini siku za Jumanne na Alhamisi. Siku kama ya leo anapatikana katika Hospitali yake iliyopo maeneo ya Sinza Madukani. Karibu na Guest ya Namnani. Nyumbani kwake ni Kinondoni Mtaa wa Kasaba nyumba ya mwisho kwenye kona, kabla hujafika baa maarufu sana inayoitwa Patchoto.”

Inspekta Jamila aliposikia jina la Sinza, Karibu na Namnani moyo wake ukamlipuka na akaazimia kwenda muda ule ule kwa Dokta Masawe.

Akamshukuru shoga yake na akaagana naye,kisha akatoka nje ya ofisi ile akaielekea gari yake tayari kwa safari ya Sinza kwa Dokta Masawe.

Akiwa hatua kama tatu hivi, kutoka eneo alipoegesha gari yake, Inspekta Jamila aliona kitu kisicho cha kawaida katika gari yake!

Kwani alipoondoka pale katika eneo la maegesho ya magari, vioo vya gari yake vyote vilikuwa vimefungwa kama kawaida yake, ila wakati huu pale aliposimama, aliweza kuona kioo cha upande mmoja kipo nusu mlingoti!

Yaani kimefunguliwa nusu. Moyo wake ukaenda mbio akihisi kuwa ameshaibiwa na vibaka!

Akiwa mwenye hasira aliiendea gari yake, nakuanza kuikagua kwa nje kabla hajapanda. Lakini gari yake yote kule nje ilikuwa salama usalimini!

Akatazama Lock za milango, akaziona kama alivyozifunga ndivyo zilivyo kaa!

Alipofungua mlango ili aingie ndani ya gari, alipatwa na mshangao asioutegemea!

Bahasha ya khaki ilikuwa imewekwa ndani ya gari yake, katika kiti cha dereva.

Inspector Jamila aligeuka kushoto na kulia, ili kuangalia kama kuna mtu anaeshughulika nae, akaona kila mtu aliekuwa katika eneo lile, alikuwa yupo katika hamsini zake!

Akaingia ndani ya gari yake huku akiwa na tahadhari zote katika kichwa chake.

Aliichukua ile bahasha na kuiweka katika kiti cha pembeni na kuwasha gari, huku akikipandisha kile kioo na kutumia vioo vya pembeni vya gari yake, akawa anatazama kama kuna mtu yeyote anaeshughulika nae, kwa mara nyingine kukawa kupo shwari!

Aliiondosha gari kwa mwendo wa pole, akielekea Sinza kupitia Barabara ya Morogoro.

Alipofika Magomeni Mapipa, akaegesha gari yake katika kituo cha basi, kisha akaiangalia kwa mara nyingine ile bahasha, akaichukua na kuifungua.

Ndani ya bahasha ile kulikuwa na karatasi iliyoandikwa maneno yafuatayo;

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

 Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Shawishi Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)