HAA! KUMBE TAMU (1)

Zephiline F Ezekiel
0
Mtunzi: Frank Masai

SEHEMU YA KWANZA
ILIPOISHIA...
Hali fulani ya ubaridi ilikuwa inaendelea kuchukua nafasi kubwa kwenye Jiji lile la Mbeya,kwenye Wilaya moja inaitwa Chunya. Hali hiyo ya ubaridi ilisababisha kila mtu ajifungie chumbani kwake na kujivisha masweta mazito ya sufi.

Wale wageni waliotoka maeneo ya joto kama Dar es Salaam,walikuwa ndani ya sufi hilo na pia wakaongeza na blanket zito ambalo lilisababisha faraja iliyoletwa na joto mwilini mwao.

Wakati hayo yakiendelea humo ndani mida ya saa mbili za usiku, huku nje kulikuwa na kijana mmoja mwenye mwili kiasi, na mrefu kwenda juu huku akitanuka kifua chake kama wanyanyua vyuma au wacheza mpira wa kikapu.

Licha ya mikono yake kuvaa grovu za sufi, lakini bado alikuwa akiifikicha kwa pamoja kama mtu àpakaye mafuta au anatengeneza moto kwa kutumia Ulimbombo na Urindi.

Hakuishia hapo kwenye kuifikicha ili kupata joto litakalompa ahueni katika baridi ile kali, mara nyingine alikuwa ànaipuliza mikono na kuipumulia kwa mdomo wake ili kuipa joto na saa nyingine kuiingiza makwapani ili kuitafutia joto lililopo huko.

Macho yake hayakutulia. Kila mara yaliangalia upande wa kulia inapotokea njia ya mtaa wa pili,njia àmbayo ilikuwa haionekani vizuri kwa sababu ya ukungu uliotanda usiku ule.

Anaitwa Longino Mshama. Kipa hodari wa timu ya Chunya. Lakini usiku ule alikuwa na nia moja tu! Ya kukutana na mrembo aliyeutesa moyo wake kwa muda mrefu, mrembo ambaye anamfanya apigwe na baridi kila usiku wa mida kama ile.

Mrembo anayekwenda kwa jina la Subira Msafiri, mtoto wa tatu kati ya watoto watano wa Mzee Msafiri. Mzee ambaye anasifika kwa utajiri ng'ombe pale Chunya.

Mzee Msafiri alibahatika kupata watoto watano katika maisha yake ya ndoa. Mtoto wa kwanza ambaye alikuwa ni wa kiume,alishafariki miaka kumi iliyopita.

Mtoto wa pili ni wa kiume pia. Yeye ni mlanguaji wa bidhaa ambazo anazitoa Dar na Zanzibar na kuzileta pale Mbeya hasa Wilaya ile ya Chunya.

Wa tatu ndio huyu Subira ànayesubiriwa na Longino katika baridi kali la Mbeya. Wa nne na wa tano,hawa ni pacha. Kulwa akiwa mme na Doto akiwa mke,wote walikuwa wanamiaka mitano.

Baada ya Longino kusubiri sana,hatimaye alipata ahueni pale alipomuona fahari wa macho yake anatokea kwenye ukungu ambao ulikuwa unaendelea kutanda kwa wingi usiku ule.

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
"Nashukuru umekuja Subira."Longino aliongea kwa sauti nzito na ya chini huku akimwangalia kimwana yule mwenye rangi nadhifu ya chokleti,huku usoni akiwa kabeba uso mwembamba na macho ya duara pamoja na pua ndefu kiasi kama ya Kihindi.

"Nakusikiliza. Time inaenda si unajua home geti kali."Subira aliongea huku akionesha kweli hana muda mrefu wa kuendelea kuwa pale.

"Subira sina jipya zaidi ya kukuomba uwe mpenzi wangu. Embu nitazame jinsi navyoumia kwa baridi kwa ajili yako. Kwa nini hutaki kunielewa Subira?. Nifanye nini ili ukubali moyo wangu kuwa unakuhitaji? Naomba unielewe Subira,unanitesa mwenzako." Longino maneno yalimtoka huku uso wake kauweka katika masikitiko yasiyo na kifani.

"Umemaliza?."Ni swali la maudhi kwa kila mwanaume ambaye angeulizwa na mwanamke wakati anamtongoza, lakini kwa Longino lilikuwa kama pipi. Sijui kwa nini, labda kwa sababu mapenzi ni upofu ndio maana swali lile kwake halikumkera.

"Nakuomba uelewe hayo machache niliyoyaongea, nakupenda Subira."Longino alizidi kuonesha uhitaji wake mbele ya mwanadada yule gwiji la urembo pale Chunya licha ya kuwa ndio kwanza yupo kidato cha tano.

"Tayari umemaliza au unaendelea."Sauti ya kijasiri ilimtoka Subira huku mdomoni mwake akiwa anasindikizwa na bazoka na wakati huo mikono ilikuwa kiunoni na mguu mmoja aliutikisa kama anayesubiri mwanamke mwenzake amalize ili aanze yeye kumchamba.

"Ndio nimemaliza Suby."Sauti ya upole ilimtoka Longino lakini haikumfanya Subira asiseme alichokusudia.

“So, its my turn.” Subira aliongea Kiingereza huku bado yale manjonjo ya kutafuna jojo yakiendelea mdomoni kwake kama kocha mstaafu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson.

“Nadhani sina la nyongeza hadi hapo Suby. Waweza nipa msimamo wako.” Nafasi ya kuongea iliwekwa wazi na Longino na sasa mwanadada alikuwa tayari kumwaga vumbi la shombo.

"Nisikilize we kinyago cha mpapure.”Longino alilegea ghafla na kuwa kama samaki aliyechina baada ya kuitwa jina lile, lakini ulegevu ule haukufanya shombo zitokazo mdomoni mwa Subira kukwamia kooni.

“ Haya matawi anayaweza twiga, we sungura huyawezi. Tafuta saizi yako, hii saizi ni large huiwezi we small,itakupwaya bure. Na hata ukijaribu kunibana ili nikutoshe, utaambulia patupu kwani sitakuwa tayari kuharibiwa na wewe mfuga panzi." Subira alimtolea shombo Longino, kisha akageukia kule alipotokea kwa ajili ya kuondoka. Lakini kabla hajaondoka, alimgeukia Longino.

"By the way. Sivaagi mabati kama haya. Hizi levo za dhahabu au silva. Hayo mabati kawavishe darasa la tano, nikutakie baridi njema."Maneno yalimwendea Longino yakifuatiwa na kutupiwa cheni, hereni na bangiri alizozinunua juzi kabla ya siku hiyo.

Longino baada ya kutupiwa urembo ule wa kike kwenye uso wake,aliinama taratibu na kuokota vile vito vya shaba ambavyo Subira aliviita mabati.

Kuna vingine vidogo kama hereni, ilimpasa awashe kurunzi ya simu yake ili avione na kuviokota.

Hakika àlikuwa katika fadhaha kubwa hasa pale aliponyanyua macho yake na kumuona Subira akitokomea gizani huku ukungu ukiongeza ladha ya kutoonekana kwa mwanadada yule mwenye manjonjo mengi kama pishi la sikukuu.

Longino alikuwa karibu atokwe na chozi la mfadhahiko, lakini alivumilia huku akijiahidi moyoni mwake kutokata tamaa hata kama itachukua miaka mia kumpata kisura yule.

Aliviangalia tena vile vito alivyotupiwa na Subira,kisha alikumbuka jana yake baada ya kuvinunua siku moja liyopita.

Hela aliyotumia kununulia vito vile aliipata baada ya kutoka kambini ambapo timu yao ya mpira ilijichimbia. Siku ile ya Ijumaa, walipewa ruhusa ya kwenda kusalimia nyumbani kwao.

Kwa kutumia fedha kidogo ambazo alipewa na mfadhili wa timu ile ya Chunya, aliweza kununua vito vile kwa ajili ya mwanamke anayeutesa moyo wake, mwanamke ambaye badala ya kuuthamini upendo huo, anamwachia aibu ya moyo mwanaume.

Baada ya kupumzika Ijumaa ile yote, Jumamosi yake ndipo alimtafuta Mercy, rafiki wa karibu kabisa wa Subira.

Mercy hakuwa mbovu kisura wala hakuwa na nyodo kama za Subira. Mara nyingi alimsikitikia sana Longino kwa kumfatilia mtu ambaye alikuwa hana muda kabisa na yeye.

Uzuri wa Mercy, Longino hakuuona japo binti yule msomi wa kidato cha tano pia, alijitahidi kila kukicha ajipendezeshe mbele ya macho ya Longino.

Hakika Mercy alimchagua Longino, lakini angefanya nini na wakati dume lenyewe limekula yamini ya kuwa na Subira tu!?.

Swali hilo ndilo likawa kikwazo cha Mercy kumpata Longino.

*****

Mercy kusikia anaitwa na Longino, alifurahi sana hasa ukizingatia ni wiki mbili hajamuona mwanaume yule kutokana na kambi waliyokuwa wamewekewa.

Furaha ya Mercy ilihitimishwa na kuingia kisusunu pale alipopewa zawadi za kumpelekea rafiki yake kipenzi, Subira. Uso wa Mercy ulipoteza tabasamu lake halisi na kubaki tabasamu la kuchonga lililokaa ili lisipoteze maana katika kichwa cha Longino.

Alijua wazi Subira hatokuwa na shukrani kwa vile vichache ambavyo Longino aliacha kumnunulia mdogo wake kipenzi, Jesca.

Mdogo ambaye alipata ajali mbaya enzi za utoto wake, na àjali hiyo ikaaribu miguu ya mtoto yule hivyo kumfanya àwe anatembelea kiti tangu anaumri wa miaka mitano hadi sasa hivi anatimiza miaka kumi na moja.

Mercy alitimiza wajibu wake kwa kumpelekea vito vile vya shaba Subira. Na kama àlivyotegemea kuona na kusikia, Mercy wala hakuumiza kichwa juu ya tabia ya rafikiye.

Na hata pale msonyo wa kifedhuri ulipomtoka Subira baada ya kuambiwa Longino anamuhitaji kesho yake, Mercy hakuutilia maanani kwa kuwa tayari mjumbe alishafikisha ujumbe kwa muhusika.

****

Longino hata baridi hakuihisi baada ya maneno yale ya kashfa kutoka kwa Subira.

Alipohakikisha hajaacha kitu kati ya vile alivyotupiwa na Subira,alianza kujikongoja taratibu huku akili yake ikiwa kama imeganda kwa sababu ya maneno aliyoyasikia muda mchache uliopita.

Alipofika nyumbani alimkuta Jesca,mdogo wake akiwa anajisomea kitabu chenye hadithi ya My Rose, lakini lengo la Jesca kufanya hivyo, ilikuwa ni katika kuvuta muda ili kaka yake aje maana hakujisikia kulala bila kumuona kaka yake ambaye alitoka usiku ule.

"Huyoo karudi."Jesca alimkaribisha kaka yake kwa shangwe huku akinyoosha mikono ya kutaka kumbate dogo la kaka yake kipenzi.

"Oooh! Katoto kangu,mmwah."Kaka naye alijibu mapigo akiwa na furaha.

"Naona unasoma peke yako. Mama tayari àmelala?." Longino alimuuliza mdogo wake juu ya mzazi mmoja wanayeishi naye kutokana na ajali îliyomvunja miguu Jesca, kumpeleka kaburini baba yao.

"Mama kalala. Nataka na mimi unisomee hadi nilale."Jesca àlideka mbele ya kaka yake huku anampa kitabu alichokuwa akikisoma.

"Haya. Ila kabla sijasoma nataka kukupa zawadi,"

"Zawadi gani?."

"Fumba macho."Longino alimtaka mdogo wake afumbe macho naye akafanya hivyo,na hapo ndipo alipomvisha cheni ile ya shaba lakini yenye mvuto kwa kuiangalia.

Dogo alipofumbua macho,alijawa na furaha na kumkumbatia kwa nguvu kaka yake huku akitamka kwa hisia maneno "nakupenda kaka".

Longino alikabwa na donge la uchungu alipokumbuka alichofanyiwa na Subira na sasa mdogo wake anamuonesha thamani ya vile vito vilivyoitwa mabati na mshenzi mmoja.

Mshenzi ambaye hata ungekuwa wewe ungemuita mshenzi,lakini kwa Longino, aliona kawaida tu. Siku zote alijua hakuna marefu yasiyo ncha, hivyo muda wake ukifika, atampata tu yule mwanamke. Hakutaka kufikiria marefu hayo yasiyo na ncha yanaweza kutokea kwake pia, na ndicho ambacho alitakiwa kukifanya. Alitakiwa kuachana na mapenzi ya kujimbeleza na badala yake aangalie mwenye nia naye.

"Yaani huyu Subira wakunitupia hivi vitu na kuviita mabati?. Vitu ambavyo mdogo wangu anaviona kama dhahabu.

Huyu anajua nimevitoa wapi hivi? Anajua nimetoa shilingi ngapi ya kununulia hivi vitu? Anajua nimeacha kununua vingapi kwa ajili ya familia yangu?.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

  Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Zaidi Naomba Share App kwa Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)