TOROJO BAMIA (18)

Zephiline F Ezekiel
0

SEHEMU YA KUMI NA NANE
ILIPOISHIA...
Alipofika aliingia ndani na kujifungia chumbani kwake, akiwa na mawazo mengi, kwa kuiona aibu yake ya kukaa na MJ kama ndugu ipo nje.

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
Akili yake haikumfikiria MJ kutokana na maneno ya Lily kuonesha anamponda hata MJ.

***

Lily baada ya kupata uhakika kuwa Shuku kula kulala, pamoja na mbwembwe zote kumbe hakuwa tofauti na yeye. Wote walimtegemea mwanaume mmoja, aliamua kumpigia simu MJ. Baada ya simu ya MJ kuita ilipokelewa.

“Haloo.”

“Haloo MJ mai bebi.”

“Niambie Lily.”

“Ukweli nimeujua.”

“Kwa hiyo?”

“Sasa nimejikabizi kwako naomba usiniumize tu.”

“Nakuhakikishia wewe kuwa malkia wa moyo wangu.”

“Kama ni hivyo, nitafurahi sana.”

“Siku zote mtoto mzuri kama wewe unatakiwa umilikiwe na wanaume wenye fedha kama mimi.”

“Nimeamini, nitazidi kukupenda, kwa hiyo nije home kama kawaida?”

“Noo, bado Shuku ni rafiki yangu na sipendi nimuumize zaidi, ila nitakachikifanya kwa sasa tutakuwa tuna kutania hotelini. Baada ya muda mfupi nitakununulia jumba la kifahari hapo nitakuja kama kwangu.”

“Siyo kama kwako mpenzi, bali kwako.”

“Sawa nitakuwa nakuja kwangu.”

“Nitafurahi sana mpenzi wangu, vipi Shuku akijua?”

“Kwa sasa hawezi kujua.”

“Bebi penzi kikohozi na wanao pendana hawana siri.”

“Kwa sasa tutafanya siri, kuna fedha nitampa Shuku afanye biashara kisha kila mtu atakuwa na maisha yake, hapo hata akijua hawezi kufanya kitu.”

“Kwa hiyo leo?”

“Kwa furaha yangu, mwisho wa wiki tunaruka na ndege kwenda Arusha kula raha.”

“Wawooo mpenzi wangu, usinitie kichaa cha mapenzi.”

“Tulia mtoto mzuri ule raha, punguza mapepe.”

“MJ nitatulia kwako, naomba usinitese jamani.”

“Siwezi nakupenda sana Lily, nimeamua mpaka kuitoa siri ya rafiki yangu kipenzi kwa ajili yako, amini nakupenda.”

“Hayo ndiyo maneno, kipi kinafuata?”

“Jiandae usiku nakupitia, sasa na raha kwenda mbele.”

“Najua mpenzi wangu.”

Lily alikata simu na kuruka juu kwa furaha, alimkimbilia dada yake na kumkumbatia kwa furaha.

“Vipi mdogo wangu?”

“Yaani MJ kachanganyikiwa kusikia Shuku nimempiga chini, ameniahidi vitu vingi.”

“Isiniambie.”

“Yaani wiki ijayo Arushaaa.”

“Kufanya nini?”

“Kula maisha.”

“Unaona ulitaka kumng’angania mshika pembe kumbe mwenye ng’ombe yupo.”

“Yaani nina bahati Shuku aliisha niingiza choo cha kiume.”

“Ndo ukome kufakamia mijanaume mitapeli.”

“Basi dada akininunulia gari lingine hili nitakupa wewe.”

“Uniambie!”

“Kweli dada.”

“Mbona wavimba macho wa mtaani watanikomaa, hivi tu napewa lifti napiga mpaka honi, vipi nilimiliki yangu mwenyewe mbona wataniroga.”

“Basi habari ndiyo hiyo.”

Usiku MJ alimpitia Lily na kwenda naye kulala hoteli mpaka siku ya pili alipomrudisha.

*****

Penzi la Lily na MJ liliendelea kwa siri huku Shuku akiwa hajui nini kilichokuwa kikiendelea. Siku zote Lily alitaka penzi lao liwe la wazi ikiwezekana awe anakwenda pale muda wote kama alivyokuwa na Shuku.

“Bebi kwa nini nisije nyumbani mi’ sijisikii raha kila siku kulala hotelini wakati una nyumba yako?”

“Si unajua nipo na Shuku?”

“Kwa nini usimuhamishe ili nihamie hapo.”

“Nilikuwa napanga kumpa mtaji kisha tuachane.”

“Basi uza gari yangu umpe huo mtaji ili atuachie tule vyetu.”

“Nimekusikia wala usiwe na shaka kila kitu kitakwenda vizuri, fedha ya kumpa ninayo kuna vitu navikamilisha ili ahame kwa hiyari yake sitaki kumfukuza.”

“Wahi basi mpenzi nina hamu ya kuwa karibu na wewe muda wote.”

“Hakuna tatizo mpenzi.”

Wakati Lily na Mj wakifanya penzi la siri, Shuku kitendo kile kilimuumiza sana cha kumtegemea mtu na matokeo yake kudharaulika machoni mwa watu. Alichoamua kuomba fedha kwa rafiki yake ili aondoke pale na kwenda kutafuta maisha mbele ya safari ili watu wasijue maisha yake.

Akiwa amekaa na rafiki yake sebuleni Shuku alionekana mtu mwenye mawazo mengi na mnyonge toka amwagwe na Lily mwanamke aliyempenda kuliko wasichana wote aliowahi kukutana nao.

Kwa upande mwingine hakumlaumu Lily kwa vile hakumweleza ukweli. Aliamini kama akianza kuishi maisha ya kujitegemea ataweza kujipanga na kutafuta mwanamke mwingine.

“Vipi best mbona kama upo mbali?”

“Kweli.”

“Tatizo nini?”

“Aisee umaskini mbaya sana.”

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Nisingeadhiliwa na Lily.”

“Bado unalo hilo, achana na yule malaya inaonekana anapenda sana fedha kuliko mapenzi.”

“Hata kama anapenda pesa, inaonekana natembea bila nguo wakati najiona nimevaa.”

“Una maana gani kusema hivyo?”

“Japo unasema mali yetu lakini siri ipo wazi kuwa mimi mpambe tu mshika pembe mwenye ng’ombe unajulikana.”

“Shuku mshikaji wangu achana na maneno ya watu, ukiwasikiliza mambo yako yatasimama yao yanakwenda.”

“Ni kweli, lakini nakuomba kitu kimoja nipe mataji nifanye biashara ili nami niishi maisha yangu mwenyewe.”

“Wazo zuri, sasa umepanga kufanya biashara gani?”

“Nimeishajipanga, we nipatie hicho kiasi.”

“Kiasi gani?”

“Milioni mbili.”

“Mbona ndogo sana.”

“Kwangu zinanitosha.”

“Nitakuongezea nitakupa kumi na ile gari dogo.”

“Nitashukuru.”

Mara simu ya MJ iliita alipoangalia ilikuwa ya Lily ambaye alikuwa na miadi naye na kwenda kwenye sherehe ya harusi ya shoga yake alikuwa inafanyika Ubungo Plaza. Hakutaka kuipokelea pale alikwenda chumbani.

“Haloo bebi.”

“Bebi upo wapi nimeishafika kitambo,” Lily alilalamika upande wa pili.

“Ooh! Sorry nilikuwa na mazungumzo na Shuku.”

“Unaona sasa, nakwambia muondoe hapo atatuharibia starehe zetu.”

“Sawa bebi nitafanya hivyo muda si mrefu.”

“Kwa hiyo?”

“Nakuja mpenzi.”

“Fanya haraka kila mtu ana mpenzi wake kasoro mimi,” Lily alisema kwa sauti ya kudeka.

“Nakuja sasa hivi mpenzi wangu.”

MJ alikata simu na kukimbilia bafuni kuoga harakaharaka na kubadili nguo kisha alipiga bonge la suti la bei mbaya na kutoka kumwahi Lily.

“Sasa best kuna sehemu nakwenda, ila masuala yako kesho nitamaliza kila kitu.”

“Mmh! Kweli mtoko wa leo si wa kawaida, hakuna tatizo we wahi, mi sina nyendo.”

“Poa wacha niwahi,” MJ alisema huku akitoka nje na kuwacha Shuku amejilaza kwenye kochi.

****

Shuku akiwa amejipumzisha chumbani kwake akiutafuta usingizi simu yake ya mkononi iliita, namba ilikuwa ngeni, aliipokea.

“Haloo.”

“Haloo Shuku, mambo?” sauti ilikuwa ya kike.

“Poa.”

“Najua hunijui, lakini kunijua si muhimu kama hili lililonifanya nikupigie simu.”

“Jambo gani?”

“Nina imani upo nyumbani sasa hivi?”

“Ndiyo.”

“Mmeagana muda si mrefu na MJ?”

“Ndiyo, kwani wewe nani?”

“Tulia basi Shuku, pupa yako itakukosesha vitu vingi.”

“Haya nakusikiliza.”

“Najua umekosana na Lily, ila mpaka sasa hujamjua mchawi wako.”

“Ni kweli.”

“Shuku, Lily bado anakupenda sana ila penzi lako limewangiwa na mtu wako wa karibu.”

“Nani?”

“Sitaki kuwa muongo ila nakuomba sasa hivi uje uone jinsi ulivyo chezewa mchezo mbaya. Shuku sifa zako nazijua lakini najua nikikuchukua itakuwa vita na Lily.”

“Naomba uniambie jina lako basi.”

“Ipo siku nitakuambia lakini leo naomba ulifanyie hili.”

“Kwa hiyo nifanyeje?”

“Njoo Ubungo Plaza kuna sherehe ya harusi. Ukifika simama karibu na maegesho ya gari nijulishe kama umefika.”

“Poa nakuja.”

Shuku alikata simu na kubadili nguo haraka kisha alitoka. Hakutaka kukodi teksi aliona atachelewa alikodi bodaboda kuwahi eneo la tukio.

Shuku alichukua robo saa kufika Ubungo Plaza. Alipofika alimpigia simu aliyemwelekeza skendo ile, baada ya muda ilipokelewa.

“Haloo, umefika?”

“Ndiyo.”

“Sogea karibu ya paking ya magari.”

“Poa” Shuku alifanya kama alivyoelekezwa alipofika karibu ya maegesho ya gari alipiga tena simu.

“Nimefika.”

“Simama hapohapo usitoke mpaka nitakapo kwambia, hakikisha macho yako hayachezi mbali na mlango wa kutokea ukumbini.”

“Sawa.”

Shuku alitulia kama alivyoelezwa macho yake hayakucheza mbali na mlango wa kutokea ukumbini, huku akijiuliza kuna kitu gani. Kingine kilichomchanganya kilikuwa amefuata nini pale hata kama akimuona Lily na mwanaume mwingine, hakuna na nguvu tena kwa vile walikuwa wameisha tengana.

Lakini kauli ya aliyempigia kuwa afike pale amuone mchawi wake ndiyo iliyomfanya aendelee kuwepo. Muda nao ulikatika na kuzidi kumfanya Shuku atamani kuondoka. Aliamua kumpigia simu kumweleza amechoka kusubiri.

Baada simu kuita kwa muda ilipokelewa.

“Haloo Shuku.”

“Vipi mbona muda unakwenda, kama bado wacha niende.”

“Nooo Shuku, vumilia kama robo saa, kila kitu kitakuwa wazi mbele ya macho yako.”

“Mmh! Sawa.”

Shuku alitulia kusubiri alichoitiwa, baada ya muda simu yake iliita, alipokea.

“Haya sasa Shuku kazi kwako kazi yangu imeishia sasa angalia mlangoni.”

Shuku alitumbua macho mlangoni aone alichoitiwa.

Kwenye mlango wa kutokea aliwaona watu wawili mwanamke na mwanaume wakitoka wakiwa wamekumbatiana kimahaba. Alituliza macho kuwaangalia baada ya sekunde chache alimgundua yule mwanaume ni rafiki yake kipenzi MJ.

Lakini mwanamke hakumwelewa kwa vile alikuwa mbali vilevile kichwa cha mwanamke kilikuwa kimelalia kifuani kwa MJ. Waliposogea karibu hakuamini macho yake kumuona MJ akiwa na zilipendwa wake Lily wakionesha ni wapenzi wa muda mrefu.

Bila kujielewa alijikuta akisogea mbele mpaka alipowakaribia karibu na kuwashuhudia wakilishana mate bila kuhofia watu waliokuwa wakitoka ndani ya ukumbi.

“Mjuniii,” Shuku alipiga ukelele kwa kulitaja jina kamili ya rafiki yake.

MJ alishtuka na kujikuta akimsukuma Lily pembeni na kumfanya aanguke chini.

“Mjuni rafiki yangu unyama gani ulionifanyia. Wanawake wote ulionao hukuridhika umeamua kuninyang’anya mpenzi wangu, kwa vile tu una pesa?” Shuku alisema kwa sauti ya kilio.

“Sa..sa..mahani Shu..shu,” MJ alisema huku akimfuata rafiki yake alipokuwa amesimama. Lakini hakufika popote Lily alijizoa pale chini alipokuwa ameanguka na kumvaa MJ.

“MJ hebu rudi, achana na mpambe nuksi mtumai mali za rafiki kumbe hana lolote,” Lily alisema huku akimvutia MJ kwake.

“Hapana Lily hebu ngoja nizungumze na Shuku najua nimemkosea.”

“MJ achana na kapuku, anapenda kula nyama wakati hana meno hebu atupishe wenye meno wajilie nyama.”

“Lily mpenzi naomba unipe dakika moja nizungumze na Shuku.”

“MJ unanipenda mimi Shuku?”

Swali lilikuwa zito kwa MJ na kujikuta akiwa njia panda asijue afanye nini. Shuku bila kusubiri, alisema kwa sauti ya kawaida.

“Mjuni nashukuru sana kwa yote uliyonifanyia, sina sababu ya kukulaumu kwa ajili ya kitendo chako cha kunidhalilisha kwa Lily. Najua umaskini wangu ndiyo unaniponza, lakini siamini msichana uliyekuwa ukimwita malaya ndiye anayevunja urafiki wetu leo, asante,”

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

  Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Zaidi Naomba Share App kwa Wapenzi wa Simulizi Wapakue(Install) App ya CnZ Media

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)