
Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA NNE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Hiyo yote ni kutokana na kwamba marafiki zake walimuudhi kupita maelezo. Alitoka chuoni huku akiwa amekasirika sana. Alipanda daladala ambayo ilimpeleka hadi stendi ambapo alipanda gari lingine linaloelekea Sakina kwa Idd.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Saa 6.00 mchana alishuka kwenye gari na kuanza kutembea kuelea nyumbani.
************
Nelson alizidi kupoteza raha baada ya kumkosa Vivian alijiuliza au huwenda yule jamaa alimfananisha Vivian na msichana mwingine? Lakini kama ndiyo hivyo mbona hakumuona mwanamke mwingine ambae anafanana na Vivian? Alipata wazo la kurudi tena eneo lile kwa siku inayofuata kujaribu kama atafanikiwa kumuona. Siku iliyofuata alirudi kwa mara nyingine tena huku akisali kimoyomoyo kusudi Mungu amuwezeshe kukutana na mwanamke ambae alihisi kuwa furaha yake haitaweza kupatikana bila kumpata maishani mwake.
Saa sane mchana Nelson aliamua kutoka nyumbani kuelekea lile eneo ambalo alikutana na Mejooli. Aliamua kutoka mapema ili saa kumi imkute maeneo yale kwasababu ndio alielezwa muda ambao Vivian anapita mara kwa mara. Kwahiyo lisaa limoja kabla tayari alikuwa ameshafika. Alianza kusubiri huku akitazama huku na kule kama macho yake yatakutana na Vivian lakini aliambulia patupu. Muda ulizidi kusonga naa jioni ya saa kumi na mbili ilimkuta bado yupo maeneo yale. Kwa bahati nzuri Mejooli alitokea na kumkuta pale.
“Aisee vipi ndugu.” Nelson alimsalimia Mejooli.
“Safi kabisa. Umefaanikiwa kumpata mtu wako?” Mejooli aliitikia salamu na kuuliza swali papo hapo.
“Hapana kaka! tangu sikuzile sijafanikiwa kabisa kumpata. Halafu isitoshe leo tena tangu saa tisa nipo hapa lakini sijafanikiwa kukutana nae.”
“Daah! Kiukweli unabahati mbaya sana kwasababu leo hii karudi mapema mno, alipita mida ya saa sita. Sijajua ni kwanini leo kawahi hivyo wakati sio kawaida yake.” Mejooli alizungumza maneno ambayo yalimchoma sana Nelson kwasababu asubuhi alikuwa kwenye mgogoro wa nafsi kwamba awahi ama achelewe.
“Unauwakika lakini ndio yeye?” Nelson aliamua kuuliza kusudi asikute anapoteza muda wake halafu mtu mwenyewe asiwe yeye.
“Ndio nina uwakika kabisa ndiyo yeye. Kipindi cha nyuma alikuwa akipita hapa na sare za shule ya sekondari Ekenywa.” Maneno ya mejooli yalithibitisha kwamba ni kweli alikuwa namfahamu Vivian.
“Haswaa umepatia kabisa.”
“Nimemfahamia njia hii hii kwasababu kipindi cha nyumba nilikuwa ni fundi wa pikipiki maeneo haya kwahiyo nilikuwa namuona kila siku anapokuwa anaenda na kurudi shule. Maeneo haya wanaume wengi wanamfahamu sana kutokana na uzuri ambao amejaliwa ila ni binti mwenye maringo ya hali ya juu.” Maneno ya Mejooli yalimfurahisha sana Nelson. Aliamini kwamba tabia ya Vivian itakuwa haijabadilika.
Baada ya mazungumzo hayo waliagana. Nelson alirudi nyumbani akiwa amenuna kiasi kwa kutofanikiwa kukutana na Vivian, ingawa alipata faraja kidogo baada ya kupata uwakika kwamba binti aliekuwa anaelekezwa na Mejooli ndie aliekuwa anamtafuta. Hakukata tamaa kwani alipanga siku inayofuata kwanzia asubuhi hadi jioni atakwenda kuendelea kumtafuta Vivian hadi ampate.
***********
Kutokana na hasira aliyoipata Vivian pamoja na mawazo juu ya Nelson, alijihisi kuumwa kwasababu mwili wake ulikuwa na joto sana. Alipofika nyumbani alimeza panado kwajili ya kutuliza maumivu ya kichwa na baada ya hapo alipanda kitandani kupumzika. Hakuweza hata kula chakula kutokana na jinsi alivyokuwa anajihisi vibaya. Alilala kwanzia mchana hadi jioni. Hali yake ilizidi kuwa mbaya, joto lake la mwili aligundua sio la kawaida, akahisi pengine anaweza akawa na homa. Kwasababu ilikuwa tayari ni jioni alipanga kama kesho yaka ataamka katika hali hile ya kuumwa basi atakwenda hospitali kupima ili aweze kubaini tatizo.
Usiku hakufumba macho kabisa, alihisi anakila dalili ya malaria kwahiyo alipanga siku itakayofuata aende hospitali kupata matibabu. Palipokucha asubuhi hakuweza kwenda chuo kwahiyo alikwenda katika zahanati moja inayoitwa ‘Upendo dispensary’ iliyopo jirani kabisa na nyumbani kwao. Alifika na kupata matibabu ambapo vipimo vya daktari vilionyesha alikuwa na malaria na taifodi. Daktari alimsisitiza anywe maji mengi ambayo ni safi na salama, pia azingatie muda wa kumeza dawa. Baada ya hapo alirudi nyumbani kwaajili ya kuanza dozi ya vidonge vya ‘mseto’ ambavyo ndiyo alikuwa amepatiwa na daktari.
Alipofika nyumbani kwao alianza dozi haraka kwasababu hali yake ilikuwa sio nzuri kabisa. Mwili wake ulikosa nguvu, kwahiyo alikuwa ni mtu wa kulala tu kila mara. Hakuwa na hamu ya chakula wala kinywaji chochote. Ingawa mama yake alimkazania sana katika suala la chakula. Upweke aliokuwa akiupata kipindi anapokuwa nyumbani kwao ilimfanya ajihisi kuumwa zaidi na zaidi. Hakuna ndugu wala rafiki ambae alikuwa na ujasiri kwa kusogeza mguu wake pale nyumbani kwao. Kutokana na akili yake ilikuwa imepevuka vya kutosha alihisi moja kwa moja mama yake atakuwa sio mtu mzuri kabisa.
“Sasa kama mama atakuwa ni mchawi inamana ndiye atakuwa ameteketeza familia pamoja na wanandugu wengine? Kwasababu vifo vyote huwa vinatokea katika mazingira ya kutatanisha kiasi kwamba kila mtu huwa anajiuliza kuna kitu gani kwenye huu ukoo wetu. Hivi hata siku nikipata mchumba wa kunioa si lazima ataogopa kutokana na vifo vya kila mara huku nyumbani kwetu?” Vivian alitafakari kwa kina tetesi za kuwa mama yake ni mchawi huku akihusianisha matukio ya vifo vya mara kwa mara katika ukoo wao. Imani kwa mama yake ilipotea kabisa akahisi kwa namna moja au nyingine ni lazima mama yake atakuwa ni mchawi kama ambavyo watu wanasema. Mawazo yale yalimfanya aumie zaidi kwasababu hali yake kiafya haikuwa njema kabisa. Aliamua kupotezea baada ya mawazo ya mvulana anaempenda kumjia tena katika kichwa chake.
“Hivi itakuwaje endapo Nelson atakuwa amempata mchumba nje ya nchi?” aliwaza jinsi ambavyo ataumia endapo atasikia kuwa Nelson atakuwa amempata mchumba ambae ni msomi mwenzake.
***********
Nelson aliamka asubuhi na mapema. Alikuwa kapania siku ile ni lazima ahakikishe anampata Vivian kwahiyo aliondoka nyumbani asubuhi sana. Alinunua zawadi zingine nyingi ambazo aliona zitamfaa Vivian. Alivaa suti ambayo aliinunua siku alipokuwa anahudhuria tafrija fupi iliyokuwa imendaliwa na balozi wa Tanzania nchini Marekani kumpongeza kwa kufanya vizuri, baada ya hapo alijipulizia marashi yenye kunukia vizuri sana. Kwa hakika alionekana kupendeza kupita kiasi. Alijua moja kwa moja ile siku sio rahisi asimwone Vivian kwahiyo alionekana kuwa mchangamfu sana kutokana na furaha iliyokuwa ndani yake. Alijua kushindwa kuonana na Vivian kwa siku zile labda asipite maeneo yale kwasababu alikuwa amejipanga kufanya mawindo yake hadi jioni ya saa moja. Alianza kusubiri kwanzia saa moja asubuhi hadi saa moja jioni bila kuonana na Vivian jambo ambalo lilimuumiza sana. Alijihisi kuchoka na pia alikasirika sana kwasababu hakufanikiwa tena kwa siku zile halafu isitoshe alikuwa amenunua zawadi nyingi sana.
Alikata tamaa ya kuendelea kusubiri kwahiyo aliondoka kuelekea nyumbaani huku akiwa amevunjika moyo. Alifika nyumbani na kunyooka moja kwa moja hadi kitandani. Hakuwa na hamu ya chakula wala kinywaji. Alijiona kama mtu mwenye nuksi ya hali ya juu. Kibaya zaidi alikuwa ameshapigiwa simu ya kuhudhuria katika interview mbalimbali za kazi lakini hakuwa amehudhuria hata moja. Yote hayo ni kwasababu alitaka kuhakikisha kwamba anafanikiwa kukutana na Vivian. Aliona kwenda kwenye interview ya kazi wakati kichwani bado anamawazo kedekede juu ya mtu anaempenda, anaweza akafeli kwahiyo ndiyo maana alikuwa amejipanga kusudi aweze kufanikisha suala la Vivian kwanza ndiyo mambo mengine yafuate.
Kutokana na kwamba alikata tamaa, siku iliyofuata aliamua kuitikia wito wa kampuni moja inayomilikiwa na mama mmoja mwenye asili ya Asia. Kampuni hiyo inajulikana kwa jina la ‘Build Africa’ ipo ndani ya jiji la Arusha. Kampuni hii ilionyesha nia ya dhati ya kumuhitaji kwasababu ilimpigia simu kwa mara kadhaa baada ya Nelson kutuma maombi yake katika kampuni hiyo kwa njia ya barua pepe. Asubuhi na mapema alifika katika ofisi za kampuni ile iliyopo maeneo ya ‘france coner.’ Aliona ni bora achangamkie nafasi ile kwasababu yeye mwenyewe alitokea kuvutiwa sana na kampuni ile. Alifanya interview ya kazi akiwa na vijana wengine 13 ambao walikuwa wamesoma katika mataifa mbalimbali duniani. Jambo lile lilimpa changamoto kidogo Nelson kwasababu ushindani ulikuwa ni mkubwa sana.
Hakuwa na uwakika kama kweli atafanikiwa katika kinyang’anyiro kile cha ajira. Alimwomba Mungu afanikiwe kusudi aweze kumsaidia mama yake ambae alikuwa katika mazingira ambayo yalikuwa ni magumu sana. Pia alitamani kuwa na kwake kwasababu alikuwa tayari amesha kuwa mtu mzima, aliona sio busara kuendelea kuishi nyumbani kwa mjomba wake ili hali anaelimu ya kutosha na anawezo wa kupata kazi katika kampuni yeyote kutokana na uzuri wa vyeti vyake. Baada ya siku mbili matokeo ya interview yalitoka ambapo kati ya wale watu kumi na tatu Nelson ndie aliekuwa amebahatika kuchukuliwa na kampuni ile. Alifurahi sana, alimshukuru Mungu kwa kumuwezesha kupata nafasi ile. Alikwenda kusaini mkataba wa ajira kwa miaka mitano. Alipomweleza mama yake kwamba amepata kazi kiukweli mama yake alifurahi sana na kumtakia kila la heri. Alipewa siku mbili za kujianda ili aweze kuanza kazi.
Pamoja na kwamba habari za kupata kazi ilikuwa ni njema kwake lakini haikuwa sababu tosha ya kufanya tabasamu lidumu usoni mwake kwa muda mrefu. Alitamani furaha ya kupata kazi, afurahie na mwanamke anaempenda. Siku mbili alizopewa kwajili ya maandalizi ya kuanza kazi, alizitumia zote kuendelea kumsaka Vivian lakini hakufanikiwa. Nafsia yake ilizidi kuteseka usiku na mchana kwani furaha ya moyo wake haikupatikana kabisa. Muda wa kuripoti kazini ulifika na ndipo alianza kazi rasmi katika kampuni ya ‘Build Africa’. Alipokuwa kazini alijitahidi kujizuia kumuwaza Vivian ili ufanisi wake wa kazi usiyumbe lakini ilishindikana kwasababu Vivian alikuwa ni kama melodi ya nyimbo nzuri iliyokataa kutoka kwenye kichwa chake.
Mwezi mmoja ulikatika akiwa bado hajafanikiwa kukutana na Vivian ingawa kila mwisho wa wiki alikuwa akitembelea maeneo ambayo alihisi ataweza kukutana nae lakini hakufanikiwa. Alipata wazo kwamba endapo atabahatika kukutana na Mejooli basi ampe namba za simu kusudi siku kijana huyo akikutana na Vivian aweze kumpa mawasiliano yake.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi