SHEREHE KUZIMU (7)

Zephiline F Ezekiel
0
Mtunzi: Frank Silaa

SEHEMU YA SABA
ILIPOISHIA...
Walianza kula zile nyama na kila mmoja alionekana kuzifurahia. Hapakuwepo na mziki kama kwenye sherehe zingine bali Mama Vivian pamoja na watu wake waliburudisha watu kwa kuimba nyimbo mbalimbali kwa lugha ambayo haikuweza kufahamika kiurahisi.

KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA NAYO...
Matukio yote yaliyokuwa yakiendelea mbele ya macho ya Vivian yalitosha kuwa jibu tosha kuwa mama yake ni mchawi mkubwa.

Kilichozidi kumshangaza Vivian ni kwamba mambo yaliyokuwa yakiendelea katika ile sherehe yake hayakuwa ya kawaida kabisa lakini wageni waliyokuwa wamehudhuria walionekana kutokuwa na habari. Aligundua lazima kuna namna imefanywa kuwapumbaza wale wageni wake wasigundue ushetani uliokuwa ukifanyika katika sherehe ile. Mama Nelson alinyanyuka kwenye kiti na kwenda kucheza ile ngoma iliyokuwa ikichezwa kwa mitindo ya kutisha. Baada ya muda mfupi alifuata mjomba wa Nelson pamoja na wageni wengine. Mwishowe Nelson naye alitaka kuingia kati kucheza lakini Vivian alimzuia.

“No! I love the traditional songs, let me join them for a moment.” (Hapana! Napenda nyimbo za asili, ngoja niungane nao kwa muda kidogo.) Nelson alisikika akizungumza na Vivian huku akitaka kujitoa kwenye mkono wa Vivian uliokuwa umemkamata sawasawa ili asichomoke.

“No! no! no!” (hapana! Hapana! Hapana!) Vivian alimzuia kabisa mpenzi wake asiingie katika ngoma ile. Mama yake Nelson pamoja na mjomba wake walionekana kutokwa na jasho jingi kutokana na jinsi walivyokuwa wanacheza ngoma ile kwa mitindo ambayo ilikuwa inaogopesha.

Sherehe ilifikia ukingoni usiku mnene na ndipo Nelson na marafiki zake walirudi majumbani mwao. Chakushangaza ni kwamba hakuna mtu hata mmoja aliyekumbuka kupiga picha katika sherehe ile ya send off, kibaya zaidi hakuna mpiga picha yeyote aliekuwa amewekwa kwaajili ya kupiga picha katika sherehe ile, kwahiyo tukio lile lilipita kama upepo kwasababu hapakuwa na kumbukumbu zozote zilizohifadhiwa.

************

Kamati ya kuzimu ndio ilikuwa ikihudumia katika sherehe ile kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda sawa. Kuzimu ilifurahi baada ya wageni waalikwa wa sherehe ile kuweza kula na kunywa. Watu wote walioshiriki vyakula vilivyokuwa vimeandaliwa kwenye ile sherehe walikuwa wameshaingia maagano na kuzimu. Kwahiyo usiku wa siku hiyo walichukuliwa wote na kupelekwa kuzimu kwenda kutambulishwa. Mambo yote waliyokuwa wakiyaona yakiendelea kule kuzimu walijiona wapo ndotoni wanaota lakini haikuwa ndoto. Miale ya radi ilikuwa ikimulika mithili ya flash za kamera, milio ya bundi na paka ilisikika barabara. Kulikuwa na harufu kali ya damu na pia mkusanyiko mkubwa wa watu ambao walionekana kufurahia damu na nyama walizokuwa wanakula.

Hofu ilitambaa kifuani mwa Vivian. Alipotazama pembeni aligundua yupo na watu wote waliokuwepo kwenye sherehe yake. Walitembea kwa mwendo wa taratibu huku wakisindikizwa na ngoma walizokuwa wakizisikia zikichezwa kwenye sherehe. Alijitahidi kujizuia asitembee lakini alishindwa, alijaribu kupiga kelele kuomba msaada lakini sauti nayo ilikataa kabisa kutoka. Mbele yake alimuona mume wake mtarajiwa analia kwa huruma anaomba msamaha. Alitamani kumbembeleza mpenzi wake lakini sauti iliendelea kugoma kutoka. Mara baada ya kufikishwa kwenye kiti cha malkia walipokelewa na kicheko cha kutisha.

“Ahahahaha!” Ahahaha! Ahahahahaha.!” Kicheko cha kutisha kilisikika lakini hawakujua kilipokuwa kikitokea.

Vivian alipomtazama vizuri yule malkia wa kuzimu aligundua kuwa alikuwa ni mama yake mzazi. Moyo wake ulilia paa! Sherehe rasmi ya kuwakaribisha ilifanyika, ambapo walinyweshwa damu na kulishwa nyama kwa mara nyingine. Kuzimu kulitawaliwa na shwangwe kubwa kutokana na ule ugeni mkubwa. Pamoja na kwamba Vivian alikuwa mbishi sana kunywa damu na nyama za watu lakini alinyweshwa na kulishwa kwa nguvu. Baada ya hapo Vivian alishtuka usingizini na kujikuta akitokwa na jasho mwili mzima huku mdomoni mwake akiwa na mabaki ya damu ambayo iliyokuwa imemwagikia.

Alishtuka sana na kujiuliza inamana ile ilikuwa ni kweli ama ndoto? Aliamua kushuka kitandani na kwenda chumbani kwa mama yake kwenda kumweleza alichokuwa amekiota. Alipofika alimwamsha mama yake kwa kumwita na kumgusa ili aweze kuamka lakini hakuamka. Mapigo ya moyo ya mama yake yalionekana kudunda sawa kabisa lakini hakuamka. Vivian aliamua kurudi chumbani kwake kulala. Palipokucha asubuhi mama yake alimkataza kuamshwa wakati anapokuwa amelala, kwa madai kwamba hapendi usumbufu. Alipomweleza habari za ndoto ya usiku alionekana kupuuza. Vivian alinyanyua simu yake na kumpigia Nelson na kumweleza kwamba ameota ndoto mbaya sana. Wasiwasi ulimzidi Vivian baada ya kusikia Nelson akimweleza na yeye ameota ndoto kama ileile.

************

Siku moja kabla ya harusi wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi walifika Arusha kuhudhuria sherehe ya harusi ya rafiki yao Nelson. Walionekana kufurahishwa na mapokezi ambayo yalifanywa na kamati kabambe iliyokuwa ikiongozwa na mjomba wa Nelson. Kiukweli Nelson alifurahi sana baada ya kuona marafiki zake wamesitisha shughuli zao kwa muda na kuamua kujumuika nae katika siku yake ya harusi. Siku iliyofuata Nelson alizama ndani ya suti na Vivian ndani ya shela. Walipendeza sana, kila mtu alifurahia mwonekano wa bwana na bibi harusi. Tabasamu zilizokuwa zikichanua katika nyuso zao zilisababisha waonekane maridadi maradufu. Wapiga picha walionekana kuwaandama sana na kamera zao zilizokuwa zikitoa mwanga kila mara. Kanisa lilifurika kwasababu Nelson alikuwa ni mtu wa watu. Mchungaji Eugen Alvin ndie alieongoza misa takatifu ya Harusi ya Nelson na Vivian.

Nderemo na vifijo vilitawala katika nyumba ya Mungu baada ya Nelson na Vivian kumaliza kula kiapo cha ndoa. Ilikuwa ni siku ya kipekee sana katika maisha yao kwasababu walisubiriana kwa muda mrefu. Hadi misa ya harusi inakwisha, hakuna ndugu yeyote wa upande wa bibi harusi aliyekuwa amefika kanisani, hata mama yake hakuonekana. Baada ya harusi kufungwa msafara wa watumishi wa Mungu pamoja na ndugu jamaa na marafiki waliongozana hadi nyumbani kwa Nelson kwaajili ya kufanya uzinduzi wa nyumba yao ya kisasa. Uzinduzi ulikwenda sawa sawia na baada ya hapo watu waliongozana hadi ukumbini kwaajili ya kusheherekea tafrija fupi iliyokuwa imeandaliwa na bwana Nelson.

Msafara ulipofika ukumbini ndipo mama yake Vivian alifika akiwa ameongozana na mama mwingine wa makamo ingawa Vivian hakuweza kumfahamu. Kamati ilihakikisha kila mtu anakula na kunywa. Bwana na bibi harusi walizawadiwa zawadi nyingi kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki. Mama Vivian pamoja na mwenzie aliekuwa ameongozana nae walikabidhi zawadi ya pesa shilingi laki tano. Pamoja na zawadi hiyo aliyoitoa lakini alimnong’oneza mwanae na kumweleza kwamba kuna zawadi nyingine kubwa kamwandalia kwahiyo ipo siku atamkabidhi. Vivian alijiuliza ni zawadi gani hiyo mama yake alikuwa amemuandalia lakini hakupata jibu. Akilini aliijiuliza kwanini hakumkabidhi ile siku ya harusi, ambayo ndio ilikuwa maalumu kwaajili ya zawadi lakini napo aliishia kukosa jibu. Uchache wa watu waliohudhuria sharehe ya harusi kutoka kwa upande wa bibi harusi iliwashangaza watu wengi na hatimae kukaibuka minong’ono ya chini kwa chini. Watu walishindwa kuelewa ni kwanini mwitikio wao ulikuwa hafifu na pia kanisani hawakuonekana hata mmoja.

Jambo hilo lilimuumiza pia Nelson kwasababu alipata aibu kubwa mbele ya marafiki zake. Viti vilivyokuwa vimeandaliwa kwaajili ya watu watakaotoka ukweni vilikuwa wazi kabisa.Vivian alikuwa akilia ndani kwa ndani, alijilazimisha kutabasamu lakini hakuwa na raha hata kidogo. Alijua kabisa ilikuwa ni picha mbaya sana iliyokuwa inaonekana kwa Nelson mbele ya marafiki zake wengi waliokuwa ukumbini.

“Marafiki zangu watahisi pengine labda ndugu wa binti hawajaridhia mimi kumuoa vivian.” Nelson aliwaza, lakini alihishia kupuuzia.

Ratiba ya sherehe ilifika kwenye burudani ambapo mziki mzuri ulikuwa ukitumbuiza ukumbini. Marafiki wa Nelson kutoka nje ya nchi walikwenda kwa pamoja kwenye meza kuu kumpongeza rafiki yao kwa tukio la kipekee alilokuwa amelifanya katika maisha yake. Walipanga mstari na kupita kila mmoja kumpongeza Nelson. Alifurahi sana kuona marafiki zake wakimpongeza. Alisalimiana na kila mmoja lakini furaha yake ililipuka zaidi alipomuona rafiki yake anayeitwa Jacinthe Abroise ambae ni mzaliwa wa Nord-pas-de-calais Ufaransa lakini kwa sasa anaishi Florida nchini marekani. Nelson alipokuwa chuo kikuu cha Central Florida nchini Marekani aliamua kujifunza kozi ya lugha ya kifaransa. Rafiki huyu mfaransa alijitolea kwa dhati kumsaidia Nelson kuweza kuifahamu lugha hiyo kwa ufasaha. Kwa furaha walikumbatiana.

“Fèlicitations pour èntre arrive sain et sauf.” (Hongera kwa kufika salama.) Nelson alizungumza na mwanadada mrembo Jacinthe kwa lugha ya kifaransa wakati alipokuwa amemkumbatia.

“Je vous remercie.” (Asante.) Jacinthe alijibu.

“Felicitations pour votre marriage.” (hongera kwa kufunga harusi.) Jacinthe alimpongeza Nelson.

“Merci beaucoup, Jacinthe.” (asante sana, Jacinthe.) Nelson alisikika.

“Je vous souhaite tout le Bonheur possible.” (nawatakia wote furaha) Jacinthe alimtakia Nelson baraka katika ndoa yao.

“Bienvenenue.” (Karibu.) Nelson alizungumza na kumuacha Jacinthe akapita halafu akaendelea kusalimiana na marafiki zake wengine waliokuwa wakipita mmoja mmoja kwenye meza ya Nelson iliyokuwa mbele ya ukumbi.

Ilipofika usiku wa saa nne kamili sherehe ilifikia tamati. Nelson aliwashukuru watu wote waliokuwa wamehudhuria sherehe yake ya harusi. Aliagana na watu wote waliokuwa wamefika pale ukumbini, kila mmoja alianza kutawanyika kuondoka kuelekea majumbani kwao. Wageni wote walifikishwa hotelini kwa usafiri ambao ulikuwa umeandaliwa na kamati ya harusi. Nelson alipanda kwenye gari maalumu lililokuwa linawaendesha kwa siku hiyo na kuelekea nyumbani kwake. Hakutaka kabisa kusikia habari za fungate kwenye hoteli za kifahari aliona ni upotezaji wa pesa.

Alipanga fungate yake na mke wake wakafurahie katika nyumba yao mpya. Walifika nyumbani kwao salama na kufunguliwa geti na mlinzi ambae alikuwa ameanza kazi rasmi siku hiyo. Mioyo ya bwana na bibi harusi ilikuwa na furaha sana. Kila mmoja alikuwa anatamani wafike nyumbani ili waweze kujuana kwasababu hakuna hata mmoja aliekuwa amewahi kumjua mwenzie. Kwa ufupi Vivian hakuwahi kulala na mwanaume tangu kuzaliwa kwake na Nelson vilevile hakuwahi kulala na mwanamke.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)