
Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA NANE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Kila mmoja alikuwa anatamani wafike nyumbani ili waweze kujuana kwasababu hakuna hata mmoja aliekuwa amewahi kumjua mwenzie. Kwa ufupi Vivian hakuwahi kulala na mwanaume tangu kuzaliwa kwake na Nelson vilevile hakuwahi kulala na mwanamke.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Kiukweli walikuwa wamefunga ndoa takatifu iliyokuwa na baraka mbele za Mungu.
Baada ya kufika nyumbani wadhamini wa ndoa pamoja na watu waliokuwa wamewasindikiza waliondoka na kumwacha Nelson na mke wake. Nelson alifurahi sana alipomkuta Vivian ni msichana ambae hakuwahi kuguswa hata siku moja. Pamoja na kwamba aliwahi kumdokeza kwamba hakuwahi kulala na mwanaume tangu kuzaliwa kwake lakini Nelson aliona ni kama utani, kwa kuwaza inawezekana vipi binti mrembo namna ile akaweza kushinda changamoto za wanaume wanaodondosha mate kwaajili yake. Moyo wa Nelson aliongeza mapenzi zaidi na zaidi, kwani alimuona ni mwanamke mwenye mapenzi ya dhati na pia mwenye msimamo wa hali ya juu. Maisha yao ya ndoa yalianza kwa furaha sana kwasababu ya upendo wa dhati uliokuwa umejengeka mioyoni mwao. Masiku kadhaa baadae Vivian alibainika kuwa na ujauzito baada ya kwenda hospitali kucheki afya yake kutokana na mabadiliko aliyokuwa ameyahisi mwilini mwake.
Furaha iliongezeka zaidi na zaidi kwasababu lilikuwa ni jambo jema sana kwao. Nelson alikuwa na shauku kubwa sana ya kuitwa baba halikadhalika Vivian nae alitamani kuitwa mama. Hivyo basi kiumbe kilichokuwa tumboni kilisubiriwa kwa hamu kubwa. Nelson alihakikisha mke wake anapata lishe bora kusudi mtoto atakaezaliwa awe na afya nzuri. Mimba ilizidi kukua vema huku Vivian akiendelea kuhudhuria kliniki mara kwa mara. Maisha yao yalizidi kuwa ya furaha kila kukicha changamoto pekee waliyokuwa wanakumbana nayo ni ndoto mbaya walizokuwa wakiota mara kwa mara. Kibaya zaidi walikuwa wanaota ndoto zinazofanana, jambo ambalo liliwakosesha raha kwa wakati mwingine.
Miezi tisa ilitimia ambapo Vivian alijifungua salama mtoto wa kiume. Nelson na mke wake walifurahi sana kumpata mtoto wa kiume. Ndugu jamaa na marafiki walifurahi pia baada ya kusikia zile habari njema. Walimpigia simu na wengine walidiriki kufika nyumbani kwao kuwapongeza. Sura ya mtoto ilifanana sana baba yake ingawa rangi ya ngozi yake ilifanana na ya mama yake. Kiukweli mtoto aliyezaliwa alikuwa ni mzuri sana na hilo lilithibitishwa na watu mbalimbali waliofanikiwa kumuona mtoto. Ilikuwa ni habari njema pia kwa mama Nelson kwasababu alikuwa ndie mjukuu wake wa kwanza. Mtoto alipewa jina la ‘Alaire’ jina ambalo chimbuko lake ni Ufaransa na lina maana ya furaha. Nelson na mke wake walikubaliana kumwita mwanao jina hilo kwasababu mtoto yule alikuwa ni furaha halisi mioyoni mwao.
Jina hilo liliwavutia pia watu wengi waliolisikia. Mtoto alipofikisha miezi mitatu, wanandugu pamoja na marafiki wa karibu walijumuika pamoja katika sherehe iliyokuwa imeandaliwa kwaajili ya ubatizo wa mtoto ambapo alipewa rasmi jina hilo la Alaire. Maisha ya wanandoa Nelson na Vivian yaliendelea kuwa ya furaha siku hadi siku. Upendo ulikuwa ndio nguzo yao. Vivian alimpenda sana mume wake, kila siku alikuwa akimuombea Mungu amfanyie wepesi katika shughuli zake. Nelson alipoumwa na yeye aljihisi kuumwa kutoka na upendo wa dhati aliokuwa nao kwa mume wake. Alimpenda mume wake kuliko kitu chochote. Kwa upendo aliokuwa nao kwa mume wake alikuwa tayari kuhatarisha maisha yake kutetea uhai wake.
Vivian aliona furaha yake haitaweza kupatikana kwingine isipokuwa kwa mume wake ambae alidiriki kumsubiri kwa muda mrefu. Alikubali kuchekwa na kudharauliwa na marafiki zake kwaajili ya msimamo wake juu ya Nelson na aliapa kumpenda hadi mwisho wa maisha yake. Vivian alimuona Nelson mpya kila siku kutoka na ufundi wa mapenzi aliokuwa anaushuhudia kwa mume wake kila kukicha. Kiukweli wanandoa hawa walikuwa wakipendana sana. Upendo wao uliwavutia hata wale ambao walikuwa hawajaingia katika majukumu ya ndoa. Siku zilizidi kusonga huku furaha ikizidi kuongezeka mioyoni mwao. Alaire alipofikisha miaka mitatu alipata mdogo wake ambae nae alikuwa wa kiume. Walimpa jina la ‘Mainard’ lenye maana ya ‘imara na thabiti.’
Mambo yalizidi kuwa mazuri katika familia ya Nelson kwasababu uchumi wa familia yao nao ulihimarika zaidi. Kiukweli baraka zilimiminika kwa kasi katika ndoa yao. Watoto waliendelea kukua kwa afya njema jambo ambalo lilizidisha furaha katika ndoa yao. Nelson na mke wake walipanga kuzaa watoto watatu tu katika ndoa yao. Waliona idadi hiyo ndiyo wataweza kuimudu katika kuwapatia lishe bora, malezi pamoja na elimu bora. Kwahiyo Vivian alikuwa anasubiri kuzaa mtoto mmoja afikie ukomo wa kuzaa. Mainard alipofikisha miaka mitatu alipata mdogo wake ambae nae alikuwa ni wa kiume.
Nelson na mke wake walijaliwa sana watoto wa kiume. Mtoto wa tatu walimpa jina la Benedict ambalo maana yake ni aliyebarikiwa. Nelson alipendelea kuwapa watoto wake majina ambayo anafahamu maana yake. Nelson aliwapenda sana watoto wake. Alaire pamoja na Mainard waliandikishwa shule moja inayojulikana kwa jina la St Lucas’s academy nusery and primary school iliyopo ngulelo Arusha. Kitinda mimba alipofikisha umri wa shule alipelekwa shule nyingine iliyopo kisongo inayojulikana kwa jina St Margaret’s academy nusery and primary school. Wote walikuwa wanapelekwa na kurudishwa nyumbani kwa usafiri uliokuwa unatolewa shuleni. Alaire alionekana kuwa na akili kama baba yake kwani katika mtihani wa kumaliza darasa la saba alikuwa kwenye kumi bora ya kitaifa. Ingawa hata Mainard pia alionekana kuwa vizuri pia darasani lakini hakufikia uwezo wa kaka yake.
Vivian hakuajiriwa katika hoteli yeyote, ingawa alikuwa na diploma ya ‘hotel management’. Muda wake mwingi aliutumia katika kusimamia biashara kadhaa za mume wake, ikiwamo duka kubwa la nguo za aina zote kwa wanaume na wanawake lililokuwepo katikati ya jiji la Arusha. Siku moja wakati alipokuwa dukani kwake akiendelea na majukumu yake, alipokea simu kutoka kwa mama yake. Mama yake alimweleza kwamba siku inayofuata asubuhi na mapema anamwitaji nyumbani kuna jambo la muhimu sana anahitaji kumweleza. Vivian alijaribu kuwaza jambo ambalo mama yake alikuwa anamwitia lakini hakupata jibu. Ila alihisi pengine labda ni kwasababu mama yake kammisi kutokana na kwamba hajaonana nae kwa miaka kadhaa. Ukweli ni kwamba Vivian alikuwa akipendwa sana na mama yake na yeye alikuwa anafahamu hilo kwasababu amelelewa kama mayai.
Nafsi yake ilitawaliwa na wasiwasi mwingi kwasababu alikuwa ameshahisi kwamba mama yake ni mchawi. Aliporudi nyumban kwake mida ya jioni alimweleza mume wake kwamba ameitwa na mama yake siku inayofuata. Nelson hakuwa na kigugumizi juu ya suala hilo alimruhusu na pia alimpa salamu zake. Palipokucha siku yenyewe Vivian aliwasha gari lake aina ya Toyota RV4 na kwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwao. Alipofika alipokelewa vizuri sana na mama yake. Mama yake alimuonyesha ukarimu wa hali ya juu hadi mwenyewe akashangaa. Baada ya Vivian kupata kifungua kinywa cha maana, mama yake alimshika mkono kumnyanyua pale sebuleni walipokuwa wamekaa na kwenda chumbani. Vivian alizidi kuduwaa maongezi ya chumbani na mama yake ni maongezi gani hayo. Walipofika chumbani walikaa kitandani na maongezi yao yalianza.
“Vivian wewe ni mwanangu wa pekee niliebakiwa nae. Baba yako pamoja na ndugu zako tayari wameshakufa, ila pamoja na hayo yote uwepo wako unanifanya nisihisi hata chembe ya upweke moyoni mwangu kwasababu wewe ndio furaha yangu, hakika nakupenda sana mwanangu.” Vivian aliporomoshewa sifa na mama yake wakati walipokuwa wakizungumza chumbani kwa sauti ya chini kabisa.
“Nakupenda pia mama.”
“Unamkumbuka bibi yako Devota?” mama aliuliza.
“Ndio, namkumbuka.”
“Alipofikisha umri kama wa kwangu kunazawadi alinikabidhi. Alinieleza kwamba na mimi nitakapofikisha umri kama wake nikukabidhi na wewe mwanangu kwasabaabu alikuona unafaa kuendea kurithi mikoba yake. Na ile siku ya harusi yako nilikuahidi kwamba kuna zawadi nitakupatia. Unakumbuka hilo?” Mama Vivian alizungumza maneno mengi na mwishowe alimaliza kwa kumuuliza Vivian swali.
“Ndio nakumbuka.”
“Vizuri sana! zawadi yenyewe ni hii hapa naomba uipokee kwa mikono yako miwili.” Mama Vivian alizungumza huku akimkabidhi mwanae kibuyu ambacho kilikuwa kimezungukwa na hirizi nyingi zinazoning’inia.
Vivian aligoma kupokea na kuhitaji maelezo zaidi. “Kibuyu cha nini? Cha kazi gani?”
“Mwanangu huu ni uchawi ambao bibi yako alinikabidhi, lakini kabla hajapoteza maisha alinihusia kwamba nikupe wewe kwasababu ndio alikuchagua katika wajukuu zake wote.” Mama Vivian alizungumza huku akimtazama Vivian ambae alionekana kupoteza nguvu kutokana na maelezo ambayo alipatiwa na mama yake.
“Hapana mama sipo tayari kabisa kuingia katika mambo ya kichawi.” Vivian alizungumza huku machozi yakimlengalenga.
“Usijali mwanangu, hata mimi nilipokuwa nikikabidhiwa na bibi yako nilionyesha hali kama yako ya kukataa, lakini baada ya kukubali sikuwahi kujutia hata siku moja.”
“Kama nikikataa nitadhurika wacha tu nidhurike lakini sipo tayari kuingia katika mambo hayo kabisa.” Vivian aliendelea kumuonyesha mama yake msimamo wake.
Mama aliendelea kumbembeleza Vivian, lakini aligoma kata kata. Mama alidiriki hadi kumpigia mwanae magoti akubali lakini bado binti aliendelea kuonyesha msimamo wake. Vivian alibembelezwa kwa takribani masaa matatu lakini aligoma kabisa. Mwishowe mama yake alitamka maneno ambayo yalikuwa mazito kidogo lakini Vivian bado hakuonyesha kuogopa.
“We si unajifanya mjanja, sasa kitakacho kukuta ni kwamba utazika watoto wako wote pamoja na mume wako baada ya hapo wewe utachizika.” Mama Vivian alizungumza maneno hayo baada ya hapo alimalizia kwa kicheko cha kutisha. “Ahahaha! Ahahaha!”
Vivian alinyanyuka kwa hasira na kwenda kwenye gari lake na kuondoka. Maneno aliyoelezwa na mama yake yalimfanya ashindwe kujizuia kulia kwahiyo alilia tangu mwanzo wa safari yake hadi alipofika nyumbani kwake. Hakwenda kazini tena kwasababu aliona hataweza kwenda kufanya kazi kwa jinsi alivyokuwa amekasirishwa na mama yake. Alilia sana pamoja na kujuta kwanini alizaliwa. Alijiuliza atakuwa mtu wa namna gani endapo atajiingiza katika mambo ya kichawi, jamii itamchukuliaje, na pia mahusiano yake na Mungu yatakuwaje. Aliwaza sana Vivian huku akilia kwa uchungu sana. Siku nzima alijifungia chumbani mwake akilia sana kutokana na yale aliyoelezwa na mama yake.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi