
Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA TISA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Alilia sana pamoja na kujuta kwanini alizaliwa. Alijiuliza atakuwa mtu wa namna gani endapo atajiingiza katika mambo ya kichawi, jamii itamchukuliaje, na pia mahusiano yake na Mungu yatakuwaje. Aliwaza sana Vivian huku akilia kwa uchungu sana. Siku nzima alijifungia chumbani mwake akilia sana kutokana na yale aliyoelezwa na mama yake.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
“Hivi mume wangu akifahamu kwamba mimi nimchawi itakuwaje? No I can’t (hapana siwezi)” Vivian aliwaza huku akiendelea kulia kwa uchungu hadi mume wake aliporudi jioni akitokea kazini.
Nelson aligundua kuwa mke wake hakuwa sawa kwasababu macho yake yalikuwa mekundu halafu yamevimba kutokana na kulia sana. Alipojaribu kumuuliza kulikoni hayupo sawa alimdanganya kuwa amepata taharifa za msiba wa rafiki yake ambae walisoma nae chuo. Nelson alisikitika sana na kumpa pole mke wake na kumsihi anyamaze kwasababu kazi ya Mola haina makosa. Vivian alikataa kabisa kumshirikisha mume wake katika suala lile alilokuwa ameelezwa na mama yake kwa kuhofia kuwa upendo wa Nelson kwake unaweza ukapungua au hata wakaachana.
Vivian alizidi kuumia ndani kwa ndani. Alihisi kuchanganyikiwa pale alipokuwa akikumbuka alichoelezwa na mama yake baada ya kukataa kupokea uchawi. Lakini aliendelea kuona afadhali iwe hivyo kuliko kukubali kujiingiza katika mambo ambayo yatakuwa chukizo kwa Bwana Mungu wake. Waliendela kuota ndoto mbaya kila mara. Hakuna hata mmoja wao aliyekumbuka kumshirikisha mtumishi wa Mungu kuhusu njozi mbaya walizokuwa wakiziota kila mara. Nyumbani kwa Nelson kulikuwa na vitabu vingi sana vya hadithi na mambo mengine mengi. Biblia na vitabu vingine vilikuwepo pia kwenye listi ya vitabu vilivyopo nyumbani kwao. Nelson alikuwa ni mpenzi sana wa kusoma vitabu.
Hakuna siku hata moja inapita bila Nelson kushika kitabu cha hadithi mkononi mwake. Tabia hiyo alimuambukiza hadi mke wake nae akatokea kupenda kusoma vitabu. Magari yao yalikuwa yamejaa vitabu mbalimbali ambavyo huwa wanatembea navyo kuvisoma wawapo safarini, na pia vingine huwa wananunua wanapokuwa barabarani. Watoto nao walivutiwa na tabia ya wazazi wao kusoma vitabu kila mara kwahiyo na wao walijijengea tabia ya kujisomea vitabu vinavyozungumzia mambo mbalimbali hususani hadithi. Wakati mwingine Nelson alihisi kuwa wanaota ndoto mbaya kwasababu huwa wanasoma vitabu vya hadithi za kutisha sana ndio maana.
Ingawa Vivian tayari alikuwa ameshajua tatizo lipo wapi lakini alikuwa anaogopa kumshirikisha mume wake. Pamoja na sifa nzuri ya kujisomea vitabu kwa wanandoa hawa lakini walijisahau sana kwasababu hakuna hata mmoja wao aliekumbuka kunyanyua Biblia takatifu na kuisoma. Vitabu vya Mungu walivifunua siku mojamoja walipokuwa wakienda kanisani na baada ya hapo wanavirudisha kwenye kabati la vitabu hadi siku nyingine ya ibada ifike. Hawakuwa na tabia ya kusali kabisa wakati wa kulala wala kuamka na hata wakati wa kula hawakuwa na utaratibu wa kumshirikisha Mungu.
Watoto nao walifuata nyayo zao, hawakuwa na msingi mzuri wa imani ndani yao. Wanandoa hawa wangejenga tabia ya kumuheshimu Mungu kwa kila jambo wafanyalo, watoto pia wangeiga ile tabia kama ambavyo waliiga tabia ya kusoma vitabu kutoka kwao. Tabia hiyo ilisababisha mizengwe ya mama mkwe isiishe katika familia yao.
***********
Miezi sita baadae Mama Vivian alimchukua mwanae pamoja na mume wake na kuwapeleka kuzimu kwaajili ya kushuhudia sherehe ya mtoto wao Alaire akiliwa nyama. Aliamua kutekeleza agizo lake kwa mwanae kwamba watoto wote watakufa pamoja na mume wake na pia yeye atakuwa kichaa. Vivian na Nelson walifikishwa kuzimu na kupokelewa na nyimbo ambazo zilikuwa ni za kutisha sana. Walishindwa kuelewa walipokuwa lakini kilichokuwa kinaendelea kilikuwa kinawatisha. Vichwa vyao vilikuwa vikitazama huku na kule kuangalia walipokuwepo lakini walishindwa kubaini. Wote walijawa na hofu mioyoni mwao.
Baada ya kuona kwamba kule panatisha walianza kulia kwa huruma nyingi. Walikaa pembeni ya kiti cha malkia wa kuzimu ambae ndie mama yake na Vivian. Zilikuwa zikimbwa nyimbo ambazo hawakuelewa maana yake kwasababu lugha iliyotumika haikueleweka. Uchangamfu wa watu wa huko uliashiria kwamba kulikuwa na sherehe kubwa. Baada ya dakika kadhaa walimuona mwanao Alaire ameletwa mbele yao ambapo kulikuwa na meza kubwa ambayo ilikuwa imetapakaa damu. Alipandishwa juu ya meza hiyo na kulazwa kwa mgongo. Muda huohuo sauti iliyoambatana na kicheko kikali cha kutisha huku ikifuatiwa na sauti ya bundi ilisikika.
“Achinjwee.. Ahahahaha! Ahahahaha!”
Mwanaume mmoja ambae alikuwa ameshika kisu kikali alisogea alipokuwa amelazwa Alaire na kumchinja kama kuku. Vivian na Nelson kwa wakati huo walikuwa wakilia sana pindi mtoto wao alipokuwa akichinjwa mbele yao. Walitamani kunyanyuka na kwenda kuzuia mwanao asichinjwe lakini hawakuweza kunyanyuka kwani miguu yao ilikuwa mizito sana. Damu yote ilikingwa na baada ya hapo walianza kunywa kwa kuigombania. Vivian na mumewe walinyweshwa damu ya mwanao, nyama pia walikula, ingawa walifanya hayo yote kwa kulazimishwa. Sherehe ya kumla Alaire ilipokwisha kule kuzimu Nelson na Vivian walirudishwa duniani.
***********
Nelson na Vivian walizinduka kwa pamoja usingizini huku wakihema kwa pupa. Nelson aliwasha taa na kuangalia saa ya ukutani inaonyesha ni saa nane na nusu usiku. Ndoto aliyokuwa ameiota ilikuwa ni ya kutisha sana. Vivian alishindwa kuzungumza chochote kwasababu moyo wake ulikuwa ukienda kasi sana. Alikuwa anahema mithili ya mtu alitoka kufukuzwa muda mfupi uliopita.
“Duuh! afadhali ni ndoto.” Nelson alizungumza.
“Kwani umeota ndoto gani?” Vivian alimuuliza mume wake alichokuwa amekiota huku akionekana kukosa amani kabisa.
Nelson alimsimulia mke wake kila kitu. Vivian alishtuka sana kwasababu alichokuwa amekiota ndicho alichokuwa anasimuliwa. Kwamaana hiyo yule Nelson aliekuwa nae ndotoni ndie mume wake na mtoto aliekuwa akiliwa nyama kuzimu ndie mwanae. Mwili wake uliishiwa nguvu ghafla. Nelson alipata wazo la kwenda chumbani kwa wanae kwenda kuangalia wapo katika hali gani. Alifungua mlango taratibu na kwenda kumwamsha Alaire ambae wamemuota muda mfupi uliopita.
“Alaire! Alaire!” baba alimwita mwanae kipenzi.
“Kimya.”
“Alaire!” Nelson aliendelea kuita huku akimtingisha mwanae ili aweze kuamka lakini kimya kiliendelea kutawala. Nelson aliweka mkono wake juu ya kifua cha mwanae kusikilizia mapigo ya moyo lakini aligundua kuwa mtoto amefariki. Alishindwa kujizuia na kuanza kulia kama mtoto mdogo. Alishindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea katika familia yake ni kitu gani. Alirudi chumbani kwake baada ya kuhakikisha kwamba Mainard na Benedict wao wapo sawa. Alipofika chumbani kwake alimweleza mke wake kwamba Alaire amefariki dunia. Vivian alianza kuangua kilio cha uchungu sana usiku huo wa manane. Moyo wake ulijawa na hasira sana kwasababu alijua fika tukio lile lilifanywa na mama yake. Harakaharaka walimpakia kwenye gari na kumuwaisha hospitali ya Mount Meru ambapo huko napo daktari alithibitisha amefariki.
Kifo cha mtoto wao wa kwanza kilikuwa ni pigo kubwa sana katika familia yao. Ni mtoto ambae walimpenda sana kwasababu alikuwa na tabia za kipekee. Mainard na Benedict walimlilia sana kaka yao kwasababu walikuwa wanampenda sana. Kiukweli kifo cha Alaire kiliwaumiza watu wengi sana kutokana na umri wake bado ulikuwa mdogo halafu isitoshe kapoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha sana. Baada ya siku kadhaa mtoto alizikwa na maisha yaliendelea kama kawaida. Japokuwa moyo wa Nelson na Vivian ulibaki na majozi makubwa sana ya kupotelewa na mtoto wao mpendwa. Alaire aliacha maumivu makubwa ndani ya mioyo ya wazazi wake. Haikuwa kazi rahisi kwa Nelson na mke wake kumsahau mwanao mpendwa. Walikosa raha, muda mwingi walinyong’onyea kwasababu furaha yao ilikuwa imepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Utata wa kifo cha mtoto wao mpendwa pamoja na ndoto za kutisha zilisababisha wawe watu wa kukosa raha muda wote. Amani ndani ya mioyo yao ilitoweka pindi walipokuwa wakiona giza linaingia. Kiukweli kwa jinsi ambavyo walikuwa wanauchukia usiku wangekuwa na uwezo wa kuzuia usiku usiingie basi wangefanya hivyo ili kujinusuru na ndoto mbaya za kutisha kila wakati. Mara zingine Nelson na mke wake walikuwa wanaamua kucheza karata hadi panakucha ili tu wasifumbe macho yao na kuangukia katika ndoto zilizosheheni umauti ndani yake.
Walidiriki kuchukua biblia na kuweka chini ya mito yao kama kinga lakini haikuwa suluhisho kwani ndoto mbaya ziliendelea kama kawaida. Kilichokuwa kinawakondesha ni kwamba walikuwa wanaota ndoto ambazo zinaukweli mtupu ndani yake. Walizidi kuwa watu wa mashaka mashaka kila mara. Bosi kazini alishuhudia ufanisi wa Nelson ukishuka siku hadi siku, kwahiyo alimuandikia barua kwaajili ya onyo kusudi aweze kujirekebisha. Furaha iliyokuwa imetawala katika ndoa yao iliendelea kutoweka. Ingawa Nelson alikuwa katika wakati mgumu kuhusu mambo waliyokuwa wanapitia katika ndoa yao lakini mkewe Vivian ndie aliekuwa akipata wakati mgumu zaidi kwasababu alikuwa anafahamu dhahiri aliekuwa anawafanyia vile ni nani na pia makusudio yake yalikuwa ni yapi. Alizidi kuwaza na kujiuliza inamana ni kweli mama yake atawauwa watoto wake wote halafu na mume wake atakufa? aliishia kudondokwa na machozi kutokana na mambo mazito aliyokuwa anapitia.
Moyo ulimuuma sana, alimuona mama yake ni zaidi ya shetani. Aliwaza inawezekana vipi mama aliyemzaa anamfanyia mambo ya kinyama namna ile. Baada ya kuwaza sana siku moja alimua kumuendea mama yake kumbembeleza kusudi asiendelee kuiangamiza familia yake. Alipofika nyumbani kwao alimkuta mama yake ambapo alianza kuzungumza nae kwa upole na moyo wa huruma ili mama yake asiendelee kumtendea yale aliyokuwa amemtamkia baada ya kukataa kupokea uchawi. Vivian alilia sana huku akimpigia mama yake magoti aweze kubadili mawazo yake lakini mama aliendelea kushikilia msimamo wake wa awali.
Alimweleza kwamba njia pekee ya kukwepa vifo vile ni kukubali kupokea uchawi. Tena alimsihi afanye haraka mno kwasababu vifo vingine vitafuata siku sio nyingi. Moyo wa Vivian uliendelea kuwa mgumu kupokea uchawi aliokuwa anapewa na mama yake. Aliona kuliko awe mchawi ni bora yale aliyokuwa anaelezwa na mama yake yaendelee kutokea. Baada ya Vivian kuona kwamba mama yake amekataa kubadili mawazo yake aliamua kuondoka na kurudi nyumbani kwake huku akiwa na msongo mwingi wa mawazo. Siku zilizidi kusonga mwili wa Vivian ulizidi kudhoofu kutokana na mawazo. Alikonda sana hadi majirani wakawa wanashangaa kwanini alipungua ghafla wakati alikuwa na mwili mzuri wa kunawiri.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi