SITOISAHAU FACEBOOK (3) - CnZ Media

CnZ Media

Jisomee Simulizi Mpya Kila Siku

Jumatatu, 29 Aprili 2024

SITOISAHAU FACEBOOK (3)

UMEWAHI KUONA AU KUSIKIA KUHUSU PICHA ZA AI?
Sasa naomba nikufundishe bure kabisa nawewe uzitengeneze kirahisi kabisa


SEHEMU YA TATU
ILIPOISHIA...
Tulipofika Makambako nilianza kuifikiria familia yangu niliwaza kumjengea mama yangu nyumba ya kifahari kisha nimtoe baba yangu katika ulevi sugu kwa kumuwekea pombe za kisasa ndani. Hizo niliamini zitamnenepesha badala ya kumkondesha. Wadogo zangu waliokuwa wakisoma shule za kata nao nadhani walitakiwa kusoma shule zenye hadhi ya mshahara nitakaokuwa napokea dada yao.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI

SASA ENDELEA...
Tena wote nawapeleka shule za bweni!!! Nilijiapiza huku pua zangu zikinusa kwa mbali harufu nzuri ya sabuni ambayo nilitumia asubuhi kuoga katika hoteli ya kifahari mjini Dodoma.Nilitoa tabasamu hafifu kisha nikaendelea kuuchapa usingizi.

Nilifika Mbeya salama. Dereva teksi wa kwanza niliyekutana ndiye alipata bahati ya kuniendesha msichana ambaye nilikuwa na malengo makubwa kama mimi. Alitakiwa kujisifu kama angekuwa kichwani mwangu.Alinifikisha hadi hoteli maridadi yenye hadhi ya kulaliwa na watoto wa vigogo na vigogo wenyewe. Nililipia na kulala hapo kesho yake mapema nikawa Tunduma halafu mwisho ikafuata safari ya Ndola. Hata ule uchovu haukusumbua mwili wangu.

Ndani ya basi tulilokuwa tumepanda walikuwepo watu mchanganyiko. Hakuna aliyekuwa na hadhi kama mimi. Yaani nilikuwa najisikia kuwa na uwezo hata wa kuamuru basi hilo lisimame na likasimama lakini sikufanya hivyo.Majira ya saa kumi na moja jioni kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nilikanyaga ardhi ya nchi tofauti na Tanzania. Isabella ndani ya Ndolla

Mwanzo wa safari ya kwenda Marekani!!! Nilijiwazia hivyo.Nilitegemea kuhangaika sana baada ya kuwa nimeshuka pale kituoni. Lakini la!! Haikuwa hivyo. Nilipotelemka tu. Nilitumia dakika moja tu kushangaa wanawake wawili waliokuwa wamependezea katika mavazi yao ya suti walinipokea begi langu dogo huku wakinisalimia kwa nidhamu kubwa sana.Niliwajibu kwa tabasamu, sasa nilianza kuamini kuwa Dokta Davis atakuwa ni mtu mkubwa sana. tofauti na mwonekano wake.Niliongozwa hadi katika gari aina ya Noah, nilitaka kuingia humo lakini nikaambiwa hilo ni kwa ajili ya mizigo. Nikacheka moyoni huku nikiwaza kuwa laiti kama ningepewa hilo gari. Chuo wangekoma!!Mh!! Mzigo gani sasa?? Nilijiuliza. Hakuwepo wa kunijibu.

Baada ya hapo nikapelekwa katika gari iliyokuwa na milango sita.Hapo nikafunguliwa milango nikaingia ndani. Niliokutana nao mle ndani wote walikuwa na nyuso zilizong’aa tofauti na ule wa dokta Davis. Japo walikuwa weusi na sura zao zikitangaza roho flani hivi isiyokuwa na ukarimu sanalakini walitabasamu. Naishi kama mfalme nchi za watu?? Mwalimu Nchimbi natamani ungeyaona haya goodbye umasikini!!!! Nilijitamba kichwani mwangu huku nikikaa vyema na kuzijibu salamu za watu pale ndani.Safari ikaanza. Sikuwa naujua mji hata mmoja lakini safari nayo haikuwa fupi.

Nilitamani sana niulize kuwa pale ni wapi lakini ningeanza kumuuliza nani?? Hilo likawa swali. Laiti kama dokta angekuwepo hapo sawa.Nikiwa bado nashanga shangaa hapa na pale mara mwendo ulipungua kisha honi ikapigwa. Geti likafunguliwa na watu waliovaa nguo nyeupe sana. Gari zikaanza kuingia, yetu ikiwa ya pili kuingia.Tulipotaka kushuka milango ilifunguliwa na akina kaka wenye kila sababu za kuitwa watanashati na wanamazoezi. Nikazidi kuvimba kichwa kwa mema haya niliyokuwa natendewa.

Nikiwa bado sijafungua kinywa kuzungumza tangu nijibu salamu garini, walinifuata akina dada watatu wakanielekeza kwa ishara za mikono niwafuate. Sikuwa na kipingamizi niliwafuata. tuliingia katika chumba kilichokuwa na mvuto hata kwa yule asiyejua ubora wa chumba. Lakini mimi nilikuwa naujua ubora niliambua.“You have to re-dress madame” (Unatakiwa ubadili mavazi yako).Waliniambia kwa pamoja. Sauti zao tamu zilinikonga moyoni.

Wakanipa maelekezo na baada ya dakika kadhaa nilitoka mle ndani nami nikiwa nang’ara katika mavazi meupe sana.Nilikuwa nimependeza sikuhitaji kumuuliza mtu.Sasa tukarejea katika magari tena. Mi nilijua tumefika mwisho kumbe lile lilikuwa geti la kwanza tu.Mwendo wa dakika tano tukashuka tena. Tukaingia geti jingine kubwa. Hapo tukatelemka na kuanza kutembea juu ya kapeti jekundu.Red kapeti!!! Niliwaza. Nikafanya tabasamu.Nikiwa juu ya lile kapeti nikajihisi kuwa na hadhi ya Rihanna, Beyonce ama Lady Gaga. Kisa tu nipo juu ya zulia jekundu.Hapa kama ni kazi nimepata!! Nilijiaminisha.

Nilikuwa makini katika kulikanyaga lile zulia jekundu, sikutaka kuonekana mshamba katika hilo. Nilijilazimisha kutembea mwendo wa kilimbwende wakati niliamini kuwa iwapo nitathubutu kuingia katika mashindano ya ulimbwende basi nitashika nafasi ya mwisho ama sitapata walau kigezo cha kusimama jukwaani kama mlimbwende. Maana nilikuwa cha ufupi na nilikuwa na dalili ya kuwa kibonge.Niliongozwa hadi katika chumba kikubwa sana, kila kitu pale ndani kilikuwa cheupe kasoro ngozi yangu ambayo ilifanya kama uchafu pale ndani. Sikujali!!!

“Utalala hapa ndani…na hawa watakuhudumia.” Nilipewa wakinamama wawili kwa ajili ya kunihudumia. Umri wao sidhani kama unatofauti sana na wa mwalimu Nchimbi yule mama yangu mzazi. Lakini matabasamu yao ni kama walikuwa na miaka kumi na nane.Ungekuwa wewe ungejisikiaje. Mwenzako nilijisikia kama malkia.Nilipata huduma zote za msingi hadi nilipopitiwa na usingizi na kuamka siku iliyofuata. Baada ya kuwa nimeoga na kupewa nguo nyingine nyeupe tena nilikaribishwa kifungua kinywa.Ilikuwa kufuru nyingine tena niliyoweza kuishuhudia.

Meza ilikuwa imesheheni kila aia ya makorokoro. Kazi kwako mlaji kujihudumia. Kiaibuaibu nikajinyima kula nilivyovitamani nikala nilivyovizoea. Na ushamba pia ulichangia. Kuna vyakula sikuelewa kama vinaliwa kwa kijiko ama uma, harufu yake nzuri ikabaki kunisurubu. Nikaogopa kujaribu!!!Majira ya saa tano asubuhi niliongozwa tena kuelekea katika ile gari ya milango sita. Nikaingia humo kwa namna ileile kama malkia. Safari yetu ikaishia katika sehemu nyingine ya kifahari. Sikuwa naielewa nchi ya Zambia hivyo sikujua lolote.

“Mukuba Hotels.” Hilo ndilo neno nililoweza kulisoma baada ya kuunyanyua uso wangu juu. Sikujua maana ya Mukuba. Lakini bila shaka zilikuwa lugha za huko kwao. Hii hoteli ama jumba la kifalme!! Nilijiuliza.Tuliingia hadi ndani huku mimi nikiwa mfuata mkia nisiyejua lolote linaloendelea mbele. Baada ya kukatiza kona kadha wa kadha sasa tukakutana na mlango ulioandika kwa maandishi yenye rangi ya dhahabu!! Dr. Davis. Moyo wangu ukapiga kwa nguvu. Paa!!Ina maana Davis anaishi hapa? Nilitamani kuuliza ila nikasita.Nikiwa nasubiri ajitokeze mtu kwa ajili ya kubisha hodi ili tuweze kuingia ndani maana sikuona mahali pameandikwa ‘PULL/PUSH’ mara mlango ule wa vioo ulianza kufunguka wenyewe, tukaingia ndani.

Sasa tulikuwa watu watatu pekee!! Wale wawili baada ya kuingia ndani pamoja nami wakatoka nje. Bila kusema neno!!Sasa nikabaki peke yangu.Kiti cha kuzunguka kilichokuwa kimegeuziwa ukutani kikazungushwa taratibu. Vazi la suti likanisabahi, kisha uso ukanyanyuka.“You are most welcome!!” Alinikaribisha. Kisha akatabasamu. Alikuwa anafanana na Davis lakini sikutaka kuamini. Labda ndugu yake au au au…“Ndo mimi mbona unashangaa.” Aliniwahi. Ni kama alijua nilichokuwa nawaza. Alikuwa ni Davis. Sauti yake ilikuwa ileile.

Nikachukua nafasi. Bila kusema lolote alibonyeza kitufe mara kikashuka mfano wa kitrei cha kuwekea vyombo.“Unatumia kinywaji gani.” Aliniuliza mimi nikiwa bado nashangaa.“Aaaah!! Chochote.” Nilijiumauma.Akabonyeza vitufe kadhaa, kikaondoka na kurejea tena baada ya dakika tano.Maajabu ya nane ya dunia. Kile kitrei kilikuwa na glasi mbili za juisi. Akatwaa moja akanipatia. Sijawahi kuona tangu nizaliwe!!“Asante.” Nilimshukuru. Hakujibu.Dokta Davis aliyekuja Tanzania hakufanana hata kidogo na huyu. Huyu alinuka pesa tena pesa nyingi.

“Karibu Ndolla Zambia, hii ni ofisi yangu ndogo ya huku, nyingine ipo Lusaka, Accra na kubwa zaidi ipo Washington.” Alinielezea kwa sauti iliyojaa ujivuni. Lakini alikuwa amechangamka!!Nilikuwa makini kumsikiliza.“Isabela…. .”“Abee!!.” Niliitika.“Kampuni yangu imeamua kufanya kazi na wewe.” “Nashukuru sana Dokta.” Nilishukuru, hakujali hilo akaendelea“Unauchukia umasikini?.”“Nauchukia kuliko niavyoweza kujielezea.” Nilisisitiza.“Na….anyway..unaenda sana kanisani.”“Aaah!! Kiukweli ni mara chache chache.”“Kwa nini?.”“Aaah!! Mambo huwa yanakuwa mengi sana.”

“Ok!! Achana na hayo…Isabella kazi uliyopata hapa ni kazi nyepesi na kila mwezi itakuingizia shilingi milioni sita laki sita na elfu sitini na sita kila mwezi.” Alizungumza Dokta bila wasiwasi, alimanusura nipoteze fahamu. Mwili ukawa wa baridi. Nikajaribu kujishtua huenda ninaota, haikuwa hivyo. Hali ile ilikuwa halisi.Nilikuwa Zambia na nilitangaziwa dau hilo kubwa.“Unawazungumziaje wanaume kwa ujumla?.” Davis hakujali ule mshtuko wangu akanitupia swali jingine, bila shaka milioni sita kwake si lolote si chochote.“Aaah!! Kiaje labda” Nilimuuliza huku nikifinya finya mikono yangu.“Vyovyote vile lakini hasahasa katika kazi ya mapenzi.”

“Viumbe waongo, wasiokuwa na huruma, wanyanyasaji na…”Nilishindwa kuongea nilikuwa nimemkumbuka John, mwanaume aliyeamua kuachana nami kisa sina pesa. Sasa hapa nazungumzia juu ya kupata pesa.“Labda ukiambiwa uwape adhabu utatoa adhabu gani kwao.”“Dah!! Sijui watoweke duniani…aaah!! Sijui ila nawachukia wanaume wenye tabia hii.” Nilimjibu huku nikilegeza koo kwa kugida funda mbili za juisi ile. Ilikuwa tamu sana. sijui tunda gani lile!!!

“Safi sana…kumbe kazi utaiweza kabisa lakini lazima kwanza ubadili kwanza mawazo yako hayo ya kuombea wanaume watoweke. Lengo la kampuni yangu mimi ni kuwabadili wanaume kuacha na mfumo huo wa unyanyasaji na pia kuwafunza wanawake kuepukana na vishawishi vya wanaume wadanganyifu. Tunaamini kuwa utaweza kutuwakilisha vyema katika nchi yako. Ukimuelimisha msichana mmoja kwa siku basi ujue umeielimisha jamii kubwa sana.” Aliongea kwa umakini mkubwa huku akiwa amenikazia macho. Nilikwepesha kutazamana naye.

“Nitaweza hata usitie shaka.” Niliikubali kazi. Zikaangushwa karatasi nne mezani nikasaini mkataba mnono.“Baadaye kidogo pesa ya utangulizi itaingizwa katika akaunti yako.” Alimaliza Dokta.Tunaweza kuzunguka zunguka kidogo uitazame ofisi yangu. Lilikua ombi la Dokta nikakubaliana nalo.Tulizunguka kona tofauti tofauti. Nilikuwa nikimtazama Davis kwa kuibia ibia na yeye pia alifanya hivyo. Yale mawazo ya kumfanya awe mpenzi wangu yakawa yananisumbua akili nilitamani kumwambia lakini mdomo ukawa mzito.Laiti kama nikiwa naye!! Hata hii ofisi pia itakuwa mali yangu!! Niliwaza.*

MWANZA
Ulikuwa usiku wa kipekee sana kwangu, ndio kwanza nilikuwa nimerejea jijini Mwanza, kwa usafiri bora wa ndege. Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu.

USIKOSE SEHEMU IYOFUATA

Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni