JULIANA (3)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mwandishi: Emmy John Pearson
SEHEMU YA TATU
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Baada ya kuvumilia sana, baada ya kulia sana akaamua kuupiga konde moyo wake na kumfuata mwanaume huyo. Hakuogopa tena, alikuwa tayari kukataliwa lakini mwisho wa siku awe amemwambia mwanaume huyo kuhusu hisia zake, kwa nini aogope? Kwa nini ateseke? Kwa nini aumwe na wakati kulikuwa na daktari wake.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
Akamuomba Gideon muda wake, alitaka kuonana naye sehemu, wazungumze mawili matatu lakini siku za kwanza mwanaume huyo alimkatalia kwa kumwambia kwamba hilo lisingewezekana, na kama alitaka lifanyike basi aende na Juliana.
“Gideon!”
“Nimemaanisha Halima! Siwezi kuja peke yangu, ukitaka nije na Juliana,” alisema Gideon kwani alijua ni kitu gani kingetokea huko.
“Hapana Gideon! Ninahitaji uje wewe tu!”
“Haliwezekani!”
“Gideon!”
“Nimesema haiwezekani!”
Gideon hakutaka kubaki mahali hapo, akaondoka zake na kumuacha msichana huyo akimwangalia tu. Halima aliumia moyoni mwake, alitamani kumsimamisha mwanaume huyo lakini halikuwezekana kabisa.
Alimpenda, hakutaka kumuacha hivyohivyo, hakutaka kukata tamaa, aliamini kwamba kama angeendelea kumuomba sana mwanaume huyo mwisho wa siku angemkubalia na hivyo kukutana faragha na kuzungumza.
Halima alijua kusumbua, alijua kupiga simu kiasi kwamba ikaonekana kuwa kero kwa Gideon hali iliyomfanya kukubali kuonana naye kwani kwa jinsi alivyokuwa akisumbua, alijua kabisa kuna siku Juliana angejua kile kilichokuwa kikiendelea.
“Aya nimekuja! Unahitaji nini?” aliuliza Gideon baada ya kuonana na msichana huyo.
“Gideon! Nimeshindwa kuvumilia. Ninakupenda mno. Nimekuwa nikitamani sana kuwa nawe, umenitesa sana moyoni mwake, sijiwezi, nimekuwa mtu mwenye mawazo sana juu yako, najua kwamba una mtu lakini sidhani kama Juliana anaweza kukuondoa moyoni mwangu,” alisema Halima huku akimwangalia Gideon aliyeonekana kushangaa.
Halima alikuwa msichana mrembo sana, tena zaidi ya Juliana. Gideon alishangaa, ilikuwaje msichana mrembo kama huyo amtongoze na wakati kulikuwa na wanaume wengi waliokuwa wakimfuata? “Unanichanganya Halima,” alisema Gideon.
“Gideon! Nakuchanganya!”
“Inakuwaje msichana mrembo kama wewe uniambie kwamba unanipenda? Kuna wanaume wengi wanakufuata na kukuhitaji, inakuwaje uje kwangu?” aliuliza Gideon.
“Kwa sababu nakupenda.”
“Lakini nina mtu!”
“Hata kama Gideon! Ninakupenda, ninakuhitaji, naomba uwe wangu,” alisema msichana huyo.
Gideon alibaki kimya, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mpenzi wake, Juliana. Ni kweli Halima alikuwa mzuri wa sura, alipendeza na kuvutia machoni mwake lakini kumsaliti Juliana kwa ajili yake aliliona jambo gumu sana.
Alikumbuka jinsi alivyoteseka kwa ajili ya Juliana, zaidi ya miezi mitatu alijifanya mlokole akishinda na Biblia, iweje leo aje kumsaliti msichana huyo kiwepesi namna hiyo?
“Haiwezekani!” alisema Gideon.
Huo ndiyo ulikuwa msimamo wake, hakutaka kabisa kuwa na Halima, moyoni mwake, hakukuwa na msichana aliyekuwa na nafasi kubwa kama Juliana.
Siku ziliendelea kwenda mbele, msichana huyo hakutulia, aliendelea kumsisitizia mwanaume huyo kwamba alikuwa akimpenda sana lakini Gideon hakuwa mwepesi kukubaliana naye. Moyoni mwake kulikuwa na msichana mmoja tu, Juliana ambaye kwake alikuwa kila kitu.
Juliana akaanza kuingiwa na hofu, kila alipokuwa akimwangalia mpenzi wake aliona kabisa kukiwa na utofauti, hakuwa na furaha kama kipindi cha nyuma, hakuwa amechangamka kama siku chache zilizopita.
Alimzoea sana, mabadiliko hayo yakamtia hofu na kuanza kumuuliza, kama mpenzi wake alitakiwa kujua kila kitu. Alipomuuliza, Gideon hakumwambia ukweli, alimwambia kwamba hakukuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, alikuwa kawaida kama zamani.
“Hapana! Hebu niambie mpenzi wangu. Kuna nini?” aliuliza Juliana huku akimwangalia Gideon.
“Hakuna kitu!”
“Una uhakika?”
“Ndiyo mpenzi! Naomba uniamini,” alisema Gideon, hapohapo akamsogelea Juliana na kumkumbatia, akampiga mabusu mfululizo kwenye paji la uso wake na mdomo.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, Gideon hakutaka kabisa kumsogelea Halima, kila alipokuwa akimuona alikuwa akimkwepa. Msichana huyo hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kuchukua simu yake na kuanza kuwasiliana na mwanaume huyo huko.
Bado Gideon hakutaka kuelewa, hakuwa tayari kuona akitembea na msichana mwingine zaidi ya Juliana. Halima alijitahidi, alipambana kwa nguvu zote kulichukua penzi la Gideon lakini ikashindikana kabisa, hivyo alichokifanya ni kuanza kumtumia picha mbalimbali.
Zilianza picha za kawaida ila kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele msichana huyo akabadilisha picha zake na kumtumia picha za nusu utupu mpaka zile za utupu kabisa. Gideona aliziona, akachukia mno moyoni mwake kwani alijua madhara ya kuwa na picha zile katika simu yake. Hapohapo akampigia Halima.
“Ndiyo unafanya nini?” aliuliza Gideon huku akionekana kuwa na hasira sana.
“Kwani nimefanyaje mpenzi?
“Nani mpenzi wako? Hivi unaona mimi ni mjinga mpaka kunitumia mapicha yako. Wewe mwanamke nielewe. Usinitumie tena picha zako,” alisema Gideon kwa hasira. “Nitashindwa kujizuia. Ukikata simu, nakutumia tena!” alisema Halima na kukata simu.
Gideon alifikiri ulikuwa utani, msichana huyo hakukoma, akamtumia tena na tena kitu kilichomfanya kuwa na hasira kupita kawaida.
Hofu yake kubwa ilikuwa ni mpenzi wake, Juliana, alijua kwamba endapo msichana huyo angeendelea na tabia yake ya kumtumia picha hizo kila siku basi kuna siku ingetokea balaa endapo tu msichana huyo angeziona.
Hakutaka hilo litokee kwani kwenye kitu ambacho hakutaka kabisa kuona kikipotea mikononi mwake kilikuwa ni mpenzi wake, Juliana, msichana mpole, mnyenyekevu na aliyekuwa na mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwake.
Kazi kubwa ya Gideon ilikuwa ni kuzifuta picha za msichana huyo. Alizituma nyingi tena huku zikimuonyesha akiwa kama alivyozaliwa na nyingine zikiwa ni video ambazo zilimuonyesha akicheza mtupu na wakati mwingine akifanya matendo yasiyoandikika hadithini.
Gideon alichukia lakini hakuwa na jinsi, moyo wake ulishikwa na ghadhabu kiasi kwamba akaamua kuiblock namba ya msichana huyo ili asiweze kupokea ujumbe wowote kutoka kwake.
“Gideon! Nahisi kuna kitu kinaendelea, hebu niambie kuna nini,” alisema msichana Juliana huku akimwangalia mpenzi wake.
“Hakuna kitu!” “Umekuwa ukiniambia hivyo mara nyingi na kila ninapokuangalia nagundua kwamba kuna kitu, naomba uniambie, kuna nini mpenzi wangu!” alisema Juliana.
Majibu yake hayakubadilika, hakutaka kumwambia kuhusu msichana Halima kwa kuamini kwamba wawili hao wangeweza kugombana. Siku zikaendelea kukatika huku ugomvi baina yake na Halima ukiendelea kila siku.
“Ngoja nifanye kitu,” aliwaza Gideon, alipata njia ya kumzuia msichana huyo asimfanyie mchezo ule tena.
Akamfuata rafiki yake aliyeitwa Fred na kumwambia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Fred hakuamini, alimjua Halima, alikuwa msichana mrembo aliyekuwa akitongozwa na wanaume wengi na kuwakatalia, hakuamini kama msichana huyo angeweza kufanya vitu vya kipumbavu kama hivyo.
“Kwa Halima! Hapana Gideon! Labda useme wakina Stella lakini si Halima huyu,” alisema Fred huku akimwangalia Gideon.
“Niamini! Huyu msichana mchafu sana. Alinitumia mapicha yake mengi sana ya utupu utupu,” alisema Gideon.
“Kwanza hebu nizione.”
“Uone nini?”
“Hizo picha. Nataka nione akiwa mtupu anafananaje!” alisema Fred huku akionekana kuwa na mshawasha wa kuona picha hizo.
“Nilizifuta!”
“Gideon! Unapata picha za utupu za Halima unazifuta! Daah! Sasa huo si ndiyo ushahidi wenyewe! Halafu picha za Halima kweli unazifuta kaka, tena unaniambia mimi bila kunificha! Haki ya Mungu ningekuwa Syria, ningevivisha mabomu nije kujilipua mbele yako, hutakiwi kuishi kabisa, Mungu kakupa pumzi za kuishi, wewe unazitumia kufuta picha za utupu za Halima! Haupo siriazi kabisa,” alisema Fred huku akimwangalia Gideon kwa macho yaliyoonyesha mshangao mkubwa.
Gideon hakutaka kujali, alichokuwa akihitaji ni kusaidiwa na kijana huyo tu, alimwambia dhahiri kwamba walitaka kufanya mchezo ambao ungemfanya msichana huyo kutokutuma picha tena au kumsumbua na jambo zuri ambalo lilitakiwa kufanywa ni kumfuata na kumwambia kuhusu picha hizo za utupu.
Kwa Fred wala hakukuwa na tatizo, akakubaliana na Gideon kwamba kitu hicho kingefanyika kwa haraka sana na hivyo baada ya kuachana, jioni ya siku hiyo akamtafuta msichana huyo na kumuomba kuonana naye kwa ajili ya kuzungumza.
“Uzungumze na mimi?” aliuliza Halima, kama kawaida yake akabinua kidogo midomo.
“Ndiyo!”
“Hapana! Nipo bize sana,” alisema huku akichukua mkoba wake na kuanza kuondoka.
“Sawa. Tutakutana kwenye Mtandao wa Global Publishers kwa ajili ya kuzioa picha zako za utupu,” alisema Fred, hakutaka kubaki mahali hapo, huyo akaanza kuondoka zake.
Halima akashtuka, hakuamini kile alichokisikia, alihisi kwamba alisikia vibaya alichokuwa ameambiwa na mwanaume huyo, akahisi damu yake ikianza kuzunguka kwa kasi mwilini mwake, mapigo ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, hakutaka kubaki mahali hapo, kwa kasi akaanza kumfuata Fred.
Kwa kuwa naye alijua kwamba msichana huyo alikuwa akimfuata, akaongeza mwendo, japokuwa Halima alikuwa akiita ili asimame lakini hakusimama, aliendelea kutembea kwa mwendo wa haraka.
Moyo wake ukawa na hofu kubwa, aliufahamu mtandao wa Global Publishers, aliamini kwamba kama picha zake zingetolewa katika mtandao huo, mwisho wa siku zingemaliziwa katika magazeti kitu ambacho kingemfanya kupata aibu ya mwaka ambayo hakuwahi kuipata maishani mwake.
Hakukuwa na picha za utupu alizowahi kupiga zaidi ya zile ambazo alijipiga na kumtumia Gideon, moyo wake ukaanza kujuta, kitendo chake cha kuonyesha mapenzi kwa mwanaume huyo kwa kuamini kwamba angependwa kukaonekana kuanza kumtia aibu ambayo hakuwahi kuifikiria kabla.
“Naomba unisubiri wewe kaka,” alisema Halima huku akikimbia kumfuata Fred.
Fred akasimama, msichana huyo akamsogelea, alikuwa akihema kwa nguvu, alichoka kukimbia, tayari macho yake yalibadilika, yakawa mekundu kwani tayari machozi yalianza kukusanyika machoni mwake. Alimwangalia mwanaume huyo huku akionekana kutia huruma sana, kwa sababu alikuwa amedharauliwa, naye akamuonyeshea dharau msichana huyo kwa kumwangalia juu mpaka chini, halafu akamsonya.
“Naomba uifiche aibu hii!” alisema Halima.
“Eti msichana mzuri unatuma picha kwenda kwa mwanaume, hata aibu huoni. Sasa dawa yako moja tu, picha zako nawapa watu wa magazeti ya udaku ili ukome, tutafanya kama tulivyofanya kwa msichana Salma,” alisema Fred, yote ilikuwa ni kumtisha msichana huyo, hakukuwa na kitu kilichotokea, ila aliamua kulitumia jina la Salma kwa kuamini kwamba msichana huyo angeamini kwamba kulikuwa na mtu ambaye naye alifanyiwa mchezo kama huo.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni