JULIANA (2)
Zephiline F Ezekiel
5 min read
Mwandishi: Emmy John Pearson
SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Juliana! Naomba umsahau Gideon yule wa nyuma. Amekufa! Huyu ni Gideon mpya aliyezaliwa mara ya pili. Ningependa uje kushiriki ibada kanisani kwetu kama hutojali,” alisema Gideon huku akiachia tabasamu pana.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
“Kanisa gani?”
“Living Water. Nakuomba uje Juliana uuone utukufu wa Mungu!” alisema Gideon.
“Nitaangalia.”
“Nashukuru!” aliseema Gideon.
Gideon akaondoka huku akiwa na matumaini makubwa ya kumpata msichana huyo mrembo, alimfikiria sana kichwani mwake na kila muda alikuwa akiliandika jina lake kwenye karatasi, alimpenda kwa moyo wake wote.
Juliana alikuwa na wasiwasi, hakumwamini sana Gideon, hata kitendo cha kumwambia kwamba aliamua kuyabadilisha maisha yake na kumkabidhi Mungu bado ilimpa hofu mno.
Aliona haikuwa rahisi kwa mtu kubadilika kwa kipindi kifupi namna hiyo, alihisi kwamba inawezekana mwanaume huyo aliamua kutumia nafasi hiyo ili kumnasa kiulaini kwani kwa kipindi kirefu alikuwa amemsumbua.
Mawazo hayo yalipotea baada ya kukumbuka sura ya Gideon, jinsi alivyokuwa akizungumza naye, alionekana kama mtu aliyemaanisha kile alichokuwa akimwambia. Moyo wake ukagawanyika pande mbili, moja ilimuamini lakini upande mmoja haukumuamini kabisa.
“Ngoja nimpe nafasi ya kwenda huko kanisani, kama amebadilika au hajabadilika nitajua tu,” alisema Juliana.
Jumapili ya siku iliyofuata wakatangulizana kanisani. Gideon alifurahi, hakuamini kama suala hilo lingewezekana kwa haraka namna hiyo. Alitamani kumwambia ukweli kwa mara nyingine kwamba alikuwa akimpenda lakini hakuona kama kulikuwa na uharaka wa kufanya hivyo.
Alichokitaka ni kuweka ukaribu mkubwa, aonekane kuwa mtu muhimu katika maisha ya msichana huyo. Hilo liliwezekana, kwenda kanisani pamoja, kusoma Biblia pamoja kukawafanya kuwa karibu.
Kila kona wakawa wawili, alipokuwa Gideon ilikuwa ni rahisi kumuona Juliana, na kama hakuwa naye basi hakuwa mbali kutoka hapo alipokuwa.
Hilo liliendelea kwa miezi mitatu mfululizo, Gideon hakutaka kujifanya kuwa na presha, alitaka kufanya mambo kiuhakika na mwisho wa siku kumuingiza msichana huyo katika kumi na nane zake.
“Ataingia tu! Hapa ni mwendo wa kujifanya nimezama kiroho mpaka nimchukue. Huyu binti nina mipango naye sana tu ila naye shetani ananiwekea kauzibe tu,” alisema Gideon huku akikenua.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao ya kila siku, ukaribu ukaongezeka kiasi kwamba Juliana akaanza kujisikia hali ya tofauti moyoni mwake. Moyo wake ukaanza kuhisi mapenzi, akaanza kumuona Gideon kuwa mtu muhimu katika maisha yake kupita kawaida.
Hakuwa mtu wa kumpigia simu, japokuwa walikuwa na ukaribu lakini alitaka mwanaume huyo awe anampigia simu kitu ambacho hakikuwa tatizo lolote lile.
Mambo yakabadilika, badala ya Gideon kumpigia sana simu sasa ikawa zamu yake.
Kila mara ilikuwa ni lazima ampigie simu mwanaume huyo. Alikuwa akizungumza naye na muda mwingi alikuwa akichekacheka. Aliichukia hali iliyokuwa ikijitokeza moyoni mwake, alitamani kuiondoa lakini alishindwa kabisa, alikikataza kichwa chake kumfikiria Gideon lakini hilo lilionekana kuwa jambo gumu mno.
Moyo wake ukafa na kuoza, akawa hasikii kitu chochote kile. Walikuwa wakizungumza mambo ya kawaida kwenye simu, safari ya Waisrael kutoka Misri kwenda Kanaani, Jinsi Daniel alivyonusurika kuliwa na simba kwenye shimo kubwa, Yesu alivyolisha watu elfu tano kwa mikate na samaki lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele, mambo yakabadilika na hatimaye kuanza kupiga stori za kina Ommy Dimpoz na Harmorapa, shoo zao, upinzani mkubwa wa Kiba na Diamond, na mwisho wa siku kabisa kuanza kuelezea hisi kali zilizokuwa mioyoni mwao.
“Hapana Juliana. Hatutakiwi kuzungumzia mapenzi lakini,” alisema Gideon, tayari akajiona kuwa mshindi, alijiona kufanikiwa kumuingiza msichana huyo katika mikono yake, naye akaanza kumletea mapozi.
“Gideon! Pleaseee…you are hurting me, you love is killing me,” (Gideon! Tafadhali..unaniumiza, penzi lako linaniua) alisema Juliana, Gideon hakuamini masikio yake.
“Juliana!”
“Abee!”
“Ni wewe kweli au?” aliuliza Gideon.
“Kwa nini unauliza!”
“Umebadilika! Yesu hapendi, si unajua hilo?”
“Najua lakini…Gideon naomba nikuone! Naomba nikuone!”
“Haina shida. Ila niahidi kitu kimoja!”
“kipi?”
“Hatutozungumzia kuhusu mapenzi. Nataka niingie kwenye mfungo wa mwezi mzima kuyaombea masomo yetu,” alisema Gideon.
“Sawa,” aliitikia Juliana kwa sauti ya upole.
Alishindwa kuvumilia, moyo wake ulikufa na kuoza. Penzi likautafuta moyo huo vilivyo, akawa hajiwezi tena, akashindwa kujificha na hivyo kumwambia Gideon hali halisi.
Kwa upande wa Gideon, alifurahi, aliona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa msichana huyo. Alipoambiwa, akaingizia maneno ya dini lakini wakati mwingine alikuwa akijilaumu kwamba kwa nini alikuwa akimtesa msichana huyo na wakati yeye mwenyewe alimpenda na kumtaka tangu zamani?
“Hapa nikiremba kibwegebwege mtoto ataondoka. Hainaga kuremba, ngoja nifanye kweli. Kama mambo ya kanisani tutakwenda Mbinguni,” alisema Gideon.
Akakaa kitandani, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Juliana tu. Wakati mwingine alihisi kwamba huo ulikuwa utani kwamba msichana huyo alikuwa akimtania na haikuwa kweli kwamba alikuwa akimpenda. Usiku huo, Juliana hakutulia, kila wakati alikuwa akimtumia meseji Gideon kwamba asimtese kwani yeye ndiye alikuwa kimbilio lake na kwamba kama angemtesa basi angejiua.
“Ujiue?”
“Gideon! Naomba usinitese mpenzi. Nakuomba!”
“Tutaongea hiyo kesho wala usijali!”
“Sawa. Nakupenda.”
“Ahsante!”
“Jamaniiiii!”
“Sasa unataka nisemeje?”
“Kwani hunipendi?”
“Nijibu! Hunipendi?”
“Nakupenda!”
“Naomba usinisaliti mpenzi!”
“Kwani tayari tushakubaliana?”
“Gideon! Hata kama ila naomba usinisaliti!”
“Daaah! Aya!” baada ya hapo, akazima simu yake na kulala.
Asubuhi ilipofika, akachukua simu yake na kuiangalia, akakutana na ujumbe murua kutoka kwa Juliana, alizielezea hisia zake ni kwa jinsi gani alikuwa akimpenda, jinsi moyo wake ulivyokuwa kwenye mapenzi ya dhati, hakuwa akijiweza, kwake, mwanaume huyo alikuwa kila kitu.
Gideon akatabasamu, akainuka kutoka kitandani, akachukua taulo lake na kwenda bafuni kuoga. Huko alichukua muda mwingi kumkumbuka Juliana, alimpenda sana lakini hakutaka kujilainisha kwake kwani kwa kipindi chote cha nyuma yeye ndiye alikuwa akihangaika sana lakini msichana huyo hakujali.
Alipofika chuo, Juliana akamfuata, kabla ya kuzungumza kitu chochote kile, akamkumbatia. Wanachuo wengine wakabaki wakishangaa, hali hiyo ikazua maswali mengi na wengine kuamini zile tetesi zilizokuwa zikisema kwamba watu hao walikuwa wakitoka kimapenzi.
“Juliana! Huogopi macho ya watu?” aliuliza Gideon huku akiwa amekumbatiana na msichana huyo.
“Sijali!”
“Unahisi watasemaje? Wapendwa kukumbatiana na kugandana namna hii kama ruba?” aliuliza Gideon kwa sauti ya kunong’ona.
“Hata Biblia imeandika salimianeni kwa busu takatifu!”
“Ila si kukumbatiana!”
Juliana akatoka mikononi mwa Gideon na kubaki wakiangaliana. Sura ya msichana huyo ikabaki kwenye tabasamu pana lililomchanganya zaidi mwanaume huyo kiasi kwamba moyo wake ukazidi kumpenda japokuwa kwa kipindi hicho hakutaka kumwambia kitu chochote kile.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao. Wakati mwingine Juliana alikuwa akienda nyumbani kwa Gideon ambapo huko walipata muda wa kuzungumza sana na kila Juliana alipotaka kulala na mwanaume huyo kitandani akawa akikataa.
“Sasa mimi nitalala na nani?” aliuliza Juliana, alionekana kukasirika kwani kila kitu alichokuwa akikihitaji, Gideon hakukubaliana nacho kabisa.
“Muda bado!”
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”
“Basi ngoja niwafuate watu wanaoona muda tayari,” alisema na kuanza kuvaa nguo zake harakaharaka.
Gideon alimwangalia Juliana, msichana huyo hakuonekana kutania hata mara moja, alionyesha kumaanisha kwamba alikuwa radhi kulala na mwanaume mwingine kama tu Gideon asingekuwa radhi.
Hakuwa na jinsi, alimuumiza sana msichana huyo, alipokuwa akivaa, akamshika mkono na kumvutia kwake, akamwangalia machoni na kutoa tabasamu.
Juliana alishindwa kuyatuliza macho yake usoni mwa Gideon, alikuwa akijisikia aibu na hivyo kuangalia chini. Gideon akaanza kuzitoa nguo zake na hatimaye baada ya dakika chache zikaanza kusikika sauti za kitanda kikilalamika.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuwa wapenzi, hawakulala siku moja bali waliendelea kufanya hivyo kila siku. Mapenzi yao yakawa radhi, wakasahau kuhusu Biblia, hata mafundisho ya kanisani hawakuyakumbuka kabisa.
Walipendana kwa mapenzi ya dhati, kwa kuwa Gideon hakuwa na uwezo mzuri kifedha, msichana Juliana ambaye alitoka katika familia yenye uwezo ndiye aliyekuwa akigharamia kila kitu, kuanzia kodi ya nyumba ya mwanaume huyo mpaka chakula.
“Gideon! Ninahitaji kuwa nawe maisha yangu yote,” alisema Juliana huku akimwangalia Gideon.
“Hakuna shida mpenzi. Ninakupenda, nipo tayari kuishi nawe mpaka kifo kitakapotutenganisha,” alisema Gideon huku akimwangalia msichana huyo.
“Kweli?”
“Niamini mpenzi. Ninakupenda sana!”
Wakati wakilifurahia penzi lao jipya, nyuma ya pazia kulikuwa na watu ambao waliumia sana kuwaona wawili hao wakipendana na hivyo kuanza figisufigigu na miongoni mwa watu hao alikuwa msichana Halima.
Kwa kumwangalia, alikuwa msichana mrembo, mwenye ngozi ya maji ya kunde, alikuwa na uzuri wa ajabu na wanaume wengi walikuwa wakimpenda mno.
Halima hakuwa msichana mwepesi, alikuwa mgumu, watu wengi walimfuata kwa pesa na magari bado hawakuweza kumpata, wengine walimtumia zawadi mbalimbali lakini hawakuweza kufanikiwa kulipata penzi la msichana huyo.
Halima alikufa na kuoza kwa Gideon, alimpenda, kwake alikuwa mwanaume mwenye taswira ya ajabu, aliuburuza moyo wa msichana huyo kiasi kwamba kuna wakati akawa hajiwezi.
Alichukia mno alipoona Juliana akiwa na mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati. Usiku alipokuwa kitandani alikuwa akilia sana, alimuomba Mungu ampate Gideon katika maisha yake kwani ndiye mwanaume aliyeonekana kuzaliwa kwa ajili yake.
Mapenzi yalimliza, wivu ukamchoma mno moyoni mwake, akawa hajiwezi na muda mwingi alikuwa akiziangalia picha za Gideon zilizokuwa katika simu yake ambazo alimpiga kisiri na kuzibusu.
Alikuwa tayari kufanya chochote kile lakini mwisho wa siku awe na mwanaume huyo, alikuwa tayari kupoteza kila kitu lakini awe na mwanaume huyo aliyekuwa wa ndoto katika maisha yake.
Baada ya kuvumilia sana, baada ya kulia sana akaamua kuupiga konde moyo wake na kumfuata mwanaume huyo. Hakuogopa tena, alikuwa tayari kukataliwa lakini mwisho wa siku awe amemwambia mwanaume huyo kuhusu hisia zake, kwa nini aogope? Kwa nini ateseke? Kwa nini aumwe na wakati kulikuwa na daktari wake.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni