JULIANA (6)
Zephiline F Ezekiel
5 min read
Mwandishi: Emmy John Pearson
SEHEMU YA SITA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Jamani! Basi tukampoteze,” alishauri Juliet.
“Tumpotezaje?”
“Tumuue!”
“Sawa. Ngoja nikafanye mipango, mwanamke yule hatakiwi kuishi. Kwanza pale alipokuwa tayari maiti,” alisema Gideon.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
Hakukumbuka chochote kuhusu mke wake, alimchukia, kila alichosema Juliet alimsapoti, hakukumbuka kwamba zamani hakuwa na pesa lakini msichana huyo alimpenda hivyohivyo, hakukumbuka kwamba utajiri aliokuwa nayo, chimbuko lake lilikuwa kwa wazazi wa mwanamke huyo huyo, hakukumbuka kitu chochote kile, kitu pekee alichokuwa na hamu nacho kwa wakati huo ni kumuua Juliana tu.
Akarudi nyumbani huku akiwa na muonekano mwingine kabisa. Akamkuta Juliana akiwa sebuleni amekaa akimsubiri. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake kila siku, hakukubali kulala na wakati mume wake hakuwa amerudi nyumbani.
Ilikuwa ni lazima kukaa sebuleni mpaka mwanaume huyo atakaporudi nyumbani hapo. Alipokuwa akija, hakuzungumza naye, alimsalimia mwanaume huyo lakini alikuwa kimya, hata salamu hakutaka kabisa.
Siku hiyo Gideon alipoingia, alionekana kuwa tofauti, alipoufungua mlango na kumwangalia mke wake, tabasamu pana likaonekana usoni mwake.
Juliana akashangaa, hakuamini alichokuwa akikiona, hakuwahi kuliona tabasamu la mume wake tangu alipoanza kuugua, leo iweje mwanaume huyo atoe tabasamu pana kiasi hicho?
Kwa tabu sana akasimama na kumfuata mume wake, alipomfikia, akamkumbatia, kwa furaha aliyokuwa nayo moyoni, Juliana akaanza kulia, hatimaye mume wake wa zamani, mume wake yule aliyekuwa kipindi cha nyuma alikuwa amerudi pasipo kugundua kwamba mwanaume huyo alikuwa na jambo lake moyoni mwake.
“Nimekukumbuka mke wangu,” alisema Gideon huku akimwangalia Juliana.
“Nimekukumbuka pia,” alisema Juliana huku akilia kwa furaha.
Wakaongea mengi kama wanandoa, wakaondoka na kuelekea chumbani.
Kila kitu alichokuwa akikifanya, moyo wake ulimuuma mno, hakutaka kumshika mkono Juliana lakini kwa kuwa alitaka kumuua, ilikuwa ni lazima kufanya hivyo.
Akamuacha chumbani na kumwambia kwamba aende jikoni kuchukua chakula na kula. Akaondoka na kuelekea huko ambapo kitu cha kwanza kabisa ni kuchukua simu na kumpigia Juliet.
“Vipi? Umemuua?” alisikika Juliet kwenye simu.
“Bado!”
“Acha ujinga. Unasubiri nini sasa?” aliuliza msichana huyo.
“Ndiyo naandaa mazingira!”
“Au bado unampenda?”
“Walaaa!”
“Au bado unampenda?”
“Walaaa!”
“Au unataka kuendelea kuwa na maiti yako hiyo?”
“Hapana mpenzi!”
“Sasa kwa nini unachelewa? Hebu muue bwana nije niishi na wewe na kukuuonyeshea jinsi mapenzi yanavyotakiwa kuwa,” alisema msichana huyo.
“Sawa laazizi! Nipe dakika kadhaa!”
Simu hiyo ni kama ilimuhamasisha kufanya kile alichoambiwa. Akachukua chakula na kurudi chumbani, akatulia kwa muda, alitakiwa kufanya hilo haraka iwezekanavyo lakini hakujua ni kwa namna gani angeweza kumuua Juliana.
“Ngoja nitoke naye! Nikifika huko, namuua na kurudi na maiti yake,” alisema Gideon na hivyo kumgeukia mke wake.
Alichokifanya ni kumwambia mke wake kwamba alitaka kutoka naye kwenda sehemu fulani kwa ajili ya kupumzika, alikuwa na mazungumzo naye juu ya hali yake na aliamini kwamba endapo angezungumza naye basi furaha aliyokuwa nayo kipindi cha nyuma ingerejea tena.
Kwa Juliana hakukuwa na tatizo, alifurahia sana kwani hakukuwa na mwanaume aliyekuwa akimpenda kama ilivyokuwa kwa mume wake, akakubaliana naye pasipo kujua lengo la mwanaume huyo lilikuwa ni kumuua.
Wakatoka nje huku Juliana akijikongoza mpaka ndani ya gari, akakaa na kutulia tuli. Akili yake ilikuwa ikifikiria mbali kabisa, ukaribu ambao mumewe alimuonyeshea siku hiyo ulimkumbusha jinsi walivyokuwa katika kipindi cha uchumba.
Kabla ya kwenda kwenye gari, alichokifanya Gideon ni kuchukua kisu na kukiweka kiunoni, alitaka kumuua na kumshikisha kisu kile kuonyesha kwamba mwanamke huyo alikuwa amejiua.
“Kwa mpango huu! Hakuna atakayebisha kama amejiua,” aliwaza huku akiingia garini.
Hakutaka kugundulika hivyo kila wakati uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana lililomfanya Juliana kuona kwamba mumewe alikuwa na furaha kubwa, hata chuki aliyokuwanayo moyoni haikuwa ikionekana usoni.
Gideon akaliwasha gari na kuondoka mahali hapo. Njiani, Gideon ndiye alikuwa mzungumzaji sana, alimchangamsha mkewe kwa mameno mengi, alitaka kumuonyeshea kwamba kila kitu kilichokuwa kimetokea kipindi cha nyuma kilitokea kwa bahati mbaya lakini mapenzi yake yalikuwa kwa mke wake huyo.
Safari yao ikaishia katika Ufukwe wa Coco ambapo ndipo alipotaka kufanya mauaji ndani ya gari kabla ya kumchoma kisu kisha kumtupa huku akimshikisha kisu hicho ili kuonyesha kwamba mwanamke huyo alijiua kwa kujichoma kisu.
Gari liliposimama, Juliana akabaki akishangaa, hakujua sababu iliyomfanya mumewe kusimamisha gari mahali kama hapo. Hakuwa na hofu naye kwani alihisi kila kitu kilikuwa salama kabisa.
Wakati akifikiria hayo tayari Gideon akaanza kukishika kisu chake kilichokuwa kiunoni, alitaka kummaliza Juliana hapohapo garini kisha kumtoa na kumshikisha kisu kile kuonyesha kwamba alijimaliza mwenyewe.
“Moja, mbili, tat…” alihesabu kabisa.
Wakati akihesabu, ghafla akasikia simu yake ikianza kuita, akashtuka, haraka sana akaichukua kutoka mfukoni mwake na kuipeleka sikioni hata bila kuangalia mpigaji alikuwa nani.
“Umemaliza?” ilisikika sauti ya Juliet kwenye simu.
“Bado!”
“Kwa hiyo umeshindwa? Basi usinijuejue,” ilisikika sauti hiyo.
“Hapana! Sijashindwa! Naomba dakika chache kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Gideon huku akionekana kuogopa kumpoteza msichana mrembo kama Juliet.
Wakati akizungumza na Juliet kwenye simu, Juliana alibaki akimwangalia, mumewe alikuwa akizungumza kwa kukatishakatisha maneno kitu kilichoonekana kuwa na hofu kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Gideon alitumia sekunde chache, alipomaliza, akashusha pumzi nzito, akajigusa kiunoni kuangalia kama kisu chake kilikuwepo, alikiona na hivyo kujiandaa kukichukua kwa ajili ya kumchoma Juliana.
Hata kabla hajafanya hivyo, simu yake ikaanza kuita tena. Moyo wake ukapiga paaa kwani alijua kabisa kwamba mpigaji alikuwa Juliet, haraka sana akaichukua na kuipeleka sikioni.
“Nimekwambia nipe dakika chache,” alisema Gideon mara baada ya kuipokea simu.
“Kaka! Kuna tatizo nyumbani…” Ilisikika sauti ya Halima, msichana wa kazi aliyekuwa naye nyumbani kwake.
“Kuna tatizo?”
“Ndiyo! Jesca anaumwa sana, mwili wake umeanza kushika joto mno,” alisikika Halima.
“Nani? Jesca? Anaumwa sana? Mwili umeshika joto?’ aliuliza Gideon mfululizo.
Gideon alichanganyikiwa, hakuamini alichokuwa amekisikia kwamba mtoto wake wa pekee, Jesca alikuwa akiumwa mno usiku huo. Japokuwa alikuwa kwenye hatua za mwisho kumuua mke wake ndani ya gari, hakutaka kufanya hivyo bali akakiacha kisu chake, akawaha gari na kuondoka mahali hapo.
Juliana aliishiwa nguvu, aliposikia kwamba mtoto wake alikuwa akiumwa alichanganyikiwa, alimpenda mno, alikuwa kwenye maumivu makali, familia yake ndiyo ilikuwa kila kitu, alimuuliza mumewe mara kwa mara kuhusu Jesca lakini hakujibu kitu kwani naye alichanganyikiwa mno.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika nyumbani, harakaharaka wakateremka na kuanza kuelekea ndani. Japokuwa Juliana alikuwa akiumwa sana lakini akajikaza mpaka kufika chumbani ambapo wakamkuta mfanyakazi akiwa na mtoto sebuleni huku akimbembeleza anyamaze kwani alikuwa akilia sana.
“Tatizo nini?” aliuliza Gideon huku akimshika Jesca.
“Sijui ila nadhani ni maralia. Mwili wake umechemka sana,” alisema mfanyakazi huyo.
“Jesca…Jesca tatizo nini mama?” aliuliza Juliana huku naye akimgusa mtoto huyo kupima joto la mwili wake.
Alikuwa kwenye hali mbaya, Jesca hakujibu chochote kile zaidi ya kuendelea kulia. Hawakutaka kubaki mahali hapo, haraka sana wakamchukua, wakampakiza ndani ya gari na kuanza kuondoka mahali hapo.
Garini, kila mmoja alikuwa kimya, Juliana alimpakata mtoto wake huku mumewe akiendesha gari hilo. Gideon akasahau kabisa kuhusu Juliet, wakati huo kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mtoto wake aliyekuwa kwenye hali mbaya tu.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika hospitalini ambapo moja kwa moja wakateremka na kuanza kuelekea ndani huku wakiwa wamembeba mtoto huyo. Manesi walipowaona, wakaleta machela, wakampakiza na kuanza kuelekea ndani.
Walikwenda mpaka katika chumba kimoja kilichoandikwa ICU kwa nje na kuambiwa wasubiri hapo.
Hawakutulia kwenye mabenchi yaliyokuwa mahali hapo, walitaka kujua kile kilichokuwa kikiendelea humo ndani.
Baada ya saa moja, mlango ukafunguliwa na mwanaume mmoja mnene aliyekuwa na koti jeupe na kuwaambia kwamba mtoto wao alishikwa na maraliia kali hivyo walitakiwa kuondoka na kumuacha hapo apumzike kwanza.
“Siwezi kuondoka na kumuacha mtoto wangu!” alisema Juliana huku akimwangalia daktari.
“Sawa. Ila hutoweza kumuona kwa kipindi hiki!”
“Haina shida. Ila kuondoka mahali hapa siwezi,” alisema Juliana.
Alimaanisha, ilikuwa vigumu kuondoka na wakati mtoto wake alikuwa kwenye hali mbaya kupita kawaida. Vile alivyosema ndivyo alivyomaanisha kwamba kamwe asingeweza kuondoka mahali hapo hapo na wakati mtoto wake alikuwa kwenye hali mbaya kupita kawaida.
Kwa sababu muda ulikuwa umekwenda sana, Gideon akaondoka kwa ajili ya kununua chakula, alipofika ndani ya gari tu, simu yake ikaanza kuita na alipoangalia jina la mpigaji, alikuwa Juliet, kwanza moyo wake ukapiga kwa nguvu, hakutegemea kwamba msichana huyo angepiga tena simu huku akiwa hajafanya kile walichokuwa wamekubaliana.
“Umekwishamuua?” lilikuwa swali la kwanza hata kabla ya salamu.
“Bado!”
“Bado? Kwa nini? Hutaki kuishi na mimi? Mbona hutaki kunisikiliza? Mbona hutaki kufanya ninachotaka ukifanye hubby?” aliuliza Juliet huku akijifanya kulia kwenye simu.
Kwa jinsi moyo wake ulivyokuwa ukimpenda msichana huyo, Gideon akajisikia vibaya moyoni mwake, alijiona kama mkosaji mkubwa. Alitamani kumuomba msamaha kwani kilio chake kiliuumiza mno moyo wake.
“Kwa nini lakini hubby?”
“Naomba unisamehe! Kuna tatizo liilitokea,” alisema Gideon.
“Tatizo gani?”
“Mtoto wangu anaumwa sana. Tumemleta hospitalini. Ila nilikuwa katika hatua za mwisho kukamilisha mpango wetu,” alisema Gideon.
“Kwa hiyo akiwa anaumwa ndiyo mama yake hawezi kufa?” aliuliza Juliet huku akionekana kuwa na hasira.
“Hapana!”
“Kumbe tusemeje? Mimi najua hunipendi tu! Najua unataka kunichezea,” alisema Juliet huku akilia kitu kilichomfanya Gideon kusikia uchungu mno kwenye simu.
Alitamani hata kumpigia magoti msichana huyo, alikuwa akimpenda mno na alikuwa na hamu ya kufanya kile alichotakiwa kufanya ili kumpa furaha lakini kutokana na hali ilivyokuwa nyumbani hapo alishindwa kabisa.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni