MTU WA UFUKWENI (4)

0
Mwandishi: Andrew Mhina

SEHEMU YA NNE
ILIPOISHIA...
Hata babu yake alikuwa akimshauri atulie na kuangalia masomo tu kwa kuwa kila kitu kipo sawa ila Ramson aliendelea na msimamo wake na bidii katika mashamba hasa kusimamia na kufanya kazi.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI

SASA ENDELEA...
Mwisho wa yote Mzee alinyamaza kwani hakuona kama kuna tatizo kwakuwa katika masomo Ramson hajawahi kupoteza maks zake. Alishikilia namba moja kwa kila mtihani na kazi za nyumbani alikuwa yuko vizuri. Kutokana na bidii yake babu yake alikuwa akimnunulia nguo nzuri sana kila mara hadi kusheheneza mavazi tele ya thamani. Nguo na viatu vya shule alinunuliwa pea nyingi. Alikuwa akibadilisha viatu kila siku na nguo zake za shule zilikuwa safi kila mara.

Mara kwa mara alipewa zawadi ya kuwa Mwanafunzi msafi shuleni kwao. Na mtaani mara tu baada ya kumaliza kazi zake za shamba alikuwa akivaa mavazi mazuri na mifukoni mwake hakupungukiwa na hela. Pamoja na yote hayo Ramson hakuwahi kujihusisha na tabia za uhuni. Wasichana wengi walimfuata wakimtaka urafiki, mitaani na hata shuleni, lakini alibaki kuwaheshimu kama dada zake tu.

Kati ya mambo aliyoyazingatia ni pamoja na wosia wa babu yake aliokuwa anamwambia kila wakati kuwa: “Mambo yote mazuri ni mazuri kwa wakati wake, ukiyaharakisha yanakuwa machungu kuliko shubiri!”Pia mzee huyo alikuwa anamwonyesha baadhi ya vijana kijijini hapo wanaougua ukimwi na wale waliopoteza maisha yao kwa sababu ya kuharakisha mambo. Haya yalikuwa mausia mema kabisa na kwa busara alizokuwa nazo Ramson alizingatia na kujiepusha na mambo yote mabaya.

“Nimesema hilo wazo nililotoa linafaa sana kumbambikizia huyu mwendawazimu! Unajua kama tutasema kuwa ni mwizi hiyo inaweza ikakubaliwa na watu wengi kwa sababu ya jinsi anavyopiga pamba za ghali kila mara.” Alisema kijana mmoja aitwaye Rafa katika moja ya vikao vyao vya kutaka kumharibia Ramson sifa. “Lakini wewe hujafikiri vizuri juu ya wazo lako hili! Nakwambia mwanangu hapo umekurupuka; hebu angalia mwenyewe jamaa alivyo na bidii katika kazi ninani asiyejua hilo? Kama tukiulizwa kuwa tuna ushahidi gani tuna lipi la kuonyesha?”

Alimaliza kwa hoja Abuu kijana aliyekuwa akijihusisha na biashara ya kuuza misokoto ya bangi kwa wahuni wote kijijini hapo. “Aaaa! Hilo mwanangu mbona rahisi? hujaona mtu akibebeshwa zigo la bangi na kuhukumiwa kwenda jela mvua kadhaa kumbe msala ulikuwa sio wake kabisa? Sawa kabisa Mchizi! unajua hapa la maana ili huyu mtoto asizidi kutunyanyasa na kuonekana sisi hatuna inshu kutokana na mambo yake kuwa safi inabidi kumchomea nguru! Hebu basi Tumsikilize bwana mipango tuone mbinu zake atakazotuambia.” Alisema Alen aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo aliyekuwa amekaa kimya muda wote.

Wote walimgeukia Beka ambaye alisifika kwa kutoa mawazo ya hapo kwa hapo na yenye viwango vikubwa. Huyu bwana alikuwa na akili nyingi sana katika kupanga mambo mabaya! mipango ya kuiba na hata kuua. Kuna wakati waliwahi kufanya uhalifu katika duka la mhindi kijiji cha tatu kutoka kilipo kijiji chao. Waliiba mashine ya kukatia miti iitwayo Chensoo!

Walipogundua kuwa mfanyakazi yule amewagundua walikwenda kuificha mashine ile na kurudi kinyemela ili kumfuatilia wajue kuwa atafanya nini! Walipofikawakamkuta amemwamsha mhindi na walikuwa katika harakati za kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi. “Umesema iko nafahamu miji ote ee”! Aliuliza mhindi huyo. “Ndiyo mzee nawafahamu wote wako kijiji kile anakoishi Kishori!”

“Basi kimbia bana nenda ambia polisi wao nakamata miji ote sawa?” Mhindi alimwamrisha aliamrisha mfanyakazi wake aitwaye Kihoba.Naye alianza safari usiku huo akielekea Kituo cha polisi. Kituo cha Polisi kilikuwa umbali kama wa dakika tano hivi. Baada ya kutoka aliteremka kilima kidogo kwa tahadhari, lakini kabla hajaenda mbali alivamiwa na kundi la akina Beka na asubuhi yake alikutwa amekufa kando ya njia. Msako wa kutafuta wauaji haukufanikiwa na mhindi yule wala hakujitokeza kuzungumzia habari za wizi uliofanyika dukani kwake. Hii ilisababisha uchunguzi kukosa mwelekeo mzuri. “Tunakusikiliza Beka.” Alen alimshtua Beka kwenye lindi la ukimya akiwa anatafakari njia ya kufanya. “Okay! Nimeona kwa wakati huu tunaweza kufuatilia nyendo za kijana mahali atakapokuwa kesho baada ya kutoka shule. Kisha tutajua la kufanya baada ya hapo. Kwa sasa inabidi tumtume dogo Sam ili afuatilie hilo halafu akitujulisha ratiba yake ya kesho usiku huu huu tutajua la kufanya sawa?” Wote wakakubaliana na Sam alitumwa kumfuatilia.

Baadhi ya wanakijiji walikuwa wamemzunguka Ramson akiwa shambani kwao. Zogo lilikuwa limetanda mahali hapo kila mmoja akitoa shutuma kwake na wengine wakitaka kumpiga. Chini yake kulikuwa na mfuko wa nailoni wenye vitu mbalimbali vya dukani; mzigo uliosemekana kuwa Ramson aliuiba dukani kwa Mpemba. Ramson alivimba uson kwa kipigo na alichaniwa nguo zake katika kurupushani ya kumlazimisha kubeba mzigo ule na kuelekea Kituoni.

“Jamani siwezi kubeba mzigo huu, sio wangu na sijahusika kuiba vitu hivi.” alijitetea Ramson huku akilia kwa uchungu. “Kijana usitutanie kabisa beba mzigo wako na uongoze njia twende kituoni; tulizani ni kijana mpole na mchapakazi kumbe ni mwizi tu!”Alisema jamaa mmoja aliyekuwa mstari wa mbele katika kutoa adhabu kwa Ramson.Mwishowe walimnyanyua kwa nguvu na kumbebesha mzigo ule huku wakimpiga vibao na wengine wakimchapa kwa fimbo. Walimfikisha kituoni na kumfungulia jalada na hatimae wakamwingiza mahabusu.

Ramson alikuwa katika wakati mgumu sana, sio kwa kipigo alichokipata bali kwa uzushi aliofanyiwa. Katika maisha yake hajawahi hata kufikiri kuhusu wizi. Mpaka kufikia umri alionao alikuwa ameshayamudu maisha yake kuliko hata baadhi ya wakaazi wa kijiji hicho. Mbali na mashamba mengi aliyokuwa nayo babu yake na mifugo, mbali na kuwa urithi wote wa mali hizo ni wake, lakini yeye mwenyewe alikuwa akisimamia mashamba ya marehemu baba yake kwa bidii sana.

Alikuwa na maisha mazuri na hakuwahi kupungukiwa na kitu. Huo ndio ukweli binafsi wa maisha yake, ukweli unaojulikana na baadhi ya wanakijiji, ukweli ambao umefumbiwa macho na masikio ili kumdidimiza katika shimo la takataka na kuuchafua utu wake. Moyo wa Ramson uliuma sana kuliko maumivu yenyewe, kwa kupakwa matope na kuharibiwa sifa yake aliyojaribu kujitengenezea kwa umakini mkubwa. Hili ni doa lisiloweza kufutika kwa baadhi ya vichwa vya watu. Uelewa wa mambo kwa watu unatofautiana kulingana na fikra kuwa tofauti.

Jambo moja zuri sana linaweza kufanyika kati ya watu, lakini uzuri wake ukapatiwa tafsiri nyingi na watu waliopo. Wengine watasema ni zuri sana wengine watatoa kasoro uzuri wake na wengine watasema ni baya. “Haiwezekani nizushiwe mambo mabaya kiasi hiki! ina maana watu hawaoni badii yangu na uadilifu wangu ndani ya kijiji hiki?” Hivyo ndivyo alivyokuwa akitafakari Ramsoni katika chumba kidogo cha mahabusu kilichokuwa na harufu mbaya ya mikojo. Hali ya mawazo mbalimbali yalipita kichwani mwake akiwa hajui la kufanya katika kiza hicho kigeni katika maisha yake. Alijiona akiwa katika kona mbaya sana! kona iliyokusudiwa kuharibu mipango ya maisha yake ya baadaye.

Mawazo ya kuwa mtu maarufu mwema na mwenye kusababisha maendeleo kwa nchi yake viligeuka kuwa ndoto ya mwendawazimu. Kashfa ya wizi ilimvunja nguvu kabisa na kumwathiri kifikra. Aliwakumbuka wazazi wake aliotaka kuwaenzi katika maisha yake kwa kuwa mtu mchapakazi na msomi.

Alifikiri juu ya bidii zake katika kazi na uaminifu wake kwa jamii iliyopo kijijini hapo. Baadaye alishindwa kuelewa kuwa ninani aliyeleta mzigo ule pale shambani tenandani ya kibanda chake cha kupumzikia baada ya kazi? Hofu ilimkamata alipofikiria kuwa babu yake atakapopata habari hizi atamchukuliaje? moyo wake uliuma sana na ghafla machozi yalimtoka kwa huzuni kubwa.

“Nafikiri tuna sababu ya kujipongeza maana yule mtanashati ameingia matatani!” Alisema Beka kwa majivuno huku akiwasha msokoto wa bangi. “Ule mchezo ulikuwa kiboko mtu wangu. Pale hachomoki au mnasemaje masela wangu!” Aliropoka Alen mkuu wao wa kundi.

“Unajua watu wengi huingia matatani hivihivi kwa kubambikiziwa kesi bila wao kuhusika?” Alisema Abuu kisha akaendelea. unajua kwanini watu wangu wa nguvu? Ninakumbuka kupata taarifa nyingi ndani aidha ya mitandao na hata kwenye Televisheni zikizungumzia habari za matukio yaliyowapeleka watu wengi gerezani au kukutanishwa na kitanzi.

Kesi hizo si za kweli bali wamebebeshwa tu kama hivi! Upelelezi mwingine unafanyika juu juu tu na kuacha ukweli wa jambo ukipepea na kupotea machoni mwa sheria dhidi ya mtuhumiwa. Wengi walipewa mizigo ya madawa ya kulevya kwenye mabegi yao ya safari bila wao kujua. Wanapofika Airport wanashangaa wakati wakiingizwa matatani.

Ili ujue kweli wamebambikiwa ni pale mtu anapokiri kuwa mizigo ile ni yakwake wakati wachunguzi wakishaipima na kuona kuwa kuna madawa ya kulevya. Hawezi kukana begi lake wakati anajua halina chochote ndani kibaya, baadaye watu hawa hufunguliwa mashtaka na kufungwa kizembe sana, kumbe hawakuhusika. Mchezo huu kaucheza vizuri sana Beka kwa yule mtoto wa marehemu!” Alisema Rama kwa Utani zaidi huku akisababisha wengine kuangua kicheko cha dhihaka.

“Ninakumbuka jinsi Nilivyomfuatilia baada ya kuiba pale kwenye duka la mpemba. Nilibeba ule mzigo nikifuatana na dogo Sam kumfuatilia kijana mpaka shambani kwao. Alipofika hakukaa sana kwenye kibanda alitoka na kuelekea kwenye kisima chao ili achomeke mpira wa kunyweshea. Kwakweli yule kijana nimemhusudu sana kwa bidii zake. Kuna wakati ninafikiri kufuata nyayo zake lakini ninajiona nimeshachelewa.

Kuanza kugumu heri mwenzetu ameyakuta yametayarishwa na babu yake na marehemu baba yake. Sasa ukiambiwa wewe uanze mpaka kufikia hatua ile utasota sana na siajabu usifikie kutokana na kukosa zana za kazi na mtaji. Baada ya kumwona akienda kuchomeka mpira kisimani, niliingiza ule mzigo kwenye kibanda chake na kutoka mbio. Nilimpigia mpemba nikiwa njiani karibu na kijijini kumwarifu kuwa baadhi ya bidhaa za dukani kwake zimefichwa kwenye shamba la Mzee Kihedu na kijana wake ndiye mwizi.”

Alihitimisha Rama sehemu ya taarifa ya kazi aliyopewa na kundi lile. “Enhee! Mpemba alivyokuuliza wewe ninani ulimjibuje?” Aliuliza Alen. “Swali hilo aliuliza mwanzoni wakati akipokea simu, lakini aliposikia taarifa za kupatikana kwa baadhi ya mali zake akasita ili asikilize kwa makini.

Mwishoni ndio akauliza kwani ninaongea nanani?! Nililisikia sana swali hilo ila nilikata simu kabla sijajibu lolote.” Umefanya vizuri dogo ila hakikisha namba yako unaibadilisha mapema k

USIKOSE SEHEMU IYOFUATA

Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)