MTU WA UFUKWENI (5)

0
Mwandishi: Andrew Mhina

SEHEMU YA TANO
ILIPOISHIA...
Mwishoni ndio akauliza kwani ninaongea nanani?! Nililisikia sana swali hilo ila nilikata simu kabla sijajibu lolote.” Umefanya vizuri dogo ila hakikisha namba yako unaibadilisha mapema kwa sababu inaweza ikagundulika tukaingia matatani.” Alisema Aleni kwa msisitizo.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI

SASA ENDELEA...
Mawazo yake yalikatishwa ghafla sana kwa kishindo cha kufunguliwa kwa mlango wa chuma wa mahabusu hiyo. Mara baada ya kufunguliwa mlango kwa makeke ya aina yake askari mmoja mweusi na mwenye macho makali alijitokeza na kuita Ramson Kimbe!” Ndani ya chumba kile cha mahabusu hakikuwa na wahalifu wengine..

Hivyo Ramson aliitika na kusimama. “Njoo nje mara moja.” Aliamrisha askari yule na Ramsoni alimfuata mpaka mapokezi. Moyo wake uliruka mapigo kama mawili mfululizo baada ya kumwona babu yake amekaa kwenye kiti akimsubiri. Uso wake wa upole lakini wenye aina fulani ya mshangao ulimtuliza kidogo Ramson na kumsalimia kwa unyonge kidogo. “Shikamoo babu.”

“Marahaba Mjukuu wangu, pole sana kwa matatizo. Nimekuja kukutolea dhamana mengine tutakwenda kuyaongelea nyumbani.” Baada ya Ramson kukabidhiwa vitu vyake, wakaanza safari ya kurudi nyumbani. Njiani walikuwa kimya sana. Kila mmoja akiwaza lake moyoni kati ya Ramsoni na babu yake. Nyumbani walimkuta Bibi akiwa katika majonzi ya aina yake huku akiwa kashika tama.

Alipomwona Mzee Kihedu na mjukuu wake alishangilia sana! “Ooo mjukuu wangu! pole sana kwa matatizo!” Alimkumbatia mjukuu wake na kumshika mkono na kuingia naye ndani. ..Kisha akaendelea..“Pole sana Ramson kwa matatizo. Tunajua jinsi tunavyochukiwa katika kijiji hiki cha Tabu ya nini! Hizo zote ni njama tu za watu wabaya wanaoyachukia maendeleo yetu.”

Alisema bibi sauti ya majonzi akionyesha kuwa alikuwa na mzigo mzito sana moyoni mwake. “Usiogope Ramsoni tutafanya mpango kesi hii haitaenda mahakamani, niko tayari kutoa kiasi chochote cha fedha kulipa, lakini sitakuwa tayari uathirike kisaikolojia.” Alisema babu kwa msisitizo na kumfanya Ramson apate nafuu kubwa moyoni mwake kwa kujua kuwa kumbe familia yake haijaamini njama za maadui zake.

Hii ilimpa nguvu hata ya kuelezea jinsi ilivyotukia. “Kwakweli sijajua ninani walionifanyia njama hizi, maana wamesababisha jina langu kuchafuka kabisa kijijini hapa.” Hilo usijali sana Kijana wetu njama zao zitafichuka na ukweli utajulikana na wewe utabaki msafi kama ulivyo!”

Hakuna ubaya unaodumu katika vita kati yake na wema. Wema ni kama nuru na ubaya ni kama vile giza. Giza linatoroka na kupotelea mbali pale nuru inapotokea. Waswahili wana msemo wao wa busara usemao”“Ukweli ukisimama uongo hujitenga.” Iko siku Mabaya yanayofanyika kijijini hapa yatabainika, na wabaya wote na njama zao Watawekwa wazi.” Babu Kihedu alisema hayo kwa uchungu mkubwa.

“Nenda kaoge mjukuu wangu ubadili nguo ili upate chakula.” Bibi alimwambia mjukuu wake. Ramson alifanya hivyo huku akipata moyo wa matumaini kwa maneno ya babu na bibi yake. Baada ya matayarisho yote alipata chakula na kwenda kupumzika. Mzee Kihedu alirudi Kituoni asubuhi ya pili na kukutana na mkuu wa kituo.

Nia yake ni ili mambo hayo yasiende mahakamani. Mpemba aliitwa na kutakiwa wayamalize kwa kulipwa vitu vilivyoibiwa. Baada ya kuzungumza machache Mzee kihedu alimwambia Mpemba:“Iko siku Ammi utajagundua wabaya wako. Ninakumbuka wakati Ramsoni akiwa Chekechea ulivunjiwa duka lako hadi ukaanza upya kujenga na kulianzisha tena. Hali hii ilijirudia mara nyingi na wahalifu hawajawahi kutiwa ndani.

Leo Mjukuu wangu ndio anabambikiwa tatizo hili la wizi. inaniuma sana.” Alisema Mzee Kihedu kwa masikitiko.“Lakini Mzee kihedu kumbuka anayeshikwa na manyoya ndiye mwizi wa kuku; kwa hiyo usilalamike zaidi ya kulipa gharama na kukaa vema na mjukuu wako umkanye tabia zake hizi.Alimalizia Mpemba kwa maneno yake yanayoonyesha kutokuamini maneno ya Mzee Kihedu. Mzee Kihedu alilipa vitu vile vilivyotolewa kizibiti na gharama za mlango uliovunjwa kisha akaondoka kituoni hapo.

Miaka ilizidi kukatika na umri uliongezeka. Ilikuwa tayari miaka kumi imepita ikimaanisha kuwa tayari Ramson alikuwa ameshamaliza kidato cha sita. Majibu ya kujiunga na Chuo Kikuu hayakumpa nafasi hiyo, hivyo kumfanya aendelee na shughuli za shamba. Mengi yamepita magumu na ya kuumiza dhidi yake kijijini hapo.

Hakukuwa na nafuu yoyote kuhusiana na shutuma juu yake kuwa yeye ni mwizi wa nazi za watu, pamoja na mifugo kama vile kuku, mbuzi na ng’ombe. Vitu hivyo sio kwamba vilisingiziwa kuibiwa tu, bali ni kweli kabisa vilichukuliwa lakini lilikuwepo genge la wizi lililofanya kazi hiyo. Kwa sababu ya tabia ya uvivu Wanakijiji wa Taabu ya nini hawakutaka kupata tabu ya kuchunguza. Hivyo shutuma zote zilitupwa kwa Ramson. Ramson akawa Gumzo mitaani, mashambani, mpaka kwenye visima vya maji. Kama kulikuwa na habari kila wakati basi habari zote zilimhusu Ramson.

Ramson alikuwa kila siku akiomba Mungu siku zote ili ukweli ujulikane na kumtakasa mbele ya wanakijiji hao waliomchukia. Kijiji kilimchukia sio Ramson tu bali hata Mzee Kihedu na mkewe kwa shutuma kuwa alikuwa anafuga jambazi nyumbani kwake. Vijana walijitenga na Ramson naye pia alijitahidi kujilinda kila wakati akiogopa kudhuriwa. Genge la akina Alen lilizidi kufanya uhalifu kwani lilikuwa tayari na kinga; Kinga yao kubwa haikuwa hirizi ya kichawi bali Ramson alikuwepo kuzipokea shutuma zote!

“Mambo haya yatakuwa kwangu mpaka lini babu?” Aliuliza Ramson siku moja wakiwa wamekaa mezani na babu yake wakipata chai ya asubuhi. “Wewe vumilia tu mjukuu wangu, Mungu hamfichi mnafiki siku moja kila kitu kitakuwa wazi!” Alijibu babu yake. “Ni sawa babu hayo unayoyasema lakini mambo haya yamedumu kwa muda mrefu sana na kila siku maadui wanaongezeka juu yangu.

Sijui nifanyeje ili Genge hili linalofanya uhalifu hapa kijijini likamatwe na kutiwa mbaroni? Askari wetu hapa kijijini nao wamekaa tu kama raia, sina shaka kuwa inawezekana kuwa wanashirikiana na hawa wahalifu.. Kwakweli haki haiwezi kupatikana mapema juu yangu kwa mzigo huu wa lawama niliotwishwa bila kujulikana nitautua lini!

Unajua babu kila wakati ninafikiri kujiunga na jeshi la Polisi ili siku moja nije kukisafisha kijiji chetu maana kimechafuka kwa uovu! Lakini ni ajabu kuwa maovu hayo yote amebebeshwa mtu mmoja tu!”Alisema Ramson kwa upole wenye Uchungu mkubwa. “Iko siku kila kitu kitakuwa shwari mjukuu wangu, tuendelee kumwomba Mungu atatusaidia.” Hayo ndiyo maneno pekee babu yake Ramson aliyokuwa akimwambia Mjukuu wake kila wakati.

Ilikuwa ni mapema sana asubuhi kuliposikika zogo na kelele kutoka kona moja ya kijijihiki cha Taabu ya nini. Kelele zilizidi kuongezeka na watu walikuwa kama vile wako kwenye maandamano. Sauti hizi zilisikiwa vema na Ramson na babu pamoja na bibi wakati wakijiandaa kwenda shambani. kila baada ya muda kidogo kelele hizi ziliongezeka na kusogelea makaazi yao.

“Kuna nini leo mbona kuna maandamano?” Aliuliza bibi Namkunda baada ya kuchungulia dirishani na kuona watu wengi vijana kwa wazee, mbeleyao akiwepo mwenyekiti wa kijiji. “Ngoja nitoke nione kuna nini asubuhi yote hii, alisema hivi huku akifungua mlango na kutoka nje. nyuma yake alifuatiwa na Ramson! “Hatumtaki Ramson ahame kijiji hiki!!.. Ramson hahitajiki katika kijiji cha Tabu yanini! atatufilisi.

Ramson ni mwizi hatumtaki ama sivyo tutamwangamiza!!!”Hizo ni nyimbo zilizokuwa zikiimbwa na wanakijiji waliokuwa tayari wameizingira nyumba ya Mzee Kihedu. Umati wa watu ulijazana nje ya nyumba hiyo huku wakipiga kelele na Mwenyekiti akiwa kasimama mbele ya watu hao kwa hasira. “Jamani kuna nini tena asubuhi yote hii?” Aliuliza Mzee Kihedu kwa hamaki kidogo!!

“Mzee Kihedu miguu yote hii unayoiona imekanyaga hapa ni kwa sababu tumefikia mwisho kukaa na mjukuu wako katika kijiji hiki. Wizi wake akaufanyie huko mbali lakini kijijini hapa aondoke.” Alisema Mwenyekiti kwa ghadhabu sana huku akiitikiwa na watu wote waliofika hapo. “Kwani Ramson kafanya nini tena? Unajua ndugu mwenyekiti habari zote zinazoongelewa si vizuri zichukuliwe juu juu bila ya kufanyiwa uchunguzi! Inawezekana Ukweli ukajulikana.” Alisema Mzee Kihedu kwa utaratibu kama ilivyo kawaida yake.

“Mzee Ninakuheshimu sana! sidhani kuwa kuja kwangu hapa na watu wote hawa unaweza kutushawishi kwa Propaganda zako ili tumwache kijana wako aendelee kuwatia hasara wanakijiji wangu. Mimi mwenyewe ameshaniibia mbuzi wangu wawili. Nasema inatosha Ramson aondoke huo ndio uamuzi pekee wa kijiji!”

Alipomaliza kuzungumza aliwaamrisha watu wake watawanyike. “Nafikiri umenielewa, aondoke mapema sana maana sitegemei kuwa baada ya amri hii ataendelea kuwepo kesho kijijini hapa.” Alisema Mwenyekiti wakati watu wakitawanyika huku kila mmoja akisema lake kuhusu Ramson. Hali ilikuwa tete sana kwa familia hii kutokana na amri hiyo mbaya iliyotolewa dhidi ya Ramson.

Kila mmoja alichanganyikiwa na kukosa pa kuanzia ili kulitatua swala hili. Wazo la kuhama halikuwepo kwenye akili zao kwa maana hakukuwa na sehemu nyingine ambayo Ramson anaijua ya kuishi. Alipopajua tangu utoto wake ni hapo kijijini. Kijiji cha Tabu yanini ndipo mahali Mzee Kihedu alipozaliwa na familia yake aliikusudia ikae hapo na kuangalia mali zake, mali alizozitafuta kwa muda mrefu sana.

Hakuwa na mrithi zaidi ya Ramson vile vile hakuwa na ndugu wa karibu zaidi ya Ramson. Hali hii ilikuwa na utata wa aina yake. Alihisi kuwachukia watu wa kijiji hiki na mwenyekiti wao.“Ninashindwa nifanyeje kwa sasa lakini babu usiwe na wasiwasi, mambo yote yatakuwa shwari tu.” Alisema Ramson akiwa kasimama kwenye pembe ya nyumba, babu yake akiwa amekaa kwenye kiti akiwa kajiinamia. “Unafikiri tufanyeje mjukuu wangu kuhusu jambo hili? Mazao ndio hayo bado madogo mavuno bado mpaka labda baada ya miezi miwili.

Juzi ndio tumeuza ng’ombe wetu wanne wa kienyeji ili tununue Ng’ombe wa Kisasa.Tulifurahi sote kuwa sasa tutapata maziwa kwa wingi ya kuuza. Hapa nilipo sina akiba ya hela nyingi za kusema kuwa uende kupangisha nyumba mjini na kufanyia biashara. Unafikiri tufanyeje?” Aliuliza Babu akiwa anatafakari kwa undani cha kufanya. “Babu yangu na bibi naomba msihuzunike juu ya hili. Nitakwenda mjini na kuangalia ninini cha kufanya halafu nitajitahidi kuja ili nitoe taarifa kuwa niko wapi.

Najua Mungu amenipangia maisha mazuri sana mbali na kijiji hiki cha Tabu yanini. Maisha ni popote babu. Kuna msemo usemao kuwa ‘’Mwanamme hana kwao’’. Sijajua kuwa ni msemo wa busara sana, lakini haya ya leo yanaufanya usemi huo kuwa na maana kwangu.

USIKOSE SEHEMU IYOFUATA

Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)